Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza katika wizara hii muhimu ya Nishati na kwanza naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuendelea kutupa afya na uzima ili tuendelee kuwatumikia Watanzania wenzetu waliyotuamini na kutuleta katika jumba hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kabla ya yote niruhusu nitoe pongezi nyingi sana sana kwa kiongozi wetu, Rais wetu, kipenzi chetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya katika Sekta ya Nishati na kutambulika kama champion katika masuala ya nishati siyo tu Tanzania bali Afrika na duniani.
Mheshimiwa Spika, niruhusu pia nimshukuru Waziri mwenye dhamana ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Naibu wake Waziri, Katibu Mkuu na Manaibu Makatibu Wakuu kwa ushirikiano mkubwa ambao wamekuwa wakiutoa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo nami pia naihudumu kama Makamu Mwenyekiti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niruhusu pia nitoe pongezi nyingi kwa kazi kubwa inayofanywa na mashirika yaliyo chini ya Wizara ya Nishati, yaani TANESCO, REA, TPDC, EWURA, PDPA na PURA hapa wapo wananchi wazalendo na wasomi wa nchi yetu wanafanya kazi kubwa sana ya kutafsiri miongozo inayotolewa na nchi yetu kwa vitendo na kuleta tija katika Sekta ya Nishati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kweli ninataka Watanzania wajue kupitia nafasi hii yangu ya mchango, kwamba tunapoona umeme unawaka kama sisi tulivyo humu Bungeni tunapata mwangaza, tujue wapo Watanzania wenzetu saa hizi wataalam wengine wapo chini ya ardhi umbali wa mita 150, au 200 wakiangalia hayo matabani na hizo dira zinazoendesha shughuli za umeme kila siku wanapokezana usiku na mchana. Kwa hiyo, wapo watu wanaofanya kazi kubwa sana ya kizalendo ya mafanikio haya tunayoyaona. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kwanza na kutoa shukrani kwa Serikali kwa mkoa ambao nami pia ni Mbunge wa Kigoma kuunganishwa katika gridi ya Taifa na niseme jambo hili sio tu limeipunguzia gharama TANESCO kwa kutumia umeme wa mafuta ambao ni gharama kubwa na ambao Serikali imekuwa ikiweka ruzuku, lakini pia unachochea uchumi wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivi leo ninavyoeleza hapa Bungeni, tangu umeme wa gridi ya Taifa umekuja kipo kiwanda cha WHI (Tanzania Cement Limited) kimejengwa katika Mkoa wa Kigoma na tarehe 15 ya mwezi Mei kitafunguliwa kuanza kuzalisha cement.
Mheshimiwa Spika, jambo hili litaongeza wigo wa kodi kwa Serikali yetu, litaongeza wigo wa ajira kwa wananchi wetu, lakini pia litaongeza mzunguko wa fedha kwa wafanyabiashara katika mkoa wetu na maeneo mengine. Haya ndiyo mambo tuliyokuwa tunayaomba, tuwe na umeme wa kutosha ili usaidie katika mchakato wa kukuza uchumi wa nchi yetu. Kwa hiyo, nawapongeza sana Wizara ya Nishati na TANESCO kwa kazi kubwa hii ambayo wameifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna jambo limeelezwa hapa katika maoni ya Kamati nami ningependa kuliwekea mkazo, nalo ni uunganishaji wa umeme kwa wananchi wa mijini. Sasa hivi tumeanzisha Mradi wa REA ambao Mradi wa REA wa Nishati Vijijini umesaidia na umefanya kazi kubwa sana ya kuleta maendeleo ya nishati vijijini kwa kuwapelekea wananchi umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 kuunganishiwa umeme.
Mheshimiwa Spika, sasa hii imegeuka kama tatizo tulilonalo sasa hivi ambapo tulifika mahali tukawa tunahangaika sana sana kuwalinda na kuwasaidia kuwainua watoto wa kike, tumefanya hivyo kwa muda mrefu sasa inaonekana sasa inabidi turudi kuwasaidia watoto wa kiume maana sasa na wao wanataka kuharibika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme tumesaidia wananchi wa vijijini kuhusu umeme na nishati, lakini sasa turudi mijini maana tunatengeneza tabaka sasa katika nchi yetu. Wapo wananchi mijini ambao wanaishi mijini, lakini hawana uwezo wa kulipia shilingi 321,000 kuunganishiwa umeme. Sasa wanashuhudia mafanikio makubwa ya matumizi ya nishati vijijini lakini wao wakiwa mjini hawana nishati ya umeme. (Makofi)
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Kilumbe Ng'enda kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jesca Msambatavangu.
TAARIFA
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mchangiaji anayechangia kwa makini na vizuri sana. Pia ugawaji wa mipaka ya nchi yetu kiutawala huwa hatuzingatii hali za kiuchumi za wananchi, hivyo kuanza kuzingatia hali za mipaka kwa kuwahukumu wananchi kwamba wote wachangie kiasi kadhaa kwa sababu wapo kwenye mipaka ya mjini wakati tunapogawa mipaka huwa hatuangalii hali zao za kiuchumi ni kuwaonea wananchi wa mijini waliokaa kwenye kipato kidogo cha uchumi, hivyo kuwanyima fursa za kupata huduma kama hizi za umeme. Ahsante.
SPIKA: Mheshimiwa Kilumbe Ng'enda, unapokea taarifa hiyo?
MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Spika, nimeipokea taarifa na hii inaboresha mchango wangu kwamba sasa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, imeishauri Serikali kupitia bajeti hii kwamba tuone uwezekano wa kuwapa hawa wananchi wa mijini umeme na kulipa kwa awamu awamu kile kiwango cha shilingi 21,000 badala ya kuwanyima na kuwataka walipe kwanza ndipo waunganishiwe umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Kamati inataka hawa watu wapewe umeme halafu katika ankara zao za malipo ya kila mwezi tuweke kiwango cha pesa kama ni shilingi elfu kumi kumi kama ni shilingi elfu tano tano mpaka pale watakapomaliza, kwa sababu tunajua, kuunganisha umeme ni gharama kama hakukuwekewa ruzuku na Serikali TANESCO hawawezi kutekeleza. Kwa hiyo, tunachotaka ni kwamba uwepo utaratibu wa kuchangia wao kwa awamu.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo limeelezwa kwa msisitizo katika Kamati ni suala zima la mchango wa pesa za nje katika bajeti ya Wizara ya Nishati. Hili limeonekana katika mwaka wa fedha uliopita ambapo karibu shilingi bilioni 53.2 hazikupatikana kutoka nje, na hivyo kuathiri mradi wa gridi imara, kuathiri upelekaji wa umeme vitongojini na kuathiri ruzuku iliyotakiwa itolewe kwa PURA na TPDC katika uendeshaji wa shughuli zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme kwamba imeonekana fedha zetu za ndani zimekuwa ni za uhakika zaidi katika utekelezaji wa bajeti kuliko hata tunazoziomba kutoka nje. Kwa hiyo, tunataka Serikali sasa iwe makini kwa kile inachoomba kutoka nje, inapokiingiza kwenye bajeti iwe na uhakika na commitment ya hao wanaokileta kwamba kitaingizwa kwa wakati ili bajeti yetu isiweze kuyumba.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka nilizungumze na niipongeze sana Serikali kupitia Wizara ya Nishati ni suala zima la kupungua kwa malalamiko ya ubora wa mafuta au kutokuwepo kwa ubora wa mafuta katika vituo vya mafuta.
Mheshimiwa Spika, hatua iliyochukuliwa na Serikali kupitia bulk procurement. Hawa PBPA na EWURA, kwa kweli taasisi hizi mbili zimefanya kazi nzuri sana katika kipindi hiki. Ni vizuri ziendelee kupewa nguvu ili ziendelee kufanya kazi kwa sababu huko nyuma kulikuwa na malalamiko makubwa ya magari ya watu kuharibika kutokana na kutokuwepo kwa ubora wa mafuta katika vituo vya mafuta.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi utaratibu wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja umesaidia uwepo wa uhakika wa mafuta, umesaidia ubora wa mafuta, na pia ukusanyaji mzuri wa kodi kupitia mafuta, na hivyo kuwezesha watu kupata mafuta bora katika vituo vya mafuta.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme napongeza hatua hii na ninaomba Wizara iendelee kuzipa nguvu taasisi hizi (PBPA na EWURA) ili mafuta ya nishati yanayokuja katika vituo vyetu yaendelee kuwa bora na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa nilizungumze ni ulipaji wa fidia kwa wananchi. Sisi ambao tunahudumu katika Kamati hii kwa niaba ya Wabunge wenzetu, maeneo tuliyotembelea ambayo yanatakiwa kuwekwa miradi ya umeme kumekuwa na malalamiko makubwa ya wananchi kuchukuliwa maeneo yao kwa miaka miwili, mitatu, minne, au mitano wakiwa hawajalipwa fidia na hawaruhusiwi kuyaendeleza.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kumekuwa na malalamiko makubwa kweli na hili suala la fidia linakwenda mpaka kwenye miradi mingine ya Serikali. Ukienda kule Jimboni kwangu, kuna watu wametoa maeneo yao kwa ajili ya kutaka eneo la uwanja wa ndege liongezwe, lakini ulipaji wa fidia umesuasua kiasi ambacho unazusha malalamiko makubwa sana kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, napenda kuitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na kiongozi mahiri, makini na mwenye huruma kwa wananchi, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, iangalie kwanza kabisa kama tunachelewa kutekeleza mradi, lakini tulipe kwanza wananchi fidia.
Mheshimiwa Spika, nimeona umewasha kisemeo, kwa maana hiyo unaniashiria nishukuru.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru wewe na ninawashukuru pia Wabunge wenzangu. Ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)