Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii adhimu kwa ajili ya kuchangia katika Wizara hii muhimu na katika bajeti yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya katika kuiongoza nchi hii. Tunampongeza kwenye maeneo matatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ni kuiongoza nchi kwa amani na utulivu na mshikamano mkubwa. Amefanya vizuri sana kwenye hili eneo. Eneo la pili, kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kila mahali, kila kona, kila Mkoa, kila Wilaya, mpaka kwenye vijiji ametekeleza miradi mingi sana. Tunampongeza sana kwa kazi nzuri ambayo ameifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu, amekuwa kinara wa kutafuta vyanzo vya fedha ambazo zimesaidia sana katika kutekeleza hii miradi mingi hii ambayo imefanyika. Kwa hiyo, tunampongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapompongeza Mheshimiwa Rais, maana yake tunawapongeza na wasaidizi wake wote. Hao ndio wamefanya kazi na mafanikio haya. Bila wao kufanya kazi vizuri, mafanikio haya yasingekuwepo. Kwa hiyo, tunazipongeza taasisi zote zilizoko chini ya Ofisi ya Rais kwa kazi nzuri ambayo zimekuwa zikifanywa. Hongereni sana kwa kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Waziri Simbachawene, mnyenyekevu, mwadilifu, mtu mwenye hekima, anafanya kazi nzuri sana na anajituma vizuri sana. Kama hiyo haitoshi, yuko Naibu wake, Mheshimiwa Sangu, anafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani kwa hivi wanavyofanya kazi pamoja, basi wananchi wa kwenye maeneo yao watawarudisha tena awamu nyingine, waendelee kuongoza na waendelee kukalia hivi viti kuwa Wabunge. (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa za Utumishi wa Umma na Utawala Bora zimeshaelezwa, lakini mimi nataka niseme kazi kubwa ambayo wamefanya ni kuhakikisha kuwa, utumishi wa umma unafanya kazi, unatekeleza majukumu yao kwa weledi, kwa maarifa na kwa uadilifu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo kazi wameitekeleza vizuri sana kwa kweli. Wameitekeleza na kuhakikisha kwamba, wakati wa kutekeleza haya majukumu sheria, kanuni, taratibu na miongozo inazingatiwa ipasavyo. Kwa kweli, kwa hili tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo wamelifanya vizuri ni kusimamia utendaji kazi wa Watumishi wa Umma pamoja na masilahi yao. Tulikuwa na changamoto ya masilahi ya Watumishi wa Umma kwa kipindi kadhaa hapo, lakini sasa hivi kwa kiwango kikubwa wameshughulikia sana masilahi ya Watumishi wa Umma japo haijafikia kiwango tunachotamani kufika, lakini wamejitahidi sana kwa uwezo wa nchi yetu tulipofika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Watumishi wa Umma kwa kweli wamezingatia sana kupandisha mishahara, wamezingatia sana madaraja na maeneo mengine na bado tunahitaji zaidi kujiongeza, kufanya zaidi, ili Watumishi wa Umma wawe na afya njema, waweze kufanya kazi kwa weledi, vizuri zaidi. (Makofi).

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni kusimamia utoaji wa vibali vya ajira, na pia kusimamia ajira mbalimbali. Kwa hapa naomba nijikite kidogo kwenye eneo hili. Kazi ya kutoa vibali ni nzuri sana, ili tujue size ya utumishi wa umma, hicho ni kitu kizuri sana, lakini kuhakikisha kwamba, tunapata watu wanaostahili kuajiriwa katika nafasi mbalimbali, hiyo ni kazi nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kazi hii baada ya kupata uzoefu ndiyo maana tulianzisha Sekretarieti ya Ajira Serikalini. Hii sekretarieti imefanya kazi nzuri, lakini hapa mwishoni kumeanza kuwa na kutetereka na tunaona kabisa sasa baadhi ya maeneo hawatumii Sekretarieti ya Ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani tunapotaka kwenda sasa tunataka turudi tulipokataa na tulipotoka. Kwa hiyo, ni vizuri Sekretarieti ya Ajira tukaiwezesha kwa rasilimali, kwa vitendea kazi na kwa uwezo, ili iendelee kutoa ajira kwa watu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni muhimu, sasa hivi changamoto iliyo kubwa ni baadhi ya vijana wanaitwa kwenye interview, wanatoka Mbozi, wanatoka Vwawa, wanatoka Songea, wanatoka Kagera, kuja kufanya interview hapa Dodoma. Hii hapana, hatukubaliani nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotakiwa ni kwamba, hii Sekretarieti ya Ajira iweke utaratibu hawa vijana waitwe kwenye interview, wafanye kwenye mikoa yao kule walipo. Wekeni utaratibu, na hilo linawezekana. Sasa hivi kwa dunia ilipofika kwa Sayansi na teknolojia hatuhitaji vijana wasafiri umbali mrefu kutoka huko waje huku kwa ajili ya kuja kufanya interview halafu asifanikiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wafanye kwenye mikoa ile. Kila mahali uwekwe utaratibu mzuri, iwezesheni Sekretarieti wafanye kazi nzuri. Nina imani kabisa matatizo yatapungua na tutaondoa hizi changamoto ambazo tunazipata sasa hivi. Kwa hiyo, Sekretarieti ya Ajira ni muhimu sana tukaifanyia mabadiliko, tukaiongezea uwezo ili iweze kutekeleza hayo majukumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka miaka ya nyuma Wizara ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora tulitekeleza mabadiliko makubwa kwenye Utumishi wa Umma (Public Service Reform Program) na tulikuwa na mabadiliko mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na Local Government Reform Program, Public Service Reform Program, Legal Reform Program na maeneo mengine kulikuwa na mabadiliko mengi ambayo tuliyafanya, lakini mimi nataka nijikite kwenye eneo moja kwamba, baada ya zile reforms kutekelezwa, tumetekeleza tumefika. Je, tumewahi kufanya tathmini? Tukaangalia success stories za ile reforms na wapi tumekwama, ili tuweze kuboresha, tuweze kufanya vizuri zaidi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili kwa kweli naona kama bado hatujalifanyia kazi. Tunahitaji kulifanyia utafiti, mafanikio ya Public Service Reform Program, tunahitaji kufanya utafiti tuangalie Local Government Reforms Program kama imekidhi yale mahitaji tuliyokuwanayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya mambo tuliyokuwa tunayatarajia kwenye reforms program ilikuwa ni kuwa na mikataba ya kazi, siyo mikataba ya ajira, mikataba ya kazi (OPRAS).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwepo na OPRAS, ambapo tuliamini mfanyakazi anapofanya kazi awe na malengo ya kazi na mwisho wa mwaka tumpime kwa malengo yake. Akiwa amefanya vizuri maana yake apandishwe cheo hata mara mbili hata mara tatu kwa sababu, anakuwa amefikia malengo, lakini hilo limekufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunazungumzia watu kupandishwa hata bila ya kujali kwamba amechangia vipi katika uzalishaji, amefanya vipi katika utendaji wake wa kazi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili nadhani kuna haja ya kuliangalia vizuri ili tuhakikishe watumishi wa umma wanapanda kwa vigezo vya utendaji kazi. Kwa hiyo, OPRAS ambayo mnayo sasa hivi, hii ya mfumo, sijui kama mnaisimamia na kuhakikisha kwamba, mmei-link na performance pamoja na pay, ili kusudi waweze kupata masilahi vizuri. Sijui, lakini naamini kwamba, ile OPRAS ni kitu muhimu sana na itatusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sanjari na hilo, kwenye OPRAS tuna mashirika ya umma mengi, tuna taasisi za umma nyingi. Tuna idara zinazojitegemea, na tuna wakala. Lengo la mabadiliko ya wakala ilikuwa ni kwamba, zile zilikuwa ni idara za Serikali, baadaye zikue zianze kujitegemea ziwe mamlaka zinazojitegemea, lakini hadi tumeanzisha mpaka leo sijui kama mmeshafanya tathmini kuangalia ni wakala zipi zimefanya vizuri sasa zihame kutoka kuwa wakala ziende kuwa mamlaka zinazojitegemea, ili zipunguze kutegemea mapato au mishahara kutoka Serikalini. Hizi wakala zinatakiwa zijitegemee, zizalishe, hiyo ndiyo itatusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kumekuwa na wimbi kubwa la taasisi nyingi za umma kukimbilia kuingiza mishahara. Wanaenda kwenye Utumishi wa Umma, wote wanataka mishahara. Tutafika mahali tutashindwa kulipa mishahara kwa Watumishi wa Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mashirika yenye uwezo wa kuzalisha kibiashara tuyaache yazalishe kibiashara, yalipe wafanyakazi wao na faida wachangie kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Hapo ndiyo tutapata mapato, lakini siyo watu wameshindwa ku-perform mnawarudisha kwenye Serikali Kuu wanaanza kupata mishahara, hapana. Wazalishe kwanza, wakishazalisha ziada walete kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, itatusaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mkiliangalia hilo suala la wakala, suala la mashirika ya umma, yale yanayoweza kujiendesha kibiashara yajiendeshe kibiashara. Tutapunguza hizi hasara na mwisho, msaini mikataba ya utendaji kati ya taasisi na taasisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi ikishindwa kufikia yale malengo, hatua za kinidhamu zichukuliwe. Huo ndiyo utawala bora, na huo ndiyo uwajibikaji. Uwajibikaji ni muhimu. Hatuwezi kuendelea kwamba, eti watu wamefanya kazi, mambo hayajaenda, tuache, hapana. Lazima tuchukue hatua, hapo ndiyo tutaweza kufanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo nataka kulipendekeza ni mafunzo kwa Watumishi wa Umma. Nchi yoyote duniani inategemea Utumishi wa Umma. Mtumishi wa Umma unatakiwa uwe na weledi, uwe na maarifa, uwe na uwezo wa kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtumishi wa Umma anachofundishwa chuoni ni tofauti na kinachokuwepo kule kazini, ndiyo maana lazima anapoingia kwenye Public Service anatakiwa afundishwe Maadili ya Utumishi wa Umma, afundishwe namna ya kufanya kazi za Utumishi wa Umma, afundishwe namna na mienendo, namna ya kupanda, kila kitu kinachotakiwa kufanyika ndani ya Utumishi wa Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zilizofanikiwa, ukiangalia nchi kama Singapore, Mtumishi wa Umma anaenda kwenye mafunzo masaa 102 kwa mwaka, nchi kama India anaenda mafunzo karibu masaa 200 kwa mwaka, nchi kama China wana utaratibu huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nyingi zilizoendelea Watumishi wa Umma lazima waende ku-recharge brain, waende kusoma, waongeze ujuzi na maarifa ndipo kunakuwa na mabadiliko makubwa ya utendaji kazi katika Utumishi wa Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi hapa watu wengi wamebakizwa hawafanyi hiyo kazi. Chuo cha Utumishi wa Umma, Chuo cha Uongozi, kilitakiwa kipewe hiyo kazi; kilipewa hiyo kazi, lakini kimsingi bado hiyo kazi hawajaifanya inavyotakiwa. Tukifanya hivyo, Watumishi wa Umma watakuwa na weledi, watawajibika, watakuwa na maadili, wataweza kuchangia na kufanya kazi inayostahili na hapo ndipo tutaweza kufikia malengo tunayotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja, bajeti hizi zipite, Mheshimiwa Rais akafanye kazi vizuri, taasisi zake ziendelee kuchapa kazi, Mawaziri mkachape kazi. Mungu awabariki, ahsanteni sana. (Makofi)