Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nianze kwa kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake kwa nchi yetu. Kuiongoza nchi ni kazi ngumu, haiwezi kulingana na kuongoza kijiwe cha kahawa au shikome. Kule kwetu kuna vitu tunaviita hivyo, ni kazi ngumu, ni mfupa mgumu. Sasa tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu ameweza kuendeleza mshikamano, amani na utulivu wa nchi yetu ambayo pia ni mfupa mgumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunaelewa Mheshimiwa Rais aliichukua nchi kwenye mazingira gani? Ilikuwa ni mfupa mgumu kweli kweli, lakini tunampongeza pia kwa sababu ya miradi ya maendeleo, ambayo nayo ilikuwa ni mifupa migumu. Mradi wa maendeleo wa Mwalimu Nyerere ulikuwa ni mfupa mgumu, Mradi wa kuendeleza Makao Makuu ya Nchi, Dodoma ulikuwa ni mfupa mgumu, mradi wa kuendeleza madaraja na kuanzisha mengine ilikuwa ni mifupa migumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuendeleza Shirika letu la ndege kwa kununua na kuongeza ndege nyingine ni mfupa migumu, lakini yote hiyo Mheshimiwa Rais ameitafuna na kuisagasaga na baadhi ya miradi imekamilika. Sasa watu wengine tukimpongeza wanasema, Mbona ninyi CCM mnampongeza tu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lazima tumpongeze kwa sababu, anayoyafanya Mheshimiwa Rais. siyo ya kawaida na ndiyo maana kwenye Mkutano wetu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Januari, 2025, tulipotafakari sana tukasema tunamtuma nani kutoka CCM ili kugombea Kiti cha Urais? Sisi Wajumbe wa Mkutano Mkuu hatukusita kusema huyu huyu mtafuna mifupa migumu aende. Sasa kwa nini tusimpongeze? Kwa kweli, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, amefanya yaliyo ya kweli kwa wananchi wake na kwa Watanzania wenzake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, ndugu yangu Dkt. Dotto Biteko. Huyu naye ni simba mwendapole. Mambo yake yanaeleweka na yanajulikana pamoja na vitengo vyake. Alipokuwa Wizara ya Madini aliipandisha sana, mapato kutoka Wizara ya Madini yaliongezeka na kelele za wachimbaji wadogo wadogo zilizokuwepo zikanyamaza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati anashika Wizara hii ya Nishati, kulikuwa na vikelelekelele hivi, tulikuwa tunavisikia na Wizara hii siyo rahisi sana. Wizara hii ya Nishati na Wizara ya Madini zilipokuwa pamoja na Wizara nyingine, kama Kilimo na Utalii, siyo Wizara rahisi sana, ni Wizara ngumu. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Dotto Biteko kwa kufanya kazi vizuri, kwa usikivu wake na kwa kutuliza dhoruba zilizokuwa zinataka kujitokeza kwenye Wizara hii. Kwa kweli, nampongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nampogeza Naibu Waziri wake, ni mama mtulivu sana, ametokea kwa vijana, lakini kwa namna alivyoshika na kusaidiana na Naibu Waziri Mkuu amekuwa mama mtulivu na ambaye anaweza kufanya mambo yakaonekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana Watendaji wote wa Wizara ya Nishati kuanzia Katibu Mkuu, wao na watendaji wakubwa wote. Poleni kwa Kiongozi Mkuu wa TANESCO, ndugu yangu Nyamuhanga. Ndiyo hivyo, duniani tunapita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mambo machache tu. La kwanza ni umeme kwenye vitongoji. Tumesikia namna Kamati yetu ya Nishati na Madini ilivyosema, na kwa kweli naungananayo kwamba, tunakwenda polepole. Hatujaenda kwa kasi ambayo inatakiwa, na kama lengo letu ni kupata umeme kwenye vitongoji vyote ifikapo 2030, kwa kasi hii, bado hatuwezi kufika. Waongeze kasi ya kupeleka umeme kwenye vitongoji, kwa sababu hivi tunaviita tu vitongoji, lakini kusema ukweli ni vijiji kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vitongoji vingine ni vikubwa sana, vinatosha kuwa vijiji. Sasa watu walioko kwenye vitongoji hivyo kutokuwa na umeme ni kama tunawabagua hivi. Kwa hiyo, kwenye eneo hili, Wizara waongeze kasi ili tupate umeme kwenye vitongoji vyote ifikapo 2030.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Wilaya yetu ya Maswa, tuna vitongoji 510. Vilivyopata umeme ni vitongoji kama 200, vitongoji kama 310 hivi havina umeme kabisa. Kwa hiyo, naomba sana Wizara iongeze kasi kwenye eneo hili kwa sababu, wananchi wetu wote sasa hivi wanataka umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipengele cha pili ninachotaka kuzungumzia ni low voltage kwenye Mkoa wetu wa Simiyu. Kwa kweli, tunapata umeme kidogo kwenye mkoa wetu. Tuna umeme unaotoka Mkoa wa Mara na Mkoa wa Shinyanga kilovolt 33, lakini kwa sababu, unasafiri kutoka mbali sana unafika mkoani kwetu ukiwa kidogo sana. Sasa unapokuwa kidogo hivi, tuna umeme unaokatikakatika na usiotosha kwa shughuli za maendeleo zinazofanywa na wananchi kwenye mkoa wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tatizo kubwa linakuwepo, hasa wakati wa kuanzia mwezi wa Tano na kuendelea wakati viwanda vya pamba vinapoanza kufanya kazi yake, low voltage inaongezeka zaidi, kwa hiyo, wananchi wanapata shida sana kupata umeme kwenye maeneo yetu. Naomba sana kwamba, tatizo hili lishughulikiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali kwamba, wameanza ujenzi wa kituo cha kupozea umeme pale Imalilo, lakini tunaomba, huyu mkandarasi anaenda taratibu sana. Sababu mojawapo ya yeye kwenda taratibu ni kwamba, halipwi pesa yake kwa muda akimaliza kazi anazozifanya. Kwa hiyo, tunaiomba sana Wizara ifanye juu chini kuweza kumlipa huyu mkandarasi ili aweze kuharakisha kutandaza umeme kutoka Shinyanga mpaka Simiyu ili na sisi tuweze kufaidika na kupata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yupo mkandarasi wa pili anayejenga mitambo baada ya huyu kufikisha umeme kwenye mkoa wetu, huyu sasa hajaripoti kabisa kazini. Naiomba Wizara, huyu aripoti kazini na alipwe pesa yake; anadai advance payment, alipwe ili naye aweze kuja site aanze kazi nasi tuweze kupata umeme wa uhakika wa kilovolt 220 kutoka Mkoa wa Shinyanga. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara watusaidie kwenye eneo hili ili sisi pia tuwe na umeme wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ninalolizungumzia ni magari kwa ajili ya Watendaji wa TANESCO kwenye Mkoa wangu wa Simiyu, hasa kwenye Wilaya yetu ya Maswa. Maswa ina gari lililonunuliwa mwaka 2003, ndilo linalotumika huko field. Naiomba sana Wizara watusaidie kutupatia gari kwa muda unaotakiwa ili meneja wangu wa TANESCO wa Wilaya ya Maswa aweze kwenda field, aweze kutuhudumia na kutufikishia umeme kwa muda unaotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona umewasha mic yako, muda wangu umeisha. Nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)