Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu. Nami ningependa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye anatupatia uhai, afya njema kuyafanya haya tunayoweza kuyafanya katika Bunge hili. Pili, namshukuru Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuliongoza Taifa, lakini hususan kwenye hii sekta ya nishati. Nampongeza Waziri na Naibu Waziri Mkuu, Naibu wake pamoja na watendaji wote wa Wizara. Kusema kweli Kaulimbiu ya TANESCO kwamba Tunaiwasha Nchi, wanaitekeleza kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza wafanyakazi wa Shirika la Umeme Mkoa wa Kagera. Wanafanya kazi nzuri na kubwa ya kujituma na iliyotukuka. Nawapongeza wafanyakazi wa TANESCO Wilaya ya Muleba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kuwapongeza huku, namwomba Mheshimiwa Waziri asije akawahamisha. Wawahamishe kama wanapanda cheo. Ni wachapa kazi, wanajituma na wanastahili hizi pongezi, isipokuwa kuwahamisha labda kama anawahamisha kwa kuwapandisha vyeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia machache. Naipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa ambao umefanyika. Napongeza kwa kukamilisha Bwawa la Mwalimu Nyerere, ni hatua kubwa sana, na miradi mingine ambayo imesemwa kwenye hotuba ya Waziri wakati anawasilisha hapa mbele yetu, yote ikikamilika, na nina uhakika itakamilika, nadhani suala la umeme kukatikakatika litakuwa limekwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kidogo kuhusu Mkoa wangu wa Kagera. Kwa kipindi kirefu Mkoa wa Kagera, ukiondoa Wilaya mbili za Biharamulo na Ngara, Wilaya zote zilizobaki ziko nje ya gridi ya Taifa. Tunapata umeme kutoka Uganda, na tumekuwa na tatizo kubwa sana la umeme huo kukatikakatika, hasa katika Wilaya yangu ya Muleba. Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yake, tunamwomba atupatie mwarobaini au suluhu ya umeme kukatikakatika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika wilaya yangu, tatizo kubwa tulilonalo pamoja na kwamba tuko nje ya gridi ya Taifa, tunahitaji kituo cha kupoozea umeme katika Wilaya ya Muleba. Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu anajua kwamba Wilaya ya Muleba ni kati ya wilaya kubwa. Tunazo kata 43, hatuwezi kuichukulia kama wilaya nyingine ndogo, ni wilaya kubwa. Nimewapongeza watumishi wake. Pamoja na matatizo haya ya umeme kukatikakatika, lakini bado tuna changamoto ya vitendea kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema ni wilaya kubwa, tuna ofisi moja ya TANESCO watumishi ni walewale wachache, hawajitoshelezi. Namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu mwenye hii sekta atuangalie kwa jicho la huruma, watupatie vitendea kazi, wawaongezee vijana magari ili wakakimbizane na hizo kata 43 katikati ya kukatikatika kwa umeme wakatuhudumie kwa ufasaha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera Wilaya ya Muleba tunavyo visiwa 39. Ndugu yangu Mheshimiwa kutoka Ukerewe amechangia asubuhi hapa, anaongelea tunawafikia vipi wananchi ambao wanaishi kwenye visiwa? Kwa Wilaya ya Muleba kwa vile visiwa 39 tuna kata tano ziko katikati ya Ziwa Victoria, watu hawa wamekuwa kwenye giza kwa kipindi kirefu, Serikali ilitupatia huduma ya Juameme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kulitaarifu Bunge lako kuwa Juameme wamezidiwa na kazi, hawawezi kutosheleza mahitaji ya hizi kata tano. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu atuisaidie kwenye hizi kata tano ili nao wapate umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kusikia kwamba Serikali ilikuja na pendekezo la kuhakikisha kwamba na hawa ambao wako off grid tunawapatia mwarobaini katika kuhakikisha kwamba nao wanapata umeme wa uhakika. Kwetu Muleba biashara yetu, siasa zetu ni uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu wanahitaji zaidi umeme hata kuliko walioko nchi kavu, kwa sababu kazi yao kubwa ni uvuvi. Kwa hiyo, wangependa kupata umeme, wakawa na mafriji, wakahifadhi mazao ya uvuvi wao, hasa dagaa na samaki, wangeweza kutengeneza uchumi mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema kata tano ninaziongelea Kata za Ikuza, Mazinga, Bumbire, Kerebe na Kata ya Goziba ambazo ziko Wilaya ya kule Jimbo la Muleba Kusini na Jimbo la Muleba Kaskazini. Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hotuba yake atupe matumaini. Wamefanya kazi nzuri, wanatuhudumia vizuri, lakini na kwenye hili, tutafute njia mbadala wa kuwasaidia hawa wananchi na wapiga kura wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza kwa kazi kubwa ambayo imefanyika nchi nzima. Muleba tuna vijiji 166, vijiji 162 vimepata umeme ambayo ni 97.6%. Kwetu walimu unapoongelea 97.6% ni grade A, tena ya nguvu. Kwa hiyo, tunawapongeza sana kwa kazi kubwa ambayo wameifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, bado tuna vijiji vinne ambavyo havijafikiwa na huduma ya umeme. Najua kuwa juhudi kubwa inaendelea, lakini namwomba, kabla hatujamaliza hili Bunge, atupe neno ili na vile vijiji vya Bulungura na Bihanga ambavyo kila nikienda kilio chao ni kwamba watapata lini nishati ya umeme? Nimeongea na Mkurugenzi Mkuu wa REA, amenipatia matumaini, lakini naomba nipate matumaini makubwa zaidi kupitia hitimisho la hoja yake Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa vitongoji; nashukuru, tuna vitongoji 752; vitongoji 387 sawa na 54.5% vinapata umeme. Bado tuna kazi kwenye vitongoji. Sasa hivi tunavyoongea, zamani umeme ulikuwa ni kama anasa. Sasa hivi umeme ni hitaji la lazima kwa kila mmoja. Kila mmoja anataka umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua, kulingana na uwezo wa Serikali yetu, hatuwezi kuwafikia watu wote kwa wakati mmoja. Tungeomba, na hiyo ndiyo ingekuwa sala yetu kwa kila mmoja, kwamba iwezekane tupate umeme wa kutosha angalau miaka 10 ijayo kila mmoja apate umeme kulingana na mahitaji yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Kamati, imeongelea ujenzi wa vituo vya mafuta hasa barabara kuu na kwenye miji. Kuna kipindi nilisoma mahali fulani sikumbuki ni wapi, wanasema kitaalamu kutoka kituo kimoja kwenda kituo kingine cha mafuta inapaswa iwe kilomita saba kwa sababu za kiusalama. Sasa sijui sisi tunatumia standard ipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili naomba tuliangalie kwa macho mapana, ikitokea ajali ya moto tunaweza kuwa katika matatizo makubwa sana kutokana na ukaribu wa vituo vya mafuta hasa barabarani na mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo lingine, vituo hivi sasa vinajengwa hata kwenye makazi ya watu, kwenye misongamano ya watu, makazi vijijini watu wanawekeza kwenye vituo vya mafuta. Najua EWURA wapo wanafanya kazi nzuri, lakini na hili naomba walitupie macho waweze kulisaidia Taifa letu kwa sababu za kiusalama zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wachangiaji wengi wameongelea suala la matumizi ya gesi kwa vyombo vyetu vya moto. Nadhani hii ndiyo suluhu ya kupunguza matumizi ya pesa yetu kwenda nje. Kama Mungu ametujalia gesi yetu, tusichelewe na wala tusisite, na kama ningeshauri tungewaongezea hawa Wizara pesa kuhakikisha kwamba tunajenga vituo vingi vya gesi kuhudumia magari yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na hapa niendelee kushauri, na miaka yote tumeshauri na tutaendelea kushauri na Serikali ianze kutumia gesi kwenye magari yake tupunguze matumizi ya dola yetu kuagiza petroli kutoka nje, tuoneshe kwa mfano na wengine wote watafuata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho tunaagiza mitungi ya gesi kutoka nje, sijaona mtungi ambao unazalishwa hapa nchini. Tunayo gesi yetu, lakini bado tunatumia dola kuagiza mitungi ya gesi. Nilikuwa naangalia kwenye soko tumewajengea appetite wananchi wetu hata ukienda vijijini sasa hivi sisi tunaotoka majimbo ya vijijini; uende Muleba, Nsambo, Chuchoro, Byengeregere kule ndani kabisa akina mama wanatumia gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya kutengeneza hii appetite ya wananchi wetu, naishauri Serikali tuwatafute wawekezaji wa kuwekeza hapa nchini, tutengeneze mitungi yetu ya gesi tuweze kuwauzia hawa wananchi ambao tumewatengenezea appetite ya kutumia gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga hoja mkono kwa 100% nakwenda mpaka 250% ila naomba vijiji vyangu viwili Bihanga na Burungura tukaviwashe, wananchi wakashangilie, wakapige vigelegele kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tumeshamaliza kazi huko, tunahitaji mwanga wa kuja kuhesabu na kulinda kura zetu na kulinda kura za Mama. Nashukuru sana. (Makofi)