Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nashukuru kwa kupata nafasi hii ya kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, kaka yangu Mheshimiwa George Boniface Simbachawene na Mheshimiwa Naibu Waziri Deus Clement Sangu. Hali kadhalika Katibu Mkuu pamoja na watumishi wote wa Wizara hii, bila kusahau taasisi zote zilizopo chini ya Wizara hii ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kuifanya ya kusaidia kazi kwa kiasi kikubwa za Mheshimiwa Rais, ambaye tumeona akifanya mambo makubwa ndani ya nchi hali kadhalika akifanya mambo makubwa hata nje ya nchi. Dunia inatambua kwa hiyo, tunawapongeza sana kwa utendaji huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza, nianzie hapo alipoishia Mheshimiwa Alice Kairungi Kaijage, amekuwa ni mwakilishi sahihi wa watumishi; na ningeomba vyama vya wafanyakazi pamoja na utumishi waangalie vizuri zile kanuni zao ambazo zinamtaka kwamba agombee kwa kipindi kimoja tu, lakini kwa namna ambavyo amewakilisha ametaja taasisi ambazo amezitembelea na halmashauri hii inaonesha wazi kwamba ana passion ya kuwatumikia watumishi na kazi hii anaimudu basi wazitazame vizuri kanuni zao. Hawa ndiyo aina ya wawakilishi ambao wanapaswa kuwawakilisha watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuzungumzia Wakala wa Serikali Mtandao. Wakala hii imekuwa ikifanya kazi nzuri sana. Kila mara Mheshimiwa Rais alikuwa akihanikiza kutaka mifumo isomane; ili mifumo isomane ni lazima Wakala wa Serikali Mtandao waweze kufanya kazi na wamefanya kazi vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumeona nchi yetu makusanyo ya mapato yamekuwa makubwa. Pia, tunaona namna ambavyo compliance mbalimbali zinafanyika kwa sababu watu hawalazimiki kutembea na fedha na kwamba watu hawalazimiki kwenda kupanga foleni kulipa maduhuli mbalimbali ya Serikali; kwa hiyo, tunawapongeza sana. Sasa, tungeomba Serikali iongeze wigo wa kutanua ule mkongo wa Taifa ili uweze kufika halmashauri zile za pembezoni ili mifumo hii iweze kufanya kazi vizuri na maduhuli yaweze kukusanywa kwa urahisi zaidi kupitia wakala wa Serikali Mtandao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi tunaona wanazo programu kama ya e-office, e-utendaji ambayo hata ukiwa ofisini unaweza kuona utendaji mbalimbali unavyofanyika katika ngazi mbalimbali na hii inaongeza ufanisi hasa katika eneo hili la utumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ningependa kuzungumzia kuhusu Sekretarieti ya Ajira kama ambavyo Mheshimiwa Kamishina mwenzangu, Mama Janejelly amezungumza. Kwa mujibu wa Sheria Namba 298 Menejimenti ya Utumishi wa Umma kupitia Sekretarieti ya Ajira ndiyo yenye jukumu la kusimamia ajira zote hapa nchini; lakini sasa tumeanza kuona wanaanza kuchepuka au kuchepusha hizi taasisi na kuzipeleka katika taasisi nyingine ambazo kimsingi siyo ambazo zimejikita katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona Mamlaka ya Mapato Tanzania imetoa usimamizi wa mchakato mzima wa ajira kwa NBAA ambao kimsingi ni Bodi ya Uhasibu. Ajira ambazo zimeenda kufanyiwa kazi pale ni ajira tofautitofauti katika maeneo mbalimbali ya Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungeomba tubaki kwenye sheria yetu kama inavyotuelekeza, jukumu hili libaki kwenye Sekretarieti ya Ajira. Tumeona wamefanya kazi kubwa na wamefuata ushauri wa Bunge, kwamba ajira hizi badala ya kuzi-centralise tuanze kuzipeleka kwenye mikoa; na tumeona angalau kwa kuanzia walimu pamoja na watumishi katika sekta ya afya wamefanyiwa usaili katika mikoa. Hali hii imepunguza ule mrundikano wa waomba ajira katika maeneo ya majiji, sasa wamewekwa katika maeneo ya mikoa. Tupime ufanisi kule, tukiona kuna ufanisi wa kutosha tuendelee kuimarisha; lakini jukumu hili libaki chini ya usimamizi wa uratibu wa Sekretarieti ya Ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kuchangia ni eneo la TASAF. TASAF imekuwa ikiendelea kufanya vizuri sana na tunawapongeza kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kuifanya na niombe Serikali tunaelekea mwisho wa programu hii ya TASAF, niombe kwa wivu mkubwa kabisa kwamba tungetamani kuendelea na mpango huu wa kuzifariji hizi kaya maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma hapa katika ripoti ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 27 kwenye kishikwambi, imeeleza kwamba zaidi ya shilingi bilioni 162 ziliwasilishwa kwa kaya za walengwa 906,000 zenye wanakaya kama 3,769,582 ili waweze kujikimu na mahitaji ya msingi. Sambamba na hilo kumeanza kupita mchakato wa kuwatoa baadhi kwa kusema kwamba wame-graduate. Sasa sina shida kama wamefanya tathmini ya kina, lakini bado utaratibu huu unatakiwa ukaangaliwe upya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Jimboni Mlalo katika Halmashauri ya Lushoto ninaye mwananchi mmoja anaitwa Stanley Augustino Mrema; hana uhusiano na yule Mrema mwingine ni majina tu; huyu ni mlemavu ambaye anahitaji usaidizi wa 100%. Mama yake aliyekuwa anamlea amefariki, sasa anakaa na raia mwema tu ambaye amejitolea kumsaidia, lakini naye juzi ananiambia ameambiwa kwamba ame-graduate. Sasa nikamwambia hebu nioneshe hiyo certificate yako ya ku-graduate wala hakunionesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu nimemtaja makusudi ili Hansard zisome kwamba kuna watu wa aina hii ambao bado mpango huu unapaswa kuendelea kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tunawapongeza TASAF, wamefanya kazi nzuri sana. Zaidi ya vikundi 66,000 vyenye wanachama zaidi ya 800,000 na la kupendeza zaidi ni kwamba kati yao 80% ni wanawake, wameanzisha vikundi ambavyo vina mtaji wa zaidi ya shilingi bilioni 13 na wametoa mikopo zaidi ya shilingi bilioni 7.9, hili ni jambo jema. Katika zana ile ile ya kusema mifumo isomane tungependa kuona halmashauri zetu kupitia 10% tujaribu kuishauri Serikali kwa kuongeza uratibu kwa TASAF na Mfuko ule wa 10% uweze kuyaona makundi haya ili kuyaboresha na kuyajengea uwezo zaidi ili kuendelea kuboresha familia zao, lakini kuwafanya wawe na tija zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, sisi katika Halmashauri ya Lushoto ni wazalishaji wakubwa wa mbogamboga na matunda. Tumeona wenzetu hapa Kibaigwa wana soko kubwa la mahindi na sisi tungetamani tuwe na soko kubwa la mbogamboga. Sasa tumetenga eneo katika Kata ya Lukozi ambapo ndiyo maeneo tunakusanya zaidi mbogamboga. Tungeomba sasa ule mpango wa TASAF utufikirie na sisi kutujengea Soko kubwa la Kimataifa la Mbogamboga na facilities zake zote zikiwemo cold rooms na kadhalika ili mboga hizi tuweze kuzifunga vizuri na kuzisafirisha ndani na nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho lakini siyo kwa umuhimu, ni kuhusu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Ninawapongeza sana, Mtendaji Mkuu, Mkurugenzi Mkuu, Chalamila wanafanya kazi nzuri sana, hasa ile Programu ya TAKUKURU RAFIKI, wameendelea kutoa ushirikiano mzuri sana, ninadhani Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi. Kwenye Wizara zetu tumekuwa tukitoa elimu kupitia wao, lakini tulikuwa tunawaomba twende nao kwenye mabaraza, kwenye Serikali za Vijiji kutoa elimu kwa wananchi na walikuwa wanaendelea kutoa elimu katika eneo hili…

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shangazi, kuna taarifa. Mheshimiwa Kunambi, taarifa.

TAARIFA

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Mbunge anayechangia sasa, ndugu yangu Mheshimiwa Shangazi. Pamoja na kwamba TAKUKURU wanafanya kazi nzuri sana nchini, lakini wana changamoto ya facilities kama vyombo vya usafiri kufika eneo la tukio na kuchukua hatua kwa wakati. Hii ni changamoto kubwa sana. Kwa hiyo, ombi langu ni kwamba wapewe facilities. Ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shangazi, unaipokea hiyo taarifa ya Mheshimiwa Kunambi?

MHE. RASHIDI A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea kwa mikono miwili kabisa, ni taarifa sahihi. Ni kweli wana changamoto ya vyombo vya usafiri na wamepata kiasi lakini tungetamani Serikali ione umuhimu wa kuwapatia vyombo vya usafiri katika wilaya zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko baadhi ya wilaya bado wanapanga kwenye majengo ya watu binafsi. Sasa hii kidogo inaondoa ile dhana nzima ya utawala bora. Huwezi ukapanga kwenye nyumba ya mtu ambaye unamtuhumu halafu kesho unamchunguza; unaweza ukapewa notice ndani ya masaa 24. Kwa hiyo tunaomba, kwa kazi nzuri ambayo TAKUKURU wanaendelea kuifanya katika nchi yetu basi eneo hili nalo tuliwekee mkazo wa kibajeti ili waendelee kufanya kazi yao kwa ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. (Makofi)