Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami kuwa mchangiaji wa siku ya leo katika Wizara hii muhimu. Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kuniwezesha nami leo kwenda kusimama katika Bunge hili ambalo linakwenda ukingoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, napenda nikishukuru na kukipongeza Chama changu cha Mapinduzi kwa kunilea vyema na kuniongoza vyema kwa kuwa Mbunge wa Viti Maalum toka Mkoa wa Dar es Salaam kwa vipindi vitatu mfululizo. Siyo suala dogo, ni suala kubwa; UWT niwapongeze sana, wamenibeba, wamenilea vizuri Mwenyezi Mungu awabariki wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sasa niende kwenye Wizara. Wizara yetu ya Nishati kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuhakikisha anakuwa kinara wa nishati safi ya kupikia kwa akina mama wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wetu ametuamsha akina mama. Ajenda ya Mama Mkoa wa Dar es Salaam tumeipokea. Leo hii ukienda katika Mkoa wa Dar es Salaam matumizi ya nishati ya gesi ya kupikia ni makubwa sana kuliko matumizi ya mkaa. Ni jambo kubwa ambalo Dar es Salaam ilikuwa ni kinara wa matumizi wa mkaa, sasa hivi ukienda kila kona Dar es Salaam utakuta wanauza mitugi ya gesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, tuna matumizi pia ya umeme, tumepata elimu na tumetoa elimu ya kutosha kwa akina mama waone umuhimu sasa wa kutumia nishati ya umeme katika kupikia, ni nishati ambayo ina gharama nafuu kuliko hata ya gesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na ninamwombea Dua Mwenyezi Mungu amwezeshe, ampe afya njema aweze kwenda kupambana 2025 na ninahakikisha katika Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa Rais ana kura zote za kishindo zitajaa mpaka nyingine zitamwagika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, pia napenda nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Waziri wa Nishati pamoja na Mheshimiwa Naibu wake Waziri na Makatibu Wakuu wote wa Wizara hiyo pamoja na watendaji wote wa taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo. Hongereni sana kwa kufanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiyopingika, miaka ya nyuma tunapoizungumzia Wizara ya Nishati kulikuwa na hekaheka ambayo haieleweki. Tulikuwa na michango mikubwa mikubwa, tunaitamani lini itakuja Wizara ya Nishati tuje kuongea. Leo hii maongezi hayapo, wala kelele hazipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini kelele hazipo? Kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kujenga au kukamilisha ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Project ile ilikuwa ni kubwa mno haijawahi kutokea, lakini leo hii bwawa lile limekamilika kwa karibu 100%, siyo jambo dogo kwa nchi yetu, ni jambo kubwa sana, tunapaswa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa kishindo kwa kazi kubwa aliyoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usioaminika na hakuna aliyeamini kwamba ipo siku lile bwawa litakuja kukamilika, lakini pia hakuna aliyeamini kwamba Tanzania hii ipo siku tutapata treni inayoendeshwa na umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu tuna-enjoy sasa na SGR inayoendeshwa na umeme, watu walikuwa hawadhani kwa sababu walikuwa wanaona umeme wenyewe wa majumbani na viwandani haututoshi, je, hiyo treni itaendaje? Leo hii kuchwa, kutwa watu wanarukia treni saa saba, saa sita kila mmoja anapanga muda wa kuondoka na treni. Ni usafiri rahisi, usafiri salama ni usafiri mzuri mno.
Mheshimiwa Mwenyeiti, hongera sana kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pia na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu pamoja na watendaji wake wote, wamefanya kazi nzuri katika sekta ya umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, nimeona kuna miradi kadha wa kadha ambayo ilikuwa inaendelea pamoja na Bwawa la Mwalimu Nyerere. Pia amefanya maboresho ya miundombinu ya gesi za kwenye magari, ongezeko la vituo vya uuzaji gesi kwenye magari, maendeleo ya usambazaji wa gesi za majumbani, utulivu wa biashara ya mafuta nchini, kuimarika kwa hali ya umeme nchini, na kuimarika kwa umeme vijijini. Hayo yote amefanya na Serikali yetu hii, na yamefanyika vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua panapo mazuri hapakosi changamoto. Changamoto ni kitu cha kawaida, hata mwanadamu unapoishi wewe mwenyewe ndani kwako kuna changamoto. Katika changamoto hizo, sasa nitajikita katika mchango wangu kwa Mkoa wangu wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maboresho ya umeme, kweli kabisa katika Mkoa wa Dar es Salaam bado kuna maeneo yana changamoto ya umeme ikiwepo maeneo ya Kigamboni, Temeke, Mbagala, Buza, Kilakala, Vituka, na maeneo mengine mengi tu katika Wilaya ya Temeke na wilaya nyingine huko mara nyingi bado kunakuwa na changamoto za umeme kukatikakatika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi kubwa, tunaona jinsi Serikali inavyoendelea kubadilisha nguzo za umeme kutoka kwenye miti inayooza kwenda kwenye zege, hilo lilikuwa ni changamoto kubwa, zile nguzo kuoza ovyo ovyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya Dar es Salaam kutokana na mabadiliko ya tabianchi kumekuwa na mvua nyingi zikinyesha, lakini maji kujaa, hivyo nguzo zile zilikuwa zinakatika na zinasababisha tusipate umeme kwa masaa kadhaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali na ninaona haja kabisa ya kuiambia Serikali sasa tutoke kabisa katika Mkoa wa Dar es Salaam kutengeneza nguzo za miti, tuelekee kwenye nguzo za zege ili kuondoa changamoto ya umeme kukatika katika kutokana na miundombinu iliyochakaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kuchangia, lakini pia nataka ni-declare interest kwamba mimi ni mdau katika sekta ya biashara ya mafuta. Biashara ya mafuta imeimarika katika nchi yetu, niwapongeze sana EWURA wanafanya kazi nzuri, wameweka vigezo mbalimbali wafanyabiashara wanavipitia hivyo vigezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo changamoto tunaomba EWURA wakakae pamoja na wadau wengine wote wa mafuta wafanye tafiti, hali ya vituo vya mafuta vinaongezeka kwa kasi hali ambayo inasababisha vijana wa Kitanzania waliojikita katika sekta hiyo kuondoka na madeni makubwa, kushindwa kufanya biashara kudaiwa madeni makubwa benki na hatimaye na wengine kufilisiwa. Sasa naiomba Serikali waiangalie tena upya biashara hii, kwani ina changamoto zake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa EWURA wanaweka vigezo, watu wanavifikia. Ndugu zangu nami nitakuwa kidogo tofauti kwa sababu yawezekana natambua hilo jinsi vigezo vinavyowekwa kwa EWURA na tunamwomba Mwenyezi Mungu atujalie hivyo, hatujawahi kupata shortage yoyote katika mlipuko au nini kwenye hivyo kulingana na vigezo wanavyoviweka EWURA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto inakuja, huwezi ukajenga vituo vyote porini, magari yapo Oyster Bay, yapo Masaki, Mwenge, Temeke, Mbagala na kadhalika. Sasa utachukua vituo vyote utaenda kuviweka porini, hawa huku mjini watapata huduma wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha msingi, vigezo na masharti lazima vizingatiwe ili kuwe na usalama, lakini pia kama na wao wanaliona pia hili la kujaza wafanyabiashara, wanadhani kwamba wanakwenda kuzungusha pesa na kupata pesa, lakini kuna vijana ambao waliingia kwenye hiyo sekta sasa hivi taabani hawajiwezi tena, alikuwa anauza kwa siku lita 5,000, lakini leo hii anauza kwa siku lita 500, anashindwa kurudisha mikopo ya benki, anashindwa kulipa mapato ya TRA, anashindwa kufanya kitu chochote, matokeo yake wanaishia vijana kuuza makampuni na kutokomea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunawawezesha vijana waliopo katika sekta mbalimbali, lakini tunavyokuta kijana amejipambanua, amehangaika, amepata mtaji, lakini anakuja kupotea hivi hivi, hilo litatusikitisha. Naiomba Serikali waangalie hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia ujenzi wa miundombinu ya gesi za majumbani, naipongeza Serikali, wamefanya jitihada kubwa ya kujenga miundombinu ya gesi, naona Mikocheni wamejenga, inaelekea sasa Mbezi, Mbezi Beach na maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba tufanye win win tuhakikishe tunafanya kidogo kwenye eneo la Mikocheni, tunahama tunaenda kwenye Wilaya ya Ilala, tunawafanyia nao kidogo, tunahama, tunaenda Wilaya ya Temeke, nao waonje ile keki kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukisema tung’ang’anie eneo la Mikocheni, watu wa Dar es Salaam, akina mama wa Dar es Salaam wanasubiri gesi hiyo yenye gharama nafuu, wanaita gesi ya kupimiwa, nami wananiambia kila siku Mheshimiwa Mbunge wetu hakikisha tunaletewa gesi ya gharama nafuu, gesi ya kupimia ili tuweze kuitumia. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda umeisha?
MBUNGE FULANI: Ndiyo malizia.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, nakishukuru sana Chama cha Mapinduzi kwa kuisimamia IIani yake katika kipindi hiki cha mwaka 2025. Hakika Ilani ya Chama cha Mapinduzi imefikiwa kwa zaidi ya 95%. Hilo ni jambo la kupongeza chama chetu, na Serikali yetu imefanya vizuri hata sisi wengine tutakwenda kifua mbele na tunahakikisha tutarudi kifua mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante sana. (Makofi)