Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Meatu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kutoa mchango wangu katika hoja iliyopo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Utumishi kwa kazi nzuri wanazozifanya. Kipekee Mheshimiwa Waziri toka aingie Ofisi hiyo ametatua changamoto nyingi za kiutumishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimpongeze Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazozifanya hususan kwa kukubali kuridhia kuboresha na kutengeneza mifumo ikiwemo mifumo ya ukusanyaji mapato na mifumo mbalimbali. Tumeona kabisa mapato yameongezeka Serikali za Mitaa pamoja na Serikali Kuu, lakini Mheshimiwa Rais akaenda mbele zaidi akataka mifumo hii iweze kuunganishwa ili iweze kuleta tija zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee leo niongelee Mfumo wa Watumishi uliopo Ofisi ya Utumishi ambao umeleta maboresho makubwa katika Wizara hiyo. Wengi tulishuhudia katika miaka ya nyuma kulikuwa kuna wimbi kubwa sana la watumishi hewa, kulikuwa na wimbi kubwa sana la mishahara hewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia maboresho ya mifumo, changamoto hii imeweza kutatuliwa kwa kufanya mawasiliano ya taasisi na Wizara kwa muda muafaka ili kuwaondoa watumishi waliofariki kwenye mfumo, waliostaafu, walioacha kazi pamoja na changamoto mbalimbali ili iweze kuokoa fedha za Serikali ambazo zingeweza kulipwa kama mishahara isiyostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza pia kwa kufanya kazi ya kupunguza malimbikizo ya mshahara kupitia mfumo huu. Ni dhahiri kwamba mtumishi anaingizwa kwanza kwenye mfumo ndiyo anapata barua ya ajira, hali kadhalika hata aliyepanda daraja anaingizwa kwanza mfumo ndiyo anapata barua ya kubadilishiwa daraja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona tumepunguza kwa kiasi kikubwa mlundikano wa malimbikizo ya mishahara, lakini natambua madeni ya mishahara bado yapo. Nami nikiwa Mjumbe wa Kamati ya Bajeti nashuhudia namna Serikali inavyolipa madeni kwa watumishi yakiwemo ya likizo, mishahara pamoja na ya matibabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kupongeza, kama tutakumbuka, tulikuwa na uhakiki wa watumishi mwaka 2016 na zilijitokeza changamoto nyingi kuathiri madaraja ya watumishi, nami nilikuwa na hoja yangu ya watumishi ambao walipata barua kwa pamoja, wengine wakapandishwa madaraja, wengine wakasimamishwa kupisha uhakiki. Leo nimesimama mbele nikiishukuru na kuipongeza Serikali. Sasa, wale watumishi wa kipindi kile madaraja yao yanaenda sambamba, wote wamerekebishiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke pia, zoezi hili la mwaka 2016, liliathiri mserereko wa madaraja kwa watumishi walioajiriwa mwaka 2013, 2014 na 2015 na kusababisha watumishi hawa kutumikia daraja moja kwa muda mrefu sana. Mathalani ajira ya mwaka 2013 walikuja kupandishwa mwezi Mei, 2019. Kwa hiyo, kukawa na miaka mitano zaidi badala ya ile mitatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watumishi wa mwaka 2014/2015 wenyewe wakarekebishiwa mwaka 2021. Kwa hiyo, wakachelewa kwa miaka sita na miaka mitano. Naomba sasa Serikali kwa kuwa yale mliyafanya, na tuendelee sasa kuwarekebishia, ili waende sambamba na madaraja ambayo yanawastahili ili tuondoe ile kero.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, naipongeza Serikali, upande wa Serikali za Mitaa ilipochukua jukumu la kuwachukua Watendaji wa Kata pamoja na Vijiji kuwaingiza payroll ya Serikali Kuu. Tuliondoa mzigo mkubwa na walikuwa wakinyanyasika na wakati mwingine walikuwa hawakopesheki kwenye benki kwa sababu mishahara yao ilikuwa haitabiriki watalipwa lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu walikuwa hawaujui hata mwisho wa mwezi kwa sababu ilikuwa ni Mkurugenzi atakapojisikia kuwalipa au halmashauri itakapokuwa na mapato ndiyo itawalipa mshahara. Pia, iliathiri michango katika hifadhi ya jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaweza tukashuhudia watumishi wengi, Watendaji wa Kata na VEO wanaostaafu wameshindwa kupata mafao yao sahihi kulingana na madeni ambayo hayajalipwa na Wakurugenzi wao. Wengine wamediriki kuandika barua PSSSF kuwaomba, nilipe tu mafao yangu bila michango ambayo haijalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi, hatuwatendei haki. Naomba kwa mfano, Halmashauri ya Meatu mafao ambayo hayajachangiwa na Mkurugenzi kwa WEO na VEO ni shilingi milioni 43.7 ukiongeza na riba ni shilingi milioni 45.6. Jumla wanadaiwa shilingi milioni 89.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wengi waliostaafu wanalia, mafao yao yameshindwa kulipwa. Naiomba Serikali, kama tulichukua madeni mengine ya watumishi, naomba basi hata huu mzigo tuuchukue mtaji kwa Wakurugenzi, tuingize Serikali Kuu, ili waweze kuchangiwa ile michango yao wapate mafao yao wanayostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia mshahara wa VEO unasikitisha, ni mdogo halafu anakosa mafao yake. Huyu ana watoto wapo Chuo Kikuu, ana mahitaji yanatakiwa katika familia. Kama vipi, Serikali iweke mkakati madhubuti utakaowataka Wakurugenzi haya malimbikizo ya michango wakayalipe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, hawa Watendaji walioondolewa kwenye utumishi kwa sababu walikuwa ni Darasa la Saba, wakarudishwa, wengine mpaka leo hawajalipwa mishahara yao na Mkurugenzi. Naomba na wenyewe waweze kusaidiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu ajira mbadala ambavyo imeathiri upungufu wa walimu katika Halmashauri ya Meatu. Naiomba Serikali inieleze, kwa nini tuliiacha ajira mbadala kurudishia wale watumishi ambao walistaafu, waliofariki na kuacha kazi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalani, katika Wilaya ya Meatu, kwa miaka mitano waliohama; niongelee elimu msingi peke yake ni walimu 165 na walioajiriwa ni walimu 122. Kwa hiyo, kulikuwa kuna tofauti ya walimu 45. Ukiangalia pale haijafidia tu wale waliohama, bado tuna pengo kubwa la watumishi upande wa elimu msingi ambapo mahitaji ni walimu 1,700, na upungufu ni 650. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba basi Serikali, pamoja na inavyoendelea kuajiri, irudishe ile ajira mbadala, kwa sababu tuna pengo kubwa, kwani tunapokua na maendeleo, changamoto huwa zinakuja kutokana na maendeleo. Tuna Shule za Msingi mpya nyingi pamoja na Sekondari ambazo pia zimechangia upungufu wa walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali pia ilifanyie kazi hili. Pia, wale watumishi wanaojitolea ambao hawajaajiriwa, tuliambiwa kwamba tutaletewa mkakati ili wasomeke pia itakapotoka ajira wawe wanatambulika. Tofauti na mwanzo walipokuwa wakiomba, Wakurugenzi wanapeleka watu ambao hata hawajajitolea kwenye yale maeneo husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa miradi mizuri tuliyopewa na TASAF. Tumepewa mabweni Bukundi, Imalaseko tumejengewa Daraja la Mawe zuri, tuna zahanati nzuri Itongo nyumba za watumishi Iramba Ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)