Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukerewe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Naanza kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, ambaye kwa mara nyingine katupa fursa ya kusimama kutoa mchango wetu, hususan kwenye bajeti ya Wizara hii ya Nishati.
Mheshimiwa Spika, naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa uwasilishaji mzuri pamoja na Kamati, zaidi kwa utendaji wake katika Wizara hii. Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati hongera sana na Mwenyezi Mungu akubariki wewe pamoja na Naibu wako na timu nzima mnayoshirikiana nayo kwenye Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais. Kihistoria huko nyuma tulikuwa na changamoto nyingi sana kwenye sekta hii ya nishati, lakini leo tunapojadili Hotuba ya Bajeti ya Wizara hii kuna mabadiliko makubwa, mojawapo ikiwa ni kuongezeka kwa kiwango cha umeme tulichonacho.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2024 wakati tunajadili tulikuwa na megawati 2,000, lakini leo tuna megawati 4,000 baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Nina kila sababu ya kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa sana anayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama wengine walivyotangulia, ninakupongeza wewe vilevile kwa namna unavyoendesha Bunge letu hili. Kwa kweli, wewe ni bingwa sana na Wanambeya wanastahili kukupa unachostahili, kura nyingi na kurudi Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina hoja chache kwenye sekta hii. Kwanza, kuna kazi kubwa imefanyika kwenye Wizara ya Nishati, hususan kwenye kuboresha miundombinu na kusambaza umeme. Kazi kubwa sana imefanyika na tukiangalia kwenye energy mix, proportionality iliyopo katika uzalishaji kwenye njia ya maji, mafuta gesi na kadhalika, imeegemea sana kwenye eneo la maji.
Mheshimiwa Spika, kama walivyosema wachangiaji kadhaa, natamani pia tuwekeze kwenye eneo la upepo pamoja na nishati ya jua. Hii inaweza kutusaidia sana kujenga uwiano mzuri na kuwa na tahadhari iwapo linaweza likatokea lolote kwenye eneo moja ambalo tumewekeza sana, ambalo ni eneo la maji.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwenye energy mix ninashauri vilevile tuwekeze sana kwenye eneo la umeme jua pamoja na upepo. Kwa sababu, ninaamini, kama Taifa, tuna maeneo mazuri tu ambayo tunaweza kuwa na vyanzo vizuri vinavyoweza kutusaidia kupata umeme wa uhakika kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, nije kwenye Jimbo la Ukerewe. Ukerewe, kama yalivyo maeneo mengine nimekuwa nalisema mara kwa mara hapa, tuna changamoto moja kubwa ya kukatikakatika sana kwa umeme.
Mheshimiwa Spika, hii ni kwa sababu, pamoja na kwamba, tunapata umeme kutoka kwenye chanzo cha umeme kutoka Kibara, lakini voltage drop ni kubwa sana mpaka kufika Ukerewe. Kwa maana hiyo, umeme unapofika Ukerewe; moja, unakuwa na nguvu kidogo, lakini inapotokea hitilafu yoyote katikati ya safari hapa, Kisiwa cha Ukerewe chote kinaathirika kwa kukosa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa natambua, tuna Mradi wa kuongeza nguvu ya umeme na kuvuta kutoka Bunda kwenda Ukerewe na kujenga substation kwenye eneo la Magea pale Ukerewe. Mradi huu unasuasua sana na ni kwa sababu, baada ya kufuatilia, wananchi wanaopaswa kulipwa fidia kwenye eneo ambako mradi huu unapita, hawajalipwa fidia.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali, Mheshimiwa Waziri tafadhali, wananchi wa Ukerewe wanapata shida sana kutokana na kukatikakatika kwa umeme. Hali yao ya kiuchumi inaathirika, hali ya kipato kwa ujumla wake inaathirika na hali ya kimaisha inaathirika kwa sababu ya tatizo hili la kukatikakatika kwa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba hawa wananchi, basi walipwe fidia, ili huu mradi uendelee kuwa na kasi yake na uweze kukamilika. Ile substation ijengwe, wananchi wa Ukerewe wapate umeme wa uhakika. Kwa hiyo, naomba sana Wizara ilipe kipaumbele jambo hili, ili wananchi wa Ukerewe waondokane na adha ya kukatikakatika kwa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, ni kuhusu umeme wa visiwani. Nimeona kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri, Ukurasa wa 53, inaongelea juu ya usambazaji wa umeme kwenye visiwa 120 kwenye mradi wa kupeleka umeme kwenye maeneo ambayo yako nje ya gridi ya Taifa, Mheshimiwa Manya amegusia katika mchango wake.
Mheshimiwa Spika, Ukerewe tuna visiwa zaidi ya 30. Katika visiwa hivyo, natambua kazi kubwa iliyofanywa na Wizara kwa sababu, ukiondoa visiwa katika vijiji 76 tulivyonavyo, vijiji 14 viko kwenye visiwa vidogo. Vijiji vingine 62 mpaka mwaka 2020 tulikuwa na vijiji 18 ambavyo havikuwa na umeme, lakini leo vyote vina umeme.
Mheshimiwa Spika, pia, vile vijiji 14 vilivyoko katika visiwa vidogo bado vijiji vitatu pekee, ni vijiji 11 ambavyo vimepata umeme kupitia umeme jua, lakini vijiji hivi na vitongoji vyake kupitia kampuni zilizowasambazia umeme, wanapata umeme saa tano asubuhi, saa nne usiku umeme unakatika. Achilia mbali umeme ule wananunua shilingi 2,000 kwa unit. Kwa hiyo, wananchi wanateseka sana, wanaishi maisha magumu na maisha yao ya kiuchumi yanaathirika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mradi huu mnaotarajia kuuleta ninawaomba sana, wananchi wa visiwa hivi wameteseka sana kwa muda mrefu kupitia umeme jua kwa kampuni ambazo zimewapelekea umeme, basi mradi huu uanze haraka na ukamilike haraka. Natamani Ukerewe ndiyo wawe wanufaika wakubwa kwenye mradi huu ili wananchi hawa kutokana na mateso waliyoyapata huko nyuma waweze kusahau uchungu ambao wamekuwanao kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Wizara iliangalie sana hili, lakini mbali na hivi vijiji, kuna visiwa vingine zaidi ya 30 ambavyo bado havina umeme. Kwa hiyo, kuja kwa mradi huu itakuwa ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wale. Mheshimiwa Waziri, nakuomba sana muutumie mradi huu kama mkombozi kwa wananchi wa Ukerewe, hasa wa visiwa vidogo, kwani wanapata wakati mgumu sana na hasa hawa ambao wanapata umeme kupitia umeme jua. Wanalipa unit moja kwa shilingi 2,000 na bado wanapata umeme kwa saa chache sana.
Mheshimiwa Spika, naomba sana Wizara iliangalie kwa uzito mkubwa. Natamani hata wakati wa kuhitimisha hoja, Mheshimiwa Waziri akasema lolote kuhusu maeneo haya ya visiwa vidogo, hasa Visiwa vya Ukerewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, naunga mkono Taarifa ya Kamati. Taarifa ya Kamati katika Ukurasa wake wa 12, wanaongelea juu ya gharama ya kuunga umeme kwenye maeneo ya mjini na vijijini. Ni kweli kwa mwongozo uliopo, kupitia Mradi wa REA ambao umefanya kazi kubwa sana, na ninampongeza Mkurugenzi wa REA, wamefanya kazi kubwa sana. Kwenye Jimbo langu tuna vitongoji vingi sana ambavyo vimepata umeme, na juzi nimepata taarifa, vitongoji vingine 96 vitapata umeme hivi karibuni.
Mheshimiwa Spika, ili kuweka uwiano sawa kwenye gharama ya kuvuta umeme kwenye maeneo haya, tukitoa umeme kwa wananchi wa vijijini kwa shilingi 27,000/= na wananchi wa mjini wakapata umeme kwa shilingi 300,000/= tutakuwa hatutendi haki kwenye maeneo haya. Kuna wananchi wanaishi mjini, sawa, lakini kiwango chao cha aina ya maisha wanayoishi inawezekana wako chini zaidi ukilinganisha na baadhi ya wananchi walioko vijijini.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba liangaliwe hili kupitia taasisi zinazohusika, fanyeni tathmini, mtoe mwongozo mpya ili tujenge uwiano kwenye maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, natoa pongezi kwa Meneja wangu wa TANESCO, Wilaya ya Ukerewe. Pamoja na changamoto zote hizi amekuwa anafanya kazi kubwa sana kuhakikisha kwamba, wanazitatua kwa haraka na wananchi wanaendelea kupata nishati ya umeme. Kwa hiyo, nina kila sababu ya kumpongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, atuangalie sana watu wa visiwa hasa vya Ukerewe ambao tuko off grid. Mazingira yetu ni magumu sana kwenye nishati ya umeme, hasa vile visiwa vidogo ambavyo wananunua umeme kwa bei kubwa, lakini wanaupata umeme kwa saa chache, wanahangaika sana. Naomba sana msaada ili kuwasaidia wananchi hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)