Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi. Awali ya yote, nitumie fursa hii kumpongeza na kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajadili Ofisi ya Rais, Utumishi. Wizara hii kwa mujibu wa sheria, Waziri mwenye dhamana ni Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Yeye tunampongeza kwa sababu tumeona mabadiliko makubwa katika Utumishi wa Umma nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale ambao wanatoka kwenye utumishi kama mimi, tutakumbuka miaka michache tu iliyopita, kila aina ya kada ya Utumishi tulikuwa na wimbi kubwa sana la madai ya watumishi, malimbikizo, madai ya safari za kiutumishi, madai ya uhamisho na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa kipindi kifupi ndani ya utendaji na utekelezaji wa kazi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumeshuhudia kupungua kwa kiasi kikubwa kwa malalamiko ya Watumishi wa Umma. Kwa kweli kwa dhati kabisa tunamshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Simbachawene. Mheshimiwa Waziri kwanza wewe ni darasa, sisi Wabunge hasa wale wachanga wenzangu tumekuwa tukijifunza mambo mengi kupitia kwako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ambalo nataka niliseme leo kwa dhahiri, Mheshimiwa Simbachawene wewe ni mkweli sana. Siyo tu ndani ya Bunge, lakini hata kwenye Vyombo vya Habari tumekushuhudia ukizungumza ukweli na kuwashibisha Watanzania juu ya mambo ya ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Simbachawene tunakushukuru na tunakupongeza sana. Kaka yangu Mheshimiwa Deus wewe ulikuwa Mwenyekiti mwenzangu nafahamu. Wewe ni mtu mwema, kiongozi hodari na uwezo wako hauna mashaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza na kuwashukuru sana Watumishi wote wa Umma nchini kote. Kama kuna Mbunge aliyekuja humu ndani, amemtegemea Mtumishi wa Umma. Kama kuna mwananchi yupo nyumbani anapata maji, anapata umeme, anasafiri kwenye barabara na anapata matibabu anahudumiwa na Mtumishi wa Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza sana Watumishi wa Umma kokote mlipo Tanzania, kazi yenu ni kazi njema, Mwenyezi Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ingelikuwa uamuzi wangu, baada ya mchango wa Mheshimiwa Janejelly na baada ya mchango wa Mheshimiwa Ally Kassinge, nisingesimama kuzungumza. Mheshimiwa Janejelly amezungumza vizuri, kwa ufasaha kuhusu changamoto za Utumishi wa Umma kwa sasa. Mheshimiwa Janejelly amezungumza namna ambavyo Sekretarieti ya Ajira imeamua kukunja mikono na kuacha kazi zake kwa taasisi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianzie hapa. Ajira za Tanzania ni mali ya Watanzania wote, nami inamwelewa sana Mheshimiwa Simbachawene. Aliwahi kuzungumza akasema, hizi ajira ambazo tunatangaza ni chache sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania ambao wanazihitaji ni wengi kupita maelezo, lakini tunatumia vigezo mbalimbali angalau kuwapata wachache wanaohitajika, lakini haina maana kwamba, hao Watanzania ambao hawapati ajira hawana sifa. Namnukuu Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni nini? Watanzania wengi wenye sifa wanatamani kuajiriwa siyo tu kwenye Serikali, hata kwenye mashirika binafsi, lakini ajira zilizopo ni chache. Sasa, ni namna gani Serikali inatoka kwenye lawama? Hakuna namna ambavyo Serikali itatoka kwenye lawama ya ukosefu wa ajira nchini kwa sababu huyu ndio mzazi, mama na baba wa Watanzania ambaye tunategemea alishe Watanzania wote kwa matarajio yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kutoa ajira Serikalini na kuipa taasisi fulani ifanye mchakato wa ajira na usaili, halafu ikwambie hawa ndio wa kuajiriwa, waajiri, hili halipo sawa. Halipo sawa kwa sababu wewe ndio unajua unamhitaji mtumsihi wa namna gani kwenda kufanya shughuli gani? Wewe ndio unajua njaa ya Watanzania kwenye soko la ajira, na mahitaji ya Serikali katika ajira ambazo zimetangazwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uki-hire na ku-outsource ukampa mtu binafsi akaenda kutafuta watumishi akakuletea wewe, hilo ni bomu ambalo mwisho wa siku Watanzania tutapata tabu nalo. Ni lazima kama Serikali tukubali, kama mtoto unayemlea, uliyemzaa mwenyewe hashibi chakula unachompatia, hawezi kwenda kushibishwa kwa jirani. Huwezi kumwambia mjomba wake mlishe huyu labda ataridhika, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kukwepa. Nafahamu tunakwepa pengine upendeleo kwenye ajira na vitu vya namna hiyo, lakini mwisho wa siku mwarobaini wake siyo ku-outsource usaili na udahili wa wanafunzi. Hii siyo sahihi, na haileti picha nzuri kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tuliyoiamini ina vyombo vya ulinzi na usalama na vyombo vya kiutumishi. Tunategemea vyombo hivyo vi-screen viondoe upendeleo na vifanye vetting na viwasaidie Watanzania kupata watumishi wanaotakiwa, siyo abadani kutafuta kampuni na kuikabidhi jukumu la ajira. Hiyo haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo haikubaliki, tunatamani kuona Serikali yetu inafanya jambo hili hasa ukizingatia kwamba jambo la ajira ni jambo la kiusalama. Lazima Serikali yetu ifanye kazi hii kwa mikono yake na siyo kumpatia mtu mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mfumo wa Ajira, sasa watoto wanaitwa kutoka Mara, Tanga, Zanzibar wanakusanywa kwenye Majiji mawili au matatu. Gharama ya huyo mtoto kusafiri na kwenda kuishi haiangaliwi na bado atashindwa kwenda kuingia kwenye usaili, ataambiwa hana sifa. Hii haipo sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwapunguzie gharama hawa watu wanatafuta ajira na wanatoka kwenye kaya masikini. Kwa nini hii mifumo ya ajira wasiende kufanyiwa usaili kwenye maeneo yao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru na kuwapongeza sana TAMISEMI, wameanza kufanya hivyo kwenye Ajira za Ualimu na Afya. Leo nimeona Tangazo la Polisi, nawashukuru na kuwapongeza Mambo ya Ndani wameenda kufanya hivyo, wanafanya screening kule kwenye mikoa wanapotoka wananchi. Suala la kuwaita sehemu moja, hii haipo sawa, tunachochea mambo ambayo hayakubaliki kimsingi na kimaadili ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumzia watumishi haki zao, kwanza, mtumishi anatumia akili ubongo, hatumii nguvu. Anatumia akili, kama ni mwalimu kufundisha, kama ni daktari kufanya matibabu, lakini anatumia zaidi akili. Lazima awe free na ametulia aishi katika mazingira tulivu. Lazima ahudumiwe vizuri na aishi katika mazingira ambayo yanamruhusu kuwekeza muda na maisha yake kwenye utumishi zaidi kuliko kwenye mambo mengine. Je, hili tunalifanya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtumishi wa Umma kuomba uhamisho tu siku hizi imekuwa ni Jihad; mimi nataka kuhama hapa nikahudumie wazazi wangu, wapo sehemu fulani. Namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Simbachawene na mwaka 2023 alisimama, na mwaka 2024 alitoa tamko na waraka kwamba anayeamua kuifuata familia yake aruhusiwe kuifuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni njia ya kuendelea kujenga maadili ya nchi yetu, lakini Mheshimiwa Simbachawene bado wanazuia wale wanaowafuata wake na waume zao, hawapewi uhamisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo lazima tuamue kama kweli tuna dhamira ya kuwasaidia watumishi ili waweze kuwa productive kwenye maisha na maeneo yao ya kazi. Ni lazima tukubaliane kwamba Waraka uliotolewa na Serikali wa kumruhusu mtumishi kumfuata mwenza kwa ajili ya kwenda kukaa kwenye eneo ambalo anaweza kuhudumia familia yake vizuri, liweze kukubaliwa na lichukuliwe ni kipaumbele katika hamisho za watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalize na suala la TASAF. Niliwahi kutembelea Korogwe na niliwahi kusema humu ndani. Nilipita Korogwe nikakuta familia moja masikini sana, babu ana miaka zaidi ya 80, mke wake ana miaka zaidi ya 70. Mke wake ni mgonjwa, dhaifu na bahati mbaya hawakuwahi kupata mtoto na hawana ndugu, wanaishi pale Korogwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, with time nikaja hapa nikaomba, jamani zipo kaya ambazo mnasema zime-graduate. Kaka yangu Mheshimiwa Shangazi amesema asubuhi, wana-graduate, lakini hawapewi vyeti. Zina-graduate lakini bado ni masikini wa kupindukia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikaomba, jamani hebu fanyeni uchunguzi, zile kaya ambazo bado ni masikini ziendelee kusaidiwa kupitia Mpango wa TASAF, ili waweze kunusuru maisha yao. Nataka nikwambie, baada ya miezi sita yule mama alifariki kwa njaa, matatizo na shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana wananchi wa Korogwe, walikuwa wanachanga, kila mwanamke alikuwa anatoa chakula kupelekea ile kaya, lakini watu wa TASAF walikiri walisema, ame-graduate, hastahili tena kuhudumiwa na TASAF. Hii siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuangalie hao wanaoambiwa wame-graduate wana-graduate kwa mtindo gani, na katika mazingira yapi, kwa nia ipi? Nadhani kama tunaelekea mwisho wa huu Mfuko wa TASAF, lakini tunapoenda kuanza mfuko mwingine lazima tuangalie haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, hii habari ya ku-graduate tuangalie tuone, kama ina tija kwa wananchi ama haina tija kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ile habari ya kuwafanyisha kazi eti ni Mradi wa TASAF, sioni kama ina tija kwa sababu wengi wanaokwenda kutumika kwenye hizo kazi ni wazee na watu wazima ambao hawana uwezo wa kufanya hizo kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi hii, na ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)