Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Awali ya yoyote nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema ambaye amenijalia leo kusimama ndani ya Bunge hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara ya kwanza ikiwa ni bajeti yangu ya kwanza nikiwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, nichukue nafasi hii kwa moyo wangu wa dhati kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwanza kwa kuniamini na kuniteua katika nafasi hii, na pili, kuendelea kuniamini, nami nimeendelea kuwepo katika Ofisi yake hii nikimsaidia pia Waziri wangu Mheshimiwa Simbachawene. Hakika namshukuru sana Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nawashukuru na kuwapongeza viongozi waandamizi wasaidizi wa Mheshimiwa Rais, akiwemo Makamu wa wetu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango; Waziri Mkuu wetu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa; Naibu Waziri Mkuu wetu Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko na viongozi wote waandamizi wanaomsaidia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee, nashukuru sana na kumpongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa George Boniface Simbachawene kwa kazi nzuri anayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejiona ni mtu mwenye bahati kufanya kazi na Mheshimiwa Simbachawene. Katika mambo matatu ambayo ninajivunia, kwamba nimeingia kwenye darasa jipya, kwanza, ni uchapakazi. Ni kiongozi mchapakazi; pili, ni kiongozi mwenye hekima na busara ya hali ya juu. Ukiwa na Mheshimiwa Simbachawene utachota hekima na busara, hasa sisi vijana ambao tunachipukia katika uwanja wa siasa, kwetu amekuwa mwalimu mzuri katika suala la hekima na busara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa alilonalo Mheshimiwa Simbachawene ni upendo, siyo mchoyo wa maarifa. Uzoefu wake na utajiri wa maarifa alioupata katika nyanja mbalimbali alizotumikia Serikali, anakushirikisha mpaka wewe mwenyewe unaona kwamba hili ni darasa tosha. Kwa kweli namshukuru sana Mheshimiwa Simbachawene. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuwapongeza viongozi waandamizi katika Ofisi ya Rais, nikianza na Katibu Mkuu Kiongozi, Mheshimiwa Balozi Dkt. Moses Kusiluka, bila kusahau Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Ikulu ndugu yangu Mahendeka ambao wote hawa wakishirikiana; na pia na Katibu Mkuu Utumishi ndugu yangu Juma Selemani Mkomi, wote wamekuwa wakitoa ushirikiano mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kumsahau Naibu Katibu Mkuu wetu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ndugu Xavier Mrope Daudi, wote hawa wakishirikiana pia na viongozi wote walio chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wamekuwa ni nguzo imara ya kutoa ushauri wote wakiwa na nia ya kuunganisha nguvu ya kumshauri Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri huo wote ni kazi ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kutimiza majukumu yake. nawapongeza wote na Wakuu wa Taasisi zote zilizo chini ya Ofisi ya Rais Ikulu, Utumishi na Utawala Bora kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia Spika wetu wa Bunge, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, anafanya kazi kubwa ambayo pia inafanya tunaendelea kujifunza mambo mengi, hasa katika Bunge hili la Kumi na Mbili. Tumeona kazi kubwa anayoifanya; na hata katika Bunge la Dunia huko IPU, anafanya kazi ya kutuheshimisha Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wasaidizi wake, akiwemo wewe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati yetu ya Utawala, Katiba na Sheria pamoja na Makamu Mwenyekiti wetu ambaye anafanya kazi kubwa, ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Kyombo na Wajumbe wote wa Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli tumefurahi sana kufanya kazi na ninyi. Kama Wizara ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, tunafurahi sana kwa kuwa ushauri wetu, maelekezo yenu yametujenga zaidi katika kutekeleza majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja ya Wizara hii. Tangu ilivyoanza hoja ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ikaja hoja ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI na baadaye ikaja hoja yetu sisi Utumishi, Waheshimiwa Wabunge wote michango yao imetujenga sana. Wametupa michango ambayo yote nia yake ni kujenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuwaahidi, kama mlivyotupa sifa ya kuwa wasikivu, usikivu huo huo tulionao tutauendeleza ili yale mliyotushauri tuhakikishe yanatokea na sisi sote tuone kwamba yale mlitichangia katika Wizara yetu yanajenga na yanaleta tija kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na jambo moja ambalo limezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge wengi, suala la TASAF. Nitaanza kwa kutoa historia ndogo kidogo. Dunia ilikutana mwaka Septemba, 2015 katika mkutano mmoja maarufu unasema, UN Sustainable Development Goal Summit ambao lengo lake Septemba, 15 ilikuja kutafakari dunia namna gani itakavyopambana na changamoto zinazoikabili dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa ambalo lilikuwa linaisukuma dunia, lilikuwa ni uharibifu wa mazingira, umasikini uliokithiri na mambo yanayoendana na haya. Ndipo pale wakaja na malengo ya maendeleo endelevu, tunayoyaita SDGs 17 ambazo ni Sustainable Development Goals 17. Sasa hizi zilikuwa casted kila nchi na bara likaenda kutekeleza kwa namna ambavyo lingeweza kupambana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwetu nichukue fursa hii kuendelea kumshukuru Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na kutafuta mbinu nyingi ya kufikia hiyo ajenda tunasema 2030 kwenye TASAF amechukuea initiative kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TASAF katika programu ya tatu alikuwa na mpango wa kunusuru kaya masikini. Waheshimiwa Wabunge wameiongelea kwa namna nyingi. Mimi naomba nieleze namna ambavyo Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki cha awamu ya pili ya TASAF Mheshimiwa Rais aliweza kutoa fedha shilingi trilioni 1.1. Lengo la fedha hizi ni kwenda kunusuru kaya masikini zilizokuwa zinaishi kwenye wimbi kubwa la umasikini, ambapo fedha hizi zimefanikiwa kufikia kaya 1,378,916. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kaya hizo, kuna wanakaya milioni tano, fedha hizi zilienda kufanya nini? Hapa nataka nieleze kwa sababu kuna mambo mengi yameelezwa. Hizi fedha zilikuwa siyo za kugawiwa tu, zimetengenezewa programu maalumu. Programu ya kwanza iliyofanyika kupitia Programu ya TASAF, kwanza ilikuwa ni kwenda kutoa ruzuku kwenye kaya maskini na ile ruzuku ilikuwa inatolewa kwa kutolewa masharti maalumu. Kama familia ina watoto wanaosoma shule, utakavyokuwa unahimiza watoto kwenda kusoma na ndivyo kipato cha kaya kitaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unahudhuria vizuri clinic na hospitali, hicho kipato cha kaya kitaongezeka. Kwa hiyo, hii ilisukuma mwamko wa kwenye jamii, jamii ikaamka ikawapeleka watoto wengi shule, jamii ikaamka ikaanza kuhudhuria kwenye matibabu, jamii ikaamka ikaingia pia katika programu ya kuwekeza na kuweka akiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka ninavyoongea hivi, kupitia programu ya TASAF tayari kuna wanufaika 880,000 ambao wamenufaika na programu hii, wanajiwekeza katika vikundi vya akiba na kukopa, ambapo fedha walizowekeza huko ni takribani shilingi bilioni 13 na katika fedha hizo shilingi bilioni 13 tayari mpaka sasa wanakopeshana shilingi bilioni 7.9. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni achievement kubwa. Maana yake ni nini? Kwanza, wamepata discipline ya ujasiriamali; pili, ni financial literacy kwa maana ya menejmenti ya fedha. Kwa hiyo, hatukuishia tu hapo, katika kaya hizi, amesema Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara kuhusu habari ya Bodi ya Mikopo. Naomba niseme, success story na hii, sifa kubwa imwendee Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipoanza mahusiano kati ya TASAF na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, watoto waliokuwa wanatoka kwenye kaya maskini walikuwa 656, leo hii ninavyoongea katika Bunge hili, tayari watoto wanaonufaika kutoka kaya maskini kupitia Programu ya mahusiano (MOU) iliyoingiliwa kati ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu na TASAF ni vijana 12,500 ambao wananufaika na wanapata mkopo kwa 100%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikutoe hofu Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara, jambo hili tumeliwekea utaratibu mzuri, waratibu wetu wa wilaya wanawatambua hawa watoto, wanawapeleka TASAF Makao Makuu, wakifika TASAF wanawapeleka Bodi ya Mikopo Elimu ya Juu, wakifika pale hakuna urasimu, hakuna bureaucracy yoyote, kijana anapata mkopo 100% na Serikali inaisimamia hili ili litokee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, haijaishia hapo, tumeenda mbali zaidi. Kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, hawa vijana wanaotoka kaya maskini watakapokuwa wamemaliza Darasa la Saba na wakashidwa kuendelea, wanapata fursa ya kwenda VETA chini ya ufadhili wa mifuko ya kuwezesha wananchi kiuchumi iliyo chini ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi zote ni initiatives ambazo lengo la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha katika zile SDG, ikiwa SDG one, goal one ilikuwa ni no poverty, kuondoa na kutokomeza umaskini, anatekeleza kwa vitendo na kwa kweli Mheshimiwa Rais amefanya jambo hili na kwa kweli anastahili pongezi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikimalizia hapo, TASAF kuna jambo limezungumzwa sana, wazee kujitolea, na wazee kufanyishwa kazi. Naomba hii dhana iwe wazi, TASAF haina programu ya kulazimisha wazee kufanyishwa kazi. Ile kwanza ni hiari na tume-limit age kati ya miaka 18 mpaka hapo 65; na hiyo ni hiari ya mtu kwenda kufanya hiyo kazi, halazimishwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge, na kwa kuwa jambo hili ni shirikishi, sisi tutaongeza usimamizi kuhakikisha kwamba wale wazee wengine wanaopenda tu kwamba mimi nikafanye kazi, lakini baadaye inaonekana kwamba TASAF wanalazimishwa kwenda kufanya kazi, kwa hiyo, niwaondoe shaka Waheshimiwa Wabunge, hili jambo tutaliweka vizuri na kuhakikisha kwamba linaondoa sintomfamu ambayo ipo (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye suala la watumishi, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais, amefanya incentive kubwa sana. Nikianza na suala la malimbikizo ya mishahara, jambo hili Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo mahususi na tumeanza kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niliaarifu Bunge lako Tukufu kwamba mpaka tulivyokuwa tunafunga mwezi Machi, tayari tulikuwa tumetambua watumishi takribani 130,464 ambao walikuwa wanadai malimbikizo, na hii fedha ya kuwalipa ilikuwa ni bajeti ya shilingi bilioni 207. Naomba niendelee kuwahakikishia kuwa Serikali ipo kwenye mpango wa kuhakikisha hawa watumishi tunamaliza kuwalipa malimbikizo yao ya mishahara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie Bunge lako Tukufu kutoa rai kwa waajiri. Baadhi ya waajiri wamekuwa na kasumba ya kutokuleta mapema madai hayo ya malimbikizo, wanakaa nayo huko, hatimaye wanafanya madai hayo yanakuwa ya muda mrefu, wanasababisha malalamiko kwa watumishi wakati Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo na ameruhusu bajeti hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wetu ulikuwa, kati ya mwaka huu wa fedha na ujao tuwe tumemaliza wa zamani ili waje wapya, hao ambao tutakuwa tunawa-sort na idadi yao itakuwa ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, kwenye suala hili tutalisimamia na niendelee kuwasisitiza waajiri, na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, ifikapo tarehe 31 Mei wale waliokuwa pending ambao hawajaleta Ofisi ya Rais - Utumishi madai hayo ya malimbikizo ya mishahara wayalete ili tuyafanyie kazi, tuyahakiki na baadaye tuyapeleke Hazina kusubiria malipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la madaraja (promotion). Waheshimiwa Wabunge wengi wameongelea na wamegusia hasa kundi kubwa la walimu waliopata ajira mwaka 2008, 2009, 2012 na 2013, pia wengine walioachwa huku, naomba kwanza nishukuru kwa pongezi zenu kwa Mheshimiwa Rais ku-acknowledge kwamba kazi kubwa imefanyika katika kupandisha watumishi madaraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwape neno lingine la matumaini. Katika mwaka huu wa fedha tunaokwenda kuumaliza tayari, tumetenga bajeti ya shilingi bilioni 226 kwa ajili ya kwenda kupandisha madaraja watumishi 219,042; na hili tunaenda kulisimamia na mpaka kufika Machi tayari tulikuwa tumebakiwa na watumishi 48,042. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili niwasisitize pia waajiri, kama kuna mtumishi mwenye sifa ambaye alikuwa anastahili kupata hiyo promotion wahakikishe tarifa zinakuja Ofisi ya Rais, Utumishi ili sisi tuchakate. Lengo la Mheshimiwa Rais anataka tunapoanza huko mbele tuwe na wale wapya wanaodai promotion na siyo wa zamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, yale makundi 2009, 2008, 2012, na 2013 niwaondoe shaka. Tunaenda kusimamia kuhakikisha madaraja yao wanayapata kwa mserereko ili walingane seniority na wale wenzao waliowatangulia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, hoja ni nyingi, lakini tuahidi, hoja zote zile mlizotoa tutawajibu kwa maandishi kila Mbunge na tutamfikishia hoja zote. Kwa kuwa muda ni mdogo, tungeweza kumjibu kila mmoja, na kutoa ufafanuzi wa kila mmoja, lakini zote tumezipokea, mtaona tutawajibu; na kwa sababu bado tupo ndani ya Bunge hili, tutaendelea kutaarifiana namna ambavyo tunatekeleza majukumu haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)