Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Yustina Arcadius Rahhi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia bajeti ya Wizara hii ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora. Hata mimi nampongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wake. Kusema ukweli, kipindi hiki ameweza kuweka mifumo mizuri ambayo watumishi wa umma wanaweza kufanya utendaji mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawapongeza sana, lakini vilevile nampongeza sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa sana aliyoifanya katika kipindi hiki na hasa kupeleka fedha nyingi kwa wananchi kwenye majimbo yote, hususan kwenye kata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata katika Wizara hii tunaona maono ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuweza kusaidia maono ya vijana, ambapo kuna changamoto kubwa sana ya ajira. Kwa hiyo, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameliona hili kwa vijana wake na ndiyo maana ameweza kujenga fursa nyingi za ajira kupitia Wizara hii. Nampongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake ameweza kutoa ajira rasmi zaidi ya 149,000, hongera sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na vilevile amejenga fursa nyingi za ajira nje ya mfumo rasmi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, alivyoweza kupeleka fedha nyingi za miradi ya ujenzi kule kwenye kata na kule kwenye majimbo, hii imejenga fursa kwa sababu, kuna vijana, kule kuna local artisans wameweza kufanya kazi ya ujenzi. Kwa hiyo, hii imekuwa ni fursa ya ajira. Pia kule kuna akina mama ntilie, nakuna wazabuni ambao wameweza kupeleka vifaa. Hii bado ni ajira, nampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maono yake pia, kuendelea kuwekeza katika viwanda, hii ni sehemu ambayo inaweza ika-accommodate hii nguvukazi kubwa sana, ambapo tunajua kwa Watanzania ukiangalia demography ya idadi ya watu, Tanzania zaidi ya nusu ni vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna kila sababu ya kuangalia hii changamoto kubwa ya ajira kwa vijana, lakini uwekezaji pia alioweza kuufanya kwenye kilimo, kilimo kimekuwa kinavutia kwa vijana. Kwa bahati nzuri sana, sasa vijana angalau wamepata ajira, wanazalisha mbogamboga na wananenepesha mifugo kupitia BBT. Hongera sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, vijana wa Tanzania wanakuangalia na vijana wa Tanzania wana changamoto kubwa sana ya ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu vilevile ni juu ya Sekretarieti ya Ajira, nawapongeza sana. Kuna mambo mengi sana tumeshauri kwa Sekretarieti ya Ajira na kwa bahati nzuri wamesikia japokuwa kuna changamoto ndogo ndogo bado zipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kusogea kufanya usaili kwenye mikoa, mimi nawapongeza sana, mnawasaidia wale vijana ambao uwezo wao wa kuja kuwa-centralize, kuja kwenye usaili ni mdogo. Sasa tunapowafuata mikoani kule, kwa kweli, tunawasaidia sana, lakini changamoto ni kwamba, wanadahiliwa vijana wengi sana kuliko ambavyo ikama inahitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, wanaotakiwa labda ni vijana 50, labda idara fulani inahitaji vijana 50, halafu unawaita kwenye usaili watu zaidi ya 2,000 au 4,000, halafu ilivyo sasa hivi unawaita kwenye mitihani (interview), wanaanza written day one, baadaye unafanya selection unawapeleka kwenye oral. Ile written wanafanya the same day; wanafanya leo mchana, baadaye unamwambia selected, ili aingie oral kesho yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi hawa 2,000 au 4,000, kweli kuna uhalali upi kwamba umeweza kupitia makaratasi yote haya, ili uone kwamba umemtendea haki? Umemsaili, amesogea sasa kwenda kwenye oral? Ni kwa nini pengine hata isifanyike screening? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii tumeshashauri tu kwamba, kwenye screening tuangalie waliohitimu muda wa nyuma zaidi. Kwa mfano, kuna wahitimu wamemaliza vyuo tangu 2017, 2018, 2019, unamwita siku moja kwenye usaili pamoja na yule aliyemaliza mwaka wa 2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yule ambaye ameshakaa miaka 10 uraiani, anayejua bodaboda yake, anayejua alikuwa kwenye kilimo chake, anayejua alikuwa kwenye mifugo yake, namna gani anaweza aka-compete pengine na huyo ambaye amemaliza mwaka jana, 2024!

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu bad enough, una m-select yule aliyemaliza mwaka 2024 na yule ambaye ana miaka kumi huku nyuma unamwacha. Ni vizuri sana tukafanya screening kuliko kuendelea kuwasumbua na wengine wamejitolea na taarifa zao zipo. Nafikiri tuendelee kutenda haki, lakini kwa kweli, imeleta mwanga na matumaini kwa vijana wa wakulima vijijini kwa jinsi usaili huu ulivyoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo ni gumu sana, baada ya kupelekwa kwenye oral, ni nani anatakiwa kupeleka majibu kwamba, sasa huyu ameajiriwa au hajaajiriwa kwa sababu, jambo gumu zaidi ambalo vijana wanaendelea kutusumbua, hizi barua za ajira zinaendelea kutolewa kama kijiko. Unakaa wiki moja, wameajiriwa sijui vijana wangapi, unaendelea wiki ya pili wameajiriwa wengine, mwezi huu wameajiriwa hawa, mwezi ujao wameajiriwa hawa. Wale wengine wanaendelea kuwa na matumaini wakisubiri barua, pengine ajira hakuna na wanaendelea kutusumbua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, Mheshimiwa Waziri upo hapa, hiyo intake ambayo mmeshaifanyia usaili, wapate barua kwa kipindi kimoja na majina yatolewe kwenye mtandao wote, ili wale vijana kule sasa wapate amani, wajue kwamba, yupo kwenye ajira, au hayupo kwenye ajira. Vinginevyo, tunaendelea kuwaweka kwenye tension isiyo na sababu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliseme hili la TRA ambalo nami limenisikitisha vibaya sana. Kuna vishoka huko mitaani, kitu kinachosikitisha, wanajifanya wanawajua watu wa hii bodi ambayo imeteuliwa, ambayo kazi imekuwa outsourced, wanawaibia vijana huko. Ujue kwamba ajira ni changamoto, wanapita kwa vijana wanachukua shilingi laki tano, au milioni, milioni tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo ni baya sana. Angalau Sekretarieti ya Ajira sasa hivi tumeona kabisa matumaini makubwa kwamba wanatenda haki na wanaenda vizuri. Mimi nafikiri huu mfumo, Mheshimiwa Waziri atakuwa ameshauelewa, maana Serikali hii ni sikivu. Hii ajira ya TRA ni changamoto, vijana wanaibiwa, vijana wamekuwa stressed. Kwa vyovyote vile, tumeomba na tunaomba Waziri alishikilie hili, lirudi katika Sekretarieti ya Ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine ni kuhusu stahiki za watumishi. Watumishi hawa wachache wanatakiwa kuwahudumia Watanzania walio wengi na wawahudumie wakiwa na utulivu, wawahudumie wakiwa na morali ya kazi. Ukim-frustrate Mtumishi wa Umma ujue huduma inayotolewa kwa wananchi pia haitakuwa bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, suala la kupandisha cheo ni stahiki na ni haki. Muundo wa Utumishi unataka kila baada ya miaka mitatu Mtumishi wa Umma apande cheo daraja moja, lakini mtumishi hujamwonya, hujamfukuza kazi, hajaomba likizo bila mshahara, anakaa zaidi ya miaka sita, mingapi, humpandishi cheo! Hivi hili ni kosa la nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa mfano mdogo tu ambao Mheshimiwa nitamwomba Mheshimiwa Waziri tuufuatilie. Kuna walimu wameajiriwa mwaka 2008/2009, 2014/2015, hao mpaka sasa hivi hawajapata promotion yoyote, yaani hawajapanda daraja hata moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri afuatilie, na kama lina ukweli, wapande sasa kwa mserereko. Wakipanda kwa mserereko, ningepaswa kujua, natamani sana kujua, Mheshimiwa Waziri, wala nisifikirie kushika shilingi. Bajeti yako ya sasa imezingatia kuweka bajeti kwa kila arrears ya hawa ambao wameachwa na sasa wapande kwa mserereko? Kwa hiyo, natamani sana kulijua, pamoja na watumishi wa idara nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni madeni ya watumishi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Rahhi, muda wako umeisha tafadhali. Hitimisha tafadhali.

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante.