Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Emmanuel Lekishon Shangai

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Nishati. Nitangulize kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunilinda niweze kuwa hai na kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Ngorongoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiwafanyia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nampongeza kwa kupitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kuwa mgombea wa Urais kupitia Chama chetu cha Mapinduzi. Pia, nampongeza Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi kwa kupitishwa kuwa mgombea mwenza wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawapongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati pamoja na Naibu Waziri wake, Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakurugenzi pamoja na watendaji wote wa taasisi zilizopo chini ya Wizara yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba naunga mkono hoja kabla ya kuchangia ili baadaye kule mbele nisije nikasahau. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu pamoja na Naibu Waziri wake, mmekuwa mkifikika. Kiuhalisia mmekuwa ni watu ambao mnatupokea kama Wabunge na kutusikiliza na kutatua changamoto zilizopo ndani ya wilaya zetu na majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, amepokea Wizara hii ikiwa na changamoto. Nakumbuka wakati anateuliwa na Mheshimiwa Rais, tulikuwa na tatizo la mgao wa umeme, na kwa wakati huo alikuwa kwenye cross road kwamba nichague njia ipi? Hata hivyo, kwa kuwa yeye ni kiongozi mtulivu, ameweza kutuvusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, angepokea kiongozi mwingine ambaye hafikirii vizuri, angetupeleka kwenye kununua ma-generator au kukodisha, lakini kwa kuwa yeye ni kiongozi aliyetulia, ametusaidia, tumeenda kama nchi na sasa tumetoka kwenye mgao wa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu anapokea Wizara, tulikuwa na tatizo hilo la mgao wa umeme, lakini kwa sasa hivi tunapozungumza kutokana na mikakati iliyowekwa na Wizara, kwa sasa tuna utoshelevu mzuri wa umeme ambao umefika 100%. Hiyo, ni hatua kubwa sana na kwa kukamilika kwa Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ni mapinduzi makubwa sana kwenye sekta hii ya nishati. Kwa hiyo, nawapongeza sana kama Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kwa Wilaya yangu ya Ngorongoro na Jimbo la Ngorongoro kwa ujumla, wakati Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani mwaka 2021, Wilaya ya Ngorongoro kulikuwa na umeme kwenye kata tatu tu na vijiji vitatu, lakini leo tunapozungumza, umeme kwenye Wilaya ya Ngorongoro kwenye Tarafa ya Sale na Loliondo, umeme umefika kwenye kata zote 17 pamoja na vijiji 40. Kwa hiyo, ni hatua kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Wizara hii, wamefanya kazi kubwa, nami kama Mbunge, nimekuwa nikiwafikia, na kweli wamekuwa wakinisikiliza na kufanyia kazi yale ambayo wananchi wetu wanahitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, tuna umeme kwenye vitongoji nane. Densification; vile vitongoji kwa ajili ya densification au ujazilizi, kwenye maeneo hayo yote ambayo umeme ulifika kipindi cha nyuma, vile vitongoji ambavyo vimeachwa, vitongoji 12 navyo vimepata umeme. Pia, tuna vitongoji vingine 12 ambavyo umeme umefika katika yale maeneo ya migodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Ngorongoro pia ina migodi mbalimbali. Kwa kipindi cha nyuma hatukuwa na umeme, lakini kwa sasa hivi umeme umefika na wananchi wale ambao wanajishughulisha na shughuli za uchimbaji wananufaika na umeme na uzashaji wao umeongezeka mara dufu. Kwa hiyo, nawapongeza pia kwa hilo kwa sababu ni kazi kubwa iliyofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, pia tuna umeme kwenye vile vitongoji 15. Kwa Wilaya yangu, vile vitongoji 15 vya jimbo tayari vitongoji 13 vimewekwa nguzo, vimebaki vitongoji viwili tu. Kwa hiyo, tuna uhakika mpaka mwisho wa bajeti hii ya mwaka 2024/2025, nafikiri vitongoji vile umeme utakuwa umewashwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, katika vijiji vyote 40 ambavyo kuna umeme bado kuna vijiji vitatu ambavyo umeme haujawashwa; Kijiji cha Naan, Kijiji cha Piyaya na Olalaa. Hata hivyo, nina uhakika baada ya muda mfupi umeme pia utawashwa katika yale maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo nataka kusema, kwa Wilaya yangu ya Ngorongoro, kuna maeneo kwa mfano, tuna vijiji 65, lakini vijiji ambavyo vina umeme ni 40. Kwa hiyo, vijiji 25 havina umeme. Ninaamini kwamba Wizara itaangalia namna na wao wapate umeme hata kama ni umeme wa jua waweze kupata kwenye hivyo vijiji 25 ambavyo bado havina umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nilihitaji kuliongelea ni kwamba kwenye Wilaya ya Ngorongoro, umeme umekuwa ukikatika sana. Hili ni tatizo ambalo wananchi wanaona kama vile umeme kwao siyo manufaa, kwa sababu umeme unatoka Longido, tunachukulia line ya Longido unasafiri kilometa nyingi mpaka ufike kwenye Wilaya ya Ngorongoro. Kwa hiyo, kwa siku moja umeme unaweza ukakatika zaidi ya mara 10 na wakati mwingine unaweza ukakatika saa nne usiku na kurudi labda kesho saa nne. Kwa hiyo, wananchi wamekuwa wakipoteza mali zao, umeme unaporudi na kukata ghafla tunajua madhara yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Wizara itusaidie jambo moja la kuhakikisha kwamba, kwenye hii bajeti tunaenda kujenga substation Wilaya ya Ngorongoro ambayo itatusaidia kuondoa tatizo la umeme. Najua sasa hivi Serikali ina mpango wa kujenga substation hapo Makuyuni na kuendelea mpaka kule Engaruka, lakini huo ni mkakati wa muda mfupi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa muda mrefu kwa ajili ya Wilaya ya Ngorongoro na wananchi waweze kunufaika na umeme, ni lazima tuwe na substation ya kule kwetu ya KV 132 kama walivyofanya wataalamu wetu. Wataalamu wetu wanafanya kazi kubwa sana. Ngazi ya mkoa na ngazi ya wilaya wanafanya kazi kubwa kila wakati, pamoja na mazingira magumu yaliyopo ndani ya Wilaya ya Ngorongoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme ukikatika leo uko katikati Mundarara, wataalamu wale wanatoka Ngorongoro zaidi ya saa nne kwenda kuangalia tatizo na wale wa Longido waliopo kule. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara tuangaalie namna kama tunaweza kujenga hiyo substation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, tumepata mitungi ya gesi. Mheshimiwa Naibu Waziri, nafikiri kuna siku nilikwambia hili, kwamba kwa Wilaya ya Ngorongoro unapeleka gesi kule Loliondo ambapo kutoka Tarafa ya Ngorongoro ni kilometa 400 na kule ndiyo makao makuu; naomba, kwa kuwa kazi hii inafanyika kwa Watanzania wote, basi wataalamu pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, kwa sisi ambao tuna mazingira magumu na jiografia yetu kwa ajili ya upatikanaji wa hizo gesi, tungegawa kwa zile tarafa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tarafa ya Ngorongoro, Sale na Loliondo kuwepo na wale wasambazaji, kwa sababu haiwezekani unapitisha mitungi kwenda mpaka Waso, mwananchi aliyepo Engaresero atoke aende Waso akafuate mitungi na kurudi tena zaidi ya kilometa 70. Kwa hiyo, tuweke mikakati ambayo itawasaidia wananchi kupata hiyo mitungi kwa urahisi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na niwapongeze sana. (Makofi)