Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, kwanza, nami pia nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kunipa uhai na afya njema na kuweza kusimama kwenye Bunge lako hili Tukufu kwa siku ya leo.

Mheshimiwa Spika, nakupongeza sana wewe mwenyewe kwa namna unavyoliendesha ama kutuongoza katika hili Bunge. Nasema kwamba hatukukosea kukupa nafasi hiyo, lakini pia nawaomba Wanambeya 2025 wasikuache nyuma wakurudishe tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, kwa kumsaidia Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, anafanya kazi kubwa sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati pamoja na msaidizi wake Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya kwenye hii Wizara ya Nishati. Kwa kweli hongereni sana Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati pamoja na Mheshimiwa Judith. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, nampongeza Katibu Mkuu na Watendaji wote, wakiwemo Mameneja wetu wa Mkoa wa Geita pamoja na Wilaya ya Nyang’hwale kwa kazi nzuri ambazo wanazifanya. Nawaomba Wanabukombe, wapo hapa, 2025 turejesheeni Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, kwani anafanya kazi kubwa sana na hajawaangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi sana kwenye miradi ya maendeleo kwenye nchi yetu na hususan Wilaya yetu ya Nyang’hwale. Mimi kama mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Nyang’hwale tunasema kwamba Mama anatudai, na hususan kwenye upande wa nishati.

Mheshimiwa Spika, hivi ninavyozungumza, Jimbo la Nyang’hwale lina vijiji 62 na vitongoji 273. Vijiji vyote 62 vina umeme na vitongoji 88 pia vina umeme. Hongera sana Mama kwa kazi kubwa unayotufanyia sisi Wananyang’hwale. Tunasema 2025 tupo na wewe, hatutakuangusha na kura zote tutakupa Mama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza, nianze kwa kuunga mkono hoja hii iliyopo mbele yetu. Ni hoja ambayo imesheheni na imeeleza vizuri mipangilio na mipango mizuri kuhusu masuala ya nishati namna gani tunakwenda huko mbele.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Nyang’hwale sisi tunasema hivi, Mama tunamuunga mkono kwenye lile suala la kusema tunataka tuondoke kwenye kutumia kuni tutumie nishati safi. Sisi Wananyang’hwale tumemuunga mkono na tunafanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nitoe ushauri kidogo kwenye hili suala. Wapo hapa wasambazaji wa mitungi na gesi, tunaiomba Serikali na ninaishauri ipunguze gharama ya mitungi ya gesi, lakini pia na gesi yenyewe kwa sababu wananchi wetu kule vijijini vipato vyao ni vidogo. Wamemuunga mkono na tunakubali kutumia kabisa nishati iliyo salama na nishati nzuri ambayo ni ya gesi, punguzeni gharama za mitungi pamoja na gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi Wananyang’hwale tunasema kwamba usambazaji wa umeme umefanyika, lakini kuna baadhi ya maeneo kwenye Jimbo la Nyang’hwale nadhani pia na kwa nchi nzima, wananchi wamehamasika kuutumia umeme kwa kufunga viwanda vidogo vidogo. Umeme huu umeenea maeneo mengi kwenye Jimbo langu, lakini kuna baadhi ya viwanda vimefungwa zile transformer zimezidiwa.

Mheshimiwa Spika, nawaomba sana Wizara, fanyeni tathmini ya kwenda kuzunguka na kubaini zile transformer ambazo zimezidiwa, mtuwekee transformer kubwa ili wananchi waendelee kufunga mitambo kwa ajili ya uzalishaji wa miradi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna transformer ambazo zilianza kufungwa za KVA 50, kwa kweli zimezidiwa. Pia, naomba nishauri kwamba kwenye migodi yetu midogo midogo pia na penyewe nendeni mkafanye tathmini, transformer zinahitajika ziende kule ili wananchi wetu na wachimbaji wetu waendelee kutumia umeme huu ambao sasa hivi tunao mwingi. Mtuwekee transformer maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Nyang’hwale wananchi wangu wanaulalamikia Mgodi wa Nyanzaga. Nyanzaga wanaenda kuchukua umeme mkubwa kutoka kwenye Mgodi wa Barrick, Bulyanhulu kuupeleka Nyanzaga, lakini kuna wananchi ambao wamepitiwa na mradi huu, wameshafanyiwa tathmini leo takribani zaidi ya miaka mitatu hawajalipwa.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri Mkuu alichukue hilo, awasiliane na hawa; kwa nini hawataki kulipa kwa wakati na sasa hivi ni zaidi ya miaka mitatu tathmini imeshafanywa?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba walichukue hilo ili wananchi wangu waweze kupata hiyo fedha ili iweze kuwasaidia kwa mambo mengine. Kwa leo hii mimi napenda sana kuipongeza Wizara kwa kazi nzuri mliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, naungana na ushauri wa Kamati. Leo hii Serikali imeamua kumfungia umeme mwananchi wa kijijini kwa gharama ya shilingi 27,000 lakini kuna wananchi ambao wapo mjini na maisha yao na nyumba zao ni kama zile za watu wa vijijini. Kwa nini, na hawa wananchi waliopo mjini na hasa ambao wapo kwenye ile miji inayonyanyukia mfano Mji wa Kharumwa, nao wasifungiwe kwa shilingi 27,000 tuondokane na ile shilingi 500,000 ama zaidi ya shilingi 500,000? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ukiangalia tunawapelekea umeme vijijini kwa gharama ya shilingi 27,000 na yawezekana yule unayempelekea umeme huo, mteja yupo mbali anataka apelekewe kwa nguzo tatu au nne. Huyo huyo aliyepo mjini hahitaji hata nguzo moja, ni kuvuta tu waya, kwa nini naye asilipe gharama ya shilingi 27,000?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali na kuishauri ijaribu kuangalia hizo sheria kwamba na sasa tuwafungie hawa kwa shilingi 27,000 ili tuweze kuwaongezea na wao kuweza kutumia umeme wanufaike kama wale watu wa kijijini. Leo hii unakuta mtu ana nyumba ya kawaida kabisa mjini lakini kijijini ana nyumba nzuri kabisa anaenda kufungiwa kwa shilingi 27,000. Huyu mwenye kipato cha chini na nyumba yake ni ya kawaida ananyimwa umeme kutokana na kwamba hana uwezo, lakini uwezo wa shilingi 27,000 anao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawaomba sana chukueni ushauri wa Kamati kaliangalieni upya. Wapo wananchi mjini, lakini uwezo wao ni mdogo, nao wafungiwe kwa shilingi 27,000.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)