Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chumbuni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu na kukushukuru wewe pia kwa kunipatia nafasi kuwa miongoni mwa watakaochangia hotuba yetu hii ya Wizara ya Nishati, ambayo imewasilishwa leo hii asubuhi na Mwenyekiti wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nichukue nafasi hii kumpongeza na kumshukuru kwa njia zote Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi ambavyo amekuwa anafanya kazi kubwa sana. Sote ni mashahidi, na kwa jinsi ambavyo ameisimamia sekta hii ya nishati, wapi ameikuta, wapi ilipo na wapi inaelekea? Anahitaji pongezi kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, pia kiranja ambaye anaongoza ndani ya Wizara yetu hii ya Nishati; Waziri wetu Mheshimiwa Dkt. Dotto na Naibu wake wamekuwa ni msaada mkubwa sana kwa Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha yale malengo yake ambayo anayo katika sekta hii ya nishati yanaweza kukamilika kwa muda na wananchi wote wanaona nini kinafanyika ndani ya Wizara hii ya Nishati. Hongereni sana kwa Mheshimiwa Waziri na Naibu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitumie nafasi hii kuwapongeza Katibu Mkuu, Mameneja wote pamoja na Wakuu wa Idara za Distribution ambao ndio msaada mkubwa katika kuhakikisha Wizara hii inafanya yale ambayo wananchi wanayategemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wakati anaingia madarakani, ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ulikuwa umefikia 37%. Kwa hali ambayo tuliokuwanayo, ni wachache ambao walikuwa wanaweza kuona au kuhisi kama tunaweza kulikamilisha na kwa muda ambao umepangwa na kuweza kuleta matumaini ambayo sasa hivi sote tunajivunia humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ningependa nitumie nafasi hii nami nitoe mchango wangu ambao siyo mkubwa, lakini una nafasi yake katika Kamati yangu. Mimi ni Mjumbe wa Kamati hii ya Nishati na Madini, napenda nili-clear hili kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niishauri taasisi yetu ya REA, imekuwa humu ndani tangu tumeanza kuchangia asubuhi, na Wajumbe wengi wamekuwa wakilalamikia bei ya shilingi 27,000. Mimi ninachokiona, tatizo ambalo lipo, tafsiri ya shilingi 27,000 inakuwaje? REA wametoa mwongozo wao kuwa 27,000 ni mita 30 kutoka kwenye chanzo cha umeme, lakini wananchi wengi miongoni mwao wakiwemo na Wabunge wengine humu ndani, wanajua kila kijiji ndiyo shilingi 27,000. Sasa hapa kilichopo ni tafsiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa nichukue nafasi hii niwashauri REA; na Kamati yetu imeshakushauri sana REA kupitia Waziri wetu wa Nishati, kwamba utolewe mwongozo. Wananchi vijijini wengine wako mita, 30 na ukisema mita 120 ndiko kijijini zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu ambaye anakaa nje kidogo ya mji maana yake akikaa mita 120 maana yake huyu ndio maskini zaidi, hana uwezo wa kujenga mjini. Sasa anapokaa mita 120 maana yake anatakiwa alipe zaidi ya shilingi 512,000 ambayo tafsiri sisi kama Kamati ya Nishati na Madini tulisema wenzetu wa REA wachukue juhudi, na juhudi ambayo wanatakiwa kuchukua ni kuweka bei moja, kwamba vitongoji na vijiji wote wapewe definition moja ya kulipa kiasi chochote, hata kama itakuwa zaidi ya shilingi 27,000, basi iwe ni bei ambayo ni elekezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, wananchi wamekuwa wakienda REA kulalamika, kwa nini mnatufanyia bei hii kubwa zaidi ya hivi? REA wanasema sisi tunafuata mwongozo wa EWURA. EWURA nao ukiwauliza ni kwa nini mnapanga bei hii? Wanasema, tumeshatoa justification, shilingi 27,000 ni kutoka wapi mpaka wapi? Kwa hiyo, hii imekuwa ikileta mchanganyiko mkubwa, ndiyo maana kila Mjumbe ambaye anasimama hapa jambo la mwanzo anaanza na bei ya umeme ya shilingi 27,000 na jinsi gani kitongoji na umbali wa mita 100 unakuwaje? Ningependa niwashauri wenzetu wa Nishati kwamba, hili walichukulie kwa uzito ambao uliokuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu kukatika kwa umeme. Jambo hili ni kutokana na tatizo la miundombinu, hakuna ambaye hafahamu. Vilevile, asubuhi hapa tumepata taarifa, Mheshimiwa Waziri amesoma, tunao umeme, sasa hivi uzalishaji wetu tumefika megawati 4,000 which is good na jambo zuri. Tujipongeze kutokana na wapi tulikuwa na wapi tumefika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nataka niuweke hapa sasa katika Wizara hii ya Nishati, lakini katika kitengo cha TANESCO. Umeme tunaouzalisha nchini tunao mwingi, zaidi ya 4,000, lakini usambazaji sasa, transmission line, hazipo za kutosha. Umeme ambao tunapigia kelele humu ndani, tuna umeme Bwawa la Mwalimu Nyerere, 2,115, lakini ukitoka Bwawa la Mwalimu Nyerere umeme unakuja mpaka Chalinze, ukitoka Chalinze umetulia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu ya Nishati sasa hivi ina mradi mkubwa, ambapo miezi miwili iliyopita tulishuhudia pale Zuzu Wakandarasi wamepatikana ili kutoa transmission line kutoka Chalinze mpaka hapa Zuzu ya 400 kilovolts. Hii itasaidia sasa kuutoa ule umeme kule ukaja hapa, halafu hapa tukajenga line nyingine kutoka Zuzu kwenda Singida, na Singida tutapata line nyingine ambayo inaunganisha sasa ile ya Arusha kwenda mpaka Namanga ili kuweza kutimiza ile azma na nia ya Mheshimiwa Rais kuuza umeme nje ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezo wa kuuza tunao, umeme tunao tunachokosa tu ni transmission. Wananchi wengi wana hamu na wana haraka ya kuupata umeme kama wanavyoona sehemu nyingine. Kweli nia ipo, Serikali mipango yote hii imeiweka sisi Wajumbe wa Kamati tuna-declare humo kuwa mipango yote iko wazi na Serikali imekuwa ikifanya kila aina ya juhudi. Kikubwa zaidi, tuhakikishe usambazaji wa umeme mkubwa wa kilovoti 400 tuhakikishe unaenda kwa haraka na Serikali iweke bei yake hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, napenda niwapongeze Wajumbe wenzangu wa Kamati kwa kuweza kuisimamia Wizara hii ya Nishati kuweza kufanya haya yote ambayo mnawasifu Waziri na Naibu wake na Watendaji. Bila ya mwongozo wetu sisi kama Kamati yasingefikiwa. Kwa hiyo, nasi pia mtupigie makofi tuseme tumewasimamia, tunajipongeza sana, ahsanteni sana. (Makofi)
MBUNGE FULANI: (Alizungumza bila kutumia kipasauti, hakusikika).
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Wewe siyo Kamati yako, haikuhusu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)