Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi uliyonipa ili nijumuike na wenzangu kuipongeza sana hii Wizara ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambayo mtumishi namba moja ni Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akisaidiwa kwa karibu na Waziri George Boniphace Simbachawene. Tunawapongeza kwa namna ambavyo wanaliendesha jopo hili la watumishi wa umma kwa ajili ya kuhakikisha kwamba maendeleo yanapatikana na huduma kwa wananchi zinapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wawakilishi wa wananchi pia tunashukuru sana kwa hatua zinazoendelea za Serikali za kuendelea kutoa nafasi za ajira. Vijana wetu sehemu mbalimbali wanapata ajira kwenye maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niungane na Wakristo wote pamoja na watu wote duniani kuomboleza kifo cha Papa Francis.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amezungumza hapa na mimi ninataka kurudia juu ya msiba wa Marehemu Boniphace Gissima Nyamo-Hanga, Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO. Kwa moyo wa dhati kabisa ninasema kwamba alikuwa miongoni mwa watumishi bora sana hapa nchini na tutamkumbuka kwa alama alizoziweka. Amekamilisha Bwawa la Mwalimu Nyerere kwa 100%, amepunguza kwa kiwango kikubwa katakata ya umeme iliyokuwa haina maelezo, ameendelea na alikuwa kwenye hatua nzuri pia hata ya kuvunja mikataba mibovu ya TANESCO iliyokuwa inalisumbua Taifa letu. Vilevile kiongozi huyu alikuwa anaendelea kufanya tathmini hata ya kuona namna ya kupunguza gharama za umeme. Tutamkumbuka sana mzalendo huyu, ni moja ya watumishi ambao ni kielelezo kikubwa kwenye Taifa na Taifa letu limepoteza mtu makini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais aliunda Tume ya Maboresho ya Kodi na akaipa miezi sita, miezi hiyo sita imekwisha, hiyo tume tunaitaka sasa iwasilishe hiyo ripoti kwa sababu tuna hamu kubwa ya kujua mapendekezo waliyoyaleta. Mimi kama nilivyosema nitapeleka kwao, nilipeleka maoni na mapendekezo ya kurasa 235 ambayo yalikuwa na mambo mengi humo ndani. Pia ninawapongeza kwa sababu walinijibu kwa wakati; na ninataka ku-share na Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipowapelekea zile kurasa 235 za mapendekezo na maoni sekretarieti ya hiyo tume ilinijibu kama ifuatavyo: “Mheshimiwa Mpina, tunakiri kupokea maoni yako kuhusu maboresho ya mfumo wa kodi nchini. Maoni na mapendekezo uliyoyatoa ni mazuri, yameandikwa kwa ufasaha na tutazingatia katika uchambuzi ili kupata mapendekezo ya pamoja ambayo kwa hakika yataleta maboresho ya mfumo wa kodi nchini. Tunakushukuru sana. Nami ninawashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninalotaka kulizungumza hapa ni kuhusu mihuri ya Wenyeviti wetu wa Vitongoji. Wenyeviti wetu wa Vitongoji waliondolewa mihuri, sababu ya kuondolewa mihuri haina msingi wowote. Tunaomba Wenyeviti wetu wa Vitongoji warejeshewe mihuri yao. Zilikuwepo sababu zilizokuwa zinatolewa, eti wanauza ardhi, mara wanafanya kile, mara wanafanya kile. Hatujawahi kufanya hivyo, hata Wizara ya Ardhi wapo watumishi ambao wanagawa viwanja zaidi ya viwili, hatujawahi kuinyang’anya mamlaka Wizara ya Ardhi kwa sababu kuna baadhi ya watumishi wa umma wamegawa ardhi mara mbili. Kwa hiyo, Wenyeviti wetu wa Vitongoji warejeshewe mihuri yao. Mheshimiwa Waziri wa Utumishi asimamie hilo kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeongea na mimi niongezee sauti kwa wenzangu waliyozungumzia mishahara ya wenyeviti wa vitongoji, wenyeviti wa vijiji, wenyeviti wa mitaa na madiwani. Tumezungumza muda mrefu sitaki kuongea lakini nilishawishi Bunge hili, hii ndiyo bajeti ya mwisho. Tukifika kule mwisho bajeti ya Serikali tuikwamishe mpaka pale mishahara ya viongozi hawa itakapopatikana. Hatuwezi kuendelea kukubali tena maelezo mengine zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiandaa hii bajeti yetu ya utumishi na kama tunavyojua, kwamba Wizara ya Utumishi na Utawala Bora kwa kweli ndiyo engine ya utekelezaji wa majukumu yote ya Serikali. Ukitaka kufanikiwa unafanikiwa kwenye Wizara hii, ukiamua ku-fail, una-fail kwenye Wizara hii kwa sababu ndiyo inayoendesha shughuli zote za Serikali. Kwa hiyo, tunataka kuona kwamba kupitia bajeti hii watumishi wetu wakiwa wanaboreshewa mishahara yao, tunataka kuona kupitia bajeti hii madai yote ya watumishi wa umma, malimbikizo ya mishahara, madeni ya posho za uhamisho, madeni ya posho za likizo na maslahi mengine muhimu, hatutaki tena watumishi wetu kuendelea kudai madai hayo ambayo ni halali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tuliyapitisha kwenye bajeti husika, hatujui ni kwa nini walienda kukopwa wakati bajeti ilipita hapa. Kwa hiyo, tunataka mwaka huu kupitia bajeti hii, maslahi ya watumishi kabla hatujaondoka Bungeni hapa tarehe 27 Juni, tuwe tumehakikisha watumishi hao wamelipwa mishahara hiyo. Mheshimiwa Waziri wa Utumishi analo jukumu la kuhakikisha kwamba mambo haya yametekelezwa. Suala la kupanda kwa mishahara lisiwe jambo la hisani tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa sana pia nimesoma kiambatisho namba saba kinachohusu taasisi zilizofanyiwa tathmini za usalama wa mifumo ya TEHAMA ambapo ni mifumo 112 tu ndiyo ambayo ilifanyiwa tathmini; lakini nadhani tuna mifumo takribani 800 kama sikosei. Sasa hizi tathmini za kiusalama zinapofanyika kwa udogo namna hii tunapata matatizo makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunategemea mifumo ya TEHAMA kukusanya kodi, tunategemea mifumo ya TEHAMA kwa ajili ya kusimamia matumizi ya Serikali. Sasa hivi mifumo mingi ina matatizo makubwa na ina changamoto nyingi. Mifumo imeanzishwa na kuanza kutumika ikiwa wakati mwingine kanzidata na server bado zinamilikiwa na vendor; lakini mifumo mingine inaruhusu fedha mpaka kuingia kwenye mifuko ya watu, kwenda kwenye akaunti za watu. Halafu bado una changamoto hii kubwa ya mifumo yako kufanyiwa ukaguzi. Mkaguzi, CAG amelia juu ya ku-paralyse kwa mifumo yetu ya ukusanyaji wa mapato juu ya ku-paralyse kwa mifumo yetu ya usimamizi wa matumizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hili jambo litaendelea na mifumo ya TEHAMA ndiyo hii ambayo tunaitegemea, kama mfumo unaweza ukakaa haukaguliwi usalama, mfumo unaendeshwa hujakaguliwa usalama, maana yake mtu yeyote anaweza aka-temper nao, mtu yeyote anaweza akaingia kwenye mfumo huo akabadilisha takwimu, mtu yeyote anaweza akaingia kwenye huo mfumo akafuta kumbukumbu usalama wa Taifa letu uko wapi? Usalama wa mapato yetu uko wapi? Jambo hili linasimamiwaje? Hawa e-GA wana tatizo gani la kushindwa kuli-manage jambo hili? na Waziri wa Utumishi anatuambia nini kuhusu uwezo wa e-GA katika kusimamia jambo hili? Ni kwa nini mamlaka zinavunja sheria?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi taasisi ambazo zinasimamia miongozo na sheria ya Serikali Mitandao ni 40% tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto hii ya muda, ninashindwa hata sijui nitaongeaje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema ni kwamba utawala bora uko wapi Mheshimiwa Waziri Simbachawene? Taarifa ya CAG, PPRA, FAU, TAKUKURU zinaendelea kuripoti wizi wa fedha za umma kwa kiwango kikubwa, lakini kuingia mikataba ya usiri ambayo haina baraka za Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambayo haijabarikiwa na Bunge hili na mikataba hiyo ikaendelea, halafu tuko na Waziri wa Utawala Bora, tuko na Serikali inayosimamia Utawala Bora, haya mambo yanawezekanaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini 40% ya watumishi wa umma hawafanyi kazi na ni taarifa ya Waziri Mwenyewe. Watumishi wengine wamewekwa benchi na mwenzangu amezungumza, kwa fitina tu na chuki ndani ya mamlaka, lakini wameachwa tu na anayefanya hivyo ameachwa tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukabidhi rasilimali za umma kwa wageni. Kwa mfano machimbo ya wachimbaji wadogo, taarifa za CAG kutokufanyiwa kazi, mifumo, mikopo na matumizi ya fedha za umma hata nje ya bajeti. Mambo haya yanaruhusiwaje, Waziri wa Utumishi uko hapa, Waziri wa Utawala Bora uko hapa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu kuna manju mmoja aliwahi kuimba, “tumoghagi jozwa, olonosabha jilaleja bhademi”, anaitwa Mwanacholicholi. Ni kwa nini tunashindwa kuchukua hatua mahali ambapo sisi tunaweza kuchukua hatua? Kwa mfano, taarifa ya nchi yetu kulipa shilingi trilioni 1.438 katika Mahakama. Tovuti ya ICSID inaonesha kuwa baadhi ya makampuni yamelipwa baada ya kupewa tuzo katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro na Uwekezaji na Biashara, ambapo mpaka sasa hivi nchini kwetu tumeshalipa shilingi trilioni 1.438, tena kwa siku za hivi karibuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi taarifa zinaoneshwa kwenye Tovuti ya UCSID shilingi trilioni 1.438 lakini Bunge hili halijawahi kuelezwa na Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Bunge hili halijawahi kuelezwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Bunge hili halijawahi kuambiwa jambo lolote isipokuwa kule kwenye Tovuti ya UCSID ndio wanaonesha tu, shilingi trilioni 1.438 ambapo fedha hizi sisi hatujawahi kuzipitisha na hatujawahi kuombwa kibali na hatujawahi kuambiwa kwa nini Serikali ilienda kushindwa katika madai hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine mpaka sasa hivi Serikalini ni kuhusu kashfa ya wahamiaji haramu kuajiriwa Serikalini. Wote tunakumbuka kwamba Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (CDF) Jenerali Jacob John Mkunda alitupa taarifa akisema, “Baadhi ya waomba hifadhi hao na wakimbizi au familia zao wameajiriwa Serikalini kwa nafasi mbalimbali na wengine wamepewa teuzi Serikalini katika nafasi zenye maamuzi”. Nafasi za Watanzania zimechukuliwa na wageni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tuna mfumo gani wa utumishi ambao unaweza ukaruhusu mpaka mtu mgeni akaajiriwa? Tuna mfumo gani wa utumishi hapa nchini ambao unaweza ukaruhusu mtu ambaye siyo raia wa nchi hii akapata uteuzi ndani ya Serikali? Tuna mfumo gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, yanawezekanaje haya? Taarifa hii kwa sababu ilishatolewa, Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, una shida gani? Una kigugumizi gani kuitolea taarifa kikamilifu ndani ya Bunge hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni akina nani ambao wameajiriwa ndani ya nchi ambao sio raia wa Tanzania? Ni akina nani ambao wameteuliwa ndani ya nchi yetu ambao sio raia wa Tanzania? Ni akina nani hao na vyeo vyao na hatua zilizochukuliwa na Serikali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shida gani? Kiongozi Mkuu wetu wa Majeshi ametoa nyeti kama hii, halafu inanyamaziwa, haitolewi taarifa, mwaka 2024 na hata mwaka huu, 2025, tatizo ni nini Serikalini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)