Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyerwa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia kuendelea kuwepo katika Bunge hili kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Kyerwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais na kumpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya kuhakikisha anamtua ndoo mama kichwani. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na timu yako kwa ushirikiano mkubwa ambao mmekuwa mkinipa ninapokuja ofisini kufuatilia miradi ya maji kwa ajili ya Wilaya ya Kyerwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze RM wa Mkoa wa Kagera kwa kazi nzuri na ushirikiano anaotupa sisi Wabunge bila kumsahau kijana wetu Kashonele anayekaimu pale Wilaya ya Kyerwa, kwa kweli anafanya kazi nzuri na niombe sana Mheshimiwa Waziri ikikupendeza kijana huyu amekaimu zaidi sasa hivi ya miezi sita ikiwezekana mpe kabisa nafasi hii kwa sababu anaweza kazi, ninaomba sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru Mheshimiwa Waziri kwa miradi ambayo umetupa Kyerwa tunakwenda vizuri, lakini miradi hii imekuwa na madeni mengi. Mmejitahidi kuwa mnatulipa kidogo, lakini wanadai hela nyingi sana. Wakandarasi hawa hizi hela wanakopa kutoka benki na wanapokopa hizi hela kutoka benki, benki haiangalii Serikali imelipa au haijalipa, wanaendelea kulipa riba na mwisho wa siku hawa wakandarasi tusipowaangalia wanaenda kufilisiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, tuombe sana Waziri wa Fedha wakandarasi hawa waweze kulipwa ili wakamilishe hii miradi. Kwa mfano nina Mkandarasi huyu Otonde amefanya mradi pale Kikukuru wa zaidi ya shilingi bilioni tano mpaka sasa hivi mradi umefika 75% anadai zaidi ya shilingi bilioni 3.1; kuna huyu Jamta mradi wa Lunyinya - Chanya anadai shilingi bilioni 2.2; Mradi wa Kaisho Isingiro anadai shilingi milioni 420, kuna huyu Amri Karim anadai shilingi milioni 200. Miradi hii iko kwenye hatua nzuri na bila Mheshimiwa Waziri kuwalipa hawawezi wakakamilisha miradi hii, wametoka site wananchi wanasubiria maji na unajua kipindi hiki wale wanaotafuta Ubunge wanasema ni miradi hewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana Mheshimiwa Waziri Wana-Kyerwa wanahitaji maji hawahitaji kuona mabomba tu yametandazwa wanachohitaji ni maji. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, ninajua wewe ni kijana mpambanaji hebu pambania hii miradi iweze kukamilika vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Waziri niliomba visima vya maji mkanipatia visima vya maji ambavyo tumechimba kwenye Kata ya Nyakatuntu, Nyaruzungura, Kamuli, Nyakakoni, Songambele na Omuchwekano. Naomba sana miradi hii ikamilike, wamechimba lakini kwa kweli kasi inayoendelea siyo nzuri na unajua tunao ule mradi mkubwa na tuliomba hivi visima wakati tunasubiria mradi mkubwa. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa wazirimiradi hii ikamilishwe. (Makofi)
Kwa hiyo nakuomba sana Mheshimiwa Waziri tunajua unachapa kazi nzuri sana hatuna mashaka na wewe kwa hiyo niombe sana miradi hii iweze kukamilishwa haraka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilisemee hizi fedha za tozo ambazo tumepitisha sisi kama Bunge; fedha hizi zimekuwa zikiletwa kidogo, lakini zinakuja kwa kuchelewa, fedha hizi tumezipitisha sisi Wabunge, niombe sana kama kuna uwezekano tupitishe azimio, fedha hizi ziwe zinakuja moja kwa moja kwenye Wizara ya Maji kwa sababu tumeshazipitisha tunatamani tuone miradi hii inakamilika wakati mwingine fedha zinakuja zimechelewa, watu tunaweza tukaanza kumlaumu Mheshimiwa Aweso, lakini mimi ninajua kwa jianzi ambavyo amejipanga Mheshimiwa Aweso anatamani kuona miradi hii inakamilika sasa bila kumpatia fedha miradi hii haiwezi kukamilika. (Makofi)
Kwa hiyo niombe sana Bunge hili tulijadili na ikiwezekana tupitishe azimio miradi hii iweze kupewa hela na iweze kukamilika na Watanzania waweze kufurahia matunda ya Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninakushukuru ahsante sana. (Makofi)