Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Shukrani Elisha Manya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu, ambaye anaomba bajeti ya shilingi trilioni 2.2 ili kuweza kutekeleza majukumu yake kwa mwaka ujao wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitangulie kuunga mkono hoja, lakini pia nikiungana na maoni ya Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, moja ya eneo ambalo Serikali yetu imefanya vizuri sana katika hatua ya maendeleo ni katika kutoa huduma ya nishati. Hii imetokana na ukamilishwaji wa Mradi mkubwa wa Bwawa la Nyerere na ule Mradi wa Rusumo ambayo ni miradi ya hivi karibuni iliyokamilishwa katika awamu hii.

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, ni kweli kwamba tumekuwa na nishati ambayo ni imara na ni furaha kwa Watanzania kwamba tumeweza kufikia hatua hii ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, nawapongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Naibu wake na Watendaji Wakuu wote wa Taasisi za Wizara hii ambao kwa utaalamu wao na ushirikiano wao wameweza kutufikisha hapa ambapo Watanzania tuna furaha kwa sababu ya hatua hii kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yote haya yameweza kutufikisha kuwa na uwezo wa Gigawatt nne za nishati katika nchi yetu. Nikisema Gigawatt nne nina maana ya zile zile Megawati 4,000 ambazo ndiyo capacity yetu kama Taifa. Ni kweli kwamba pia Serikali imeendelea na ukarabati na uboreshaji wa gridi ya Taifa kwa ujenzi wa njia za kusafirisha umeme katika maeneo mbalimbali katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili tunaomba Wizara yetu na Serikali yetu iendelee na jitihada hizi na kwa kutumia REA, basi nishati ya umeme iweze kuwafikia hata wale wa vitongoji ambavyo bado havijafikiwa na umeme.

Mheshimiwa Spika, utakuta maswali ya Wabunge wengi wakati wa maswali na majibu ni kuhusu vitongoji ambavyo havijafikiwa na umeme. Kwa hiyo, tunaomba hatua inayofuata sasa iweze kuhakikisha kwamba vitongoji vyote nchini vinafikiwa na huduma ya nishati ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kuboresha njia za usafirishaji umeme, naomba niwakumbuke Watanzania waliopo visiwani, maana mimi natoka Ukerewe na Ukerewe ina visiwa vingi sana, 38 kwa ujumla wake. Kwa sababu ya njia za usafirishaji umeme kuwa chakavu, mara nyingi sana umeme unaofika visiwani hata mahali pale kwenye gridi ni umeme ule ambao umepungua nguvu, na kwa jinsi hiyo unakuwa hauwezi kutosheleza mahitaji ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiacha kwamba umeme huu unafika ukiwa na uwezo mdogo sana, wale ambao hawapo kwenye gridi na badala yake wanatumia zile gridi za solar, mahitaji yao ni makubwa kuliko uwezo wa zile gridi za solar. Mara nyingi umeme huu unapatikana kwa saa chache katika siku nzima. Kwa hiyo, inakuwa kama kuwepo kwa zile mini grid za solar katika visiwa hivi haziwasaidii sana wananchi kwa sababu nyakati nyingine umeme unapatikana mchana pekee yake, halafu usiku inabaki ni giza na hivyo inaonekana kwamba suluhisho yawezekana siyo tu hizi mini grid. Wizara ione jinsi ya kuwafikishia gridi ya Taifa hata wale walio katika visiwa pale itakapokuwa inawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, utagundua bado eneo la uchimbaji mdogo linahitaji kufikishiwa umeme ili waweze kufanya shughuli zao kwa gharama ambayo ni nafuu. Hili ni eneo ambalo pia Serikali inaweza ikaliangalia ili uchumi wetu uweze kuwa jumuishi na watu wote waweze kufurahia maendeleo ambayo yamepatikana kutokana na kuongezeka kwa nishati nchini.

Mheshimiwa Spika, nirejee katika vyanzo vyetu vya nishati ya umeme. Katika taarifa na hotuba ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu ameitoa, vyanzo vyetu vinaendelea kuwa maji yanatoa asilimia karibu 70 halafu na gesi asilia kama 25% hivi lakini umeme wa jua ni 0.1% pekee.

Mheshimiwa Spika, sasa tutakapokuwa na viwanda vingi na shughuli nyingi za uchumi zimechachamaa hapa nchini, Gigawatt nne haiwezi kuwa ni umeme tutakaojivunia sana. Hii inatupelekea kwamba lazima tuone sekta hii ni sekta ambayo ni dynamic, itahitaji kuongeza vyanzo vingi sana vya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa umeme wetu mwingi 70% unatokana na maji, lazima kama Serikali tuweze kuona kwamba kuna kihatarishi cha mabadiliko ya tabianchi. Kwa hiyo, hili ni jambo ambalo katika mipango yetu kila wakati kama Wizara ya Nishati lazima tuliangalie kwamba umeme wetu mwingi unatokana na maji na maji ni jambo ambalo linaweza likaathirika haraka sana na mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa jinsi hiyo, mradi wetu wa LNG ni mradi mkubwa. Tungeomba sana yale majadiliano baina ya Serikali na kampuni za nje yaweze kukamilika kwa wakati na kwa sababu ni mradi mkubwa wa kimkakati na kwa sababu pia utahusisha kusainiana mikataba, tujifunze kutoka uzoefu wa nyuma, maslahi ya Taifa yazingatiwe sana katika mradi huu mkubwa wa LNG. Ikiwezekana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu atuambie hata angalau kwa kionjo, lini tutarajie kukamilika kwa mradi huu mkubwa wa LNG? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, Mradi wa CNG ni mradi mzuri. Wale ambao tunatumia Uber kule Mjini Dar es Salaam, mtu wa Uber anakwambia akiweka gesi yake pale ya shilingi 15,000 anasafiri mwendo mrefu kweli miezi inakatika. Sasa tungeomba Mradi huu wa CNG uongeze vituo katika hii njia kuu ya Dar es Salaam hadi Dodoma na Mwanza kuwe na vituo vya kutosha ili watu wengi waweze kuwa na hakika ya kwamba nikifunga gesi kwenye gari yangu, basi nikifika kule Dodoma au Mwanza nina sababu ya kutoathirika nikarudi tena kwa chanzo kingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa way forward; wapi tuelekee? Wenzetu wa Kenya ambao tupo nao katika bonde la ufa, uwezo wao wa kuzalisha jotoardhi ni Megawati 890. Sisi potential yetu kama Taifa ni Megawati 650, ningetamani kwamba tuendelee kuweka fedha nyingi huko ili tafiti zinazoendelea zikamilike ili hiki nacho kiweze kuwa chanzo ambacho kitakuwa kina-boost pale mabadiliko ya tabianchi yanapokuja, tunajua tunaweza tukaenda upande wa pili wa jotoardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, dunia imeanza kupinga matumizi ya makaa ya mawe kama chanzo cha nishati. Naomba tusiache wakati bado nafasi hii ipo na yenyewe kiwe ni chanzo ambacho mnaweza mkakitumia.

Mheshimiwa Spika, pia katika literature, Singida na Makambako ni mahali ambapo upepo wake unaweza kuzalisha umeme, ningetamani katika hotuba zijazo za Wizara ya Nishati, tuwe tunakumbuka chanzo hiki hata kama kwa sasa hatukitengei fedha, lisiwe ni jambo ambalo litaondoka katika mipango yetu kwa sababu speed ya upepo tayari ipo, inajulikana, ni suala la kuweka turbans na kupata namna nyingine ya kupata njia ya nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwa sababu naona umewasha kisemeo, niseme kwamba wananchi wanachotamani ni kupata umeme wa kutosha, na umeme unaopatikana kwa bei nafuu. Nadhani malengo ya mwisho kabisa ya Serikali yawe ni kuona kwamba umeme wetu unapatikana kwa bei ambayo kila Mtanzania ataweza kumudu, na kwa jinsi hiyo uchumi wetu utakuwa unawagusa watu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)