Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Joseph Zacharius Kamonga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi niweze kuchangia Bajeti hii ya Wizara ya Nishati. Niungane na Wabunge wenzangu wote kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Daktari Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri sana anayoifanya kwenye sekta hii ya nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nampongeza pia Mheshimiwa Dotto Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati. Kwa kweli kazi anayoifanya ni nzuri sana. Alipokuwa Njombe niliweza kueleza changamoto za Kata ya Lumbila na Kata ya Kilondo kule Jimboni kwangu, Mheshimiwa Biteko aliunda timu ya wataalam mchanganyiko wa TANESCO na REA, waliweza kwenda Kijiji cha Nkanda, walienda Kijiji cha Lumbila, Kijiji cha Chanjale na sehemu ile ya Kata ya Kilondo. Nashukuru sana Kamati ile ambayo aliunda iliweza kuleta matokeo makubwa, kuna hatua mbili, tatu tulisogea kwenye changamoto za umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kumtuma Naibu Wake Mheshimiwa Judith Kapinga Jimboni Ludewa ambako aliweza kutusaidia kutatua changamoto ya umeme katika Kata ya Milo, Kata ya Mawengi ambao ulikuwa una mzalishaji binafsi anaitwa Jumah. Wananchi wale walikaa miezi tisa gizani, lakini baada ya ujio wa Mheshimiwa Waziri hatua za haraka zilichukuliwa na wananchi wale wa Mawengi, Milo waliweza kuwashiwa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika, Mheshimiwa Kapinga alitusaidia kutatua changamoto ya umeme wa Madope ambao unasambaza kwenye vijiji 20, na ulikuwa ni umeme ambao unazalishwa na mzalishaji binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo haya yalikuwa na changamoto za mgao wa umeme kwa zaidi ya masaa 12. Kwa hiyo, kwa kitendo cha Mheshimiwa Waziri kumtuma Naibu wake tuliweza kutatua changamoto hizi kwa kiasi kikubwa, kwani wazalishaji hawa binafsi waliweza kuingizwa kwenye gridi ya Taifa na mgao ulimalizika pale pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani zangu hizi naomba pia kuwakumbusha watu wa REA. Kulikuwa kumetengwa kiasi cha shilingi bilioni sita ambayo walikuwa wapewe watu wa Madobe kwa ajili ya kurekebisha changamoto ya miundombinu ya umeme wa Madope. Ninapozungumzia hili, nitoe pole nyingi sana kwa Mheshimiwa Waziri kwa kuondokewa na Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO. Nina imani barua za mwisho mwisho alizozishughulikia ni pamoja na barua hii ya Ludewa ya shilingi bilioni sita ambazo zinapaswa kutoka REA kwenda TANESCO kwa ajili kwenda kurekebisha miundombinu ya umeme wa Madobe. Kwa hiyo, nitoe pole nyingi na tumwombee marehemu apumzike kwa amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa REA walitenga hizi shilingi bilioni sita kwa sababu mzalishaji binafsi aliyejenga miundombinu ya umeme ule wa Madope, nyaya ambazo aliziweka zilikuwa ni milimita 20 wakati standard ya TANESCO kwa sasa ni milimita 100. Kwa hiyo, inatakiwa zile nyaya zibadilishwe, nguzo zile ambazo ziliwekwa nazo zilikuwa chini ya kiwango, nyingi zilikuwa zinadondoka na zilikuwa zinadondoka na kusababisha kukosekana kwa umeme muda mwingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sasa wameunganishwa kwenye gridi ya Taifa, maana yake umeme unavyokatika kutokana na miundombinu hii ambayo nimeisema, basi Wilaya nzima inaathirika na kuleta kero kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukipokea hizi shilingi bilioni sita, kwa sababu bajeti yote ilikuwa ni shilingi bilioni nane, lakini hizi zipo na barua zile za mwezi Septemba kulikuwa na correspondence kati ya TANESCO na REA. Wiki iliyopita nilimwona Mheshimiwa Naibu Waziri, namshukuru alinisikiliza. Kwa hiyo, fedha hii tunaiomba iweze kuharakishwa ili Meneja wa TANESCO wa Mkoa aweze kwenda kufanya operation kule au kwa kutumia wakandarasi ili wafanye kazi kubwa kwa muda mfupi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru pia nimeona katika tangazo kwenye mfumo wa NEST vitongoji ambavyo havikuwa na umeme takribani 35 vimeweza kuingia kwenye orodha. Hii itaondoa kero kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nilikuwa na Mheshimiwa Mkuu wangu wa Wilaya, tulifanya mkutano pale Ludewa Mjini, baada ya kutoka kwenye Baraza la Madiwani tukafanya mkutano na pale Makao Makuu ya Wilaya. Kuna wananchi wengi wanaotoka maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, waliomba sana niweze kufikisha hoja hii Bungeni kwamba tuweze kusaidiwa kutatua hii changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Ludewa sasa lina uwekezaji mkubwa. Kuna mwekezaji anakwenda kuchimba dhahabu Irininda, pia kuna wawekezaji pale Kata ya Lubonde Kijiji cha Mkiu wanakwenda kuchimba hizo zinaitwa rare earth element/minerals. Kwa hiyo, wataweka pale migodi yao wanahitaji umeme mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika kuna Liganga na Mchuchuma. Mheshimiwa Jafo alitembelea Jimboni kwangu, ilionekana kwamba, uwekezaji unakuja kuanza mapema sana. Sasa uwekezaji huu unakwenda sambamba na uwepo wa umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitumie fursa hii kuomba Bunge lako Tukufu kupitia Wizara hii tuweze kuletewa kituo cha kupoozea umeme pale Ludewa, kwa sababu kwa sasa tunategemea kituo cha kupoozea umeme ambacho kipo Madaba, ni kilometa nyingi sana, ni zaidi ya kilometa 200 kutoka Wilayani Ludewa. Kwa hiyo, kituo hiki kitakuja kusaidia wawekezaji hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio hao wawili tu niliowasema, Kijiji cha Mdilidili pia kuna wawekezaji wameshaleta mitambo mikubwa kwa ajili ya uchimbaji wa madini mbalimbali pale. Kwa hiyo, nao watahitaji umeme mkubwa sana. Kwa hiyo, tukiletewa kituo cha kupoozea umeme, na huu uwekezaji wa Liganga na Mchuchuma unavyoanza, kwa kweli tutakuwa tumepiga hatua kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Wilaya ya Ludewa tuna changamoto ya gari la kubebea nguzo. Ilitokea Kata ya Ibumi, kuna nguzo ziliungua au kata nyingine ambapo zinahitajika kubadilishwa nguzo. Kwa mfano, Kisaula, au Iwela, ilichukua muda mrefu kwa sababu ma-engineer wa TANESCO walikuwa hawana gari la kubebea nguzo, lakini namshukuru Meneja wa Mkoa amekuwa mwepesi kuwasaidia kuwaazima gari. Kwa hiyo, ili tuweze kutatua changamoto za wananchi kwa haraka, naomba Wizara hii iweze kutuletea gari lile lenye winch kwa ajili ya kubebea nguzo ili changamoto za wananchi ziweze kutatuliwa kwa haraka zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuomba hili gari la kubebea nguzo, napenda pia kuomba Wizara hii iweze kutuma wataalam wake pia Kata ya Kilondo ili wakaangalie ule mradi wa umeme wa Maji. Kwa sasa nimshukuru Mkurugenzi Mkuu wa REA, kwa maelekezo aliyopewa na Mheshimiwa Waziri, alituahidi anatafuta mkandarasi aende kuwafungia solar wananchi wale wakati wakisubiri mradi wa umeme wa maji kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wale wananchi wako tayari hata kukabidhi mradi huu Serikalini kwa sababu ule mradi ulikuwa ni mali ya Serikali ya kijiji. Kwa hiyo, wako tayari hata kukabidhi Serikalini na wale wakina Mwambeleko ambao walikuwa wanazalisha umeme wao, wanachohitaji ni wananchi wapate huduma. Kwa hiyo, wanaomba wataalam waende wakaangalie ili waweze kupata ruzuku kutoka REA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme huu wa solar, kule Ziwa Nyasa kunakuwa na dhoruba, mawimbi makali. Kunapokuwa na mawimbi, kunakuwa na mawingu. Kwa hiyo, kukiwa na mawingu umeme huu wa jua unaweza usipatikane wakati wote. Kwa hiyo, wanaomba sana mpango ule wa kuzalisha umeme wa kutumia maji uendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijahitimisha, kuna ule mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Kikonge ambao kwenye jimbo langu, wananchi wa Liugai wameshakwenda kufanyiwa uthamini tangu mwaka 2024. Kwa hiyo, wananchi wale robo tatu ya kijiji wameshafanyiwa uthamini na wameambiwa wakati wowote wanaweza kulipwa fidia ili wahame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Serikali iweze kwenda kutoa kalenda ya utekelezaji wa mipango hii ili wananchi wale nao waweze kupanga ratiba zao za kilimo, kwa sababu maeneo hayo wanayategemea kwa kilimo. Wanaomba sana waweze kujua ni lini wananchi wale wa Liugai watalipwa fidia ili mradi huu uweze kutekelezwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, naomba tu, kuna shule tatu; Shule ya Sekondari Lubonde, nimetembelea juzi, haina umeme, na iko kwa hawa wazalishaji binafsi ambao tayari wameshaingia kwenye gridi ya Taifa. Kuna Shule ya Sekondari Mount Masusa ambayo iko Kata ya Lupanga na Shule ya Sekondari Madilu. Shule hizi zina watoto wengi na wanafanya vizuri. Kwa hiyo, tunaomba Serikali iweze kuwapelekea umeme haraka ili watoto hawa waweze kutumia katika masomo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, nashukuru sana kwa kupewa nafasi hii, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)