Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nianze moja kwa moja kwa kumpongeza Waziri Simbachawene pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri mnayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, simsifii Mheshimiwa Simbachawene kwa sababu tu nimemwona, ila niseme ni Waziri anayefikika, Waziri msikivu, halafu anatekeleza. Licha ya kwamba ni Senior, hata sisi Form One tunamkaribia, yaani tunaweza kueleza shida. Kwa hiyo, aendelee hivyo. Leo nimepata nafasi ya kuona hata viongozi wengine anaowaongoza kwenye Wizara hapo nje, yaani ukiwaangalia tu wana furaha, inaonekana ni jinsi gani anafanya kazi vizuri na hao viongozi wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza moja kwa moja na yale ambayo wenzangu wameyazungumza kuhusu ajira zile za TRA. Kama alivyosema Mheshimiwa Janejelly, Mheshimiwa Husna, hizi ajira zimeleta maneno huko nje, zimeleta maneno kwa sababu kila mtu alishangaa. Hawa NBAA wanakuwa na nguvu gani ya kuwanyang’anya ninyi kazi yenu mnayotakiwa kuifanya? Ilikuwaje wao ndio wakafanya hiyo interview na siyo Sekretarieti ya Ajira? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna malalamiko mengi, wale waliotoka mbali wanafika pale kwenye chumba wanawaambia, jina lako halipo. Hebu fikiria mtoto ametoka Ukerewe. Kwa hiyo, hili jambo limekuwa baya kiasi kwamba nimeona nishauri ikafanywe review ya kilichotokea na ikiwezekana kuwaondoa kabisa hao. Taasisi nyingine zisifanye hizi interview, badala yake Sekretarieti ya Ajira ndiyo ifanye hiyo kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu nimeshangaa Mheshimiwa Simbachawene, jambo limekwenda, wamekaa kimya, yaani wamewanyanyasa au imekuwaje? Nimeshangaa sana. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Omari.
TAARIFA
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kumpa taarifa mchangiaji. Kwanza wafahamu nini maana ya NBAA. NBAA ni National Board of Accountancy and Auditors. Ni Bodi ambayo inasimamia Wahasibu na Wakaguzi, pamoja na mambo ya kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiutaratibu wenzetu wa TRA, kimsingi nadhani hawakufanya kosa kuwakabidhi NBAA kwa sababu inaweza ikafanyika katika taasisi nyingine zozote zile. Kwa hiyo, tusije tukaikosea Bodi ya NBAA kwa kuiona kwamba ni taasisi ambayo haiwezi kusimamia kazi hii, ahsante. (Makofi)
MWENYEKITI: Ninadhani Mheshimiwa Mbunge alimaanisha competency ya suala la kuajiri. Competent entity katika context hii ni Sekretarieti ya Ajira. (Makofi)
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Ntara, unapokea taarifa?
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei. Halafu hata amenipotezea muda wangu. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwani ile Sekretarieti, nchi inachagua Sekretarieti ya Ajira, ina maana wale mle ndani wote ni mambumbumbu? Mle ndani wanazo taaluma zote, ndiyo maana wanaweza wakafanya usaili. Watu wamechaguliwa Sekretarieti ya Ajira, wewe unafikiri wale ni vilaza? Wale wanaweza kuajiri au kufanya interview katika sekta zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekretarieti ya Ajira ni combination ya watu wenye utaalamu. Hilo tusilikwepe, Mheshimiwa Waziri Simbachawene, nendeni mkafanye review, chukueni madaraka yenu, simamieni utaratibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kulizungumzia leo ni hili la kuhusu shughuli za vyuo vikuu. Mheshimiwa Waziri, unajua nilisema vyuo vikuu vinatakiwa vijitegemee. Kazi ni kubwa, viwe huru katika taaluma. Wizara ya Elimu inaweza kuingilia tu kwenye mambo ya sera, labda na kuviwezesha, lakini kwenye taaluma tuviache vyuo vikuu viwe huru. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nasema hivyo? Tuliongea wakati ule, tumeongea mwaka jana, 2024 kwamba hakuna Wahadhiri, wamepungua sana, Maprofesa ndio usiseme. Vyuo vikuu vikiachwa huru vinaweza vikaajiri. Leo hii wanafanya interview, wale Tutorial Assistants, wakishafanikiwa, majina yanapelekwa Utumishi, eti ndiyo wapate ajira. Jamani, tunaua kabisa value ya chuo kikuu. Wale wanatakiwa wafanye interview wenyewe, waajiri kama tulivyoajiriwa sisi wengine tulivyobaki pale kwenye vyuo vikuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wao wanaweza wakajua huyu Mhadhiri ana miaka 61, ana miaka 65, anaweza kuendelea kufundisha, wao ndiyo waamue. Usiwapangie eti Mhadhiri vyuo vikuu miaka 65 aondoke. Hivi mimi hapa mnafikiri siwezi kufundisha? Nina miaka 65. Leo Prof. Ishumi bado anafanya kazi, Prof. Rwekaza Mukandala bado anafanya kazi chuo kikuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe wakati nasoma Ph.D, aliyenisimamia ni Profesa aliyekuwa na miaka 80. Hawa watu hapa kichwani huwa zinafanya kazi. Bado zinafanya kazi, kwa hiyo, tukifanya hivyo vyuo vikuu havitakuwa na shida ya Wahadhiri wala Maprofesa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wanashindwa kuchukua Maprofesa kutoka nje ya nchi. Nawaambia, ukienda kwenye vyuo vyetu vikuu, yaani vimekuwa ni local Universities. Sijui niziite local school, I don’t know, kwa sababu, unakuta pale chuoni Mhadhiri Prof. Komba, Prof. Haule, na hawa Wapare wanaitwaje?
MBUNGE FULANI: Mbaga.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Prof. Mbaga, Prof. Mosha. Tunataka mchanganyiko. Wapewe uwezo wa kuleta Maprofesa kutoka nje ya nchi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaambia ukweli, tusilichukulie mzaha hili jambo. Yaani nakwambia, vyuo vikuu hadhi yake inashuka, I am telling you. Tuwaache, tuwaache wafanye interview pale, waajiri Assistant Lecturers, waajiri Professors kutoka nje ya nchi. Ndiyo maana ya University, lakini ukichukua walimu wote wametoka Tanzania, hiyo university, hilo neno halipo tena. Tuwaache! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mnawawekea umri wa kustaafu, waacheni. Nimesema waacheni, wao wanajua huyu Prof. Shumi anapiga kazi. Leo Prof. Ndalichako ataweza kwenda kuendelea kufanya kazi chuo kikuu! Sasa, huyo amefikisha miaka 65, eti mnampa mikataba. Nasema freedom ndani ya university iendelee. Hilo nitalisema, hii ni mara yangu ya nne ninalizungumza hilo. Tuwaache! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua wale ni watu wa kujitegemea kabisa, wanayo mabaraza yao, yaani ile ni Serikali inayojitegemea ya chuo kikuu. Wanayo mabaraza yao. Pale, kuna Baraza, kuna Senate, kuna vikao, leo ninyi mnaenda kuwatawala tawala, unawaambia hapa hapana, unasema huyu ana miaka 70; jamani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Prof. Ndakidemi pale, amesema kwa mfano akitoka hapa anaenda kufundisha. Bado anafundisha chuo kikuu. Hili leo nimelisema kwa sauti, na Waziri Mkuu yuko hapo. Nililizungumza mbele yake na leo Wizara ya Utumishi, hebu naomba wafanyeni hawa kuwe na autonomy ndani ya university. Tukifanya hivyo, nakwambia universities zetu zitaonekana kabisa zina value. Otherwise, we are killing this area of university. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kwa ubora wake, kuna hili suala la maadili. Suala la maadili nalisema kwa sababu gani? Ndiyo tulitunga sheria. Tunaangalia maadili kwa watumishi wa umma. Hapa nikifanya jambo ovyo ovyo tu, nenda unaitwa ofisi ya maadili, lakini kuna hizo private sector, hivi hamuwezi kubadiliasha hizi sheria?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna private areas ambapo watu maadili ni ya ovyo. Leo tumesikia jambo moja la mtu sijui anaitwa Mwijaku, sijui Mwanjaku huko, amekwenda amechezea wanafunzi katika vyuo vikuu. Sasa hayo maadili yanakwenda wapi? Polisi watamchukua, na ninyi wa maadili je? Yaani nimeona hivi vitu tuviangalie. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Maadili Mzee Mwangesi apige kote, hebu angalieni kama mnaweza kubadilishabadilisha kanuni hapo. Kama wote ni Watanzania, wanaharibu mambo, maadili ya ovyo, lakini mtumishi wa umma anapelekwa kwenye maadili; huyu wa private sector anayefanya vitu vya ovyo katika hii jamii, lini atapelekwa kwenye maadili? Hili mlichukue na mkalifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, naomba sana, kama kuna kiongozi wa TASAF hapo, nafikiri yupo. Wanafunzi wa vyuo vikuu wanaokuwa na shida sana ya fedha ili waweze kulipa ada, Mheshimiwa Waziri mlolongo unakuwa ni mrefu kiasi kwamba mpaka waje wapate sijui hiyo idhini ya hela, tayari wenzao kule wameshasoma. Naomba unikutanishe na huyo bosi wa TASAF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ndio mwakilishi wa vyuo vikuu jamani, na ninataka nirudi hapa. Naomba mnikutanishe na kiongozi wa TASAF tuone namna gani tutasaidia wanafunzi wa vyuo vikuu. Kama wanahitaji msaada wa fedha za TASAF, wapate mara moja. Akisema Mwakilishi wa Vyuo Vikuu kwamba huyu ana shida, kwa nini msimwamini? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani mimi naweza kumchukua tu mtoto nikasema huyu ni maskini, wakati kweli sio maskini! Naomba kwa hilo tena mlifanyie kazi. (Makofi)
(Hapa, kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Muda umeisha?
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, muda wako umeisha. (Makofi)
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)