Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arusha Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kushukuru tena kupata nafasi ya kuweza kuchangia kwenye Bunge lako Tukufu, na nitajielekeza kwenye hoja tatu tu. Kuna mambo ya Utumishi, pia kuna mambo ya Utawala Bora ambapo najua TAKUKURU wamo humu ndani na masuala mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka yangu yote inayokaribia mitano katika Bunge hili nimekuwa najenga hoja kuhusiana na ujenzi wa Stendi ya Jiji la Arusha. Sasa watu watashangaa naongelea stendi kwenye Utumishi, lakini hapa kwa sababu kuna utawala bora, wapo TAKUKURU ambao nadhani wana kazi ya kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alifanya kazi kubwa, katutafutia mradi ambao unaitwa Mradi wa TACTIC ambao unakwenda kuweka historia kwa kujenga stendi ya kisasa kwenye Jiji la Arusha. Mchakato wa kumpata mzabuni unavyokwenda unatia mashaka na ndiyo maana hapa nataka niwaombe TAKUKURU waongeze sikio na jicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilitangazwa tender kwa ajili ya kumpata mkandarasi tarehe 19 Januari, 2024, mkandarasi akapatikana kwa shilingi 23,591,762,064/=. Baada ya kupatikana huyu mkandarasi, Mkurugenzi wa Jiji akatoa barua (Letter of Acceptance) kwa mkandarasi tarehe 27 Mei, 2024 na mkandarasi huyo alikuwa anaitwa MS China Jiangxi Cooperation for International Economic and Technical Corporation.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo Mkurugenzi akapokea maelekezo kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI ya kutaka Mkandarasi aliyeshinda kwa shilingi bilioni 23 asipatiwe kazi badala yake apatiwe kazi Mkandarasi aliye-bid kwa shilingi 31,036,152,000/=.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelekezo hayo ambayo tofauti yake sasa ya aliyeshinda kama lowest bidder na huyu wa pili anatakiwa kupewa ni shilingi bilioni 7.4 ambayo ingeokolewa ingesaidia barabara, ingesaidia vivuko na vitu vingine, na tungekuwa tumeongeza heshima kwa jitihada za Mheshimiwa Rais kwenye kutafuta fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, michakato ikaendelea ikaonekana kuna ugumu, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha ambaye alipokea maelekezo uliyoyasema kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, 12 Septemba, 2024, ilipofika tarehe 3 Februari, 2025 akai-cancel tender hiyo. Baada ya kuona kwamba aliyeshinda bid ni ndogo huku na maelekezo mambo yakakutana katikati hapo mchakato ukafutwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchakato ulipofutwa ikatangazwa tena tender na moja ya kigezo, walisema mkandarasi awasilishe ushahidi wa kuwa amefanya miradi isiyopungua ya dola milioni 46 na aliwasilisha miradi siyo chini ya dola 147,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, tender ikatangazwa tena wakati tayari Mkandarasi alishapewa na notice ya kuwa awarded kwamba ameshinda hiyo contract. Tender ilipotangazwa…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mrisho Gambo samahani…
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo.
MWENYEKITI: Hayo unayozungumza nafikiri yameshapelekwa kwenye Kamati ya Maadili, yataenda kujadiliwa kule. Kama una hoja nyingine ya ziada naomba uzungumze. (Makofi)
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Hapana. Hili jambo ni jipya kabisa, halihusiani na zile hoja nne za asubuhi. Ni jipya kabisa, naomba nipate haki ya kuchangia, kwa sababu…
MWENYEKITI: Si ni jambo la hilo soko ambalo unazungumzia?
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Hapana, Siyo soko. nazungumzia stendi, ni jambo jipya kabisa.
MWENYEKITI: Hiyo stendi pia si imezungumziwa asubuhi?
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Hapana. Haijaingia kwenye hizo hoja. Hili ni jambo jipya kabisa. Naomba nipate nafasi ya kuchangia kwa sababu TAKUKURU wapo hapa na Wizara hii inahusika na TAKUKURU…
MWENYEKITI: Basi naomba ujitahidi usiguse jambo lolote ambalo limeshazungumzwa asubuhi na kupelekwa maamuzi yake kwenye Kamati ya Maadili.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadaye ikatangazwa tena tender, akapatikana Mkandarasi mwingine mmoja akashinda kwa shilingi bilioni 30, mwingine shilingi bilioni 31. Anataka apewe aliyeshinda kwa shilingi bilioni 31 siyo wa shilingi bilioni 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa kuna jambo la kufanya kwa wenzetu wa TAKUKURU kupitia Ofisi ya Rais, Utumishi, ili tukaokoe hizi fedha ambazo Mheshimiwa Dkt. Samia anazitafuta kwa jasho na damu dunia nzima ili kuwasaidia wananchi wa Jimbo la Arusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizingatia maelezo yangu mimi simtuhumu mtu hapa, naeleza scenario na ninatoa nafasi kwa taasisi zinazohusika zikafuatilie ili ukweli ukijulikana hatua zichukuliwe, ikiwa vinginevyo tutakubaliana pia na matokeo. Kwa hiyo, na hao waliopo sasa hivi, mmoja ameshahamia kule PPRA ambao kwa maoni yangu mimi, wote hawa mmoja 30 mmoja 31 bado wanazidisha gharama zile zile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ikichunguzwa na ikadhibitika, tutafute namna yoyote ikiwezekana, akipatikana aliye-bid chini tutaweza kuokoa gharama kubwa zaidi na wananchi watapata stendi yao kama Rais alivyokuwa anaifanyia kazi pamoja na masuala mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona hilo jambo niliseme kwa sababu ni jambo naona lina maslahi mapana katika Jimbo letu la Arusha Mjini na stendi ambayo kama isingekuwa haya mambo niliyoyasema hapa, pengine siku nyingi tungeshapata mkandarasi na kazi pengine ingeweza kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kwenye upande huu wa Utawala Bora ambayo pia na TAKUKURU wapo, nataka nitumie fursa hii kwa kweli kutoka kwenye dhati ya moyo wangu kuwapongeza sana TAKUKURU na hasa kupitia Mkurugenzi wake Chalamila na wasaidizi wake walioko Mkoa Arusha na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tuna changamoto kubwa sana kwenye upande wa bodaboda. Kuna hela zilichukuliwa kwenye akaunti, waliochukua walikuwa wanajulikana, nimelalamika Bungeni kwa muda mrefu, lakini wahusika hawakupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nazungumza nikiwa na furaha kwa sababu tayari TAKUKURU wameshamkamata mmoja wa wahusika walioiba fedha za bodaboda, ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa umoja huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado wanaendelea na jitihada za kuwatafuta wahusika wengine. Tunaomba wahusika wote watafutwe na wanapokamatwa wapelekwe Mahakamani. Lengo letu sisi, zile fedha zipatikane, zirudi ili zikawasaidie bodaboda kama malengo yetu ya awali yalivyokuwa wakati tunatafuta zile fedha za kuweza kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawapongeza sana TAKUKURU najua mmefanya haya kutokana na uongozi imara wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ili waweze kuhangaika na rushwa na ufisadi kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ni kuhusiana na TASAF. Wenzetu wa TASAF, na hili Mheshimiwa Simbachawene analijua vizuri. Tulikwenda pale na Mheshimiwa Mhagama kabla hajawa Waziri wa Utumishi, akaenda, na Askofu Sosi yuko pale, akaahidi kwamba kile kivuko kitajengwa na TASAF na akatoa mpaka deadline, lakini mpaka leo kivuko hakijajengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilienda kumtembelea Askofu akanipa hizo concern, nikamfikishia Mheshimiwa Waziri Simbachawene na akaongea na Baba Askofu, akaelekeza Kivuko cha TASAF cha Betheli ambacho kiko Shule ya Msingi Kijenge na chenyewe kijengwe. Mpaka leo bado hakijajengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie fursa hii kuomba watu wetu wa TASAF wakipe uzito kivuko kile kwa sababu, pale kuna shule ya msingi watoto wanasoma, pale kuna watu wanaabudu kwenye Kanisa, kikitengenezwa kitasaidia sana kuondoa changamoto kwa wananchi wetu wa Kata ya Kimandolu pia na eneo la Kijenge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Mradi wa TASAF kule Engutoto Block ‘J’ ulipitishwa kwenye vikao vyote vya halmashauri, fedha pia zilipatikana lakini mpaka leo kile kivuko hakijajengwa na wananchi walishaambiwa na walishaandaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Simbachawene na kivuko hiki cha Block ‘J’ kule Engutoto Njiro na chenyewe pia kiende kikajengwe kwa sababu kilifuata taratibu zote na kikapitishwa na fedha zikatoka, lakini mwisho wa siku kivuko bado hakijajengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nini kilitokea? Kuna mamlaka ya kufuatilia ndiyo maana wakati mwingine tunapewa malalamiko kwamba Mbunge hahudhurii vikao. Nilihudhuria kikao cha Baraza la Bajeti la juzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya bajeti ikasomwa pale, taarifa inamalizwa kusomwa, hata hatujaijadili, tukaambiwa kuna kiongozi anakuja kama mgeni. Kiongozi akaja pale, watu wakaanza kulia, bajeti ikafungwa na ndiyo bajeti yenyewe ambayo imeletwa TAMISEMI kwenye vikao haikujadiliwa. Sasa hapo utawala bora uko wapi?
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo…
TAARIFA
MWENYEKITI: Taarifa iko wapi?
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niko hapa.
MWENYEKITI: Ndiyo Mheshimiwa Kimei.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingetaka ni-interrupt hoja za mwenzangu, lakini nataka niipongeze sana TASAF kwamba wamejenga kivuko pale kwetu Samanga kwenda Sembeti, na kivuko hicho kimetembelewa na Kamati. Kamati ilihusika na imekiona ni cha hali ya juu sana. Kwa hiyo, na huko kwake itafanyika tu, asiwe na wasiwasi. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mrisho Gambo unaipokea Taarifa hiyo ya Mheshimiwa Dkt. Kimei.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea, maana najua imenisaidia pia kuendelea kujijenga jimboni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sekunde kidogo kwa sababu dakika zangu amechukua Mheshimiwa Kimei.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa malizia nusu dakika, muda umeisha, kengele imelia.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nitumie fursa hii kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu, kwa kweli kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametatua changamoto nyingi sana za watumishi, wana miaka mingi walikuwa hawajapanda madaraja, lakini kwa Mheshimiwa Dkt. Samia walipanda madaraja. Mishahara ilikuwa haijapanda kwa Mheshimiwa Dkt. Samia mishahara imepanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, malimbikizo yalikuwa hayajalipwa, lakini kwa Mheshimiwa Dkt. Samia malimbikizo yamelipwa. Bado watumishi wamenituma nimshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia, lakini naomba niendelee kumkumbuka na ikiwezekana apandishe mishahara yao na siyo tu watumishi wa umma, lakini pia watumishi wa sekta binafsi ambao kiuhalisia mishahara yao imekuwa midogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta binafsi zinajiamulia wakati mwingine kwa sababu malengo yaliyowekwa ni madogo wanatembelea mule mule. Kwa hiyo, tunaomba mtusaidie pia kuwasimamia angalau kima chao cha chini cha sekta binafsi kifanane angalau na kima cha chini cha Serikali ambacho ni kikubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana na ahsante sana. (Makofi)