Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilwa Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi jioni ya leo kuweza kulihutubia Bunge katika kuchangia Wizara yetu ya nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natangulia kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwezesha miradi mingi tangu alipoingia madarakani tarehe 19 Machi, 2021. Kwa hakika miradi mingi imetekelezwa katika kila kona ya nchi, mikubwa na midogo kwenye sekta nzima ya nishati ukianzia kwenye umeme wenyewe kwa maana ya bwawa la Mwalimu Nyerere, lakini hata kule kwenye umeme wa REA, miradi ya gesi siku hadi siku uwekezaji umekuwa ukiongezeka na tumeanza kupata tija kubwa kwa kupata umeme mwingi katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri na uwekezaji mkubwa ambao ameufanya katika sekta hii ya nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda pia kutoa shukrani kwa Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati, dada yangu, mtani wangu Judith Kapinga kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuifanya tangu alipoingia madarakani katika nafasi hii, kwa kweli ametuonesha utofauti na kule tulikotoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa miradi umeimarika, umekuwa na usimamizi makini katika Wizara yake, pia miradi kwa kweli imekuwa ikitoa matunda kwa haraka sana. Hata ile ambayo ilikwama kwa miaka mingi sasa imeanza kutoa matunda na tija kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bwawa la Mwalimu Nyerere ni kielelezo tosha, lakini kule Kusini tulipata mradi wa kuhamishwa kwa ule mtambo wa umeme wa gesi, megawatt 20, Mtwara; pia pale Somanga ukarabati unaendelea wa kituo kile cha kuzalisha umeme megawatt 7.5. Kwa kweli mambo yanakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu mwaka 2024 tulimlalamikia baada ya kuwa tumekumbwa na kadhia ya mafuriko yaliyotokana na mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya ambapo nguzo nyingi ziliondolewa ambazo zilikuwa za miti. Tunashukuru Mheshimiwa Naibu Waziri Waziri Mkuu alilifanyia kazi, tumeona sasa hivi nguzo za zege zimekuwa zikisambazwa na hivyo kuimarisha huduma ya upatikanaji wa umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo maombi au ushauri ufuatao, kwamba, kwenye njia ya umeme wa gridi ya Taifa, kwa sababu tayari Serikali imeanza kushughulikia jambo hili kutokea gridi ya Taifa ambayo inatokea Songea, itapita Tunduru - Masasi kwenda mpaka Mnazi Mmoja na baadaye Lindi na Mtwara, tunaomba ule mradi uboreshwe au utekelezwe kwa kasi zaidi kusiwe na delay ili sasa kwa kuwa transmission line zinaenda kuboreshwa, tuna uhakika gridi ya Taifa ikifika Lindi na Mtwara, basi huduma ya umeme itapatikana zaidi.
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa inatokea wapi? Mheshimiwa Yahya.
TAARIFA
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana mchangiaji, anachangia vizuri sana. Kwa suala la gridi ya Taifa naomba niipongeze sana Wizara kwamba ile changamoto ya wananchi wa Jimbo langu kutolipwa fedha za fidia, wameanza kulipa kuanzia jana. Jambo hili nalipongeza sana.
MWENYEKITI: Mheshimiwa unaipokea hiyo Taarifa?
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipokea kwa mikono miwili, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukiwezeshwa zaidi kuboresha ile miundombinu ya zile nguzo za zege kwa sababu hazijafika maeneo yote, zimepita kwenye barabara kuu tu, nina hakika na hii gridi ya Taifa itasaidia sana kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya umeme ambayo bado kwa kiasi fulani inaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napongeza juhudi ambazo zimefanyika kwenye mradi wa REA na tuliongozana wakati fulani na Mkurugenzi Mkuu wa REA mwezi Agosti mwaka 2024, tukaweza kwenda kutembelea baadhi ya miradi kule Zinga na maeneo mengine na tukagawa na mitungi ya gesi. Tunaishukuru Wizara kwa kweli kwa kuweza kuwaona wananchi wa Jimbo la Kilwa Kaskazini na Kilwa kwa ujumla, lakini sasa kuna changamoto kwenye vile vinavyoitwa vijiji miji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kidogo mimi nimepitapita huko kwenye Local Government, sielewi hivi vijiji miji vinapatikana katika sheria na taratibu zipi? Kwa sababu ninavyojua kuna Majiji, Manispaa, Miji na kuna Mamlaka za Miji Midogo. Sasa unakuta kwa mfano, pale Somanga Kaskazini na Somanga Kusini ambako wenzetu wa TANESCO wamekuja na definition yao, wanasema eti ni vijiji miji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nafikiri turudi kwenye standards zetu za nchi ambazo zinapatikana kupitia Wizara yetu ya TAMISEMI katika kutambua haya maeneo. Kama bado ni Kijiji kama ilivyo Somanga Kusini na Kaskazini wanapaswa kulipa shilingi 27,000, na hili jambo tumelizungumza tangu mwaka 2023, mwaka 2024, mwaka 2025, Wabunge wengi wamechangia kuhusu jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara iharakishe hili jambo ili kuwapa fursa hii miradi ya REA ilete tija zaidi kwa wananchi wetu wa vijijini. Kwa hiyo, nilikuwa naomba pale Somanga Kaskazini, Somanga Kusini na vijiji vingine vya Wilaya ya Kilwa, basi viweze kulipa shilingi 27,000 ili waweze kunufaika na hii miradi ya REA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la vitongoji 15 katika Jimbo langu vinakwenda kusaidiwa katika ule mradi wa vitongoji 15 kila Jimbo, lakini kuna mradi wa ujazilizo. Kwa jimbo langu kuna vitongoji 14. Kwa hiyo, jumla vitongoji 29 vimelengwa kuboreshewa huduma ya umeme. Sasa ile miradi inakwenda taratibu sana, kuna delay kubwa sana katika ile miradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Wizara iweze kutekeleza hii miradi kwa speed inayotakiwa ili wananchi wetu waweze kupata tija kwa haraka na hatimaye waweze kutumia huu umeme kama fursa kwa ajili kuendeleza uchumi na maisha ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa mradi wa REA katika jimbo la Kilwa Kaskazini tuliwahi kukaa tukakubaliana na wenzetu wa REA na TANESCO kwamba, kuutoa umeme kutoka Kandawale kuupeleka katika Kijiji cha Ngarambilihenga ni kilomita 27, wakati kuna Kijiji cha jirani kule Rufiji kinaitwa Ngarambe Matingi ni kilomita saba tu ambako tayari umeme wa REA ulishafika.
Mheshimwia Mwenyekiti, kwa hiyo, tulikubaliana na wakatekeleza, kukawa na balance ya kilomita 20. Hii kilomita 20 tukakubaliana kwamba basi iende itoe umeme kutoka Kijiji cha Zinga kwenda katika Kitongoji kinachoitwa Nambunju. Ule umeme umetengenezwa tu kama nguzo 40 halafu hatuoni kinachoendelea, na kwa taarifa tulizonazo, mradi umekwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba kwa kuwa mradi sasa umekabidhiwa TANESCO, waharakishe hoja hii ili watu wa Zinga, Nambunju waweze kupata umeme haraka na kuweza kuutumia kwa ajili shughuli za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa gesi na petroli mara nyingi wenzetu wa TPDC wamekuwa wakiongelea zaidi masuala ya gesi, lakini bado wana jukumu la kufanya exploration ya petroli vilevile kuendeleza upatikanaji wa hii nishati ya petroli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo letu na Jimbo jirani la Kilwa Kusini kumekuwa na miradi ambayo ilitelekezwa kama miaka 19 hadi 20 iliyopita. Ukienda Kinjumbi pale, ukienda Pande, ukienda Likawage kuna alama pale zimeachwa na watafiti walikuwa wametoka Ujerumani na Canada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba Serikali ikumbuke ile miradi, Mungu akijalia pale tunaweza tukapata nishati ya petroli ikasaidia vilevile katika uendelezaji wa Taifa letu kiuchumi, na pia ikazalisha ajira pia kwa wananchi wetu wa maeneo husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala la CSR, Serikali yetu na hasa Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu ulipotembelea kwa mara ya kwanza Mikoa ya kusini ulishuhudia namna ambavyo wananchi ambao wanaishi katika maeneo ambayo aidha, kuna uzalishaji wa gesi au kuna mikuzo ya gesi imepita, namna ambavyo bado hawajanufaika sawasawa na fursa hiyo kuwepo katika maeneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilijaribu kuomba katika Bunge lililopita la Bajeti kwamba pale Somanga ambako kuna uzalishaji wa nishati ya umeme, megawatt 7.5 bomba linalotoka Songosongo linapita pale na kuna plant pale ya ku-control valve zile za gesi, pia lile linalotoka Mtwara na kuna kituo kikubwa pale cha ku-control ile gesi, basi angalau mngetusaidia kuweka umeme angalau mitaani, lakini hilo zoezi bado halijafanyika, ningeomba lifanyike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Kata zangu tatu ambazo bomba la gesi kutoka Mtwara linapita, Kata ya Miteja yenyewe ndiyo bado ina huduma duni sana katika Kituo cha Afya. Akina mama wanahangaika kwenda maeneo ya mbali kufuata huduma ya afya. Kwa kweli watu wanaseka sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kwa kweli atuangalie katika eneo hilo ikiwezekana hata kama ikibidi kwa awamu, anaweza akatuletea shilingi milioni 250 au shilingi milioni 300 tukaanza kujenga kituo cha afya pale Miteja, baadaye kadri siku zinavyosonga mbele fursa ikipatikana zaidi, basi tutaendelea kujenga na hatimaye kuweza kukamilisha. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru; na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na labda nikumbushie tu jambo moja. Mmetuzoesha Wabunge utaratibu wa kutuwekea mabanda pale, tunapata elimu motomoto ya mambo ya nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunashuhudia kwa vitendo kwenye Majimbo yetu na maeneo tunayotoka, namna ambavyo Wizara yako inatekeleza majukumu yake, lakini mwaka huu naona kimya, sasa sijui kuna tatizo gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)