Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chato
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba pia leo kwa mara ya kwanza kabisa nihutubie Bunge lako Tukufu kwa niaba ya Watanzania wote, nikiwakilisha Jimbo la Chato. Nianze sasa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai mkubwa na kupata fursa ya kuongea na kuunga mkono hoja hii ya Wizara ya Nishati na Madini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa nguvu kubwa kabisa nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa na kuaminika kwa Watanzania wote kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Makamu wa Rais, mama yetu Mheshimiwa Suluhu Hassan, kwa mara ya kwanza kupata Makamu wa Rais kwa akinamama hapa Tanzania. Ni historia kubwa, Watanzania wote tunajivunia na hasa akinamama wenzetu. Tunawapongeza sana akinamama kwa kuwakilishwa na Makamu wa Rais wa akinamama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee pia kumpongeza Waziri Mkuu. Nampongeza Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa kwa kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kadhalika kwa aina ya pekee kabisa nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Ally Mohamed Shein kuchaguliwa kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa aina ya pekee nimpongeze sana Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wangu anavyonisimamia na kuniongoza katika kusimamia majukumu makubwa ya Wizara ya nishati na madini. Nawashukuru sasa kwa nafasi ya pekee wananchi wangu wapendwa, wananchi wa Chato walivyonichagua kwa kura nyingi na wananchi wote kuwawakilisha kama Mbunge wao, naamini wataendelea kunirejesha mpaka uzee wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa aina ya pekee sasa, niishukuru sana familia yangu, wazazi wangu walivyovumilia kwa kipindi chote katika kutekeleza majukumu yangu ya Wizara ya Nishati na Madini, nawapongeza sana Mwenyezi Mungu awajaalie uhai na uzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, sasa nijielekeze kwenye kuunga mkono hoja. Kabla sijasahau, niseme naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, waliochangia ni wengi, zaidi ya Wabunge 109, lakini naweza nisijibu hoja zao zote, nitakachofanya, tuombe sana Bunge lako Tukufu kwa ridhaa ya Kanuni za Bunge, itambue ushiriki wa Waheshimiwa Wabunge hawa 109 kwa sababu sitaweza kuwataja, lakini waingie kwenye Hansard. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nianze sasa na kujielekeza kwenye hoja za msingi. Kambi ya Upinzani Bungeni imetoa hoja za msingi sana katika kuonesha kuwa na wasiwasi kana kwamba tutaweza kupata kweli nishati ya umeme ya kuweza kutufikisha kwenye uchumi wa viwanda? Wamekuwa na wasiwasi kwamba, sasa hivi tuna takriban megawatts wanasema 2,780 ndiyo ilikuwa maximum.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mnyika kwamba hizo megawatts 2,780 ambazo tulikusudia kuzifikisha, sasa nimhakikishie miaka mitano ijayo tutakuwa na zaidi ya megawatts 3,000; lakini kuja kufikia mwaka 2025 tutakuwa na zaidi ya megawatts 10,000. Ili kumthibithishia sasa, nimweleze tu kwa upande wa nishati ya gesi, sasa hivi tuna installed capacity nyingi za kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama unavyofahamu, pale Kinyerezi tuna megawatts 150 ambazo tayari tunazo. Tunaendelea kupanua megawatts 185, tutakuwa nazo; Kinyerezi II pia tutakuwa na megawatts 240, unatambua Mheshimiwa Rais alizindua hivi karibuni. Tunaendelea na kuwekeza kwenye nishati hiyo hiyo; tutaendelea kuwa na Kinyerezi III ambayo itakuwa na megawatts 300; lakini bado upo uwezekano mkubwa kuwa na Kinyerezi IV megawatts 320. Bado tuna Somanga Fungu, tuna megawatts 350; bado tuna Kilwa Energy, megawatts 320 na kadhalika. Huo ni umeme wa gesi na tuna uhakika kwamba umeme utakuwa mwingi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee tu kusema, tutakuwa na umeme mwingi wa uhakika sana hasa kwenye nishati ya maporomoko ya maji. Tunatarajia kuwa na megawatts 80 za kutoka Rusumo ambazo tutazigawanya megawatts 26.7 kila nchi. Hizo ni nguvu kubwa, itasaidia sana kwa wananchi wa Ngara na maeneo ya jirani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bado tuna umeme wa Kakono wa maji, sasa hivi tunatumia umeme wa kutoka Uganda kwa wenzetu wa Kagera. Sasa tutaachana na umeme wa Kagera kwa kutoa Uganda, tutaanza kutengeneza umeme wetu. Pale Kakono tutakuwa na megawatts 87 na tutausafirisha kwa kilomita 38.8 kutoka Kakono mpaka kwenda Kyaka. Huo ni umeme wa uhakika, nataka niwahakikishie wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunazo nguvu nyingi za umeme, tunapozungumza tutaachana na matatizo ya umeme, tuna uhakika na hizo ni takwimu za kisayansi. Niendelee sasa kusema tu, kuwa na nguvu ya umeme na bila kusafirisha bado haisaidii, niwahakikishie sana Watanzania kwamba sasa nguvu kubwa ya umeme tutakayokuwa nayo kama tulivyoeleza kwenye taarifa yetu ya bajeti, tunaanza sasa kuusafirisha umeme huo ambao utatatua tatizo kubwa la kukatika kwa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tatizo la kukatika kwa umeme wananchi naomba niwaeleze, ni kwa sababu ya mambo yafuatayo: kwanza, umeme tulionao ni kweli una low voltage. Ili kuondokana na low voltage, sasa tunakuja na umeme mkubwa wa Kilovoti 400 na huu umeme utatapakaa nchi nzima. Nianze kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakuwa na umeme wa kilovoti 400 tunaosafirisha kutoka Mbeya unapita Sumbawanga, unaenda Kigoma, unaenda Mpanda mpaka Nyakanazi. Huo urefu mkubwa sana, ni kilomita 1,148. Umeme huo huo tutausafirisha kutoka Nyakanazi mpaka Geita, kilomita 133; umeme huo huo tunautoa Nyakanazi na tutautoa Geita mpaka Bulyankhulu, kilomita 50. Ukanda huo utakuwa na umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huo huo tutaanza kuzalisha umeme wa Malagarasi. Umeme wa Malagarasi ndiyo utakuwa mkombozi wa umeme mkubwa kwa wananchi wa Kigoma na maeneo ya jirani kama Ngara. Huo umeme tunaanza kuutekeleza kuanzia mwakani na utakamilika 2019. Kwa hiyo, niwahikikishie wananchi wa Kigoma na eneo la jirani kwamba tunapozungumza eneo la umeme, kwa sasa hivi tumejifunga mkanda, ni suala la kufa na kupona, Watanzania wote watapata umeme wa uhakika ifikapo 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuzungumzia suala hilo hilo la umeme. Tutausafirisha umeme mwingine; nataka niwaeleze mwone jinsi Tanzania nzima itapata umeme wa kutosha. Tutakuwa na umeme wa kutoka North East Grid na huo umeme tutaanza sasa kuutoa Kinyerezi kwa upande wa mashariki. Utatoka Kinyerezi utaenda Chalinze, utaenda Tanga mpaka Arusha mpaka Namanga kilomita 664. Kwa hiyo, Watanzania wa maeneo yale watakuwa wana uhakika wa umeme ambao haukatikikatiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la kusafirisha umeme mkubwa ni kuhakikisha kwamba umeme uliopo sasa ni mkubwa, unatosha kwa matumizi ya viwandani, matumizi ya nyumbani na biashara ndogo ndogo pamoja na biashara kubwa. (Makofi)
Waheshimiwa Wananchi na Waheshimiwa Wabunge, nataka tena niwahakikishie, tunao mradi ninaousema wa backbone. Huu mradi ni wa umeme mkubwa. Ni umeme ambao unatoka Iringa unapita Dodoma unakwenda Singida mpaka Shinyanga na unatumika kwa maeneo yote ya Kanda ya Ziwa na ndiyo umeme wa uhakika mkubwa tunaouzungumzia, siyo umeme wa kutakatikakatika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, suala la kukatika kwa umeme, baada ya miradi hii kukamilika mwaka 2018/2019 yatapungua kwa kiasi kikubwa sana. Sasa hivi niseme tu, siyo kwamba sasa hivi tuna mgao wa umeme. Hatuna mgawo, isipokuwa kuna kukatikakatika kwa umeme kutokana na sababu nilizozitaja hapo awali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka niwahakikishie hilo kwamba tunaposema kutakuwa na nguvu kubwa ya umeme, ni umeme wa nguvu kubwa utakaofaa viwandani. Naelewa Mheshimiwa Matiko anajua kwamba, kuna mgao wa umeme na dada yangu naomba uridhike kuwa tatizo hilo litapungua sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie REA na ninapokuwa najibu haya, najibu kwa ujumla wake kwa sababu maswali ni mengi sana. Nizungumzie REA. Ni kweli kabisa REA, awamu ya pili imekwenda maeneo yote tuliyopeleka awamu hiyo, lakini umeme unaishia kwenye vituo tu vya vijiji na siyo kwa wananchi. Lengo kubwa la mradi wa REA, awamu ya pili lilikuwa ni kusafirisha miundombinu ya umeme ili kufikisha vituo vikubwa na baadaye usambazaji kwenda kwa wananchi katika vitongoji uendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa awamu inayokuja, wananchi wengi wameuliza, Waheshimiwa Wabunge mmeuliza kwamba umeme unapita kwenye nyuso za watu. Sasa unakuja mradi unaoitwa underground distribution transformer. Mradi huu unaanza kutekelezwa kuanzia Januari mwakani na utakamilika miezi 18 tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la mradi wa distribution hiyo ninayosema ni ya underground, siyo chini ya ardhi Mheshimiwa Matiko kama unavyosema. Lengo lake, ni kupita kila mahali ambapo transformer na miradi mikubwa ya umeme ambapo Kilovoti 33 imepita, itakuwa sasa inatandaza umeme kutoka kwenye vituo hivyo kwenda kwenye miji ya wananchi. Kwa hiyo, umeme huo utafika kwenye kaya za wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka niwahakikishie suala kwamba kuna maeneo yameachwa, yatazibwa pengo pamoja na mradi tunaosema wa underground distribution transformer. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi mwingine huo huo ambao sasa utapita kwenye njia zilizopitisha umeme wa kilovoti 33, kutandaza umeme kutoka kwenye vituo hivyo umbali wa kilomita 10. Huo unaitwa European Union Distribution Grid na utasaidia sana kueneza umeme kwenye maeneo yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, huo mradi pia unagharamiwa takriban shilingi bilioni 58.4 na mradi ule utakapokuwa unapita, maeneo yote ambayo hayakufikiwa na umeme kwa umbali wa kilomita 10 kutoka kwenye nguzo kubwa, sasa utapatiwa umeme wa uhakika na baadaye utapitisha umeme huo huo wa kilovoti 400.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, nilikuwa nataka tu kueleza maelezo ya kina kabisa kabisa kuhakikisha kwamba umeme unaokuja ni mkubwa na utaingia kwenye Vijiji vyetu na wananchi wote watapata umeme wa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie sasa kuzungumzia kwenye suala la umeme kuhusiana na kuunganisha Vijiji kwa Vijiji. REA awamu ya tatu ni kweli kabisa, kama tunavyosema REA ya awamu ya pili inakamilika mwezi Juni mwaka huu. Tunachofanya sasa hivi ni kukamilisha uhakiki kutambua vijiji ambavyo havijapata umeme hadi leo, lakini vilikuwa kwenye scope ya REA II, lakini kadhalika ni kuainisha vijiji vyote ambavyo havijapata umeme ama vilikuwa kwenye scope ama havikuwepo kwa sababu lengo kubwa ni kupelekea umeme katika vijiji vyote vilivyosalia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge wala wasiwe na wasiwasi kwamba wanahitaji kuona orodha ama kijiji chako kitasahaulika REA ya awamu ya tatu itapeleka umeme kwenye vijiji vyenu vyote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba hili tatizo la akinamama kujifungua kwa kutumia tochi, hili tatizo la akinamama kuonekana na macho mekundu na wakadhaniwa ni wachawi, kwenye hii awamu ya tano miaka mitano hadi kumi ijayo litatokomea kabisa. Tunataka akinamama badala ya kupuliza moto wa mkaa waanze sasa kukandamiza na kuona mwanga mweupe wakati wa usiku. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwa sababu Serikali imejipanga, ina uhakika wa kuwapatia umeme wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie bei ya umeme. Umeme unapokuwa mwingi na umeme unapokuwa wa uhakika, kwa kawaida gharama za umeme zinashuka bei. Kwa sasa kwa sababu tunatumia kwa kiwango kikubwa umeme wa gesi na kiwango kikubwa sana pia umeme wa maji, tunataka sasa kuachana na umeme wa mafuta.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua tulizochukua kuachana na umeme wa mafuta ni kama ifuatavyo:-
Kwanza, mikataba yote iliyokuwa inatumia umeme wa mafuta inapokwisha sasa hatuiendelezi. Huo ni uamuzi wa Serikali. Kwa hiyo, tumeachana na umeme wa Aggreko, tumeachana na umeme wa Symbion kwenye mikataba ya dharura. Sasa hiyo ni kuonesha kwamba Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba umeme tunaoutumia ni wa gharama nafuu na unaondoa gharama kubwa kwa Serikali na wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, gharama za umeme kwa sasa kama mnavyojua, sasa hivi ili uunganishe umeme kwa wananchi wa Vijijini, ni sh. 27,000/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na hapo, Mheshimiwa Waziri wangu wakati anawasilisha bajeti yake alieleza kwa kina sana, kwanza tumepunguza gharama zote za kuunganisha na kuomba umeme, lakini kadhalika tunatarajia wananchi watakapoanza kutumia umeme mwingi wa gesi, gharama huenda zikapungua zaidi. Kwa sasa tumeanzia kuondoa gharama za umeme wanapoomba leseni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tumeanzia na kuondoa gharama za umeme wananchi wanapoomba leseni. Kwa hiyo, wananchi wetu sasa hivi, twende tuwaeleze huko kijijini hawatakiwi kuwasilisha ombi kwa kulilipia, anakwenda anajaza fomu, anaipeleka, anapata umeme, kimsingi ni bure, ukiondoa ile gharama ya kodi ya VAT 28,000. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini akiunganishiwa umeme pia, ataendelea kuutumia umeme huo, TANESCO akija kufanya service halipii kitu chochote na penyewe ni bure. Kwa hiyo, tuwatangazie wananchi wajue sera za Serikali, lakini ili kusema kwamba tuna bei ya chini, tunajilinganisha na nani? Sisi tunaeleza mambo ya kisayansi. Kwa sasa hivi sisi tunazalisha Megawatts kwa ujumla wake 1,554.12 kwa sasa kwa ujumla wake. Kwenye taarifa yetu tumesema 1,461 zipo kwenye grid lakini ukijumlisha na ule ambao haupo kwenye grid ni 1,554.12.
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu wa Kenya, kwa Afrika Mashariki ndiyo wanaoongoza peke yao wao wana megawatts 2,357, lakini nchi nyingine zote ziko chini yetu. Waganda kwa sasa wana megawatts 849, sasa hivi watu wa Burundi wenyewe wana megawatts 49 na wenzetu wa Rwanda wana megawatts 185.9, kwa hiyo, sisi ukiji-rank bado tupo juu kwa maana ya kuzalisha umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaeleze, maana yake Waheshimiwa Wabunge tunapozungumza masuala ya umeme kwa sababu tunazungumza uchumi lazima tuzungumze kwa takwimu. Sasa tunajilinganisha vipi kwa beiā¦
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri naomba umalizie. Naomba uwe unamalizia, kengele ya pili tayari.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, sijazungumzia madini, nataka nizungumzie kwenye madini, nikimbie basi niende kwenye madini nizungumze kidogo. Pamoja na kwamba nimejieleza sana kwenye masuala ya umeme, lakini pia nizungumze kidogo kwenye tasnia ya madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu kusema, kwa sasa Wizara yetu inatenga maeneo mengi kwa ajili ya kuwagawia wananchi. Tumesema ni kilometa 12,000 tunatenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Maeneo yatakayotengewa sasa leseni na utafiti unaoendelea yako ya Kasubuya hekta 498, Malengwa hekta 682, yako pia ya Geita takribani hekta 2001 na mpaka kule Chato-Msasa hekta 12,28 na kadhalika na kadhalika. Nyamongo tunaendelea kufanya utafiti kugundua maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba muda umekwisha, napenda sana nipatiwe muda niendelee kusema zaidi kwa sababu ni nafasi ya pekee lakini kwa sababu muda umekwenda sana...
NAIBU SPIKA: Wakati mwingine Mheshimiwa.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja.