Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Benaya Liuka Kapinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuchangia katika Wizara hii. Kwanza nami naungana na wenzangu kuunga mkono hoja hii kwa asilimia zote. Pili, nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati. Pia, nampongeza Naibu wake Mheshimiwa Judith pamoja na wataalam wote katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninayasema haya kwa moyo wa dhati kabisa, nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kwa namna anavyoitendea haki Wizara hii. Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kabla ya kuwa hapa, alikuwa Waziri wa Madini. Tunaona jinsi alivyoyafanya vizuri mazingira katika Wizara ya Madini. Namshukuru na kumpongeza sana. Akiwa Waziri wa Madini, aliwahi kufanya Mkutano Mkubwa wa Wadau wa Madini, Songea na ilikuwa ni historia kwetu Songea mkutano ule kufanyika. Alitupa matumaini mengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Songea, pamoja na madini mengine, kwetu sisi Mbinga ni wachimbaji wa makaa ya mawe. Kwa hiyo, kulikuwa na mambo mengi yanazungumzwa pale, lakini kupitia yeye na kupitia uratibu wake, alifanya mkutano ule. Kwa kweli, mambo yalikuwa mazuri na sasa kero nyingi zimepungua. Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa yuko hapa kwenye nishati akishirikiana na mdogo wangu, Mheshimiwa Judith, wanafanya kazi nzuri sana. Mheshimiwa Judith ni lazima nikupongeze kwa sababu, umekuwa msaada mkubwa kwa Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunafahamu Naibu Waziri Mkuu ana majukumu mengi na mazito. Kwa hiyo, Mheshimiwa Judith amechukua nafasi hii na anafanya vizuri sana. Hongera sana mdogo wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizi, nije kwenye mchango. Mchango wangu mimi leo, namkushukuru Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu. Nashukuru nini? Wakati tunaingia madarakani, mimi Benaya, hali ya usambazaji wa umeme ilikuwa ni ndogo sana. Nina vijiji 117 na kati ya vijiji hivyo, vijiji 24 tu ndiyo vilifikishiwa umeme. Siyo vyote, vijiji tisa kati ya hivyo 24 kulikuwa na harakati ya kufikisha umeme, Kwa hiyo, tulikuwa na vijiji vingi zaidi ya 96 ambavyo havikuwa na umeme. Leo hii nashukuru na ninafurahi kwamba, vijiji vyote 117 vimefikishiwa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haikuwa rahisi kufikisha umeme kwenye vijiji hivi, ilikuwa ni kazi kubwa sana, kubwa mno, kwa sababu, unaweza kuona upelekaji wa umeme umeanza awamu nyingi tu, lakini ni awamu hii ndiyo umeme umefika katika vijiji vyote 117. Kwa hiyo, ilikuwa ni awamu iliyopita, iliyofuata, lakini awamu hii ndiyo umeme umefika katika vijiji vyote 117. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naweza kuiona kazi kubwa iliyofanywa na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na mdogo wangu Mheshimiwa Judith ya kusukuma umeme kufika kwenye vijiji vyote. Hii ilikuwa ni kazi ngumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa ninampongeza sana Mkurugenzi wa REA, aliwahi kufika mpaka kijijini kwangu ninakotoka. Baada ya kuona kijiji kile kiko pembezoni zaidi na inawezekana pengine umeme usingefika, basi alifika mpaka kijijini. Alipofika pale akanipigia simu, “nipo nyumbani kwako.”

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana na ninampongeza sana Eng. Hassan, ile nayo ilitoa msukumo wa kupeleka umeme kwenye vijiji vile. Sasa tunashukuru umeme huu umefika katika vijiji vyote, lakini kwa sababu, tumechelewa sana sana kupeleka umeme kwenye vijiji hivyo kwa hiyo, tuko nyuma kwa upande wa vitongoji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzi juzi hapa tumefanya Kikao cha RCC, tulikuwa na halmashauri mbili au majimbo mawili; la mwenzangu pamoja na la kwangu, ndiyo tuko chini sana katika upelekaji umeme kwenye vitongoji. Hatujafika hata 50%; sisi tuko chini ya 40%. Mimi katika vitongoji 782 ni vitongoji 293 tu ndivyo tulivyofikisha umeme kwa hiyo, bado tuna mzigo mkubwa wa kupeleka umeme.

Mheshimiwa Spika, ilivyo vizuri, Wanambinga sisi tuna vita ya maendeleo. Sisi huwa hatupendi kukubali mmoja hapa ameweka kitu, mimi nikakosa. Kwa hiyo, sasa hivi Mbinga kuna vita kubwa sana ya kutaka kupata umeme. Nakuomba sana, tulikuwa tuna vitongoji vile 15, najua mchakato unaendelea, lakini sasa awamu hii kwa vile sisi tulikuwa nyuma sana, basi mtupe kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi tuko chini ya 50%, maana yake wenzetu angalau wamevuka 50%. Najua kuna kazi kubwa ya namna ya kupeleka umeme katika hivi vitongoji, ni vizuri tukatembea wote kwa pamoja. Siyo wengi wako mbele sana na wengine wanawabeba wenzao kwa nyuma zaidi ikiwemo Mbinga vijijini.

Mheshimiwa Spika, nakuomba sana, na hapa leo utakapokuja kuhitimisha hoja hii, utupe matumaini. Katika awamu hii unatupa kipaumbele kiasi gani nasi ili tulingane na wenzetu hata tukawazidi zaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine, Mbinga pana changamoto kubwa, nimeisema hapa na niliuliza hapa mara kadhaa. Umeme unakatika sana. Yaani kule umeme kukatika mara 20, ni jambo la kawaida. Kwa hiyo, hali hiyo inasababisha shida sana kwa wafanyabiashara wetu na wajasiriamali. Wengine wamefunga mpaka biashara kwa kuhofia, leo nitaweka kitu, umeme utakatika.

Mheshimiwa Spika, najua iko mikakati ya kupeleka hizi substation na ndiyo ilikuwa ahadi ya Serikali kutuletea substations, sasa nimeangalia hapa sijaona kwa sababu, andiko lenyewe ni refu. Najua unaweza ukatamka kitu, tutaipata lini hiyo substation ili isaidie kwa sababu, watumiaji kule ni wengi mno?

Mheshimiwa Spika, umeme ukifika, wanaotaka kutumia ni wengi mno kwa sababu ya ile niliyosema, vita ya maendeleo. Kila mtu anataka apate umeme. Sisi Wamatengo hatuwezi kukubali wewe una umeme, mimi nikose umeme. Aahaa, lazima na mimi niwe na umeme, ndivyo ilivyo. Hayo ni maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba tupate fursa, sisi Wamatengo tupate fursa umeme ufike, wote tuweke umeme. Ukiona huko kwenye maeneo mengine watu wanasuasua kufungiwa umeme, wewe lete Mbinga, wananchi wote watafunga umeme na tutachangia vizuri, TANESCO watapata fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine, nawapongeza sana kwa hamasa hii ya nishati mbadala na hapa kipekee nampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kafanya kazi kubwa sana katika nchi hii kiasi kwamba, sasa kila mtu ndani ya nchi hii anajua kumbe kuliko kutumia kuni kuna nishati mbadala, kuna gesi. Kwa kweli, hapa inabidi tumpongeze sana mama yetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pale Mbinga pamoja na ugawaji mzuri na usambazaji huu wa gesi, sisi pale tuna makaa ya mawe na makaa ya mawe yanaweza kutumika kwa kuwa, nishati mbadala. Hapa nawapongeza sana akina mama wa Mbalawala, wao muda mrefu wamekuwa wanatoa hamasa ya namna ya kutumia haya makaa ya mawe kwa kupikia na yanapika vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, hamasa hii tuliyoweka ya kusambaza gesi, tufanye hivi hivi kwenye makaa ya mawe kwa sababu, ni ya kwetu, hatuendi kuyachota kwa watu huko, ni ya kwetu wenyewe hapa hapa. Tunayachimba hapa, tunayachakata, yanakuwa rahisi then tunatumia kwa kupikia. Yanaweza kuwa suluhisho zaidi kuliko hii gesi ambayo sasa hivi, pengine zile tulizogawa wengine sasa wamegeuza viti, japo siyo vizuri sana kwa sababu, wanashidwa ku-refill.

Mheshimiwa Spika, ku-refill huko nako ni gharama kidogo. Kwa hiyo, tunaomba tuone ni namna gani tunaweza kuwafanya hawa Watanzania wa kawaida nao waweze ku-refill hiyo mitungi ambayo wanayo. Nina uhakika kwenye maeneo mengi ile mitungi ilivyoisha, pengine watu wengi hawaja-refill. Makaa ya mawe hayana ku-refill, yenyewe ukushayatengeneza ni kuweka tu mkaa mmoja au miwili unapikia vizuri chakula kinaiva. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja. Ahsante kwa kunisikiliza. (Makofi)