Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Patrick Alois Ndakidemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Mheshimiwa George Boniface Simbachawene, Mbunge; na Naibu wake Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge pamoja na watendaji wa Serikali katika Wizara hii wakiwemo Juma Selemani Mkomi, Katibu Mkuu; na Xavier Mrope Daudi, Naibu Katibu Mkuu kwa kazi nzuri wanayofanya kuwatumikia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita kwenye changamoto ya ajira kwa vijana wanaohitimu vyuo mbalimbali na mapendekezo ya kutatua changamoto hii. Jambo hili limepewa kipaumbele katika taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria. Nami nimeona niweke msisitizo kwenye hili jambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchini Tanzania, idadi ya wahitimu wa vyuo vikuu imeongezeka kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni. Hali hii imetokana na jitihada za Serikali na sekta binafsi kuboresha upatikanaji wa elimu ya juu. Pamoja na mafanikio haya, changamoto kubwa imeibuka. Wahitimu wengi wanakosa ajira baada ya kuhitimu mafunzo ya vyuoni katika fani mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira kwa vijana ni suala nyeti na muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania. Kwa mujibu wa Sensa ya Mwaka 2022, zaidi ya nusu ya idadi ya watu nchini Tanzania ni vijana wenye umri wa chini ya miaka 35. Takwimu hizi zinaonesha kuwa nguvu kazi kubwa ya Taifa ni vijana ambao wanategemewa kwa ajili ya maendeleo ya sasa na ya baadaye. Sehemu kubwa ya vijana hawa wana changamoto ya ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana imekuwa ikiongezeka kwa kasi, hali inayotishia ustawi wa Taifa na maendeleo endelevu. Ukosefu huu wa ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu ni tatizo kubwa. Wasomi wengi hukosa ajira zinazolingana na taaluma zao. Ikiwa hali hii haitapatiwa ufumbuzi, inaweza kuathiri maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Tanzania kwa miaka ijayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mantiki hii, bila fursa za ajira, ni kwamba nchi yetu inapoteza rasilimali muhimu za watu wenye elimu na ujuzi. Hali hii inasababisha Taifa letu kushindwa kufaidika na uwekezaji mkubwa uliofanywa katika elimu ya juu, hivyo basi wasomi wanakosa fursa ya kuchangia kikamilifu katika uchumi wao binafsi na wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana wetu wasomi wetu unaweza kusababisha migogoro ya kijamii na kisiasa. Kwa mfano, wahitimu wasio na ajira wanaweza kujiingiza katika vitendo vya uhalifu au maandamano, na hali hii inaweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi ambapo athari hizi zinaweza kuwa na madhara makubwa kwa umoja wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni tumeshuhudia kuwepo wa jumuiya isiyo na usajili iliyojiita Umoja wa Walimu Wasio na Ajira (NETO). Vuguvugu la watu hawa lilisababisha viongozi wao kukamatwa na Jeshi la Polisi kwani walijitokeza na kuilalamikia Serikali juu ya haki yao ya kupata ajira ambayo wameisubiri kwa muda mrefu tangu walipomaliza masomo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yakijitokeza makundi mengine yenye nguvu ya kudai haki za ajira katika fani nyingine, hii itasababisha migogoro na Serikali, jambo ambalo linaweza kudhoofisha imani ya wananchi kwa Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili la ukosefu wa ajira kwa vijana wetu ni kubwa na inatakiwa Serikali ikae na wadau mbalimbali na kuja na mkakati wa kukabiliana na suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali ni kama ifuatavyo:-

(i) Serikali ianzishe programu ya kitaifa ya kuwezesha uwepo wa ajira za muda na kujitolea. Serikali na mashirika yasiyo ya Kiserikali yanapaswa kuunda na kuanzisha programu maalumu zitakazowezesha vijana kujitolea na kufanya kazi za muda. Hii itawasaidia wahitimu kupata uzoefu unaohitajika kwa miaka ijayo. Ajira za muda na programu za kujitolea zinaweza kuwasaidia wahitimu kupata uzoefu na kuongeza uwezekano wa kuajiriwa baadaye, baada ya kupata uzoefu.

(ii) Serikali inapaswa kuboresha sheria na sera zinazohusu ajira na biashara. Ni vyema kuweka sera zinazoendana na mazingira ya sasa ya soko la ajira, pamoja na kuhakikisha kwamba sheria zinazoendana na ajira, zinatetea maslahi ya vijana. Pia ni muhimu kuweka sera rafiki za kusaidia ukuaji wa sekta zinazoweza kuzalisha ajira nyingi kama vile ufugaji, uvuvi, kilimo, utalii, na viwanda vidogo vidogo.

(iii) Serikali inapaswa kuboresha mfumo wa elimu ili kuhakikisha kwamba unawaandaa vijana vyema kwa soko la ajira. Hii inajumuisha kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi na elimu ya vitendo, pamoja na kuhakikisha kwamba mitaala inazingatia ujuzi unaohitajika katika soko la ajira la sasa na la baadaye ndani na nje ya nchi.

(iv) Serikali kupitia mabalozi wa Kitanzania waliopo nchi tofauti duniani, wawatafutie ajira vijana wetu katika nchi zenye uhitaji ili Watanzania wapate ajira katika nchi hizo. Hili linawezekana kwa sababu hata nchi yetu huajiri watumishi kutoka mataifa mengine kwenye maeneo yenye pengo la wataalamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ikilipa jambo hili kipaumbale, basi Watanzania walio wengi watapata ajira na kupunguza mzigo kwa Taifa. Kwa mfano, juhudi zikifanyika, Watanzania wengi wanaweza kupata ajira za kwenda kufundisha Kiswahili kwenye mataifa yenye uhitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali, kwani kwenye kutekeleza hili, wameanza kuhuisha kanzidata ya Watanzania wenye sifa na nia ya kuajiriwa katika mashirika ya kikanda na Kimataifa katika nyanja mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, tatizo la ajira kwa vijana nchini Tanzania linahitaji suluhisho la haraka na la kimkakati. Tunahitaji kuwa na Taifa ambalo vijana wake wana ajira zenye tija na fursa za maendeleo, na hivyo kusaidia kujenga uchumi endelevu na jamii yenye ustawi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo na ushauri wangu, naunga mkono hoja.