Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi ya kuchangia katika Bajeti hii ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nafasi ya pekee, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kweli kwa mapenzi mema ya nchi yake na hasa katika eneo kubwa kuongeza bajeti ya Wizara hii, ambapo sisi wote ni mashuhuda ambao tunaona bajeti ya ofisi hii imeongezeka kwa takribani 25.5%. Ni ongezeko kubwa na lengo kubwa ni kuendelea kufikia wananchi wake kupitia taasisi ambazo ziko chini ya Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nafasi ya pekee, nampongeza Mheshimiwa George Boniface Simbachawene na Ndugu yangu Comrade Deus Clement Sangu kwa usimamizi mzuri ndani ya Wizara hii. Tunaona, kwa sababu ni mahitaji maalumu ya ajira za watumishi wetu pia na taasisi zote zilizoko chini ya Wizara hii, wamekuwa na weledi kuhakikisha kwamba wanasimamia kwa weledi katika maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni-declare kwamba, mimi ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ambayo inasimamia Wizara hii na pia kama Mjumbe wa Kamati, niendelee kushukuru. Serikali imekuwa ikichukua yale maoni ya Kamati na kuyafanyia kazi ndiyo maana tunaona ongezeko la bajeti katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme, Kamati imeenda kukagua baadhi ya miradi ambayo inasimamiwa kwa mfano na Ofisi yetu ya TAKUKURU (PCCB) na mingine inasimamiwa na TASAF.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na miradi ya PCCB kule Rombo, kwa kweli tumeona tunaunda mradi ambao thamani ya fedha unaiona, lakini mradi wenyewe ulivyotekelezwa katika eneo hilo, kwa kweli unaakisi Taasisi yetu ya Kupambana na Rushwa kwamba, tungetamani na taasisi nyingine ziende zijifunze jinsi miradi inavyotekelezwa hasa kupitia Taasisi yetu ya TAKUKURU ambayo ni kioo cha haki, lakini na kulinda rasilimali za fedha na utumishi mwema katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, makofi mengi na pongezi nyingi tuendelee kupongeza Taasisi yetu ya TAKUKURU kwa kazi nzuri chini ya Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Mkurugenzi Mkuu, Ndugu yetu Chalamila. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona miradi ya TASAF, tumetembea maeneo mbalimbali, tumeenda Zanzibar, tumeona; tumeenda Muheza tumeona, tumeenda Bagamoyo. Miradi hiyo kwa kweli inaakisi mahitaji ya mwananchi wa kipato cha chini ambaye kwa kweli inaleta mchango katika jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia katika uchambuzi hata katika eneo la TASAF, kwa kweli pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, anazo njia nyingi za kumfikia mwananchi. Pamoja na kuleta utaratibu mwingine, lakini kupitia TASAF hii, tunaona TASAF ambayo imejiingiza katika ujenzi wa miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda pale Bagamoyo tukaona madarasa yamejengwa katika maeneo ambayo vijana wetu, watoto wetu hawawezi kufika katika shule iliyosajiliwa ilipo. Kwa hiyo, wameamua kujenga darasa kuwasaidia watoto wa darasa la awali na madarasa mengine kwa ambao hawawezi kufika kwenye shule iliyosajiliwa, na hiyo imeleta mahudhurio makubwa katika shule pia imeongeza ufaulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaona ni mchango mkubwa wa kuhakikisha kwamba, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia anahakikisha amemfikia kila Mtanzania katika eneo lake kuhakikisha kwamba, hakuna anayebaki nyuma na hiyo fursa inakuwa ni fursa sawa kwa wote. Pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona katika maeneo mengine TASAF imeendelea kujenga miundombinu ya afya ambapo tumeweza kujenga kliniki za akina mama na watoto na hiyo inasaidia kupata huduma za afya na hiyo inapunguza vifo vya watoto na akina mama. Kwa kweli ni mageuzi makubwa sana ambayo Mheshimiwa Rais anafanya kazi kupitia Taasisi yetu ya TASAF na hiyo kwa kweli inawafikia wananchi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona ujenzi wa miundombinu mbalimbali. Tumeona barabara zinazofunguliwa na TASAF, lakini tumeona katika maeneo ya vijijini, maeneo ambayo yalikuwa hayafikiki sasa yameunganishwa. Tumeona tumeenda kule Samanga na Sembeti kule Marangu daraja ambalo lilikuwa ni changamoto kwa muda mrefu, lakini TASAF imeweza kutumia zile fedha na michango ya wananchi ikaunganisha mawasiliano katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaona ajira zimepatikana katika maeneo hayo, pia, kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa katika maeneo hayo kuweza kufika katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina kila sababu ya kuiombea hii TASAF kupitia Serikali yetu Tukufu ya Dkt. Samia kuendelea kutafuta vyanzo vingine vya fedha kuendelea kuiwezesha iendelee kufanya hizi kazi ambazo zimekuwa zinainua wananchi wa kipato cha chini kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, tunaona katika maeneo ya kilimo, kuna maeneo ambayo mifereji ya umwagiliaji imeweza kuchimbwa na kuweza kuongeza thamani katika mashamba ya umwagiliaji na hivyo uzalishaji wa mazao ukaongezeka pia wananchi wakapata chakula na pia ikawainua kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika maeneo haya naomba kupitia Wizara yetu ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Rais pamoja na viongozi wa Serikali tuendelee kutafuta fedha kwa ajili ya kuwezesha Taasisi yetu ya TASAF iendelee kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona vikundi…

TAARIFA

MHE. SALUM MOHAMMED SHAAFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

MHE. SALUM MOHAMMED SHAAFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba, katika pongezi zote anazozitoa juu ya TASAF, hata mimi jimboni kwangu TASAF imenipelekea zaidi ya shilingi milioni 100.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu kwamba, TASAF inafanya kazi nzuri, inafanya kazi kubwa, na zile fedha kule jimboni kwangu zinafanyiwa kazi, ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Kyombo unaipokea taarifa hiyo ya Mheshimiwa Salum Shaafi kutoka Pemba?

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Mheshimiwa Shaafi naipokea kwa mikono miwili. Yeye ni Mjumbe wa Kamati, na pia tumekwenda wote pamoja kutembelea miradi ya TASAF, naye anaona kwa macho. Nashukuru kwa hizo pongezi kwa kazi nzuri ya Mheshimiwa Dkt. Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naendelea na mchango kwamba katika eneo la TASAF. Pia tunaona vikundi mbalimbali vya walengwa wanaotokana na TASAF vimeendelea kufanya kazi kubwa na sasa hivi tuna vikundi zaidi ya 66,000 ambavyo vina wanufaika zaidi ya 800,000, na bado vinaendelea kukusanya fedha katika akaunti zake zaidi shilingi bilioni 13, na bado kwenye mzunguko vinakopeshana zaidi ya shilingi bilioni tisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwenye eneo hili, tunajua Mradi wa TASAF mtu akisha-graduate anatoka katika uchangiaji huo. Kwa hiyo, tuombe sasa vikundi hivi viingizwe katika mfumo wa halmashauri ili sasa ile 10% na yenyewe hao walengwa ambao walikuwa wanajulikana kwamba walitoka katika kaya ambazo zinalengwa, basi waweze kupata pia mikopo ya 10% ili pale TASAF ambapo inakuwa wame-graduate, basi wananchi wetu hawa waendelee kupata mikopo kupitia vikundi vyao, ile ya 10% kutoka halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo limefanyika kwa weledi mkubwa ni ubunifu kupitia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia wa TASAF kuwa na ushirikiano na Bodi ya Mikopo. Katika eneo hilo tunaona wale vijana wote wanaotambulika kuwa wanatoka kwenye kaya zenye mahitaji, TASAF imekuwa ikisimamia na Bodi ya Mikopo imekuwa ikiwapatia mikopo kwa 100%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linaashiria kwamba Mheshimiwa Rais ameamua kutumia njia nyingine ya ziada kusaidia wananchi wake hawa kuhakikisha kwamba wanapata mikopo wanaosoma na hivyo kupunguza vijana ambao siku zote wangekuwa ni vibarua, wakawa vijana ambao wanaweza kuajiri na kuajiriwa pale wanapohitimu masomo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi naendelea kupongeza juhudi hizi za TASAF. Naomba sasa Serikali iendelee kuwa na jicho la pekee katika eneo hili kuhakikisha kwamba, taasisi yetu hii ambayo iko chini ya Mheshimiwa Rais inaendelea kupata uwezeshaji wa kufanya kazi nzuri kama tulivyoona katika sekta mbalimbali; sekta ya elimu, afya, kilimo na ya miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine utakuwa unaenda kwenye soko la ajira na hasa nitajikita katika eneo la walimu. Ilikuwa ni nia ya dhati kwa Serikali yetu, wakati wa mahitaji ya walimu wengi nchini kwetu, Serikali iliamua kutoa mikopo kwa 100% kwa hii taaluma ya ualimu. Tulipata enrolment nyingi sana kuingia Chuo Kikuu kwa walimu na kweli Tanzania sasa hivi ina hazina ya vijana wetu ambao wamehitimu katika hii taaluma ya ualimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ni lazima tukubaliane, Serikali imeendelea kutoa ajira za kutosha kwa walimu lakini bado mahitaji katika shule zetu na yenyewe bado yapo na Serikali bado inapambana kuendelea kutoa ajira zingine ili kuweza kuhakikisha kwamba shule zinakuwa na walimu wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikwambie, hata kama Serikali ingeendelea kutafuta ajira za walimu wote, kwanza hawawezi kutosha, kwani shule zetu ni chache kuliko idadi ya walimu walioko katika soko; lakini bado Serikali inaendelea kutoa mikopo ya 100% kwa walimu kuendelea kusoma. Huko mbele tutaenda kugota na walimu watakosa ajira kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni jukumu la Serikali kufanya Training need assessment, mahitaji ya taaluma ambayo inatakiwa kwa muda huu katika nchi yetu. Kama tunaona soko la walimu, wametafutwa walimu ni kweli wamepatikana lakini ajira tulizonazo haziwezi kutosha kwa wingi wa walimu tulionao, basi waweze kubadilisha mfumo na wakibadilisha mfumo wanatafuta ile taaluma ambayo nchi inahitaji kwa wingi, lakini na hawa walioko ambao wameshahitimu tuombe Serikali sasa iongeze juhudi kuwatafutia ajira za nje ya nchi katika taaluma tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanaenda kufundisha Kiswahili, wanaenda kufundisha Kifaransa, wanaenda kufundisha lugha nyingine ili sasa na hao walioko hapa katika ajira ambao wako nchini, basi wote waweze kupatiwa ufumbuzi na wote waweze kujiajiri. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naona ni kengele ya pili, ninaomba nikushukuru kwa nafasi na ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)