Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbeya Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee ninaomba kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza vyema miaka minne kwa kuongoza nchi yetu akiwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii kama vile ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji, utawala bora, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na utalii.
Pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri iliyotukuka ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kwa kuteuliwa kuwa Mgombea Mwenza wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa uzoefu na weledi wake, kama ilivyo kwa Watanzania walio wengi, nina imani kubwa kwa Mheshimiwa Nchimbi na kumtakia afya njema na kila la heri kwenye mchakato ujao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko (Mb), Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kutekeleza majukumu ya kumsaidia Waziri Mkuu, ikiwa na pamoja na jukumu la kuendelea kuisimamia ipasavyo sekta ya nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi na Spika na pia uongozi wote wa Bunge kwa uongozi mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Jumaa Aweso, Waziri wa Maji, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika ya ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii ambayo ni ya mwisho, inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi chake akiwa Waziri wa Maji, tathmini zinathibitisha mafanikio makubwa ya utekelezaji na usimamizi wa Mpango wa Kwanza na wa Pili na kupelekea Taifa letu la Tanzania kufanya vizuri mno kuinua uchumi katika kipindi hiki kigumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miezi kumi ya bajeti ya 2022/2023, Serikali kupitia Wizara ya Maji imetekeleza miradi mingi ya maji. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya inatekeleza kwa ufanisi mkubwa miradi ya vijiji vya Simambwe, Usoha Njiapanda, Tembela, Iyawaya, Izyira, Ruanda, Ilembo, Inyala, Igoma, Iwalanje, Galijembe, Tembela, Pashungu, Shigamba, Santilya, Inyala Ilembo, Mshewe, Muvwa, Njelenje, Mapogoro, Mjele, Chang’ombe, Ipwizi, Ikukwa, Simboya, Itimba, Utengule, Ihombe, Idugumbi, Iwala, Ilota, Ikhoho na pia mradi mkubwa katika Mji Mdogo wa Mbalizi. Miradi yote hiyo imetekelezwa kwa ufanisi mkubwa, ingawa kunahitajika uboreshaji wa miundombinu ya mabomba hasa katika mradi wa Mbalizi kuna upotevu mkubwa wa maji kutokana na uchakavu wa mabomba yaliyokuwepo awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio hayo makubwa, katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya bado kuna changamoto kubwa ya maji salama kwa wananchi. Pamoja na kuwepo kwa vyanzo vingi vya mserereko (gravity), asilimia kubwa ya vijiji havina maji salama. Nashukuru kwa kuwepo bajeti ya mradi mkubwa wa Mto Kiwira ambao utakuwa mkombozi wa maeneo mengi ya Mkoa wa Mbeya na hata Songwe. Napendekeza Serikali iendelee kutekeleza miradi ya maji kwa mpango wa force account ambao umeonesha mafanikio ya kupunguza gharama za miradi na pia utekezaji ni wa haraka na kwa ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Serikali iweke msukumo mkubwa wa kuharakisha utekelezaji wa miradi iliyomo kwenye Mradi wa Bonde la Mto Songwe (Songwe River Basin Development Programme - SRBDP), wenye ofisi zake Kyela, Tanzania. Mradi huu unaotekelezwa kwa pamoja na Serikali za Tanzania na Malawi, ni muhimu sana kwa sasa kutokana hasa na ujenzi wa mabwawa ambayo pamoja na manufaa mengine, yatasaidia kupunguza mafuriko ya Bonde la Kyela. Mabwawa haya yamelenga kuzalisha umeme, kilimo cha umwagiliaji, shughuli za uvuvi na hata utalii ambao unahitajika sana katika Wilaya ya Mbeya na ukanda wote wa Nyanda za Juu Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto za tabianchi, kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa mazingira na ongezeko la upungufu wa vyanzo vya maji. Uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu umepelekea misitu mingi kuharibiwa na uchomaji moto, ukataji mkaa na hata kilimo kwenye vyanzo vya maji. Napendekeza Serikali iongeze msukumo wa Wizara za Maji, Kilimo, Maliasili na Mazingira kufanya kazi kama timu moja ili kukabiliana na janga hili kubwa ikiwemo ujenzi wa mabwawa makubwa katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko. Kama ilivyo kwa athari za mafuriko ya Kyela, hata Ziwa Rukwa linaathirika sana na kujaa mchanga na udongo unaosombwa na mito kutokana na mmomonyoko wa udongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mahitaji ya maji kwenye kilimo, mifugo na hata mahitaji ya mabwawa kwa ajili ya kuzuia mafuriko ikiwemo kwenye miundombinu yetu ya reli na barabara, kuna haja na kuwepo kwa taasisi moja kuratibu na kusimamia mipango ya matumizi ya maji. Nchi yetu ina neema kubwa ya maji na hii ni fursa ya kipekee kutumia haya maji kama mojawapo ya nguzo kuu kukuza uchumi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.