Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, Sekta ambayo nimeitumikia kwa miaka 31 nikiwa fundi bomba wa kupaka grease mpaka nilipokuwa Naibu Waziri wa Nishati.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa Bajeti na speech nzuri, Naibu Waziri ambaye amevaa viatu vyangu, yaani kama vya kwako kabisa, lakini na Watendaji wote ambao nimeishi nao kwa miaka 31 ambao naamini wanaifanyia vizuri nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajibu hoja zilizojitokeza kutoka Wizara ya Nishati, nichukue fursa hii kuishukuru Serikali kupitia Wizara hii kwa namna walivyosambaza umeme kwenye Jimbo langu la Muleba ya Kaskazini. Nifikishe ujumbe wa Wanamuleba Kaskazini, asilimia 16 wanaoishi visiwani, Mheshimiwa Profesa Muhongo wanamtegemea kwamba kwa kurudi kwake, Visiwa vya Goziba, Makibwa, Bumbire na Kerebe vitapata umeme, sina wasiwasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge zilizojitokeza kwenye bajeti hii ya Nishati na Madini. Suala la EPZ Simanjiro, Tanzanite; tumeshatoa EPZ, tumeshatoa eneo tumefidia. Sasa hivi tunatafuta wawekezaji watakaoweza kutengeneza Tanzania Minerals Business Center. Nikiwaonesha picha yake kama ndoto ikiwa kweli, suala la Tanzanite litakuja kubadilika na kuwa ndoto ya mambo ya zamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Nishati na Madini, mpango wao ni kutengeneza kituo kimoja cha madini na EPZ ilianzishwa nyakati zile kwa misingi hiyo. Kwa hiyo, hilo suala halina tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru wewe na Ofisi ya Bunge kwa kuitanguliza bajeti yangu na Wizara ya Nishati ikaja baadaye. Wako waliokuwa wanasema viwanda haviwezekani, sasa angalieni, kuna power generation inaendelea kutokea, kuna power transmition inaonekana, kuna power distribution. Kama nilivyozungumza, tumieni umeme huo mpaka vijijini kwa kuanzisha viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, muwe na imani, think positive, muione glass ya maji iliyoko nusu kwamba imejaa nusu, msione kwamba iko tupu nusu. Huu umeme unakuja, maneno anayoyasema Mheshimiwa Profesa Muhongo, nina imani naye, ni mambo ya kweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala ambalo limechukua hisia za watu wengi la Mchuchuma na Liganga. Mchuchuma na Liganga, Waraka la Baraza la Mawaziri wa mwaka 96, Waraka Na. 6 ndiyo ulisukuma suala la Mchuchuma na Liganga. Sasa hivi tuko wapi? Nawaomba Waheshimiwa Wabunge, kama kuna mtu yeyote anajua makandokando yanayokwamisha Mchuchuma na Liganga aje aniambie mimi. Mheshimiwa Deo, Mzee wa Njombe njooni wote mnione.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Mchuchuma na Liganga Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati alijibu swali hapa akasema anaanza kulipa mwezi wa Sita na anayewajibika kulipa ni Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji; yaani mimi ndiyo Waziri mwenye dhamana, niwahakikishie kwamba Tanzania sasa ziko pesa za kutosha za kuweza kulipa hao wananchi. Ninachoomba ni ushirikiano wa Wabunge. Hii sitamwachia mtu, nitashughulika mimi mwenyewe na Makatibu Wakuu na Madiwani wote tuhakikishe watu wanakuwa compensated. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema kama kuna mtu anaelewa makandokando yoyote kuhusu mradi huu, anieleze. Hakuna kurudi nyuma, tunakwenda mbele. Tunakwenda na mwekezaji huyo aliyepo, aje alipe. Kama alivyozungumza Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, mradi huu katika kuujenga tutaajiri watu 3,000, lakini utakapokuwa umeanza, utaajiri watu 6,000 wa moja kwa moja. Huu mradi utakuwa na indirect employment watu 24,000, lakini utachangamsha maeneo yote ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaeleze, wananchi wote wataelimishwa namna ya kushiriki. Tuna uhakika sasa amekuja huyu mwekezaji ambaye ni Mbia wa NDC, tumekaa naye na bahati nzuri Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Mheshimiwa Dkt. Dalaly Kafumu alikuwa nami, tumekaa nao, nimewauliza, wakanionesha nyaraka, hii ni ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tujiweke tayari, tu-think positive huu mradi uweze kuendelea. Kwa hiyo, haki za watu zitalipwa. Nilichozungumza na walioliona kwenye vyombo vya habari, tunachotaka, ni lazima VETA iwepo, iwafundishe Watanzania. Nimesema mbele ya Bunge Tukufu, Watanzania watashiriki kwenye ngazi zote za utendaji kuanzia ngazi za chini mpaka ngazi za juu. (Makofi)
Waheshimiwa Wabunge, nimepata faida ya kushiriki kwenye mchakato mzima wa kampuni. Nimewaeleza nilipoajiriwa TPDC, nilikuwa pipeline operator nikifungua valve, lakini nimepanda mpaka nikawa international trader wa Chevron, nikapanda mpaka Naibu Waziri wa Nishati. Kwa hiyo, nami napenda vijana wa Kitanzania wakachakate chuma watengeneze vyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie ndugu zangu wa Kilimanjaro; Kilimanjaro Machine Tools inapoanza Mchuchuma na Liganga na yenyewe itaanza kazi. Kwa hiyo, suala la Mchuchuma na Liganga zile historia na hadithi zimefikia mwisho, tunakwenda kwenye reality na mwekezaji, pesa zimeshaingia nchini. Ule mradi utajengwa kwa gharama ya Dola bilioni tatu na Tanzania tunashiriki kikamilifu katika mradi huo. Tutakapokuwa tumefikia kikomo, tutakuwa na hisa asilimia 49.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna mtu anafahamu makandokando yoyote, asiache kuja kuniambia Mwijage ulikosea, aje twende wote. Mchuchuma na Liganga ni mradi kielelezi, kwa sababu wenyewe utachochea viwanda vingine. Badala ya kuagiza chuma ambacho ni bidhaa nzito kutoka huko Amerika na sehemu za Uchina tutakuwa na chuma hapa nyumbani kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mradi wa Mchuchuma na Liganga kutakuwepo mtambo mwingine wa kuchenjua madini yanayopatikana ndani ya mtambo huo wa titadium na vanadium yanayoendana na chuma. Ndiyo maana mradi wa Mchuchuma na Liganga ulichelewa. Chuma chake siyo cha kuchukua na kuchakata, kina taratibu zake na huyu mwekezaji amefanya research na amejihakikishia. Kwa hiyo, ndiyo maana ilani ya Chama changu inasema huu ni mradi kielelezi, ndiyo maana mpango wa miaka mitano unaitwa mradi kielelezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka nilifafanue hilo, kwa hiyo, Mchuchuma na Liganga is a reality, lakini umeme unakuja. Watu wengine wanafanya mahesabu kwamba imechukua…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, naomba umalize. Naomba umalize!
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa muda wa kuchangia bajeti hii. Niwahakikishie kwa kumalizia kwamba, umeme upo wa kutosha. Kauli za kwamba hatuna umeme wa kutosha zinawakimbiza wawekezaji lakini wawekezaji wanaijua Tanzania ndiyo maana sasa kutoka Mtwara kwenda mpaka Dar es Salaam, ukanda mzima wa gesi wa uwekezaji ndiyo sehemu ya preference ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ndugu zangu tuzungumze vizuri, tuipe imani hii bajeti kusudi wawekezaji waweze kuja, nami niweze kutengeneza viwanda, score card yangu iboreke na tajiri namba moja anione nafaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono bajeti ya Mheshimiwa Profesa Muhongo.