Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Maimuna Salum Mtanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Newala Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Newala Vijijini lina changamoto kubwa sana ya maji kiasi kwamba kila nyumba inayojengwa mwenye nyumba hujenga kisima chake cha kuvuna maji yasiyo salama sana kwa kuwa visima vingi huokota maji yanayotiririka ardhini na hayatibiwi kabisa kiasi kwamba inahatarisha afya za wananchi, lakini pia maji ni muhimu sana kwenye kilimo kwa kuwa upuliziaji wa viuatilifu vya maji/sumu hutumia maji. Naomba kushauri kwamba Serikali ikubali kujenga malambo ya kukusanyia maji yaweze kutumika kwa matumizi ya majumbani, kwenye kilimo na mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali kwenye mwaka wa fedha wa 2024/2025 ilishapeleka fedha kiasi cha shilingi 1,035,972,511.12 kwenye Jimbo la Newala Vijijini, tunaomba matokeo ya uwekezaji huo yaonekane kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madeni ya mkandarasi wa Mradi wa Miji 28; tunaiomba Serikali imlipe kiasi cha shilingi bilioni tatu alizoomba mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa Miji 28 wa Makonde. Mradi huu ndio mkombozi mkubwa wa wananchi wa Newala ambao wanapata shida ya maji kwa muda mrefu ukizingatia kuwa maeneo ya kupata maji kwa urahisi katika Wilaya ya Newala ni shida kutokana na mazingira ya kijiografia yaliyopo Newala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tufanye jitihada za makusudi ili kuwanusuru wananchi ukizingatia kuwa hali ya hewa mwaka huu haikuwa rafiki sana kwa kuwa mvua sio nyingi na visima vingi vya wenyeji havina maji ya kutosha hali ambayo inaweza kusababisha changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utunzaji wa vifaa/mabomba ya maji; wakandarasi wanaotekeleza miradi ya maji ya Mnima - Miyuyu wameacha mabomba barabarani kwa muda mrefu hasa katika Kata ya Mikumbi hali inayosababisha mabomba hayo kuungua moto, kukatwa na wananchi pamoja na kukanyagwa na magari. Hii inasababisha hasira kwa wananchi wanaosubiri huduma ya maji, lakini pia inarudisha nyuma jitihada za Serikali za kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi kwa haraka. Nashauri usimamizi wa karibu wa wakandarasi hawa ukizingatia kuwa mradi huu ni wa muda mrefu tangu mwaka 2018 na ulikuwa mradi wa miezi tisa tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bili za maji; nashauri matumizi ya prepaid mita ili kuondoa changamoto ya malalamiko ya bili kwa wananchi.