Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja iliyopo Mezani ya Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu. Jambo la kwanza naunga mkono bajeti hii na ninaunga mkono maoni yote ya Kamati yale ambayo wameyapendekeza, nami nitakuwa na mambo machache. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza nawapongeza Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na Watendaji wote wa Wizara kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Hii ni kwa sababu, hii ni Wizara ambayo ina mambo mengi kidogo ambayo yanahusu nishati kwenye Taifa letu, nawapongeza sana.
Mheshimiwa Spika, kazi yao ni njema na kuna wakati wanapitia misukosuko fulani, lakini wamekuwa pamoja nasi kutokana na ukatikaji wa umeme, unakuwa unajumuisha Taifa zima na muda mwingine Watanzania wanakuwa hawajui changamoto ni nini? Hata hivyo wamekuwa wakisimama pamoja na kuisimamia Wizara vizuri na kufanya vizuri hadi sasa hivi hali ya umeme imetulia nchini na nampongeza sana kwa hatua ambayo Mheshimiwa Waziri amekuwa akiifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kubwa ni kuwa mkweli kwamba, kunapokuwa na changamoto Watanzania unawaambia kuna changamoto; kunapokuwa kumetatuliwa Watanzania tunaona kumetatuliwa, hii imekuwa ni sifa ya Mheshimiwa Waziri kwamba ni Kiongozi ambaye pia amekuwa ni muwazi na mkweli kwa Watanzania na ndiyo maana mambo yamekuwa yakienda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya, hususan ya kampeni yake ya nishati safi ambayo inamfanya abaki kuwa champion kwenye ulimwengu huu na kwa Afrika kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi, vilevile kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Niseme wazi, tunapomzungumzia Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana na Watanzania lazima wafahamu, mambo mengi ambayo yanaendelea kwenye nchi yetu Mheshimiwa Rais amejitahidi kwa level kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, ninazungumza tu kwa mfano mambo machache ambayo Mheshimiwa Rais ameyafanya. Ukiangalia tu kwenye suala la usambazaji wa umeme vijijini, Mheshimiwa Rais alikuta ipo zaidi ya 52% lakini sasa hivi amepeleka zaidi ya 100% kwenye usambazaji wa umeme vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapomzungumzia Mheshimiwa Samia, tunamzungumzia Mheshimiwa Samia ambaye alikuta Bwawa la Mwalimu Nyerere lipo kwa 20% na sasa hivi limekamilika. Hizi ni jitihada za Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapomzungumzia Mheshimiwa Rais, tunazungumzia SGR ambayo ilikuwa na 49%, yaani unazungumzia ni 100% imekamilika. Unapomzungumzia Mheshimiwa Samia unamzungumzia Samia ambaye Makao Makuu ya Mahakama ambayo juzi ameizindua ilikuwa 30% na sasa hivi ni 100%.
Mheshimiwa Spika, unapomzungumzia Samia, unazungumzia Mji wa Serikali alioukuta una 20%, leo una 89% katika ujenzi. Kwa hiyo, tunapomzungumzia Mheshimiwa Rais, tunajua tunamzungumzia kwa takwimu na tunamzungumzia Rais ambaye amefanya kazi katika upana na ukubwa ambao kila mmoja anatakiwa ajivunie. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumhakikishie Mheshimiwa Rais, sisi kama Wabunge na wawakilishi wa wananchi, tunamuunga mkono katika uchaguzi wa mwaka huu, atembee kifua mbele kwa sababu sisi tupo pamoja naye. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mchango wangu utakuwa na mambo machache sana ambayo yamejikita kwenye Jimbo la Makete na wananchi wa Makete. Jambo la kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Kamati ya Bunge, nawapongeza kwa kufika Makete na kwenda kujua changamoto za umeme kwenye Jimbo la Makete. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Makete wakati tunaingia mwaka 2020 kwenye nafasi ya Ubunge, katika vijiji 93 ni vijiji 32 tu vilikuwa na umeme. Leo ninavyozungumza vijiji 93 vyote vimepata umeme na kijiji ambacho kilikuwa kinasumbua kijiji cha Kiguru, Mkandarasi amepatikana na anaendelea na kazi. Namshukuru sana Mkurugenzi wa REA kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa sababu kile kijiji kilikuwa kinasumbua, tunawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni rahisi mtu aliyeko Mjini kuizungumzia Makete kama unazungumzia kamji kadogo hivi, kutoka Kata moja kwenda Kata nyingine unazungumzia zaidi ya kilomita 150. Unazungumzia mazingira ambako kuna mabonde, kuna milima, kuna miinuko, wananchi wanapoona umeme umefika huko, kwa kweli wanaipongeza sana Serikali. Hata Mbunge mwenyewe, kuna eneo ukifika huamini kama umeme umefika kwenye lile eneo, ni kwamba Serikali imefanya kazi kubwa kwenye usambazaji wa umeme vijijini.
Mheshimiwa Spika, jambo kubwa tu ambalo tunaliomba ni kwamba, kuna vijiji ambavyo kumekuwa na changamoto ambayo Mheshimiwa Kirumbe Ng’enda, Makamu Mwenyekiti wa Kamati amezungumza, kwamba Makete mvua inanyesha sana. Kwa hiyo, radi zimekuwa zikipiga sana, kwa hiyo, kumekuwa na changamoto kubwa ya kuungua kwa transformer kutokana na radi nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaiomba Serikali, maeneo haya ambayo yana mvua, tuweke sana mitego ambayo inaweza kuwa inanasua hiyo changamoto ambayo tumekuwa tukiipata. Unakuta muda mrefu wananchi wanakosa umeme kwa sababu ya kubadilisha transfoma zinazoungua kutokana na radi nyingi. Kumekuwa kukitusumbua kwa muda mrefu, mathalan Kata ya Lupila, Kata ya Ukwama, Kata ya Ipepo, Kata ya Mbalache, haya ni maeneo ambayo yamekuwa na changamoto kubwa sana. Wananchi wanaomba sana muwasogezee huduma ya kupambana na radi ili kusiwe na kuungua mara kwa mara kwa transfoma hizi ambazo zimekuwa zikisambazwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kitu kingine, sisi tuna Bwawa la Rumakali, ambalo ni la pili baada ya Mwalimu Nyerere endapo litejengwa. Kwa kuwa hili ni bwawa ambalo wewe Mheshimiwa Waziri wa Nishati ulifika Makete na kwenye eneo ambalo maji yanapatikana, tunawaomba, wananchi wa Makete kwa muda mrefu wamekuwa wakisubiria ndoto hii iweze kutimia ya kuhakikisha kwamba mradi unaanza kujengwa, na tayari mlishaweka alama kwenye eneo hilo ambalo mradi utakuwa unapita lile bwawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili eneo wananchi wamesimamisha shughuli za kiuchumi kwa takribani inaenda miaka miwili sasa wakisubiria mradi utekelezwe. Tunatamani sana muweze kutuambia na kutupa majibu, ni lini fidia italipwa ili watu walipwe, wapishe lile eneo na mradi uanze kutekelezwa?
Mheshimiwa Spika, Prof. Manya amezungumza hapa, moja kati ya marejeo ambayo aliyazungumza Mheshimiwa Waziri alisema, “kwa nini tumefika leo hapa, umeme unakatika mara kwa mara au tuna shortage ya umeme nchini?” Alisema kuna wakati tulijisahau hatukuongeza vyanzo, kwa hiyo, matumizi ya umeme yameongezeka. Usambazaji wa leo umesambaa na matumizi ya umeme yamekuwa ni makubwa, kwa hiyo, vyanzo vingi vimezidiwa nguvu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ilikuwa ni hoja yake ya msingi sana, ninaamini anaendelea kusimamia hoja hiyo, kwa sababu kama tutajenga Bwawa la Rumakali pale Makete, tukaenda kuzalisha umeme wa upepo kule Makambako, tukaenda kuzalisha umeme wa upepo kule Same, tukiongeza vyanzo hivi, tunaamini kabisa kwamba, tukiwa na umeme toshelevu unaweza kutusaidia kwa sababu nchi yetu ni nchi ambayo inaelekea kuwa na viwanda na migodi mingi, kwa hiyo, tunahitaji matumizi makubwa ya umeme.
Mheshimiwa Spika, mathalan, Geita Gold Mining ni mgodi ambao umeme wake unaotumika pale unazidi matumizi yote ya Mkoa wa Iringa. Mkoa wa Iringa umeme wanaotumia hauwezi kufikia matumizi ambayo yanatumika kwa mwezi ndani ya Geita Gold Mining. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa kama migodi hiyo ikiwepo 10 au 20 na kwa sababu madini yamekuwa yakiibuliwa mara kwa mara tunatamani kuwa na umeme mwingi, nasi Makete tuingie kwenye rekodi ya kuzalisha na kulifaidisha Taifa kwenye uzalishaji wa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wananchi wa Makete wamenituma nimwombe sana Mheshimiwa Waziri na Wizara ya Nishati na wataalam wake hapa, watusaidie upatikanaji wa umeme kwenye Bwawa la Rumakali.
Mheshimiwa Spika, hii imekuwa ni story ya muda mrefu sana, mimi tokea nazaliwa nasikia kwamba kuna mradi huo na wameonesha kwamba kuna green light inakuja ya kuanza kutekeleza mradi huo, lakini sasa ni lini wanaanza kulipwa? Tunatamani waanze kulipwa mapema ili wapishe na mradi uanze. Nasi tumeupokea mradi ule kwa mikono miwili na tupo tayari kutoa ushirikiano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine tunaipongeza Serikali, Makete toka mwaka 1997 tulikuwa tunatumia lane ya umeme ya kutokea Mbeya, lakini mwaka huu wa 2024 mwezi Novemba, mmetubadilishia line sasa tunachukulia Njombe kuelekea Makete.
Mheshimiwa Spika, lane hii imetufanya tuwe na umeme wa uhakika kwenye Jimbo letu, kwa sababu tulipokuwa tunatumia umeme wa Makete tulikuwa hatuna substation, kwa hiyo, substation ilikuwepo kule Mbeya na ikawa inazidiwa nguvu, lakini sasa hivi substation tuliyonayo imejengwa Wanging’ombe inayotusaidia watu wa Makete, kidogo kumekuwa na uimarishaji wa upatikanaji wa umeme Jimbo la Makete. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaomba sana sana, changamoto ambazo zimejitokeza za kukatikakatika umeme muweze kuzitatua kwa sababu substation bado haijatengamaa, lakini tunaamini kwa jitihada ambazo Wizara hii imekuwa ikifanya mnaweza mkatusaidia utulivu wa umeme kwenye ile lane ya kuelekea Makete ukapatikana na wananchi wa Makete wakapata umeme wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivyo nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kwa sababu umeme wa Makete uliletwa na Mzee wangu Tuntemeke Mesaka Nnun'gwa Sanga, nami sasa nimekuja kubadilisha lane, nimeitoa kutokea Njombe kuelekea Makete, hii inatufanya tubaki kuwa na rekodi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni la energy saving campaign. Kama nchi ni lazima tukaanza kuwa na energy saving campaign ili kuelimisha Watanzania. Matumizi ya umeme ni sahihi lakini ni lazima tuwe na matumizi sahihi ya umeme.
Mheshimiwa Spika, Watanzania wengi tumekuwa na behavior, unaweza ukawasha umeme ukaacha taa zinawaka siku nzima na maeneo mengine tumekuwa tukifanya hivyo. Ni muhimu kama nchi tukaiga utamaduni wa Mataifa mengine ambavyo wanafanya kama Wizara, kuwa na kampeni ya energy saving. Hiki ni kitu muhimu sana kwenye nchi, siyo tu kuzalisha umeme. Tunazalisha umeme ndiyo, lakini je, tuna-save ule umeme? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana teknolojia zimekuwa zikija, kwamba, kwa sababu ya behaviours za binadamu anatoka chumbani bila kuzima taa, kwenye hoteli watu wameanza kufunga appliances ambazo mtu ukitoka umeme unajizima kwa sababu, watu wamekuwa hawana utamaduni wa kutunza energy.
Mheshimiwa Spika, kama Taifa ni lazima tuwe na utaratibu wa ku-save energy ambayo tuko nayo, ili tuweze kuendana na mifumo ya kiuchumi na kusaidia watu wetu wa TANESCO na line nyingine kuendelea kupata umeme kwa uhakika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, natamani sana energy saving campaign iwe ni moja kati ya kampeni yao, kutoa vipindi kwenye TV, shuleni na kuielimisha jamii, kwamba, unapotoka ndani ya nyumba yako uwe na tabia hii ya kuzima taa, kuzima switch, ili kuhakikisha kwamba, tuna-save umeme kwenye nchi yetu kwa sababu, matumizi ya umeme yamekuwa ya kiholela sana, kitu ambacho siyo sahihi kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nami nakutakia kila la heri kwa sababu, tunaamini kwa jitihada kubwa ambazo unazifanya na uwakilishi wako kwenye Bunge la Umoja wa Mabunge Duniani, umekuwa ukitupa heshima, kama nchi. Sisi kama Waheshimiwa Wabunge, tunajivunia na tunawaomba Wanambeya kwamba, wakupe haki yako, wakurejeshee haki yako na kwamba, mwezi wa Kumi na Moja mwaka huu uwepo hapa kwenye kuapa pamoja na sisi. Ninaamini kabisa kwamba, utaendelea kuipeperusha bendera ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunakutakia kila la heri na tupo tayari, kwa sababu, sasa hivi tunajiandaa kwenda kwenye Tulia Marathon kule Mbeya, tutaenda kuwatangazia pia kwamba, tunamhitaji Mheshimiwa Dkt. Tulia tena ndani ya Bunge letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, Mungu akubariki sana. (Makofi)