Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri wa Maji Mheshimiwa Jumaa Aweso (Mb.) na Naibu wake Mhandisi Mathew Kundo (Mb.), Katibu Mkuu Mhandisi Mwajuma Waziri, Naibu Katibu Mkuu Ndugu Agnes Kisaka Meena na wataalamu wa Wizara ya Maji kwa kazi nzuri wanayofanya. Kwa namna ya pekee niwashukuru sana watendaji wa Wizara ya Maji waliopo mkoani Kilimanjaro ambao ni Wahandisi Kija Limbe (MUWASA), Weransari Munis (RUWASA Mkoa) na Musa Msangi (RUWASA Wilaya) kwa ushirikiano wao mkubwa na Mbunge kuwapatia wananchi wa Jimbo la Moshi Vijijini maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri na timu yake wamekuwa mfano wa kuigwa kwenye kutatua changamoto za maji na kuwatua akina mama ndoo kichwani, kwani maji ni haki ya msingi kwa binadamu wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla, inatia faraja kuona upatikanaji wa maji vijijini unaongezeka kutoka 70.1% mwaka wa 2020 na kufikia 83% mwezi Disemba, 2024. Kwa upande wa mjini, upatikanaji wa maji unaongezeka kutoka 84% mwaka wa 2020 na kufikia 91.6% mwezi Disemba mwaka 2024 kama alivyoonesha kwa kina katika hotuba yake ya bajeti ya mwaka huu wa 2025/2026.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita kwenye umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji hapa nchini kutokana na uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu na pia nitaongelea changamoto za maji katika jimbo langu la Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ina utajiri mkubwa wa vyanzo vya maji. Tunayo mito mikubwa na midogo, maziwa na kiasi kikubwa cha maji chini ya ardhi. Kutokana na mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira, kuna hatari kubwa ya kuja kukabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi hapa nchini yanakabiliwa na uharibifu wa vyanzo vya maji kutokana na shughuli za binaadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa hatua walizochukua kubaini vyanzo vya maji hapa nchini. Ripoti ya Waziri imeonesha kwamba hapa nchini kuna idadi ya vyanzo 3340 ambapo vyanzo 350 vimewekewa mipaka na vyanzo 68 vimetangazwa katika Gazeti la Serikali kuwa maeneo tengefu. Kwa ujumla, maeneo ambayo Serikali haijaweka mipaka, kuna uharibifu mkubwa wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru Serikali kwani kwenye vipaumbele vya mwaka 2025/2026, uhifadhi na uendelezaji wa vyanzo vya maji umepewa nafasi kubwa kwenye utekelezaji wa bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto hii ya uharibifu wa mazingira katika vyanzo inaweza kusababisha maji kupungua na mara nyingine kuchafuka, hali inayohatarisha afya za watumiaji, jambo linaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko kwa watumiaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba yake Waziri amekiri kwamba bila maji, hakuna Taifa. Hivyo basi ni vyema kulinda vyanzo hivi vya maji kwa manufaa ya usalama wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na changamoto hii hatarishi ya uharibifu wa vyanzo vya maji, ninaishauri Serikali ichukue hatua kali zifuatazo:-
Mosi, Serikali kupitia kwa Mamlaka za Maji na RUWASA watoe elimu kwa wananchi katika maeneo husika kuhusu faida za kutunza vyanzo vya maji. Elimu hii itolewe kuanzia ngazi ya vitongoji na vijiji. Ninaishauri Serikali itenge bajeti ya kutosha ili kuwawezesha watoa elimu kwa umma kuwafikia wananchi walio karibu na maeneo ya vyanzo vya maji. Wahusika watoe elimu pana juu ya athari za uharibifu wa vyanzo vya maji na namna ya kuvitunza, ikiwa ni pamoja na kuwapatia miti rafiki na kuipanda kwenye maeneo ya vyanzo vya maji.
Pili, kwenye maeneo yanayoendesha shughuli za kilimo na ufugaji, Serikali itenge maeneo maalumu ya kulima na kufuga na iwe ni marufuku kabisa kufanya shughuli zozote za kibinadamu (kilimo na ufugaji) katika vyanzo vya maji. Mifugo itafutiwe sehemu maalumu ya kunyweshwa maji na isionekane kabisa kwenye vyanzo vya maji. Kwa kulitekeleza hili, hakutakuwa na athari za uharibifu na uchafuzi wa vyanzo vya maji.
Tatu, Serikali Kuu na Serikali za Mitaa ziimarishe sheria zote kuanzia ngazi ya Taifa hadi vijijini zitakazolenga kudhibiti uharibifu wa vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sheria kali zitawekwa kuanzia ngazi ya kijiji zitakazohusu udhibiti na uhifadhi wa maeneo ya vyanzo vya maji, basi itasaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na janga hili ambalo kila siku Serikali imekuwa ikitoa matamko, lakini ufuatiliaji wa sheria juu ya watu wanaohatarisha vyanzo vya maji unakua mdogo. Ni muhimu utekelezaji wa sheria hizi ufuatiliwe na adhabu zilizowekwa zitekelezwe kama ilivyoainishwa kwenye sheria.
Nne, katika Idara ya Maliasili, Serikali imeweka vifaa/teknolojia maalumu kudhibiti maharamia wanaowinda na kuua tembo. Ni vyema Serikali ikaanza programu ya kuweka vifaa vya kisasa ambavyo vitasaidia kuoanisha maeneo yote yenye vyanzo vya maji nchini, ili kuonesha uharibifu wowote utakaofanyika kutokana na shuguli za binadamu. Jambo hili likifanikiwa itasaidia sana kulinda na kuokoa vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jimbo langu la Moshi Vijijini, kuna changamoto ya upatikanaji wa maji ya bomba katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru sana Serikali kwa kutoa shilingi 486,192,492.42 na kutekeleza mradi wa kupeleka majisafi na salama katika Kata ya Mbokomu. Pesa hizi zimetumika kufanya uboreshaji na upanuzi wa mtandao wa majisafi urefu wa kilometa 24.7 katika Vijiji vya Korini Juu, Korini Kati na Korini Kusini. Katika mradi huu, jumla ya bomba zenye urefu wa kilometa 11.6 kati ya 24.7 sawa na 47% zimekamilika. Baadhi ya wananchi wameanza kunufaika na mradi kwa kupata majisafi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado 53% ya mabomba yanahitajika na kuna uhitaji wa fedha kiasi cha shilingi 357,682,020.98 ili kukamilisha kazi zilizopangwa na MUWASA ambazo zinalenga kusogeza mtandao wa bomba karibu zaidi na wananchi na kuwapunguzia gharama za maunganisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Kimochi ina zaidi ya wakazi 16,046. Kata hii ina Vijiji vya Mowo, Sango, Shia, Miami, Lyakombila na Kisaseni. Eneo lote linahudumiwa na MUWASA Tunaishukuru Serikali kwa kutoa shilingi 983,668,163.13 kujenga mradi wa majisafi na salama katika Kata ya Kimochi. Kazi zilizofanyika ni za upanuzi wa mtandao wa majisafi urefu wa kilometa 44.3 katika Vijiji vya Sango, Shia, Kisaseni, Mowo Lyakombila na Mdawi. Katika mradi huu, jumla ya bomba zenye urefu wa kilometa 26.5 kati ya 44.3, sawa na 59.8% zimekamilika kwa kutumia fedha kutoka Wizara ya Maji. Aidha, chanzo cha maji Muo kimejengwa kwa kutumia mapato ya ndani na wananchi wanaendelea kupata maji kutoka katika mradi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Kimochi, bado kuna uhitaji wa fedha kiasi cha shilingi 483,668,163.13 ili kukamilisha kazi zilizopangwa zinazolenga kusogeza mtandao wa bomba karibu zaidi na wananchi na kuwapunguzia gharama za maunganisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Mabogini ina wakazi wengi (57,231) na bado kuna changamoto ya maji ya kunywa katika baadhi ya maeneo. Tunaishukuru Serikali kwa kutoa shilingi 2,184,373,327.5 kutekeleza miradi ya kupeleka majisafi na salama katika Kata ya Mabogini. Kazi zilizofanyika ni upanuzi wa mtandao wa majisafi urefu wa kilometa 55.45 katika Vijiji vya Mji Mpya, Mvuleni, Maendeleo, Mtakuja, Chekereni, Muungano na Mserekia. Mradi umekamilika kwa 100%. Sasa hivi wananchi wanapata huduma ya majisafi kwa saa 24.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama takwimu za sensa zinavyoonesha, eneo hili linakuwa kwa kasi, hivyo kinahitajika kiasi cha shilingi 175,000,000 kwa ajili ya upanuzi wa mtandao wa bomba urefu wa kilometa 12 ili kupunguza gharama za maunganisho kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali kwa uwekezaji wa shilingi 387,630,957.04 kutekeleza mradi wa kupeleka majisafi katika Kata ya Uru Mashariki. Kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa chanzo kipya cha Mnini, Ukarabati wa tanki lenye ujazo wa 50m3 pamoja na upanuzi wa mtandao wa majisafi urefu wa kilometa 27. Kazi nyingine ni ukarabati wa tanki lenye ujazo wa 50m3 pamoja na ujenzi wa bomba la majisafi lenye urefu wa kilometa 15. Kazi hizi zimekamilika kwa kutumia mapato ya ndani ya MUWASA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali iendelee kutusaidia, kwani bado kuna uhitaji wa fedha kiasi cha shilingi 210,610,121.13 kwa ajili ya kukarabati mtandao wa bomba katika Vijiji vya Materuni, Mwasi Kusini na Kaskazini, Kyaseni, Mruwia na Kishumundu.
Mradi wa majisafi na salama katika Kata ya Old Moshi Mashariki, umegharimu shilingi 846,535,745.72. Kazi iliyofanyika ni uboreshaji na upanuzi wa mtandao wa majisafi kwa urefu wa kilometa 39.88 katika Vijiji vya Tsuduni, Kidia, Mahoma na Kikarara. Mradi huu umetekelezwa na kukamilika kwa 100% kwa kutumia mapato ya ndani ya MUWASA na wananchi wameanza kunufaika na mradi kwa kupata majisafi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunaiomba Serikali itutengee fedha kwa ajili ya upanuzi wa mtandao wa bomba katika Vijiji vya Tsuduni, Kidia, Mahoma na Kikarara ili kupunguza gharama za maunganisho kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Uru Kusini yenye vijiji saba (Okaseni, Kimanganuni, Rua, Kariwa, Longuo A, Kitandu na Shinga) ina wakazi takribani 31,557 na ina miradi mitatu ya Mang'ana, Kisimeni na Mbora. Changamoto ya miradi hii ni maji kidogo katika mifumo ambayo hayatoshelezi. Naiomba Serikali isaidie, kwani mbali na hivyo vijiji kuna Taasisi ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Kuna shida kubwa sana ya maji hapo chuoni. Ninaiomba Wizara iangalie namna ya kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Arusha Chini yenye wakazi 13,977 kuna shida ya maji katika Vijiji vya Mikocheni na Chemchem. Sasa hivi ni watu wa Kirua Kahe wanatoa huduma ya maji ya kuuza katika maeneo haya. Maji huuzwa kwa bei ya juu na si salama kwa matumizi ya binadamu. Kata hii inahudumiwa na RUWASA. Ninaiomba Wizara ijenge mradi kwa kutumia maji ya kutoka Mto Ronga na Kikuletwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Uru Kaskazini yenye wakazi 10,817 tunaiomba MUWASA iendelee kuwaunganisha wakazi wa Vijiji vya Msuni na Njari ili wananchi wapate maji.
Katika Kata ya Old Moshi Magharibi, kuna wakazi 8,431 na kuna mradi wa maji wa Tela Mande ambao umekamilika. Mradi huu una maji mengi sana na ya ziada ambayo kwa sasa yanahudumia wananchi wa ukanda wa milimani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji na vitongoji vya kata hii vilivyopo ukanda wa tambarare kama kile cha Mandaka Mnono na Saningo havina maji ya bomba. Ninaiomba Wizara iwapelekee wananchi hawa walioko ukanda wa tambarare maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali kwa uwekezaji wa shilingi 1,064,895,585.6 kwenye mradi wa majisafi katika Kata ya Kibosho Mashariki. Mradi huu utahusika na ukarabati wa chanzo cha Rumbanga ambapo utafanyika ujenzi wa chujio la maji (treatment plant) na upanuzi wa mtandao wa majisafi urefu wa kilometa 39.7. Tunaishukuru Serikali kwani mradi huu unatekelezwa kwa fedha za mkopo kutoka mfuko wa maji. Utekelezaji wa mradi huu umepangwa kuanza mwishoni mwa mwezi Mei, 2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali kwani Kata ya Kibosho Kindi imepatiwa mradi wa majisafi wenye thamani ya shilingi 60,000,000 utakaohusu uchimbaji kisima kirefu cha maji (borehole). Mradi huu utaanza kutekelezwa mwishoni mwa mwezi Mei, 2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema kwamba ni vyema Serikali iwekeze zaidi kwenye ulinzi wa vyanzo vyote vya maji hapa nchini ili kulinda haki ya kimsingi ya wananchi kupata maji safi na salama ya kunywa, wakiwemo wale wa Jimbo la Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.