Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Santiel Eric Kirumba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii. Kwanza ningependa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi kwa nafasi ya kwenda kugombea Urais. Pia, napenda kumpongeza Katibu wangu wa chama, Dkt. Nchimbi, kwa kuaminika, kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais mtarajiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema ndani ya miaka minne, Mheshimiwa Rais, ameweza kufanya kazi kubwa katika ofisi hii ya Utumishi. Amefanya kazi kubwa kutokana na kwamba, amezingatia vigezo vyote vya maadili, kanuni na sheria na hivyo, imeweza kuwafanya watumishi wengi kupanda vyeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuja kuangalia kwa namna moja au nyingine kwa kipindi chote cha Mheshimiwa Rais alichokaa madarakani kwa miaka minne watumishi takribani 400,000, wameweza kupandishwa madaraja. Kwa kipindi kirefu walichokuwa wamekaa, walikuwa hawajapandishwa madaraja, lakini kwa Mheshimiwa Rais, hili limewezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais pia, katika kipindi chake ameweza kuongeza likizo ya uzazi kwa mwanamke, ambaye alijifungua watoto njiti. Kwa namna moja au nyingine, utaona Mheshimiwa Rais amemgusa kila mtu. Pia, napenda kuwapongeza Mawaziri ambao wameteuliwa katika ofisi hii, ni wasikivu na wanafikika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili Mheshimiwa Simbachawene tuliweza kupambana naye sana, tuliweza kumfikia kwa ukaribu na tukaweza kupitisha sheria hii ya uzazi mpaka wiki 40, na sasa hivi hata baba anapata siku saba kwa kumsaidia mke wake ambaye amejifungua mtoto njiti. Kwa hiyo, hiyo ni hatua kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, napenda kusema, Mheshimiwa Rais ameongeza umri wa wategemezi kutoka miaka 18 hadi 21, na hii imeongeza katika NHIF wategemezi hao ni 65,000 wameongezeka, na Serikali inatumia takribani shilingi bilioni tatu katika kuwahudumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utaona hata kama tuna changamoto nyingine za kiutumishi, lakini kwa namna moja au nyingine Serikali imekuwa ikipambana katika kutatua changamoto ndogo ndogo. Kwa hiyo, kwa miaka minne ya Mheshimiwa Rais, amefanya kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba kila mtumishi na kila mwananchi kwa namna yoyote anamfikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuliongelea tena suala lingine la walimu. Mheshimiwa Rais mwaka 2024 alielekeza kwamba watumishi wa kada ya ualimu wapandishwe mshahara. Ni kweli Mheshimiwa Rais amejitahidi kuwapandisha madaraja, lakini ninyi mnaelewa, tumewekeza kwa namna moja au nyingine kwa kiasi kikubwa sana katika sekta ya elimu. Tumejitahidi kujenga madarasa, na tumejitahidi kuwashushia vitendea kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, walimu hawa wanahitaji angalau Mheshimiwa Waziri aweze kuwafikiria kwa namna nyingine. Kwa mwaka huu, kuna neno wanasema, “umejipangaje?” Lile suala la walimu kupandishiwa mshahara limefikia hatua gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wao wenyewe wanaelewa tukienda kufanya mikutano ya kata, mikutano mitatu unakuwa umeshachoka. Fikiri mwalimu huyu anafanya kazi ya kufundisha watoto, na sehemu nyingine, kama mimi ninavyotoka sehemu za kijijini, unakuta shule moja, ni kweli Serikali imeajiri, lakini hata kwetu pia tuna changamoto ya ajira ya kada ya ualimu. Unakuta kule kuna shule nyingine ina upungufu wa walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu afundishe Darasa la Tatu, afundishe la kwanza, afundishe la nne; na mwalimu huyu huyu inamlazimu kuhakikisha kuwa watoto wote wanafaulu. Watoto wale wasipofaulu, Serikali inatupia lawama shule ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda kuwaambia, kwamba hili suala la kumwongezea tena motisha mwalimu ili aweze kufundisha kwa starehe inapaswa aangaliwe kwa jicho lingine la kumpandishia mshahara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la ajira, kila mtu amekuwa akililalamikia, lakini pia mwaka 2024 kuna Mheshimiwa Mbunge aliweza kuchangia. Hili suala la ajira hebu tulishushe katika kila Halmashauri. Kila Halmashauri iwe na database ili iweze kusaidia kutatua changamoto ya ajira. Tunaweza tukawa tunalalamikia kwamba kuna changamoto ya ajira kwamba bado ajira hazitoshelezi, lakini kila Mkoa una mradi wa kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukupa mfano, katika Mkoa wetu wa Shinyanga tuna miradi ya mkakati wa SGR, tuna mradi wa kimkakati wa bomba la mafuta, tuna mradi wa umeme mkubwa wa solar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hapa Bunge nilipouliza swali kwenye Mradi wa SGR na bomba la mafuta bado takwimu zilionesha kwamba ni ndogo, lakini ukija huku ukisoma kwenye taarifa zao wanakwambia kuwa tumeajiri watu labda 400,000, tumeajiri labda watu 2,000 au 5,000. Sasa, ukija in real sense, ukienda kwenye ile miradi, wale watu wasomi wa eneo lile, hawanufaiki na miradi ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kuna wakati unakwenda kukagua miradi, ukiwauliza je, wananchi wameshirikishwaje kwenye huu mradi ili waweze kuulinda na kuutumikia? Unakuta wananchi wa eneo lile hawana taarifa ya huo mradi husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, unakuta wale watu ambao tunawapa miradi hii ya kimkakati, ajira zile wanazozitangaza wanazitangaza kwenye mtandao. Kwa hiyo, mtu lazima ajiriwe kwa kupitia mtandao. Ile inakuwa changamoto kwa wale watu ambao wanatoka katika zile halmashauri husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba, kwa sababu Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI alielekeza kwamba sasa hivi halmashauri zitakuwa zikiajiri. Ni wakati sahihi Utumishi pia kushirikiana na halmashauri hizi ili kuhakikisha kwamba ni kweli zile ajira zinazosemwa na ile miradi ya kimkakati, kweli zimewafikia wananchi ili tuache kuisubiri Serikali Kuu kuajiri, tupambane na hii miradi na kutatua changamoto ya ajira huku chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)