Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. George Boniface Simbachawene

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibakwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima kubwa, napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia hoja yetu. Tumebahatika kupata wachangiaji wengi, ukichukua wa leo 16; waliochangia Ofisi ya Waziri Mkuu, watatu; na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, mmoja; tumepata wachangiaji takribani 20. Tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa niseme tu, hoja zilizosemwa ni nyingi sana, na zote ni hoja muhimu kwa sababu zinahusu sekta ambayo ni muhimu kwa Taifa, na kwa nchi yoyote duniani. Mtumishi wa Umma kama alivyosema Mheshimiwa Olelekaita, ndiyo injini na msingi wa maendeleo wa Taifa lolote lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hoja zote hapa ni za msingi na pengine kwa sababu ya muda, tunaweza tusipate nafasi ya kuzijibu ipasavyo, nitajaribu kwa kugusa baadhi ya zile nitakazobahatika kuzijibu, na kwa wale ambao kwa namna moja au nyingine sitakuwa nimewataja au kugusa kabisa hoja zao, basi tutazijibu kwa maandishi ili ziweze kuwafikia mapema iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hoja zilizotolewa na Kamati, kwa sababu Kamati ndiyo msingi wa hoja yetu, nao ndio walioleta hoja hii hapa Bungeni. Kamati imekuwa na maeneo ya muhimu sita. Imehimiza fedha inayoidhinishwa na Bunge iweze kupatikana kwa wakati, lakini imehimiza zaidi kuimarisha zaidi misingi ya utawala bora na kuimarisha mifumo ya utendaji kazi Serikalini; na hili limesemwa na Waheshimiwa Wabunge wengine, lakini pia kuboresha mishahara na maslahi ya watumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemsikia Mheshimiwa Kassinge hapa anasema juu ya walimu na wengine mmesema juu ya wengine. Leo nimepata na ushabiki mwingine wa Ndugu yangu, Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Mheshimiwa Dkt. Kurwa kumbe naye ni mwalimu mzuri ingawa ni agemate wangu, lakini inaonekana nami alinifundisha pia mahali fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ya Kamati imekuwa ni kuboresha mafunzo kwa watumishi wa umma ambayo itaongeza weledi na ustadi, lakini kuondoa tatizo la kila taasisi kujadili na kuimarisha mifumo ya ajira, na pia kuboresha mifumo ya ufanyaji usaili. Hizi zimekuwa ndizo hoja za Kamati na ndioyo zilizojenga msingi wa michango mingine iliyofuata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niwashukuru sana Kamati ya Bunge ya Katiba, Utawala na Sheria kwa kazi kubwa ambayo mmefanya katika kipindi chote ambacho tumekuwa na ninyi, nami nimefanya kazi nanyi takribani miaka miwili na kidogo, na ndiyo maana Mheshimiwa Naibu Waziri amesema hapo, kwa kweli tumekuwa na malezi mazuri sana ya Kamati ambayo yeye ndio anayeiongoza; Mheshimiwa Dkt. Mhagama, Naibu Makamu wako Mheshimiwa Kyombo pamoja na Wajumbe wote wa Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajumbe wa Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria ni watu wazuri ambao wametenda haki na wamekuwa wazalendo kwa nchi yetu. Nawapongeza na kuwaombea kila la heri kwenye majimbo na kwa maeneo waliyotoka ya uwakilishi yaliyoletwa humu Bungeni, watambue kwamba wamekuwa na mchango uliotukuka katika kuwawakilisha huku Bungeni kupitia Kamati waliyopangwa na Mheshimiwa Spika. Kwa hiyo, naamini tutakutana hapa baada ya uchaguzi mwezi Oktoba (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja zilizosemwa ni nyingi, nianze na maeneo mahususi hasa hii inayohusu watumishi na utumishi wa umma kama rasilimali muhimu katika Taifa. Utumishi na watumishi wa umma una historia ndefu. Tulikuwa na utumishi wa kikoloni na baadaye tukapata uhuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipopata uhuru tukawa na utumishi unaofuta ukoloni na kuwa na uhuru wa kujiamulia mambo yetu wenyewe na kwa hiyo, tulikuwa hatuna wasomi na baadaye tukaja kwenye reforms ambazo zimefanyika katika utumishi wa umma na zilizopelekea mafanikio makubwa ya awamu zote za uongozi wa nchi yetu; na hata ilipokuja Awamu hii ya Sita ilikuja kuweka miguu yake kwenye utumishi wa umma, huu ambao umetupa mafanikio makubwa haya tunayoyaona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali ilivyo na matukio makubwa na mafanikio makubwa yaliyofanyika katika nchi yetu, kwa kweli ukiubeza utumishi wa umma na watumishi wa umma wa nchi hii utakuwa hautendi haki. Pamoja na changamoto zilizopo wamefanya kazi kubwa, wamefanya kazi nzuri, chochote utakachojivunia na kukiona, wamefanya watumishi hawa hawa wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jukumu letu kama ambavyo Kamati imesema kuendelea kujenga uwezo wa watumishi wa umma, na kuleta reforms mbalimbali. Niwaambie tu, tayari tumeanza kutayarisha reforms ya utumishi wa umma utakaokwenda sambamba na wakati huu wa sasa na ujao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia uchumi huu ambao tumeufikia wakati wa chini na baadaye kwenda wakati wa juu, ni lazima tubadilishe utumishi wetu wa umma. Utumishi wa umma ambao utakutana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, utumishi wa umma utakaokutana na artificial intelligence, lazima na wenyewe ubadilike uende kwa kasi ile ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania hawa waliohudumiwa kwa vipindi vyote toka tupate uhuru, siyo hao watakaohudumiwa baada ya miaka mitano ijayo. Watahitaji kasi, uwazi, umakini lakini wanahitaji haki katika kutendewa wajibu na watumishi wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme kwamba tunatambua hilo kama Serikali na tutahakikisha kwamba reform hiyo inayokuja, inayoandaliwa, basi ikiwezekana iwashirikishe wadau muhimu ikiwemo Bunge, kuhakikisha kwamba tunajenga utumishi wa umma utakaoishi miaka mingine 50 ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni ajira. Katika ajira hizi, katika kipindi cha miaka fulani nyuma ajira zilisimama; na ziliposimama zika-create gap ambayo imeleta shida sasa na kukuta baadhi ya kada zikiwa zina wahitimu wengi sana sokoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika suala la ajira kuna fursa lakini kuna changamoto lakini pia kuna maoni yametolewa mengi sana Waheshimiwa Wabunge. Nataka niseme, maoni yote yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge, kwa kweli tumeyachukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna pongezi zilizotokana na maendeleo ya utumishi wa umma, na kama kuna maarifa ambayo yametolewa hapa, sisi tunayachukuwa na kwa kweli pongezi zote ziende kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa sababu ni katika kipindi chake amepandisha madaraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, malimbikizo ya madeni ya mishahara na madeni yasiyo ya mishahara yamelipwa kwa kiasi kikubwa sana. Ufahamu tu kwamba katika kipindi cha Mama Samia, pia tumekuwa na vipaumbele mbalimbali katika nchi, na pia watumishi wa umma hawakuachwa nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi yamesemwa na wawakilishi wa utumishi, wametoa maoni yao hapa wakina Mheshimiwa Janejelly, wameeleza namna ambavyo Mheshimiwa Rais amefanya mambo makubwa kwa watumishi ukilinganisha na siku zilizopita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni mbalimbali pia yametolewa kuhusiana na ajira. Kweli idadi ya ajira zimeongezeka na zimekuwa nyingi. Katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa vibali vya ajira 149,000. Ni idadi kubwa sana, lakini hata hivyo tuna upungufu wa ajira kwa baadhi ya waajiriwa wa baadhi ya kada. Hata hivyo, ajira mbadala kwa wale wanaotoka kwa namna moja au nyingine, ikiwemo na wanaostaafu huwa wanafidiwa, ametoa vibali takribani 39,934.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu Waheshimiwa Wabunge, pamoja na changamoto zilizosemwa, lakini idadi hii ya watumishi ni kubwa sana kwa vibali tulivyovipata kwa miaka hii mitatu, lakini niwaambie tu habari njema, na waajiriwa ambao wamefanya usaili na wapo kwenye database, nataka niwajulishe tu, Mheshimiwa Rais siku ya jana ametoa kibali cha kuajiri watumishi wengine wapya. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, samahani kidogo.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ametoa kibali cha kuajiri watumishi wapya kwa mwaka huu huu, 33,212. Ajira hizi tukizigawanya tutapata za walimu takribani 10,000 lakini bado ajira mbadala na kwenye walimu tutapata pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikizungumzia kada ya walimu tu, nimejaribu kushauriana na wenzangu kwenye ofisi, tumesema kwa kweli kwenye hizi ajira sasa hatuna haja ya kufanyisha usaili upya kwa upande wa kada ya walimu. Tutakwenda kwenye database kwenda kuendelea kupakua wale waliosalia ili tuendelee kuhakikisha kwamba tunawamaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo rahisi kuwamaliza kwa sababu waliofaulu mpaka sasa hivi ambao wapo wanangojea kupatikana kwa nafasi bado ni wengi na kama tulivyosema kwamba usaili ni utaratibu tu wa kujaribu kugombania hizo ajira chache zinazopatikana, lakini kimsingi karibu wote wameandaliwa vizuri na wapo tayari kwa ajili ya kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana walipokuja wale vijana wa NETO nikasema wacha tuzungumze kwa sababu kusema ukweli wana haki ya kusikilizwa, na vijana wale walisema mambo makubwa sana, na kwa kweli mimi niliwaelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme, kama tumejenga miundombinu ya shule zetu, sekondari na msingi kwa kiasi tulichofanya, kama tumeongeza madarasa kwa kiasi tulichofanya, kama tumeongeza udahili kwa kiasi ambacho tumeongeza udahili kwa kiasi ambacho kimesemwa, kwa nini tusiongeze idadi ya walimu ili wa-fit idadi ya mahitaji inayotakiwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana hawaishii pale, nami nataka niwasemee kwa sababu huko wanasemwa sana na wenzao. Wanasema, tumesema uchumi wetu umekua, sasa tupo uchumi wa kati, lakini tukisoma ripoti ya CAG tunasikia mara kuna hela imepotea na nini na nini. Tunafikiri, hii yote ingeangaliwa sisi tungepata ajira ya kuziba hili gap na kwenda kufundisha wenzetu ambao ni watoto wanaohitaji elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukisikia hoja kama hiyo mzazi unasema huyu mtoto ni mkorofi? Sio mkorofi. Mtoto anaomba kazi unasemaje mkorofi? Sio mkorofi. Kwa hiyo, nafikiri kazi ya Serikali ni kuendelea kutafuta fursa ya kuhakikisha kwamba inaajiri idadi ya kutosha kwa mahitaji ya Serikali, lakini siyo rahisi kwa Serikali kuajiri wahitimu wake wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna Serikali duniani imewahi kuajiri wahitimu wake wote. Fani zipo mbalimbali, hii elimu tunayoisema sasa kwa sababu ya mahitaji yaliyopo na ukiangalia na upungufu tulionao, lakini kwa kada nyingine ninadhani kabisa kwamba sekta binafsi iendelee kuimaraishwa ili isaidie kuajiri wahitimu wengi zaidi. Kwa kada nyingine tunadhani kabisa kwamba sekta binafsi iendelee kuimarishwa ili isaidie kuajiri wahitimu wengi zaidi na katika kufanya hivyo, tutaisaidia nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wowote wa uchumi ni lazima uende sambamba na absorption capacity ya human capital ya nchi kwenda kufanya kazi, lakini isihesabiwe kwamba kuwa na wahitimu wengi ni balaa au mkosi. Kuwa na wahitimu wengi waliomaliza vyuo vya kati na vyuo vikuu ni mafanikio ya kujenga human capital ya maana katika nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wala tusijutie bali tuendelee kutafuta solution ya namna ya kuwapatia ajira vijana hao au wao kujiajiri na wengine kuajiri wenzao wengine. Kwa hiyo, hili nadhani ni cross cutting na ni lazima wote tulione hivyo na tushughulike nalo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi kama Serikali tumekuja na solution ambayo ilitoka hapa Bungeni na Kamati yako imeshiriki katika kutusaidia kuboresha, kwamba, katika utumishi wa umma hakuna msamiati unaoitwa ajira za kujitolea, lakini sisi tumedhani kwa kushirikiana na wadau katika Serikali, Wizara ya Elimu, Wizara ya Afya, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na wengine, tukasema tufikiri tufanye nini maana kuna kundi kubwa limekaa na wengine wanaenda kulima matikiti wakati hawakusomea matikiti na huku tuna upungufu wa mwalimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine wanaenda kufanya shughuli ambazo hawapaswi kufanya. Mfano, Clinical Officer anaendesha bodaboda wakati angeenda kutibu, na tuna upungufu pale wa daktari wa kutibu. Tukasema tuweke utaratibu mzuri wa kujitolea. Kwa hiyo, tumekuja na huu msamiati wa ajira za kujitolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni matokeo ya maoni ya Bunge hili, nasi tumefanyia kazi na katika ajira hizi tumeeleza namna ambavyo hao wanavyopatikana kujitolea watapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tumezungumzia habari ya uwazi na ushindani katika kujitolea huko, kwa sababu kwa sasa hivi, kujitolea kulikuwepo na kulikuwa kunafanyika, lakini ilikuwa ni kujuana na pengine kuonekana kwamba huyu mtu anayekuja kujitolea, amepotea hivi, pengine hana maana, lakini tumetaka kurasimisha na kuweka mfumo ambao utasaidia hao wanaojitolea waweze kupata hata stahiki zao za kujikimu wakati wanajitolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tumezungumzia hata namna wanavyopaswa kuhitimisha huko kujitolea kwao. Kwa hiyo, kimsingi, kujitolea kumewekewa mwongozo ambao utasaidia kuhakikisha kwamba wanaojitolea wanatendewa haki na wanapimwa. Pia hata utekelezaji wa majukumu hayo waliyopewa na usimamizi wao unakuwa uko dhahiri na wa wazi ili waweze kutumia ujuzi wao na kuonesha uzalendo katika kujenga nchi yao, badala ya kuonekana huko mitaani wananung’unika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa mwongozo huu utaanza kutumika mwezi Julai, mwaka 2025 na tayari umekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa hapa eneo lingine linalohusu wahadhiri wa vyuo vikuu na kwamba vyuo vyetu havina wahadhiri wa kutosha kwa sasa. Pia, suala la kustaafu mapema kama ambavyo amesema Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara na hata akina Mheshimiwa Prof. Ndakidemi, wamekuja kwenye siasa, siyo ajabu wangekuwa wanafundisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili tumefanya marekebisho makubwa. Kwanza, usaili wa wahadhiri unafanywa na vyuo vikuu vyenyewe; pili, utawala wao wa kiutumishi utafanyika na vyuo vikuu vyenyewe; tatu, umri wa kustaafu tuliuongeza na sheria hii siyo ya muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka mimi nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati iliyobadilisha hii sheria katika Bunge lile lililopita, tukauongeza umri wa kustaafu na kufanya miaka 65 lakini tukasema anaweza akaajiriwa tena kwa ajira ya mkataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya hivyo kwa sababu gani? Siyo wote wanaostaafu wakawa wana afya nzuri kama walivyokuwa kazini. Umri unapokwenda, inahitaji kidogo kufanya vetting ili kusema huyu mtu unataka aendelee na utumishi au asiendelee. Halafu utumishi wa umma unakuja kuwasajili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika utumishi wa umma na nchi yetu hii yenye misingi ya kijamaa, ni lazima tuwe na utumishi wa umma mmoja. Tusiwe na utumishi wa umma ambao ni scatter. Ndiyo maana hata katika ajira zozote zile zitakazofanyika kokote kule, basi watumishi hawa wataitwa watumishi wa umma na daftari lao la watumishi litakuwa ni hili moja ambalo liko Wizara ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukishaingiza kwenye lile daftari, hatuna maana ya kuingilia uhuru wao wa kuwapata wahadhiri, lakini pia kuwasimamia. Hayo mambo yanafanyika kwenye vyuo vikuu vyenyewe. Pia, hata hao waliotoka vyuo vikuu wameendelea kufundisha vyuo vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Taifa hatukupata hasara ya moja kwa moja kwa sababu wameenda kufanya kazi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa hiyo, nadhani siyo jambo baya, lakini tutaendelea kuhakikisha kwamba vyuo vikuu vinazalisha wahadhiri wengi zaidi kadri iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejitahidi kugusa baadhi ya maeneo yale ambayo yameguswa na Waheshimiwa Wabunge wengi, lakini nizungumzie hili la maslahi ya watumishi na hasa kwa mguso mkubwa wa maslahi na motisha kwa walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba walimu wana majukumu makubwa. Ni kweli kama ilivyosemwa hapa kwamba walimu wanafanya kazi mpaka muda ambao ni wa ziada na ni kweli kwamba walimu katika nchi yetu tumewadogosha. Nadhani Serikali tumesikia, Serikali imesikia, tutatafakari na ndiyo maana sera ya elimu na walimu katika nchi yetu sasa imeboreshwa ili kuhakikisha kwamba tunapata walimu bora na wazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma kidogo walimu walikuwa wanachukuliwa wale walimu wale wa division one na two hukuti mtu akiwa mwalimu. Ifike mahali sasa wa division one na two ndiyo wanaotakiwa kusomea ualimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukizungumzia masuala ya maslahi, hakutakuwa na hiyo dharau au mindset iliyokuwepo. Nilikuwa naongea na Mheshimiwa Profesa Mkenda, naye maoni yake ni hayo na ninadhani wakati wa bajeti yake atalizungumza hili vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana kwamba suala la walimu kuwa na maslahi yasiyotosheleza na wengine kufanya kazi kwenye mazingira magumu bila kuangalia posho za ziada au motisha, limekuwa likisemwa kwa muda mrefu, na kama Serikali tumelisikia na tunalichukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, yaliyosemwa ni mengi, lakini nimejaribu kugusa yale ya jumla, lakini yako yale mahsusi ambayo yamezungumzwa. Liko moja lilisemwa na Mheshimiwa Japhet Hasunga, amesema mambo mengi, lakini niliguse hili moja la upandishwaji wa vyeo. Kimsingi, mpaka sasa upandishwaji wa vyeo siyo automatic, unatokana na performance ya mtumishi husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma tulikuwa na OPRAS na sasa tuna PEPMIS ambayo inapima utendaji kazi wa mtumishi husika kwa siku, kwa wiki, kwa mwezi na kwa mwaka. Upimaji huu unatusaidia sana kwa sababu hausemi uongo. Majukumu yameainishwa na anaripoti kwa siku. Kwa hiyo, kama ni mtoro au kama alikuwa anarandaranda itaonesha kwamba huyu hakufanya majukumu yake ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo huu unatupa matokeo in real time, umekuwa msaada mkubwa na umeboresha sana utendaji, lakini binadamu hawaaminiki, wanaweza wakacheza nao. Kimsingi mtu hapandi automatic, ni lazima awe amefanya kazi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika, wamezungumzia utendaji wa kitaasisi kutimiza malengo. Mfumo wake unaitwa PIPMIS ambao unapima utendaji wa taasisi ili iweze ku-graduate kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine na wenyewe umekuwa na msaada mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa lilizungumzwa jambo hapa linalohusiana na Sekretarieti ya Ajira na majukumu yake kwa mujibu wa sheria, na vibali vinavyotolewa na Katibu Mkuu Utumishi kwa taasisi na baadhi ya mashirika kufanya usaili yenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, sheria inaruhusu hilo kufanyika. Katibu Mkuu Utumishi anaweza akaruhusu taasisi ikafanya usaili wa watu kwa sababu mahsusi. Pili, liko sharti kwamba, pamoja na kibali hicho, bado Sekretarieti ya Ajira itapaswa kuweka macho yake pale kuangalia kama taratibu zote zimezingatiwa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hata kama ajira zitafanyika na taasisi yoyote ile, bado jicho la sekretarieti litakuwepo. Hapa limezungumziwa jambo kuhusu Usaili wa TRA ambao unaendelea sasa na ambao kimsingi bado haujafika mwisho na umekuwa na maelezo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme, maoni yenu Waheshimiwa Wabunge, mawazo yenu na kwa sababu pia Kamati imelisema hili, na kwa idadi kubwa mmelisema, tumeyasikia na tutakwenda kushauriana ndani ya Serikali ili tuweze kuona kama kuna mambo hayako sawa, basi tuweze kuyaweka sawa ili manung’uniko haya yaweze kupungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo lilisemwa na Waheshimiwa Wabunge, ni lile la uhamisho wa watumishi. Kama nilivyosema, uhamisho wa watumishi ni jambo gumu kulitekeleza na tunaendelea kulitekeleza kidogo kidogo, lakini tunaogopa kuleta mtikisiko wa utumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba tuliwaahidi hapa katika Bunge lililopita kwamba tutafanya msawazo na katika huo msawazo tutajitahidi sana ku-balance. Siyo tu wale watakaohama kufuata wenza wao au kwa mazingira mengine ya ugonjwa kwa sababu, jamani watumishi wa umma ni binadamu. Yaani huwezi ukamwambia binadamu, utakaa hapa na nimekwambia utakaa hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba, tija yake hutaiona na kazi hiyo hatafanya, hasa kama unamzungumzia mwalimu anayepaswa kwenda kufundisha halafu ana mke wake, yupo sijui wapi, au mume wake yuko mbali, kimsingi ataingia pale darasani, anachofundisha haelewi na anaowafundisha hawaelewi kwa sababu ana kadhia zinazomkabili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi tunathamini mchango wa watumishi wa umma. Tunaamini hatuna watumishi wa umma wanaotosha, na tunajua mamlaka nyingine hasa Mamlaka za Serikali za Mitaa zinachukia sana kuhamisha watumishi, lakini ni ubunifu tu wa Maafisa Utumishi na Waajiri kuhakikisha kwamba, tunapowapelekea waajiri waajiriwa wapya, basi wana wa-place katika maeneo yale ambayo watumishi wale wametoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kama litakuwa ni jambo gumu nasi tunapochukua hatua hii, tutajitahidi sana kuhakikisha kwamba tunaifanya kwa kuangalia na kushauriana na waajiri ili tusije tukaleta mtikisiko wa utendaji kazi katika maeneo husika. Japo jambo hili kwa kweli watumishi wamelifurahia, ila ni vizuri busara na hekima zikatumika na waajiri kuhakikisha kwamba wanatoa ruhusu kwa watumishi ambao wana changamoto za kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumzwa maeneo mengine ambayo yameguswa na watumishi wengi na hasa hili la Mheshimiwa Joelson Mpina, amezungumzia mambo mengi, lakini niseme tu, yale masuala yote aliyoyaainisha na bahati nzuri umetupatia mchango wake kwa maandishi, tutayachukua na kwenda kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako yanayohusiana na mifumo, na tathmini ya mifumo yana maelezo yake. Pengine kwenye hotuba anaweza akawa hakuipata vizuri, lakini yana maelezo yake. Taasisi nyingi zimefanyiwa tathmini na zimeunganishwa na zinafanya kazi vizuri. Ile takwimu aliyoisoma kwenye hotuba yetu pengine haikueleweka vizuri, lakini kuna maelezo yake. Tutampatia na mifumo mingine yote, imefanyiwa tathmini na inatusaidia sana katika kuboresha utendaji kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mihuri ya wenyeviti, tutajaribu kushauriana na wenzetu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kwa sababu nakumbuka nilipokuwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ndipo hili lilitokea. Kidogo kulikuwa kuna misuse ya hii mihuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama imefika hatua kwamba ina kazi nyingine za msingi, basi tutajaribu kuangalia, lakini muhuri wa Mtendaji wa Kijiji au wa Mtaa nadhani bado upo, ila kuna muhuri wa Mwenyekiti. Kwa hiyo, tutajaribu kuliangalia na lenyewe kwa uzito wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya yote, Mheshimiwa Mpina tutayachukua na kuyafanyia kazi ikiwemo lile la Taarifa ya Tume ya Mheshimiwa Rais ya Masuala ya Kodi. Haya yote ni mambo yanayoendelea kufanyiwa kazi na yote tunayachukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, walizungumizia issue ya ku-graduate kwa wale ambao walikuwa wanasaidiwa na TASAF. Mheshimiwa Naibu Waziri amelizungumzia, lakini kwa sababu limezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge wengi, niseme tu, katika kupata msaada wa fedha pia kuna matumizi yasiyo sahihi ya fedha kwa wanufaika lakini wengi wao kwa kweli wamenufaika na imebadilisha maisha yao sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama kuna makosa, kule kwenye halmashauri zetu, wako Maafisa wa TASAF na tunaishi nao kule, tuwe tunajaribu kushirikiana nao katika kupeleka mawazo yetu na pia kuonesha kama kuna upungufu, basi mnaweza mka-sort out kule kule. Sisi pia kwa upande wa TASAF Makao Makuu, wanajitahidi sana kutumia taarifa wanazozipata kutoka halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja zilizosemwa ni nyingi, lakini niseme tu, kama kuna sifa na pongezi ambazo mmezitoa, zimwendee Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Rais Mwinyi, Rais wa Zanzibar wamekuwa ni manahodha makini sana katika kuendesha nchi yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda katika miradi mingi mikubwa inayofanyika ambayo mingine imesimamiwa na Ikulu na mmeona kwenye taarifa yetu, yote hiyo ni kielelezo kwamba pengine kama siyo utashi na kama siyo nyota ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, utekelezaji wake ungekuwa mgumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaye Rais makini, mwenye maono na mwenye bahati na uongozi wake. Nchi imetulia na haiendeshwi kwa vurugu, lakini bado mambo makubwa yanatokea. Tumekamilisha miradi mikubwa, sina sababu ya kuitaja, ambayo inaipaisha nchi yetu na kuipa heshima sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ukienda kule Zanzibar, Zanzibar ya Mwinyi kweli inang’aa. Zanzibar ya Mwinyi kweli inawaka. Miundombinu ya barabara, bunifu mbalimbali za kuboresha Uchumi wa Zanzibar, uchumi wa utalii na Uchumi wa Buluu, vimeibadilisha Zanzibar kwa kiasi kukubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ninayehudumu katika Ofisi ya Rais, nataka niseme kwamba, nimepata bahati kuhudumu katika Ofisi ya Rais katika kipindi ambacho kumekuwa na mafanikio makubwa kwa Serikali zote mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda niwashukuru viongozi hawa na nichukue msemo aliousema Mheshimwia Prof. Kabudi kwamba, haumpongezi kiongozi wako ila unamshukuru, na ukimpongeza ina maana kuna siku hautampongeza, lakini Mheshimiwa Kabudi anasema, lazima umpongeze kiongozi wako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi tunawashukuru kwa kazi hii kubwa waliyoifanya kwa Tanzania na ndiyo maana nataka nikubaliane na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi kwa kuwapitisha wawe wagombea wetu kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina shaka wale Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, waliyaona haya yaliyofanyika na kwa uhakika walionao juu ya kazi nzuri wanayoifanya wakaona hakuna sababu ya kuchelewa, tuwapitishe ili tukafanye shughuli nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninaamini miaka mitano ijayo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar zitakuwa na mafanikio makubwa na maendeleo makubwa sana sana. Ndiyo maana hata huko duniani kwingine Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akipewa nishani mbalimbali (awards). Tunakumbuka aliyopewa juzi ya Global Goalkeepers Award, ambayo inatambua uongozi na mchango wake katika kuimarisha afya ya uzazi na kupunguza vifo vya uzazi. Hii ni tuzo kubwa na ya heshima kubwa sana duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nikaja kuangalia kumbe tuzo siyo hiyo tu, ziko tuzo karibu 11 katika kipindi cha miaka mitatu. Kuna tuzo ya Babacar Ndiaye, inayotambua jitihada alizozifanya katika ujenzi wa miundombinu bora nchini; tuzo ya Taasisi ya Afrima ya Nchini Marekani, ambayo inatambua uongozi wake wa kimageuzi lakini ziko tuzo nyingine; tuzo ya P-Rain Africa Award; tuzo ya dhahabu ambayo inatekelezwa kutokana na malengo la maendeleo endelevu na tuzo nyingine ya Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuzo ni nyingi, lakini iko tuzo nyingine iliyotolewa na Red Cross; iko tuzo ya hapa nyumbani ya Wizara ya Elimu; iko Tuzo ya Care Impact na ipo Tuzo ya Taasisi ya International Iconic ya kutambua mchango wake katika sekta ya utalii na kuchochea ongezeko la idadi ya watalii hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuzo ya 11 ni tuzo ya Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) iliyotambua mchango wa Rais katika kuleta maridhiano, kuboresha demokrasia hapa nchini na kuimarisha upendo na mshikamano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuzo hizi ni kielelezo kwamba Rais wetu anafanya yale ambayo Watanzania wanayatarajia. Tumshukuru kwa kazi nzuri anayoifanya na tumwombee kwa Mungu amjalie uhai ili katika kipindi kingine cha miaka mitano tuendelee kupata matunda yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, sasa naomba kutoa hoja. (Makofi)