Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi jioni hii ya leo niwe mchangiaji wenu wa kwanza. Vilevile namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha jioni hii kupata uhai wa kuweza kusimama kwenye Bunge hili Tukufu na kusema machache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru sana au kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono ya kufanya mageuzi makubwa kwenye Sekta hii ya Nishati. Tukiangalia namna tulivyoweza kumaliza mradi ule mkubwa wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, kwa kweli juhudi hiyo ni kubwa sana. Siyo hivyo peke yake, hata kwenye hii ya kuwa champion wa nishati safi ya kupikia nayo ni juhudi kubwa ameifanya kwenye hii sekta ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio haya yasingeweza kufikiwa, ndoto za Mheshimiwa Rais zisingeweza kufikiwa bila kupokewa vizuri na wasaidizi wake wakiongozwa na Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Doto Biteko na dada yangu Mheshimiwa Kapinga, Watendaji Wakuu na Watendaji wote walioko kwenye Wizara Nishati wakiongozwa na Katibu Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Wizara hii nitakuwa nina mambo makubwa mawili. Jambo la kwanza litakuwa ni maombi, na la pili litakuwa ni ushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyopongeza, baada ya Bwawa la Mwalimu Nyerere kukamilika kwenye makaratasi, tayari tuna ongezeko kubwa la umeme. Naomba tu niseme ukweli hapa, kwamba sisi watu wa Mikoa ya Lindi na Mtwara bado physically hatujapata hili ongezeko kwa sababu bado tuna shida ya kukatikakatika kwa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa napo napongeza sana juhudi za Serikali. Nimeangalia hata kwenye bajeti imo, kwamba Mkoa wa Lindi na Mtwara tunakwenda kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa, ni jambo jema. Ushauri wangu kwenye hili, naomba jambo hili liharakishwe na ikiwezekana Naibu Waziri Mkuu atakapokuja kuhitimisha atuambie sisi watu wa Lindi na Mtwara, hii kazi inakwenda kukamilika lini ili nasi tufaidi hili ongezeko la kuwepo kwa umeme?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwenye hili, Wilaya ya Liwale tunapokea umeme kutoka Maumbika, na kutoka Maumbika mpaka Liwale ni zaidi ya kilomita 300; na ndiyo maana umeme wa kule unakatikakatika sana. Kwa hiyo ombi langu kwenye hili ninaomba tujengewe kituo cha kupoozea umeme Liwale ili huu umeme unapotoka Mahumbika mpaka Liwale, na sisi tuweze kuupata kwa kiwango kinachohitajika na uweze kustahimili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja nilipigiwa simu na mwananchi kutoka Liwale, ananiambia, “Mheshimiwa, hebu waambie hao watu wa Wizara, umeme unavyokatika Liwale ni nafuu wakati ule wa mgao, kwa sababu wakati ule wa mgao tulikuwa tunajua leo hatuna umeme kama siku nzima, lakini sasa kama umeme unakatika kwa siku zaidi ya mara sita, tayari unaunguza vyombo vyetu. Unaunguza majiko, unaozesha vyakula kwenye friji na mambo mengine kama hayo. Wakati ule wa mgao ananiambia kwamba wakati ule tulikuwa na uwezo wa kujua kwamba leo kutwa nzima hatuna umeme, au kesho usiku kucha hatuna umeme. Kwa hiyo, tulikuwa tuna uwezo wa kujipanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana sikubaliani naye sana, lakini jambo aliloniambia, naona kama lina mantiki. Kwa hiyo, naomba sana, sana, sana, hili jambo tuone kwamba na sisi tunahitajika kufanyiwa huo utaratibu wa kuingia kwenye gridi ya Taifa na hatimaye tujengewe substation pale Liwale ili umeme uweze kupatikana kwa urahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais kwenye Nishati Safi ya Kupikia. Hapa napo naomba nitoe ushauri mmoja. Tumejenga shule nyingi sana za sekondari, vituo vya afya na hospitali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ndugu zangu wa Serikalini, watusukilize. Pengine waanze kufikiria, tunapopeleka miradi hii ya ujenzi wa shule na zahanati, hebu waweke na package ya majiko ya gesi. Kwa sababu ukienda kumwulizia Mwalimu Mkuu wa shule fulani, anakwambia ni mpaka apate ile capitation ndipo aweze kukusanya apate fedha za kujenga mtambo wa kutengeneza gesi pale kwenye shule yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili kuungana na Mheshimiwa Rais katika kuondokana na utumiaji wa majiko ya mkaa na kuni shuleni, basi waone namna ya kuwezesha hizi shule zetu mpya tunazozijenga, hata zile za zamani tulizojenga, basi wapeleke package ambayo itaweza kujenga haya majiko ya umeme na kupunguza matumizi ya majiko ya mkaa na kuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, naomba nisisitize kuhusu hili jambo la gharama za kuingiza umeme nyumbani kati ya vijijini na mijini. Kule kwetu Liwale hatuna miji, sisi kule ni vijiji. Sasa unapomwambia mwanakijiji wa pale Liwale Mjini eti kwa sababu tu yuko mjini, wanaita vijiji miji kwamba alipe shilingi 350,000 wakati wenzake wa kule vijijini wanalipa shilingi 27,000, kidogo kunakuwa na kigugumizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hapa naomba niungane na wenzangu wote waliosema hapa kwamba, wapo wakulima vijijini wamepata fedha za korosho, wamejenga majumba makubwa mpaka ma-pub yapo kule, lakini kuingiza umeme anaingiza kwa shilingi 27,000. Mwenzangu na mimi pale mjini amegalagala amepata shilingi zake mia mbili amejenga vyumba vyake viwili na ukumbi, kuingiza umeme shilingi 350,000. Kwa hiyo, unakuta uwiano hauko sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu watafute model nzuri ya kwanza kuwatambua hao watu wa vijijini ni nani wana kipato kikubwa, na nani wana kipato kidogo? Waje na model nzuri. Hata kama wakisema kwamba watusogeze kutoka shilingi 27,000 iende kwenye shilingi 50,000, halafu huyu wamshushe ifike kwenye shilingi 100,000, angalau kidogo unaona kwamba kuna kitu kinatembea hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema tu kwamba watu wanaokaa mijini ambavyo wao wanaviita vijiji miji, kwanza namna ya kuvipata vile vijiji miji, lile jambo halijawa shirikishi. Hii elimu haijawafikia, kwamba wengi ni wapi wapo kwenye vijiji miji na wapi vijiji kabisa. Kwa hiyo, ombi langu kwenye hili, waone na watafute model nzuri ya kutuletea umeme huu kwenye hivi vijiji vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati naendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Rais na ninaendelea kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, lakini vilevile nisiache kumshukuru Meneja wangu wa Wilayani pale, anaitwa Hamisi Kaduma. Kwa kweli yule kijana anafanya lazi ya ziada. Kwa mazingira ya Liwale na namna umeme unavyokatikakatika na mvua hizi zinavyonyesha, saa saba ya usiku mtoto wa watu yuko porini na timu yake wanahangaika kutupatia umeme. Jambo hili ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linakwenda sambamba na uhitaji wa nguzo za zege, kwa sababu kule kwetu sisi eneo kubwa ni misitu. Sasa zile nguzo za umeme sana sana ni za miti. Kuna mambo mawili; aidha ziungue moto au zikipitiwa na maji zianguke. Sasa tukiletewa hizi nguzo za zege zitasadia zaidi. Najua kwamba wameanza kubadilisha nguzo, lakini naomba ziongezwe, kwani zile nguzo hazitoshi, na ule mji ni mkubwa, na mtawanyiko ni mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo niongeze na la watumishi. Unajua Wilaya yetu ya Liwale imewatanyika sana na kama nilivyosema, Mheshimiwa Rais ameweza kufikisha umeme karibu vijiji vyote 72. Mimi nina kijiji kinafika kilomita 114 kutoka Liwale Mjini. Sasa unamwambia Meneja kuwa nguzo imekatika huko kilomita 120 au 114, yuko huko na huku kwingine kilomita 80 nguzo nako imeanguka. Kwa hiyo utakuta tatizo linalokuja pale ni vifaa vya kufanyia kazi, kwamba magari ni machache. Unaweza ukakuta gari analo moja tu, na gari hilo ndilo analolitumia Meneja, na gari hilo hilo ndilo la site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana watuongezee vifaa ili tuweze kukabiliana na hizi changamoto za umeme kukatika mara kwa mara. Pamoja na vifaa, tuongezewe na watumishi. Nilijaribu kukutana naye akaniambia kuwa ikama yao pale ni 15, lakini wako nane tu. Sasa utaona; ina maana kwamba kazi ya watu 15 inafanywa na watu nane. Hapo napo waone mzigo mkubwa walionao hawa watumishi wetu pale Wilayani Liwale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nina hayo tu ya kuyasema kwa kipindi hiki; na baada ya kuyasema hayo, naomba niunge mkono hoja. Ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)