Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Urambo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi nami nichangie hoja iliyoko Mezani. Kwanza, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Pili, ninawashukuru wananchi wa Urambo na familia yangu kwa ushirikiano wao wanaonipatia. Pia, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo amenisaidia miradi mingi ya maji, umeme, barabara, na afya mingi mno kiasi ambacho wananchi wa Urambo nao wanasema ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, nichukue nafasi hii kuipongeza Wizara husika na Waziri husika Mheshimiwa Simbachawene, Naibu wake, Makatibu Wakuu na Watendaji wote kwa kazi kubwa wanayoifanya. Hongereni sana kwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nitoe kwanza kifupi yale nitakayozungumzia angalau wayapate, ili hata kama muda utaisha, basi wawe wameyapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, nitazungumzia suala la umuhimu wa TSC (Teachers Service Commission) ambayo iliundwa kwa madhumuni ya kuhudumia walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nitazungumzia umuhimu wa Serikali kurekebisha mishahara ya walimu na wafanyakazi kwa ujumla wanaopandishwa madaraja kabla hawajastaafu, ili kuwawezesha kupata haki zao, kuliko ilivyo sasa ambao wengi kwa mfano wa kwangu wapo 52 ambao hawakurekebishiwa mishahara yao na sasa hivi wanapata shida kupata haki zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, nitazungumzia kuhusu Watendaji wa Kata na Vijiji. Nianze kwa Kata ambao wanaomba posho yao iongezwe kidogo kutokana na kazi kubwa wanazozifanya, na pia zitoke moja kwa moja Serikali Kuu. Pia, wanaomba Watendaji wa Vijiji na wao wafikiriwe kupata posho, ili iwawezeshe kufanya kazi zao; na mwishoni nitazungumzia umuhimu wa TASAF kama walivyozungumza wenzangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana wote waliotangulia kuongea. Wote wameongea vizuri sana kuhusu umuhimu wa kuangalia haki za wafanyakazi. Hongereni wote mlioongea kuhusu umuhimu wa kuangalia haki za wafanyakazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nitaanza na walimu. Kwa muda mrefu suala la TSC – Teachers Service Commission limezungumziwa, nikiwepo mimi mwenyewe humu Bungeni. Kama walivyoongea wenzangu, Mheshimiwa Mwalimu Ally kule, Mheshimiwa Husna na wengine wote ambao wamezungumzia, walimu ni wengi mno. Nilikuwa ninaangalia idadi yao, wanapata kama 294,402 kwa hesabu niliyoipata. Kuwahudumia hawa watu ilionesha tangu mwanzo kwamba ni kazi kubwa sana kuhakikisha kwamba msawazisho unakwenda vizuri, yaani wote wanakwenda vizuri kwa idadi inayotakiwa katika maeneo mbalimbali, na kuwapatia haki zao kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini ndiyo maana Serikali ikaona kuna umuhimu wa kuwa na chombo kimoja ambacho kitawaangalia hawa kwa ukaribu. Ndiyo maana wa kutunga sheria hii ambayo ninayo hapa, ambayo imewapa TSC majukumu kutokana na ukubwa wao wa kazi waliyopewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaambiwa kwanza ninyi mta-appoint, mta-promote na mta-discipline teachers. Pia, wanaambiwa kwamba mtaangalia distribution of teachers. Halafu pia wanaambiwa ninyi mta-supervise teachers in service training programmes, lakini pia wanaambiwa wata-conduct research na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi ukiangalia eneo hili la (c) la sheria yake kwenye functions, wanasema appoint, promote. Mimi ninaamini Serikali iliiona hii, kwamba kuhudumia hao watu wengi siyo rahisi, kuwe na chombo maalum. Sasa, nataka niiulize Serikali je, malengo yaliyowekwa yameonekana hayafai au kuna haja ya kubadilisha? Kwa sababu kinachoendelea sasa hivi sicho kilichokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali waiangalie hii sheria upya. Je, inajibu matakwa yaliyotakiwa wakati huo? Kama haijibu, basi iangaliwe upya, lakini kuwe na sheria ambayo inaeleza wazi kabisa. Halafu kinachoendelea siyo, ukiangalia hizo TSC hasa kwenye ngazi za Wilaya, wanatakiwa watendaji kazi wanne, lakini sehemu nyingi yupo mmoja na wakiongezewa Mkurugenzi anawaazima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha wanazopata ni ndogo mno, hawawezi kufanya. Hawana usafiri, hawaingizwi kwenye system ya e-Wafanyakazi (e-Employees), ule Mfumo wa e-Wafanyakazi hawamo. Sasa, ndiyo maana hata utaona kwamba, kama walivyoongea wenzangu waliotangulia, zilipokuja hizi ajira za walimu TSC hawakuhusika kabisa, lakini wao kwa sheria hii ndiyo wameambiwa ku-appoint, ku-promote na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ombi langu la kwanza, sheria iangaliwe upya. Kwa heshima na taadhima, naomba sheria iangaliwe upya ili kama kweli ilikusudiwa, basi ifanyiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumza mwenzangu hapa, kwamba mwalimu anataka kuhama, anaambiwa wewe weka tangazo. Tangazo mtu aombe yuko Rukwa, huko amtafute Mwalimu mwingine wa Urambo anayetaka kuhama. Ni vitu ambavyo haviwezekani. Ndiyo maana walikuja na sheria hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba, narudia tena, sheria hii iangaliwe ili kweli malengo yaliyokuwepo kama bado yapo, yafanyiwe kazi, sheria hii ifanye kazi kama ilivyokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa sehemu nyingi kama nilivyosema, kazi walizonazo kutokana na sheria wamepunguziwa kabisa, kwa hiyo, naomba TSC ingaliwe upya kwa heshima na taadhima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nazungumzia suala la wafanyakazi wanaokaribia kustaafu. Naiomba Serikali iwaone wale ambao wanastahili kupandishwa madaraja, wapandishiwe madaraja yao, warekebishiwe mishahara. Mimi nina orodha ya walimu, wamechanganyika na watu wa afya pia. Ninao 52, ukitaka niwaweza kutoa hapa nikawapa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, 52 ambao mpaka sasa hivi wanahangaika, wanadaiwa na PSSSF. Walipe fedha wao ndiyo waweze kupata pensheni. Kwa hiyo, wanakwenda kukopa, ninayo orodha hapa. Wanakwenda kukopa ili wapeleke PSSSF ili waweze kupata pensheni yao. Ni haki hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali itaweka utaratibu wa watu kurekebishiwa mishahara kabla hawajastaafu, kwa kweli wapewe haki zao kama wanavyostahili. Kama nilivyosema, hapa sasa siyo walimu tu, hata na wafanyakazi wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nilitaka kulizungumzia ni Watendaji wa Kata. Wanaomba, kutokana na kazi zao walizopewa, wanaomba waongezewe posho kidogo ili waweze kufanya kazi yao; posho ya madaraka ili waweze kufanya kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, wanaiomba Serikali kwamba fedha hizi zitoke Serikali Kuu moja kwa moja ili kuondoa usumbufu wanaoupata. Pia, Watendaji wa Vijiji nao pia wanaomba waangaliwe kupata posho kidogo ya madaraka ili iweze kuwasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nilitaka kuzungumzia ni suala la TASAF. Kama alivyoongoea mwenzangu, TASAF ilipoundwa, tunaishukuru sana Serikali yetu ya Tanzania, TASAF ilivyoundwa ilikuwa ni kuwasaidia wale wasiokuwa na uwezo. Sasa, itakuwaje mtu anaambiwa, eti tayari ameshakomaa au ame-qualify, wakati unamwona kabisa ni mzee ambaye hawezi kufanya chochote?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ombi langu kwa Serikali, Serikali iongeze fedha TASAF kwa ajili ya watu wanaopata misaada ya TASAF ili wanapoingiza wengine, kusiwe na haja ya kuwatoa wale wengine ambao wanasema wamekomaa au nini. Ukiwaona wanaoambiwa wamekomaa, hawajakomaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba tu fedha ziongezwe kwa heshima na taadhima kabisa ili wale wazee waliokuwa wanapata waendelee kupata, halafu wapya waweze kuingizwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo, narudia kusema TSC iangaliwe upya, ahsanteni sana. (Makofi)