Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nami kwa kupata nafasi jioni hii kuchangia hoja iliyoko Mezani kuhusu Wizara ya Nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, naomba nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa watu wa Tunduru. Tunamshukuru sana kwa kutuletea mradi mkubwa wa gridi ya Taifa wenye thamani ya shilingi bilioni 150, tunashukuru sana, sana, sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu una changamoto, uliokuja kwa kasi kubwa sana; wananchi walipisha maeneo yao tunashukuru, lakini ule mradi umesimama kwa muda mrefu, zaidi ya miezi minne na changamoto ya umeme wa Tunduru inatokana na low voltage kutokana na umeme wa gridi ya Taifa kuwa na low voltage.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifika Tunduru sasa, kwa kasi ya usambazaji wa umeme vijijini na umeme unaoletwa Tunduru na kugawana na wenzetu wa Nayumbu mpaka Masasi, unasababisha kukatika katika kwa umeme mara kwa mara. Kwa hiyo. Ombi langu kwa Serikali na kwa Wizara, ni kuweka kipaumbele kabisa cha kuhakikisha kwamba mradi ule unaisha kama ulivyokusudiwa ili adha ya kukatika umeme Tunduru na vijijini hasa vijiji vya Jimbo vya Tunduru Kusini iwe imeisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, adha hii kwa upande wa Jimbo la Tunduru Kusini kuna vijiji vipo mpakani na Mto Ruvuma ambapo upande wa pili ni Msumbiji wanapata umeme kwa masaa nane tu. Inawezekana ukawaka kuanzia saa nane mchana, ikifika saa nne usiku, ukizima ni mpaka asubuhi, umeme haupatikani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli, adha hii shida kubwa ni low voltage ambayo inasababishwa na hii gridi ya Taifa ya KV 32 kutokutosheleza kwa niaba ya Jimbo zima la Tunduru Kusini. Katika hili lazima niwashukuru sana wafanyakazi wa TANESCO hasa Meneja wa Mkoa wa Ruvuma, Meneja wa Namtumbo, Meneja wa Tunduru Ndugu Mollel, kwa kazi kubwa sana wanayoifanya kila siku, kuhangaika kila unapokatika umeme kujua tatizo liko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kwa upande wa Tunduru, wafanyakazi hawa wanastahili tuzo na wanastahili pongezi za hali ya juu kwa sababu wamefanya ile kazi kwa moyo. Mara nyingi umeme wa Tunduru unakatika kuanzia usiku hata mchana zaidi ya mara nne mpaka mara 20 kwa kutwa. Hili jambo kwa kweli wenzetu wa TANESCO wanajitahidi kuhangaika kuhakikisha kwamba umeme unapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye umeme wa REA, tunashukuru sana tumepata miradi ya umeme jazilizi, tumepata vitongoji 15, lakini ninawashauri watu wa REA, wanapoongeza umeme jazilizi waangalie maeneo yale ambayo line za high tension zimepatikana ambazo ni meter 30 kutoka kwenye line. Tunaposema vitongoji havina umeme, maana yake ni hakuna kabisa line iliyokwenda katika maeneo yale. Sasa tunajikuta umeme jazilizi tunaenda kwenye maeneo yale yale ambayo line ya umeme imepita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, malalamiko ya wananchi wa vile vitongoji ambavyo umeme haujafika kabisa yamekuwa ni makubwa, waangalie namna ya ujazilizi huu kwenda sambamba na kuongeza line za high tension, ili yale maeneo ambayo umeme haujafika kabisa waweze kupata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili hili suala la REA, naomba ndugu zangu wa REA, hasa Mollel na mwenzake Mrope Hamisi, wajitahidi watusaidie. Kuna maeneo ya huduma za jamii, kama Sekondari ya Tuwe Macho, haina umeme. Niliongea na Naibu Waziri na niliandika barua, lakini naona bado mpaka leo ile sekondari haijapatiwa umeme, na pale tumeongeza Kidato cha Tano na Sita, ikiwezekana Mwezi Julai watoto wataanza kwenda pale na shule ile haina umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba ipelekewe umeme, pamoja na Zahanati ya Tuwe Macho, ambapo zote hizi zipo katika Kitongoji cha Zimamoto. Tunaomba kitongoji kile kipelekewe line ya umeme, ili Sekondari ya Tuwe Macho na Zahanati ya Tuwe Macho zipate umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tuna sekondari mbili mpya zinajengwa katika Kata ya Mbati iliyopo katika Kijiji cha Mdabwa, Kitongoji cha Chapakazi, line ya umeme kule hakuna. Tunaomba tusaidiwe line iende kule, ili shule ile itakapoanza kazi watoto wawe wanaendana na hali ya kisasa ya shule kuwa na umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, katika Shule ya Sekondari mpya pale Mtina, tunajenga katika Kitongoji cha Sauti Moja, Kijiji cha Muungano, napo pale shule kubwa ya amali inategemewa kuanza hivi karibuni, lakini bado kitongoji kile hakina line ya umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Wizara, watu wa REA watusaidie katika maeneo hayo matatu ya huduma za jamii tuweze kupata umeme, ili huduma zile ziende vizuri. Tunaomba sana, ili mambo haya yafanikiwe, gridi ya Taifa, kasi ya ujenzi kutoka Namtumbo kuja Tunduru pamoja na ujenzi wa extension pale Tunduru uende kwa kasi mliyokubaliana, ili na wenzetu wa Nanyumbu na Masasi wapumzike kukatikakatika kwa umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda sana nichangie ni suala la matumizi ya gesi. Tunaishukuru Wizara, mwaka 2024 tulipata mitungi ya gesi, tumegawa kwa viongozi wetu wa vyama vijijini, lakini ile mitungi haitoshi. Ili kuhamasisha zaidi, tunaomba tena tupewe angalau mitungi mia mbili mbili kila Mbunge aende kugawa kwenye vitongoji na vijiji ili tuhamasishe matumizi ya gesi. Hili jambo liwasaidia sana wenzetu wale walioko kijijini kuacha kutumia kuni na kukata miti ovyo, ili kuhakikisha kwamba, wanakwenda kisasa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia punguzeni na bei ya gesi, imekuwa changamoto kwa watu wa vijijini kwa sababu, bei ya shilingi 25,000/= kwa kilo 14 au 13 ambayo inaweza ikatumiwa kwa muda wa mwezi mmoja, watu wa vijijini wameshindwa kununua gesi hiyo. Kwa hiyo, tunaomba angalau ruzuku ile iongezwe ili wananchi wa vijijini waweze kupata mitungi ya gesi na gesi yenyewe kwa urahisi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili nitakwenda moja kwa moja kwenye ujenzi wa NLG pale Lindi, hili litakuwa ni suluhisho maalumu kwa matumizi bora ya gesi. Kama walivyozungumza Wabunge wenzangu waliotangulia, gesi nyingi tunayotumia kwenye nyumba zetu inatokana na NLG, ambayo inatoka nje ya Tanzania. Ni kitu cha ajabu wakati sisi wenyewe tuna gesi ambayo tunaweza kuweka katika form hiyo ya NLG ikasambazwa nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana jambo la discussion ya NLG lifikie mwisho. Huu wimbo wa kila siku kuhusu NLG na matokeo yake hatuyaoni kwa kweli, tunajirudisha nyuma kiuchumi. Naomba sana Serikali kwenye jambo hili iliangalie kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwenye NLG, naomba TPDC waongezewe pesa za kujenga vituo vya kujaza gesi kwenye magari. Nimefurahi kuona kwenye hotuba ya bajeti ya Waziri, amesema kuna vituo vya mobile vitakuwepo viwili Dodoma, kimoja Morogoro na vitatu pale Dar es Salaam. Ninadhani bado havitoshi kwa jinsi uchumi wetu unavyokua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kupunguza gharama ya kutumia mafuta, tunatakiwa tuweke msisitizo mkubwa kwenye suala la vituo vya kujaza gesi kwenye magari, ili matumizi ya gesi yaongezeke na matumizi ya mafuta yapungue, ili kuchechemua uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuunga mkono Mheshimiwa Mbunge mmoja, alisema kwanza tuweke lengo. Serikali ndiyo watumiaji wakubwa wa mafuta ya petrol na diesel. Tukiweka malengo ya kuhakikisha kwamba, ndani ya miaka mitatu au mitano magari yote ya Serikali yatumie gesi, inawezekana na itatusaidia kukuza uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo ni muhimu sana kwa sababu, bei ya mafuta kila siku inapanda, gesi nchini tunayo. NLG ikijengwa, gesi itatumika sana kujaza kwenye magari na speed ya matumizi ya gesi nyumbani nayo imekuwa ni changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mkoa wa Ruvuma, Lindi na Mtwara matumizi ya gesi nyumbani yatiliwe mkazo ili wananchi wafaidike na gesi yao inayochimbwa katika ardhi ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)