Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuungana na viongozi wenzangu wote kumshukuru sana, Mwenyezi Mungu kwa kutujalia baraka zake katika nyanja mbalimbali za ustawi wa Taifa letu kwa kuwa ametuepusha na majanga mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa jimbo langu la Mbulu Mjini nachukuwa nafasi hii kuungana nao kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi anavyoliongoza Taifa letu na kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 - 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli yapo mambo mengi sana yametekelezwa katika jimbo langu la Mbulu Mjini na nchi yetu kwa ujumla. Hakika haijapata kutokea hali iliyotuwezesha chama chetu kuwa na haiba kubwa sana kwa Watanzania na majirani zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa George Simbachawene, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa jinsi wanavyotumikia nafasi zao nyakati zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mwenyekiti wa Kamati yetu na Wajumbe wote Kamati ya Kudumu ya Bunge kwa taarifa yao nzuri iliyowasilishwa mbele ya Bunge letu. Hongereni sana kwa kazi kubwa mnayoifanya, Mwenyezi Mungu awabariki sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Wizara hii kwa kupokea maombi yangu ya fedha za kujengwa Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Mbulu, na kazi ya ujenzi imeanza, hongera sana kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali nzima ya Awamu ya Sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa mchango wangu kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri na Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, Serikali iangalie utaratibu mzuri wa kutoa fedha za TASAF kwa ajili ya miradi ya jamii, kwani bado kumekuwa na viporo vya miradi ambayo bado havijaanza kutoa huduma kwa jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Serikali iangalie upya utaratibu wa usaili kwa vijana wahitimu wa vyuo hususan sekta ya afya na elimu, kwa kuwa zoezi la usaili limepokelewa kwa hisia tofauti na kusababisha manung’uniko makubwa sana kwa kundi hilo. Hivyo basi, ushauri wangu ni kwamba uchujaji wa vijana wa ajira ufanywe na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa kutumia vigezo vyao vya ufaulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Wizara itazame upya mfumo wa kuratibu, kubaini kuwalipa watumishi wa mamlaka ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu ambao wana madai ya muda mrefu Serikalini kwa kuwa sisi kama wawakilishi wao, tumepokea maombi mengi ya madai yao pindi tunapopata vikao vya pamoja. Hata hivyo, kuna utata wa madeni hayo, nani amezalisha na nani anapaswa kumlipa mtumishi huyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kwa namna ya pekee, naomba Serikali ijitahidi sana kutoa fedha za bajeti ya Wizara hii muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa let,u kwa kuwa tunahitaji kufanikisha mipango yote ya Wizara ikiwemo fedha za bajeti ya uendeshaji na miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Naomba kuwasilisha.