Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sengerema
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie katika Wizara hii ya Nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini na Kamati hii inasimamia Wizara mbili; Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini. Kule Wizara hii inafanya kazi kubwa sana katika maeneo mengi ya huduma za kijamii. Hata hivyo, pamoja na kazi hii, kazi hizi zinafanywa na binadamu na hawa binadamu wanaofanya hii kazi ni watu ambao miongoni mwao ni sisi tukiwemo Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa sana aliyoifanya katika Sekta hii. Kwanza kufanya maboresho ya watendaji katika Sekta hii, lakini pia na kubadilisha mawaziri, hili ni jambo kubwa sana. Mheshimiwa Rais, anaona ni wapi pamepungua, anafanya mabadiliko na hayo mabadiliko yanafanyika kwa ajili ya kupata tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba binadamu katika hulka yake huwa anapenda akifanya jambo zuri asifiwe, siyo anafanya jambo zuri anapingwa. Hili jambo linakuwa siyo sawa. Sisi kama Tanzania ni kwamba tutapita katika hatua ngumu sana ili kwenda kujiondoa katika haya matatizo mnayoyaona ya umeme, matatizo ya matumizi ya gesi na vitu vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Rais katika uteuzi wake katika hizi nafasi. Amemteua Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko na akampa nafasi nyingine ya kuwa Naibu Waziri Mkuu. Siyo kwamba kampa nafasi hiyo kwa bahati mbaya, ni kwamba ameangalia yeye mwenyewe akaona kabisa kwamba ana uwezo wa kufanya kazi hii kwa ufasaha na Wizara hii inafanya kazi hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa naongea na kiti, lakini pia naongea na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu. Sasa yupo pale Mheshimiwa Mbunge anamnyima nafasi ya kunisikiliza, sasa linakuwa siyo jambo jema sana, naomba unilinde. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Wizara watendaji wake wanafanya kazi usiku na mchana. Watanzania wanatakiwa wajue umeme ukiwa unakatika, kuna tatizo la kiufundi au kuna tatizo gani? Kwa hiyo, hivi ni vitu ambavyo Watanzania wanatakiwa waelezwe na baadaye wataelewa, lakini hitaji la umeme pia kwa Tanzania ni kubwa mno kwa sababu imeingia kuwa sehemu ya maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wako watendaji wanafanya kazi. Sisi tunafanya kazi kama Kamati, tunapita maeneo mengi sana kuona tatizo ni nini, na tunakwenda tunaoneshwa hatua kwa hatua. Miongoni mwa watu ambao walikuwa wabishi katika jambo hili ni pamoja na mimi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekwenda mpaka underground palipo mitambo ya kuzalisha umeme, nimetembea maeneo yote yanayofua umeme katika nchi hii, na tumekwenda kule kuona kama kuna hujuma ya aina yoyote. Hakuna hujuma hata moja isipokuwa kama nchi tumelemewa na tunahitaji kazi ya nguvu kubwa sana kuwekeza katika miundombinu ya umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya umeme katika nchi hii, kwa siku, watu wanaoomba umeme tu ni karibu Megawatts moja kwa siku nchi nzima. Maombi peke yake ya mahitaji ya umeme, ni zaidi ya Megawatts 30. Sasa kama mahitaji ya umeme ni Megawatts 30, mahitaji mapya ya wananchi ambao wametengeneza viwanda huko migodini na sehemu zote, tunahitaji kuwekeza sana katika suala la umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wabunge, tunatakiwa tuishauri sana Serikali kwenye eneo hili, hatuna jinsi. Leo hata hili Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo tulikuwa tunasifia kwamba tumepata bwawa tutapunguza mahitaji ya umeme ndivyo yanavyoongezeka. Ni sawasawa na walivyokuwa wanapata hofu wawekezaji wa mabasi waliyokuwa Dodoma kwamba baada ya Treni ya Mwendokasi kuanza kazi, mabasi yao yatakosa abiria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, treni mpaka sasa hivi inajaa halafu na mabasi yanajaa na ma-traffic wako barabarani wanakamata mabasi ya akina Shabiby yamejaza watu na yanakwenda kasi. Siyo suala la kuchezea, yaani kila mnavyoongeza na mahitaji ya watu na yenyewe kuhitaji umeme ndiyo yanaongezeka kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika jambo hili la miundombinu ya umeme, mimi leo hapa nataka kushauri tu. Ni kwamba, kwa sababu tunayo makaa ya mawe na uzalishaji wa makaa ya mawe ni mkubwa, hatuna jinsi, ni lazima tuhakikishe tunatafuta wadau wa kuja kuongeza nguvu katika Sekta hii ya Umeme. Tusipozalisha kwa mahitaji ya umeme ambayo sisi tumeyapitia kama Kamati, tumegundua mahitaji ya umeme ni makubwa sana katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huko Lijualikali kuna maeneo mengi, Mto Malagarasi na kwingineko na haya maeneo yote kama vile umeme wa joto ardhi, wote unahitajika umeme wa gharama. Lazima tuwekeze kwa gharama kubwa sana katika umeme, kwani baada ya miaka 10 ijayo, hali ya mahitaji ya umeme na huu uwekezaji unaowekwa wa viwanda, hali itakuwa ngumu kuliko sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imepata matatizo juzi kwa kufiwa na Mtendaji wa TANESCO. Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema Peponi. Eng. Nyamhanga ni miongoni mwa wazalendo, miongoni mwa watu walioumia japo familia yake itakuwa imepoteza zaidi, Wizara itakuwa imepoteza zaidi, na mimi nimeumia kwa sababu tumefiwa na mzalendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yule bwana alikuwa, ukikatika umeme, kama mko naye, yaani anashika kifua, anaona tayari balaa kubwa limeingia. Sasa mtu wa namna hiyo na alivyokuwa anafanya kazi, amekufa. Alikuwa anatoka kufanya kazi; alikuwa Dodoma ametokea Sengerema; tulikuwa naye kule Sengerema, amekwenda kuangalia maeneo ya kwenda kuweka substation kule Sengerema, namna ya kuhakikisha umeme mwingine unaotokea Ibadakuli, umeme mwingine unaotokea Mpomvu Geita unakuja kupozwa Sengerema wasaidie tena kuingiza umeme mwingine Mwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile kuhakikisha tu kwamba Jiji la Mwanza na wananchi wa Mkoa wa Mwanza na Kanda ya Ziwa wanapata nafuu ya kukatikiwa umeme, yule bwana anakwenda kupata ajali anakufa, na bado alikuwa anasafiri tena kutoka kwenda nje ya nchi. Ndiyo ujue watu walikuwa wanafanya kazi; usiku kucha anatembea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wanatakiwa kujua, Mheshimiwa Rais suala la ukatikaji wa umeme linampa maumivu makubwa. Wabunge, Wajumbe tulioko katika Kamati hii tunapata maumivu makubwa, tunafanya kazi. Kwa hiyo, Eatanzania wanatakiwa waunge mkono juhudi inayofanyika katika sekta hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la gesi, hili suala la gesi nilikuwa namwomba sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, hebu waitishe semina ya Wabunge wote hata siku mbili waweze kujua aina za gesi tunazozalisha, na aina ya gesi inayoagizwa kutoka nje. Hizi gesi ziko za aina ngapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naogopa kuchukua nafasi hii mimi tena kuanza kusema hili jambo ni la kwako Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, lakini ninachotaka kukuomba suala la kutoa semina Mbunge mmoja kama Tabasam mimi nina watu zaidi ya 450,000 - 500,000 nikijua hii mifumo ya gesi yote naweza kwenda kuwaambia Watanzania walioko Sengerema bila matatizo yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hali hii, naomba tu unipe dakika moja niweze kusema ni kwamba gesi imesambazwa, Serikali iliagiza gesi na ikatoa ruzuku. Hii gesi imeleta chachu kubwa sana ya watumiaji wa gesi. Naomba sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu hii mitungi ya gesi iliyoagizwa, basi aje awaambie Watanzania, lini mitungi hii itaingia ili kusudi sasa wananchi ambao wanatusumbua kule katika Majimbo yetu wapate kauli ya Serikali, mitungi hii inaingia lini? Maana mitungi hii ina ruzuku ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani mitungi ni ya ghali na haipatikani hapa. Sisi tumetembea nchi nyingi zinazozalisha mitungi. Serikali ya Tanzania bado na yenyewe ina mipango mikubwa ya kuleta wawekezaji waje wafanye kazi hii ya kuzalisha mitungi na uagizaji wa gesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kushauri na wenyewe uagizwe kwa bulk ili kupunguza gharama, kwa sababu watu wanavyoleta gesi labda tani 5,000, labda meli dogo tani 5000. Kwa hiyo, bei za gesi zinakuja kuwa kubwa kiasi ambacho watumiaji wa nchi hii wanakuja kuwa na mzigo mkubwa wakati gesi haitakiwi kuzidi shilingi 1,500 hadi 2,000 kwa ajili ya matumizi. Kwa hiyo, mtu akinunua kilo sita anajua atanunua kwa shilingi 12,000 au kwa shilingi 10,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nyingine kama India huko gesi inauzwa gharama ndogo sana na gesi hii inatoka Brazil inapita hapa, inatoka Angola inakwenda mpaka Brazil inakwenda mpaka India. Sasa kwa hatua hiyo, tunaiomba Serikali itengeneze miundombinu ya gesi kama hivi wanavyojenga miundombinu ya kuhifadhi mafuta walete na miundombinu ya kuhifadhi gesi ili Watanzania sasa ambao lengo la Mheshimiwa Rais ifikapo mwaka 2034 Watanzania zaidi ya milioni 48 wawe wanatumia gesi kwa 80% ya wananchi, kwa mfumo huu bila kuanza kuandaa miundombinu ya gesi, hatuwezi kufika kwenye takwa la Mheshimiwa Rais na Wabunge ambao ni watetezi wa wanyonge huko kwenye Majimbo yetu tutashindwa kutimiza wajibu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)