Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipendelea kuwa wa kwanza kuchangia. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema ambaye ametulinda mpaka sasa tunaenda mwishoni mwa ngwe ya Bunge la Kumi na Mbili. Ninampongeza Mheshimiwa Waziri Simbachawene, Naibu wake Mheshimiwa Sangu, Watendaji wenu Wakuu wakiongozwa na Ndugu Juma Mkomi, wamefanya kazi, hakika wameniheshimisha na wameheshimisha wafanyakazi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Kitabu cha Luka 17:11 – 16, lakini kwa wingi wa udogo wa muda sitaisoma yote, lakini inatupatia mafunzo ya Wakoma 10 walioenda wakatibiwa na Bwana Yesu. Kati ya Wakoma 10, aliyerudi kusema ahsante ni mmoja. Sasa mimi kwa niaba ya wafanyakazi wa Tanzania, ninarudi kusema ahsante kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini ninarudi kumshukuru? Kwa kipindi cha miaka minne amepandisha vyeo watumishi 429,458, lakini ametoa kibali cha ajira, waajiriwe watumishi 149,000 na ambao wameshaajiriwa ni 102,154 na nyingine ziko kwenye mchakato. Tatu, amelipa malimbikizo ya mishahara ambayo yalikuwa ni mwiba mzito kwa watumishi 130,463 kwa thamani ya bilioni 226.5. Nne, tulikuwa na kitendawili cha kikokotoo akabadilisha, kikokotoo kikawa 40% na 33%, tuna imani Serikali itaendelea kurekebisha. Niseme ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninaongelea mambo mawili kwa sababu mengine yote wamemaliza. Ninaomba nishauri mambo mawili, nitashauri kwenye Sekretarieti ya Ajira na hamisho za Watumishi. Kwa kawaida, kikanuni na kisheria mwajiri namba moja ni Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini akakasimu madaraka hayo kwa Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu Mkuu Kiongozi akakasimu kwa Katibu Mkuu Utumishi wa Umma chini ya Ofisi ya Waziri, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Kwa hiyo, kinachofanyika Menejimenti ya Utumishi wa Umma ni Mheshimiwa Rais anafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo mwaka 2003 Serikali kwa nia njema iliamua kugatua madaraka kuzipa Wizara, Idara za Serikali na Taasisi kuajiri, kupandisha vyeo na kutunza nidhamu ya watumishi. Tulienda vizuri kidogo, lakini tulipofika 2007 moto ukawa moto, wanatangaza ajira, watu hawajafanya interview ajira zimejaa. Wanatangaza ajira walioshinda siyo wanaoingia ndani ya kazi. Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne akaunda Tume, Tume ilikuja na mapendekezo kupitia Sheria ya Utumishi, Sura ya 298, kifungu cha (29)(1) ikaunda Sekretarieti ya Ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekretarieti ya Ajira ikaanza tarehe Mosi Machi, 2010 na Katibu wake wa kwanza ndiyo Naibu Katibu Mkuu Utumishi. Jukumu walilopewa na Mheshimiwa Rais wakati anaizindua alisema, jukumu kubwa ni kuajiri Watumishi wa Serikali, Wizara zote, Idara zote na Taasisi isipokuwa wakagatuliwa madaraka Tume ya Utumishi wa Mahakama kidogo na Tume ya Utumishi ya Bunge, lakini na wenyewe, ili waajiri lazima ikama waipate kutoka Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa sababu, wale ndiyo wanatoa check number.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampenda sana Mheshimiwa Waziri na amenisaidia sana, wakati anakuja hapa kuna mambo ambayo nitaomba anipe majibu. Sekretarieti ya Ajira imevunjwa au inadogoshwa makusudi au ni kitu gani kinachoendelea?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeanza taratibu, tunaona baadhi ya Wizara zinatangaza kazi na wanaajiri, ikifika katikati mambo yanaharibika, utumishi wa umma wanaanza kulalamikiwa. Tumeona mpaka sasa watu wanatangaza tenda za kufanya ajira, kila kitu kina utaratibu wake, Sekretarieti ya Ajira ina wataalam wa kila aina wa kufanya hizi ajira na ajira tusizichezee, ndiyo maisha ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Wizara wakiwasilisha bajeti walizofanya, walizozitekeleza ni Watumishi wa Serikali, ni watumishi walioajiriwa kwa kufuata vigezo vizuri tu, lakini sasa tunaanza kweli, ninatoa mfano wa TRA, nina meseji zipo humu nyingi, TRA juzi wametoa tenda kwa NBAA ndiyo wafanye ajira. Sekretarieti ya Ajira imeenda wapi? Ninamwuliza Mheshimiwa Waziri. Sasa akija hapa, anipe majibu kama nyie ndiyo waliowakasimu tuelewe? Basi warudishe Sheria hapa tuvunje Sekretarieti ya Ajira, itakuwa haina maana NBAA kazi yake ni kuangalia wataaluma wa uhasibu, leo anaingiaje kwenye kuajiri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa moto ulio mtaani huko siyo wa kawaida, lakini wote wanalaumu Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Tuliona mfano wa kuajiri walimu hapa, vikatibuka, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ndiyo wanalaumiwa. Sasa waniambie Sekretarieti ya Ajira imeenda wapi? Inafanya nini na ni kwa sababu gani haiaminiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaanza kuamini taasisi zenye kazi nyingine, tunaanza kujikasimu madaraka ambayo tuliyafuta 2010, hii haitawezekana Mheshimiwa Waziri. Hatutaweza kukubali kuchezea ajira za watoto wa Kitanzania ambao inafanya sasa watoto wa masikini hawapati ajira kwa sababu, kwa kwenda hivi unakuta kazi zimetangazwa, NBAA imetangaza, lakini watu wameshaingia kazini. Hili hatutalikubali na hili nalisema kwa uchungu tu kwa sababu, naenda kumaliza miaka yangu mitano, waende wakaliangalie, waende wakalifanyie mchakato na leo wanipe majibu wakati wanahitimisha; hii haitawezekana, hatuwezi kukubaliana nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulisema hapa na mimi ndiyo nilishauri kwamba, waende waanzishe database ya kuweka wanaokuwa wameajiriwa wakabaki, tunavyotangaza tena turudi mule tuangalie, itasaidia kuondoa wale ambao wamemaliza vyuo mapema. Tume ya Utumishi wa Bunge inafanya, tunaajiri, tunaweka kwenye database, tukitangaza tena tunaajiri, lakini tunarudi kwenye database tunaangalia marks za wale waliopita, yawezekana hawa waliofanya marks zao ndogo kwa hiyo, tunawarudisha kwenye database tunachukua yule mwenye marks nyingi, ambaye alikuwa kwenye database tunamwajiri, huyu anakaa kwenye kusubiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna siku nilikuwa namwambia Mheshimiwa Spika, labda sasa sisi tuanze kuwa mfano wa kufundisha Sektretarieti ya Ajira, lakini ukiangalia Sektretarieti ya Ajira ipo sawasawa, tatizo linakuja watu wameanza kujipa mamlaka ambayo siyo yao. Naomba Mheshimiwa Waziri asimamaekwenye nafasi yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nije kwenye uhamisho. Menejimenti ya Utumishi wa Umma nyie ndiyo wenye mamlaka ya kuhamisha mtumishi, ndiyo wenye mamlaka ya kupandisha vyeo, ndiyo wenye mamlaka ya kusimamia nidhamu. Leo imefikia, nina barua humu na nitatoa mfano halisi, wao wanakaa wanaona mtumishi fulani anaweza akafaa kwenye sehemu fulani, mtumishi anaweza akaenda mwenye taasisi akamkataa au mwenye Wizara akamkataa au mwenye Wizara au taasisi akamkatalia huyo mtumishi kuondoka. Haya mamlaka wanayatoa wapi? Hawaogopi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, anayekuwa amehamisha ni Mheshimiwa Rais kwa kupitia Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Mamlaka hayo yanatoka wapi ya kumkataa mtumishi uliyeletewa? Kwamba, mimi huyu simtaki. Mfano mmoja ulikuwa kwenye mkoa mmoja, siwezi kutaja, mtumishi alihamishwa kwenda mkoa mwingine, yule pale akamkatalia huondoki na Mheshimiwa Mbunge wa sehemu hiyo yupo humu, akatumiwa meseji. Alivyotumiwa akaniambia, hili Mheshimiwa Janejelly lako, nikamwambia twende.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Naibu Katibu Mkuu Utumishi, tulivyofika tukamweleza akasema, hiki kitu hakiwezekani. Nikamwambia ndiyo kimeshawezekana, 14 days zimeisha yule mtumishi hajaenda, lakini mtumishi kule anaambiwa tumeandika utumishi kuomba usiondoke. Naibu Katibu Mkuu akampigia mkuu wa kule akamuuliza, hiyo barua mliyoleta ipo wapi? Nipe mliyoomba kuzuia uhamisho; barua hana, anampiga nyimbo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, alimwambia hivi, narudia kauli yake, kabla hazijapita siku tatu huyo mtumishi awe amefika kituo chake cha kazi. Kingine ni mtumishi alivyofika alituma ujumbe kwamba, kafika. Sasa kwa nini tunafika mahali watumishi tunawanyanyapaa? Kwa nini tunafika mahali kwamba, taasisi fulani zina watu fulani ndiyo wanaweza wakafanya kazi pale wengine hawawezi kufanya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenye mamlaka ya kuwapanga watumishi hao ni Menejimenti ya Utumishi wa Umma, kwa mamlaka waliyopewa na Mheshimiwa Rais kumfanyia kazi hiyo. Ni nini kinachoendelea pale, waende wakapaangalie wanipe majibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo vijana wame-stuck, sasa hivi watumishi wame-stuck, wamepelekwa sehemu fulani wamekataliwa. Mtu anawaambia, mimi siwezi kukupokea au anaenda ameshaiva kupandishwa promotion, anafika pale anasema, sisi hatuwezi kukupandisha. Sasa Serikali si moja hii? Kambi si moja hii? Wote si tunajenga nyumba moja? Sasa inafika nini tunaanza kugombania fito?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba, kuna mahali watu fulani ndiyo wanaweza wakafanya kazi pale, mahali watu fulani hawawezi kufanya kazi pale. Wamefanya mengi mazuri kwa watumishi, wamefanya yaliyo mema, lakini wasipoyaangalia haya mawili, yatachafua kazi yote ambayo wamefanya. Niwaombe, narudia kuomba, waende wakaangalie vizuri kazi zenu kwa nini zinaingiliwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga hoja mkono. Mungu awabariki sana. (Makofi)