Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na siku ya leo tupo humu Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, nampongeza kwa namna kubwa ameendelea kutuwakilisha vizuri Watanzania. Mheshimiwa Rais ameendelea kufanya kazi katika mikoa yote. Ni sawa sawa nikisema sisi wamama nyumbani unaweza ukawa na watoto 20, lakini wote unawahudumia. Ndivyo Mheshimiwa Rais ameendelea kuhudumia watoto wake wote bila ubaguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakupongeza pia kwa kuendelea kusimamia hili Bunge. Nisiposema nitakuwa nimejidhulumu. Nakupongeza sana, umeendelea kutuongoza vizuri kwa upendo, na kwa kutumia nafasi hii nawaomba wananchi wa Mbeya, nami nimewahi kuwa mkazi wa Mbeya; wananchi wa Mbeya wananisikia, na watendaji wenzangu wananisikia, Mungu akitujalia 2025 ukapate kura nyingi za kishindo. Nawaomba wananchi wa Mbeya wasipoteze tunu hii ambayo Mwenyezi Mungu amewajalia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe. Pongezi nyingi sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, ameendelea kumsaidia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika majukumu aliyompatia. Nasi Wanabukombe tunajivunia yeye, wananchi wa Geita kwa ujumla tunajivunia yeye kwa sababu ni mtoto wetu. Ameendelea kuwa kinara akituwakilisha vizuri na Watanzania wote wanaijua Geita na Watanzania wote wanaijua Bukombe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaamini wanawake wa Bukombe na wananchi wote tumejipanga, hakuna kura itakayopotea juu yake. Nampongeza mdogo wangu Mheshimiwa Judith Kapinga. Nimeendelea kumfuatilia, ameendelea kufanya kazi vizuri, kujituma, Mungu ambariki sana Mheshimiwa Judith Kapinga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa ninaomba nijielekeze kwenye mchango wangu. Nina mambo mawili tu machache. Mwaka 2024 nilisimama nikachangia hapa, nikazungumzia Bwawa la Mwalimu Nyerere, wakati huo nilitamani kuingia na kile kipimo ambacho kilikuwa kinaonesha, maana niliangalia kilikuwa kinaonesha mafundi wapo kazini, wanachapa kazi; leo nimesimama kuishukuru Serikali yangu ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ninavyoongea hivi Bwawa la Mwalimu Nyerere limeshakamilika, na hivi lina uwezo wa kuzalisha megawati 2,115. Nani kama Dkt. Samia Suluhu Hassan? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ifike mahali Watanzania tuambiane ukweli, mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Mheshimiwa Dkt. Samia ameendelea kufanya kazi kubwa katika nchi hii. Nawaomba Watanzania, ifikapo mwaka 2025 na ndiyo tuko sasa hivi Oktoba, twendeni tukamuunge mkono Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Spika, niwaulize ndugu zangu, ni nani aliyewahi kumchukia mzazi wake? Mtu mmoja asimame aniambie ni nani ambaye amewahi kumchukia mzazi wake? Kila mtu anampenda mzazi wake, ndivyo ambavyo Mheshimiwa Rais amesimama kwa watoto wake wote kuendelea kutulea na kututunza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema katika vilindi vya moyo wangu, na wewe unanifahamu vizuri mdogo wako, huwa sifichi, ndivyo ninavyosema, ifike mahali, watu wanaotaka kutugawa tuwakemee kabisa washindwe, sisi tusonge mbele, Taifa letu liwe la mfano na tumtangulize Mungu.
Mheshimiwa Spika, ninavyoongea hivi, katika Mkoa wangu wa Geita ufikishaji wa umeme kwenye Wilaya zangu zote tano ni 99.9%, sawa sawa na 100%. Nisiposema hapa, nitasemea wapi? Nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, amefanya kazi kubwa sana ya kumsaidia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mungu akubariki sana na sisi tunaendelea kukuombea baba, uendelee kupiga kazi, uendelee kumheshimisha Daktari wetu Samia nasi tunamwombea Mheshimiwa Rais wetu, tunamwahidi Mkoa wetu wa Geita anatudai, tunasubiri muda ufike tukaweke tiki tu, tulipe deni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kudaiwa ni kubaya, tunadaiwa, tuna deni na dawa ya deni ni kulipa. Nasi tumekubaliana wananchi wa Geita tutalipa deni Oktoba.
Mheshimiwa Spika, Geita shughuli kubwa ni uchimbaji wa migodi. Ninavyoongea hivi, kipindi cha nyuma migodini walikuwa wanatumia mafuta kusaga yale mawe, majenereta, lakini Serikali yangu ya Awamu ya Sita imeendelea kuwasaidia wachimbaji wadogo, wachimbaji wakubwa, na kwa wachimbaji wadogo wadogo ufikishaji wa umeme katika migodi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninajua mwanzo ni mgumu, lakini najua tutafikia pazuri. Serikali imeshaanza kuwafikishia umeme migodini, nawaomba Watanzania, hata leo mama ukishajifungua hospitali unapewa katoto kadogo, unaanza kukalealea kidogo mara kanatembea. Ninaamini ufikishaji wa umeme katika migodi ya Mkoa wa Geita tunaenda kufanikiwa kwa kiwango kikubwa sana. Naiomba Serikali yangu, Mheshimiwa Waziri unanisikia hapo baba yangu, ninaamini wataongeza kasi na wakandarasi wapo kazini.
Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Meneja wa TANESCO wa Mkoa wangu wa Geita Ndugu Joakim. Meneja yule hata upige simu una shida yoyote, anatekeleza vizuri pamoja na Mameneja wa Wilaya akiwemo Meneja wa Wilaya yangu ya Mbogwe, nimemsahau jina. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, Meneja wa Wilaya Ndugu Lugiko, kukiwa na changamoto yoyote ukimpigia simu anafanya kazi. Hivyo ninamshukuru sana Naibu Waziri Mkuu pamoja na Naibu Waziri wa Nishati kwa kuendelea kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, na ninawaomba Watanzania wote kwa sauti hii twendeni tukampe Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan maua yake, naomba kuwasilisha. (Makofi)