Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilwa Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utawala Utumishi wa Umma na Utawala Bora, inayoongozwa na bosi wangu wa kipindi hicho, kaka yangu Mheshimiwa Boniface Simbachawene. Niseme tu kwamba kwa ambavyo ametutendea haki Mheshimiwa Simbachawane kwenye maeneo mbalimbali ambayo mamlaka ilimpa dhamana ya kusimamia, amefanya vyema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ofisi hii ya Mheshimiwa Rais yeye akiwa Waziri wa Nchi, niseme tu kwamba pasipo na kupepesa macho wala kumung’unya mdomo, Mheshimiwa Simbachawene anastahili pongezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara kadhaa nimeshuhudia baada ya mijadala ya Bungeni mara nyingi yeye huwa anarudi ofisini kwenda kusikiliza hoja mbalimbali za Watanzania na kuzitatua; na mwenyewe nimemkuta ofisi akifanya shughuli hiyo nami nikiwa mteja wake amenihudumia ipasavyo. Nashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, msaidizi wake rafiki yangu, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, ndugu yangu Mheshimiwa Deus, niseme tu kwamba wana Kwela hawakufanya makosa kukuchagua, na nina imani kwa spirit ya kazi uliyonayo katika nchi yetu, na pia katika Jimbo lako, wana Kwela wanakwenda kukurudisha tena utumikie nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami katika mchango wangu, kwa upekee wake kabisa, nitazungumzia Watumishi wa Umma Kada ya Ualimu. Kwa muktadha wa mchango wangu, nitazungumzia walimu wa shule za msingi, walimu wa sekondari na walimu wa Vyuo vya Ualimu ambao kimsingi taratibu zao za kazi zinafanana, lakini pia yale ambayo yanawasibu katika mazuri na yale ya misukosuko kidogo katika kazi yanafanana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kupeleka salamu za walimu kwenda kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan zikipitia kwa Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ndugu yangu, kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene. Walimu wa Tanzania wanasema, wanamshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba sasa wanafanya kazi katika mazingira bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wameboreshewa mazingira ya ufundishaji, na mazingira ya kutunza watoto wetu. Leo hii tunapozungumza, kila kona ya nchi kuna madarasa ya kutosha, mazuri, vyoo vya kutosha kwa ajili ya watoto wetu na viko katika hali nadhifu, nyumba za walimu; ni mchakato ambao Mheshimiwa Rais ameendelea nao katika kipindi chake chote cha uongozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika hilo walimu wa Tanzania wanasema wanampongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kana kwamba haitoshi, wanasema kwamba kilio chao cha siku nyingi cha upandishwaji wa madaraja na hata yale ambayo yamelimbikizana, kipindi cha Uongozi wa Rais Dkt. Samia tumekuja kushuhudia kwamba walimu wetu wakipandishwa madaraja kila pale inapostahili kufanyiwa hivyo. Wanashukuru sana sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili wana ombi moja tu, kwamba fedha za likizo sasa kwa kweli wanashukuru wanazipata, lakini wanaomba tu, badala ya kupitia kwa waajiri wao, zitoke Hazina, walipwe moja kwa moja ili kuondoa usumbufu na adha, na pia kutofautiana kati ya mwajiri mmoja na mwajiri mwingine, hilo ndiyo ombi la walimu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, niseme tu kwamba kumekuwa na mashauri ya kinidhamu ya walimu kwa muda mrefu. Kwa uchache sana niseme kwamba kuna walimu wetu 14 ambao mashauri yao yalishathibitishwa kwamba hawana hatia na Tume ya Utumishi wa Walimu tangu mwaka 2023. Ilikuwa ni tarehe 4 Machi, 2023, Katibu wa Tume anamwandikia Katibu Mkuu Utumishi ku-clear kwamba walimu wetu hawa hawana hatia, na kwa maana hiyo wanaombewa kibali cha kurudi kazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ni walimu kutoka Halmashauri zetu mbalimbali nchini, wanaomba Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma chini ya ndugu yangu, kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene, tupe msukumo katika jambo hili ili walimu wetu hawa ambao wamesafishwa na Mamlaka yao ya nidhamu, warudi kazini waweze kutumikia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo langu la tatu la uchangiajia, nilikuwa nina rai kwamba tutoe motisha kwa watumishi mbalimbali kwa mujibu wa majukumu na uzito wa kazi zao. Hapa nijitolee tu kuwa, kama chachu ya kuanza kusaidia ofisi yetu ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora nifanye kwa uchache tu kitu kinachoitwa job analysis, kwa maana ya mchanganuo wa kazi za walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu la msingi la mwalimu ni kufundisha, lakini katika ufundishaji wake kuna vitu mbalimbali ambavyo kabla ya ufundishaji anaviandaa vikiwemo; scheme of work, lesson plan, lesson notes, log book, class journal, attendance list na vingine; na hapa nina mlolongo wa nyaraka ambazo walimu wanazitumia, hizi hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchache wake tu hizi zote ni nyaraka ambazo walimu wetu wanazitumia wanapofundisha Watoto. Hizi ni kwa uchache tu, lakini zipo nyingi. Hizi hapa zote; zipo Scheme of Work zote zipo hapa, mpaka Teaching Aid anapokuwa darasani, mwalimu analazimika kuandaa kitu ambacho itakuwa ni msaada kwa watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni Teaching Aid ya Mwalimu wa Mathematics, akifundisha product of two linear equations. Kwa maana, hapa anatafuta eneo, area of this rectangle. Hii ni kazi ya walimu wetu. Pamoja na kazi ya ufundishaji na zana zote hizi ambazo walimu wetu wanaziandaa. Walimu wetu hawa wamekuwa wakitumia reference book mbalimbali, vitabu vya kiada na vitabu vya ziada
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wamekuwa wakitoa majaribio mbalimbali ya quiz za darasani, mitihani ya kila wiki, mitihani ya kila mwezi, mitihani ya kila muhula, mitihani ya kila mwaka na wanakuwa na jukumu kubwa la kusahihisha scripts. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimkuta mwalimu amejifungia kwa wale ambao wenza wao ni walimu watakuwa ni mashuhuda kwamba, kama baba ni mwalimu, mama yuko kitandani amepumzika anamwacha baba anasahihisha scripts za watoto. Kama baba ni kada nyingine mama ni mwalimu, baba amepumzika kitandani usiku, mama anasahihisha scripts za watoto mpaka saa saba za usiku, ni lundo. Hiyo ni workload kubwa ya walimu wetu katika hii nchi yetu hii. (Makofi)
MHE. DKT. BASHIRU A. KAKURWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa. Niko hapa Bashiru, niko hapa taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa haya taarifa, karibu.
TAARIFA
MHE. DKT. BASHIRU A. KAKURWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri, siyo mara nyingi kutoa taarifa, lakini mchango wake kwa uzito wake nathibitisha anayoyasema. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ni Mwalimu, na mke wangu ni Mwalimu. Unapofika wakati wa kusahihisha, wakati wote tuko darasani, ni kama vile tumeahirisha ndoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu haruhusiwi kutoa taarifa, kwa niaba yake naye ni mwalimu anaweza akathibitisha. Hata Mheshimiwa Spika naye anaweza akathibitisha. Kwa hiyo, mchango huu una uzito wa aina yake na ndiyo maana kwa walimu motisha wetu mkubwa sana huwa ni wito. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Bashiru Kakurwa, ahsante. Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge unaipokea hiyo taarifa?
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa unyenyevu na heshima kubwa ninapokea taarifa. Niweke taarifa sahihi tu hapa kwamba aliyetoa toa taarifa ni mwalimu wangu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliyenifundisha Political Science mwaka 2001 mpaka 2004. Kwa maana hiyo, siwezi kuwa na pingamizi wala kigugumizi kwa taarifa yake. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa nakurejeshea dakika zote ambazo ametumia Dkt. Bashiru. (Makofi/Kicheko)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Pamoja na yote haya, walimu bado wanakazi ya kuingiza taarifa zao katika mifumo. Sasa hivi tunakwenda e-Government lakini walimu wetu wamekuwa na mzigo mkubwa wa kuingiza taarifa, kwani mifumo ni mingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mfumo unaoitwa Info Taaluma, kuna mfumo unaitwa PEPMIS, kuna mfumo unaoitwa BEMIS, kuna mfumo unaoitwa MadeniMIS, kuna mfumo unaoitwa SIS, mifumo ni mingi na kwa maana hiyo walimu wanatumia bongo zao kwa muda mwingi sana kufanya kazi za ziada. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiondoa majukumu ya kitaaluma ya walimu wetu, wamekuwa na majukumu mengine yasiyokuwa ya taaluma zao ikiwemo usimamizi wa miradi. Sote ni mashahidi kwamba miradi yote ambayo Serikali yetu pendwa inatekeleza katika shule zetu kwa maana ya ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, vyoo na kadhalika, wasimamizi wakubwa ni walimu hao hao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu hawa leo wamekuwa ndio ma-procurement officer, wanaingia katika mifumo kutafuta wazabuni wa kujenga majengo yetu, walimu hawa leo ndio wamekuwa ma-project manager wa kusimamia miradi katika shule zetu, walimu hawa leo ndio wamekuwa ma-engineer wa kusimamia majengo yetu katika shule zetu. Haya ni majukumu nje ya taaluma zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nani siyo shuhuda kwamba walimu wetu wamekuwa wakihusika katika majumu pia ya kitaifa? Leo hii tumeshawasha Mwenge na umeanza kuzunguka katika Mikoa yetu, lakini nani siyo shuhuda kwamba walimu wetu wamekuwa ndiyo chachu ya Mwenge? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiona vijana wa halaiki wanasherehesha kwenye Mwenge pale, ni kazi ya walimu wetu. Ukiona club za wapinga rushwa kwa ajili ya kukidhi vigezo vya Mwenge, ni kazi za walimu wetu; ukiona shughuli za Kitaifa kama vile Sensa, Uchaguzi, programu mbalimbali za lishe, chanjo mbalimbali, majukumu hayo wanatekeleza walimu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na majukumu haya ya kimsingi ya taaluma zao na ya ziada, nakuja na mapendekezo kwamba, kutokana na uchambuzi nilioufanya kwa muhtasari wake, walimu kuna kitu cha ziada wanatakiwa wafanyiwe katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirejee kitabu kitakatifu cha Biblia, kitabu cha Isaya, Sura ya sita mstari ule wa nane nanukuu: “kisha nikasikia sauti ya Bwana akisema, nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu?” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza Bunge lako Tukufu, nani atakwenda kufanya kazi kwa ajili ya kuwapa motisha, kuwapa moyo, kuwatia nguvu walimu wetu? Kila mtu ana jibu lake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitamani Bunge letu hili la Kumi na Mbili, ambalo Mheshimiwa Spika wetu ni Mwalimu, ingekuwa ni chachu ya hiki ambacho ninakipendekeza. Napendekeza kupitia Ofisi ya Rais, Utawala Bora na Menejimenti ya Utumishi wa Umma, tuanzishe Sera Maalumu kwa ajili ya Motisha kwa Walimu (Teacher Motivation Policy Framework) na itakapobidi, kwa sababu andiko linasema nimtume nani? Mimi nitakuwa namba moja kwenda kusaidia Ofisi ya Rais kuandaa framework hii ya Sera. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kassinge, ahsante sana, ahsante sana…
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, nakushukuru kwa kunivumilia na kwa kuniongezea muda ule wa kufidia. Baada ya taarifa hii, naomba kusema kwamba naunga mkono hoja. (Makofi)