Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kunipa nafasi ya kuchangia katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na kidogo kwenye Sekretarieti ya Ajira, ambayo kidogo mwenzangu amechangia. Ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kuniweka hai leo na kunipa nafasi ya kuchangia katika Bunge lako Tukufu, lakini ninaanza kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa weledi kuliongoza Taifa letu akisaidiwa na Makamu wake, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, lakini bila kumsahau Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Dotto Biteko, ambaye pia, ni Waziri wa Nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Waziri wetu, Mheshimiwa George Simbachawene, Naibu wake, Makatibu Wakuu, watendaji wote wa Wizara hii, wamefanya kazi nzuri sana pamoja na Kamati yetu. Wamekuwa wasikivu, wakisikiliza yote tuliyowapelekea na kuyatendea kazi kwa jinsi Mungu alivyowajalia na kufuata kanuni na miongozo waliyosimama nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza pia Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Rais Ally Hassan Mwinyi, pamoja na Mheshimiwa Dkt. Nchimbi kupata kibali cha kuwa wagombea wa nafasi ya Urais na Umakamu, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi. Nawapongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakupongeza wewe, Waheshimiwa Wenyeviti wote, Mheshimiwa Spika wetu na Mheshimiwa Naibu Spika. Mmekuwa mahiri sana kuongoza Bunge letu kwa miaka mitano, Watumishi mahiri wa Bunge hili na Watumishi mahiri wa Ofisi hii. Mmefanya kazi nzuri, tumekaa vizuri, tumekuwa salama katika Bunge hili, nawapongeza sana Watumishi wa Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapongeza sana vyama vya wafanyakazi. Vyama vya wafanyakazi vinaongozwa na Mwenyekiti wetu ambaye anaitwa ndugu Tumaini Nyamuhokya, Mwenyekiti ambaye ni Rais wa r ndogo, pamoja na Katibu wake, ndugu Heri Nkunda. Hawa viongozi wa vyama vya wafanyakazi wametoa ushirikisho mkubwa kwa Serikali na waajiri, ndiyo maana nchi yetu watumishi wametulia, huoni maandamano na huoni migomo, wanastahili pongezi viongozi hawa wa vyama vya wafanyakazi pamoja na wengine wote kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina pongezi kubwa sana kwa Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa yote ya Tanzania, Makatibu Tawala wa Mikoa ya Tanzania, Wakurugenzi na Makatibu Tawala wa Wilaya. Nina pongezi zao nyingi sana, nitasema kwa nini wanastahili pongezi na makofi ya jana kwa Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa hayakuwa ya bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majukumu yote ambayo nimetumikia kwa miaka mitano kwenye Bunge hili, lakini ninalo jukumu mahususi ambalo nilikuja nalo; ni uwakilishi wa wafanyakazi wa Tanzania kwenye Bunge Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Uwakilishi huu umetokana na Chama Cha Mapinduzi ambacho ni chama chenye demokrasia pana. Tunajua vyama vyote vina viti maalum, lakini Chama Cha Mapinduzi kutokana na umahiri wake na upana wa demokrasia kikaona katika viti vyake maalum angalau kitoe viti vichache, kwa ajili ya kundi maalum la wafanyakazi pamoja na makundi mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni demokrasia pana ndani ya Chama Cha Mapinduzi. Hii ipo kwenye Ibara ya 178, 79 na 130 ya Chama Cha Mapinduzi, kinatambua mchango mkubwa wa wafanyakazi katika ujenzi wa uchumi, katika utoaji wa huduma za kijamii, ndiyo maana kikaona umuhimu wa kuweka kundi hili kutoka kwenye viti vyake maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chama Cha Mapinduzi kinahitaji pongezi kubwa sana, vyama vingine vipo, lakini havina makundi haya wala havijaona umuhimu wa kutoa nafasi kama hizi kwenye jamii ya Kitanzania. Kwa nini nimesema hivyo? Katika nafasi hii nimeweza kuwatembelea wafanyakazi katika mikoa 23 ya Tanzania Bara. Nimekwenda kuonana nao uso kwa uso katika halmashauri 89, katika hizo halmashauri 23 ni za mijini, lakini niliamua kwenda pembezoni, halmashauri 64.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata ushirikiano mkubwa sana wa Waheshimiwa Wabunge wa Majimbo na Waheshimiwa Wabunge Viti Maalum, wamenipa ushirikiano mkubwa sana. Wanasema yale maendeleo kule kwenye halmashauri na mikoa ni kwa sababu, watumishi wametulia, wanafanya kwa uadilifu na uzalendo mkubwa kwa hivyo, nilipata ushirikiano mkubwa. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu kule nilipokwenda nilipata ushirikiano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule nilipokwenda wafanyakazi wanasema hivi, wameona mambo makubwa sana ambayo Mheshimiwa Rais amefanya. Pamoja na mapungufu madogomadogo, lakini Serikali ya Awamu ya Sita ndani ya miaka minne ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumekaa humu ndani na Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamesemea sana wafanyakazi na mimi nimewasemea sana wafanyakazi. Sitoyarudia, lakini wameyaona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiongea nao uso kwa uso, ukawasikiliza, ukawashauri na wao wanaishauri Serikali na wanaishukuru, japo wana machache nitayasema mwishoni. Wanasema wameona Serikali ikishusha kodi ya mapato hii Awamu ya Sita kutoka 9% mpaka 8%. Serikali hii pia, imepandisha kima cha chini cha mshahara kwa watumishi kutoka shilingi 170,000 mpaka shilingi 270,000. Serikali hii imeboresha umri wa watoto, tuliomba humu ndani wanaofaidika na NHIF kutoka miaka 18 mpaka 21 na bado wanaomba hadi 25.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ni maoni yao ya badaye, lakini pia, Serikali hii ilifuta tozo 6%, ili watumishi wale ambao walikuwa wamekopa mikopo, walikuwa wanakatwa, lakini imesababisha pesa ibaki kwa watumishi zaidi ya shilingi trilioni 1.1 baada ya kufuta hii kodi kwa watumishi ambao walikuwa wamekopa mikopo kwenye Higher Learning Institution, sorry kwenye Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, ilikuwa inakatwa 6%, watumishi kule wameniambia wanaipongeza Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Imekuwa na moyo mzuri sana kwa wafanyakazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ndani ya miaka Mheshimiwa Rais anasimamia sana mifumo mbalimbali. Ametenga pesa nyingi kwenye TEHAMA na hii TEHAMA inaongozwa na kaka yangu ndugu Ndomba. Wamefanya kazi kubwa sana, mifumo imerahisisha utendaji kazi, usimamizi wa kazi, mishahara kwa wakati, mambo yamekwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wamenituma niseme, wanasema ahsante sana. Wameona kazi ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndani ya miaka minne kwa hiyo, hilo naomba walipokee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine wamesema ajira. Ajira zilisimama miaka mitatu kwa sababu ya kupisha vyeti feki na mambo mengine. Nia ilikuwa ni njema, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ndani ya miaka minne ameingia madarakani, ametoa zaidi ya 250,000 kwenye utumishi wa umma, ametoa ajira zaidi ya 80,000 kwenye TAMISEMI, kwenye taasisi zaidi ya 100,002 ajira wanaziona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Sekretarieti ya Ajira. Mwanzoni kwa shida walikuwa wanaajiriwa tu watoto wametoka shule juzijuzi, lakini sasahivi ukiangalia imesikiliza kwamba, wale ambao wamemaliza shule muda mrefu muda wao wa kuajiriwa unapungua, lakini sasa hivi nimesikiliza juzi katika mahesabu, ajira 60,000 mia tano ni watoto wenye miaka 35 mpaka 45. Niipongeze sana Sekretarieti ya Ajira kwa kusikiliza maombi, maana walikuwa huko mitaani, muda wao wa kuajiriwa unaisha, wanaichukia Serikali. Naomba niipongeze sana Sekretarieti ya Ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo yote hayo mazuri watumishi wanasema, wanashauri Serikali izingatie suala la makazi, hasa halmashauri za pembezoni. Wamejenga ofisi mpya kule, watumishi wanatoka mbali sana na makazi ni heshima kwa mtumishi, ni heshima na stara. Wanaamini Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba, ni msikivu, kafanya mambo mengi. Suala la makazi wanaomba sana lizingatiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni wamehuisha miundo ya watumishi 160,000 kama bilioni 200 hivi, lakini wanaomba Serikali pia, suala la miundo bado ni changamoto, ina masononeko na malalamiko mengi. Suala lingine watumishi wanasema wanaomba maslahi ya watumishi wa halmashauri za mitaa yaboreshwe, yasipishane sana na watumishi wa taasisi za umma, inasababisha watumishi wa halmashauri kutaka kuhama wote kuelekea kwenye taasisi za umma kwa sababu, maslahi yanatofautiana. Wamenituma hilo niliseme, pamoja na mazuri yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanamwomba mama, pia kila fungu analolipata ahakikishe kidogo anatenga kwa watumishi. Wanashauri pale ambapo fungu litaongezeka, basi aangalie tena mishahara ya wafanyakazi iendane na hali ya maisha ya sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia vyama vya wafanyakazi ipo mikataba mbalimbali tuliingia. Wanaomba kupitia Mkutano ule wa Mei Mosi wa Arusha, mwaka jana, mikataba sita mbalimbali ya Kimataifa, kupitia ILO iangaliwe vizuri, wa watumishi wa ndani. Hii ilitolewa kwenye Mei Mosi kupitia vyama vya wafanyakazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi yamefanyika, humu ndani ni mashahidi. Nimesema sana wafanyakazi, sirudii leo, lakini wanatambua kazi nzuri ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wanatambua kwamba, aliingia bila kujua kama atakuwa Mheshimiwa Rais, aliingia akakuta mtikisiko wa kiuchumi dunia nzima, alikuta corona, alikuta mambo mengi kwenye nchi hii, lakini kama kuna wakati pesa nyingi zimetolewa kwenye maendeleo, kwenye Halmashauri ni sasa, lakini hakuwaacha watumishi. Wameona, wamesema tuna pesa nyingi mpaka zinakosa usimamizi, tunaomba mama aongeze ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, basi wanasema kwa pamoja, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mitano tena kwa maslahi bora ya wafanyakazi. Nipo tayari kuendelea na hii kazi kufikia ambapo sijafika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)