Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbinga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Bajeti ya Wizara ya Nishati. Kwanza kabisa naomba nimpongeze na kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi alivyosimamia na kuhakikisha kwamba anatekeleza mambo mengi sana yanayohusiana na Wizara ya Nishati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninaomba nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Biteko (Mb), Naibu Waziri Mkuu pia Waziri wa Nishati kwa jinsi anavyofanya kazi vizuri ya kuhakikisha kwamba anatatua changamoto za wananchi kwenye masuala ya umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Dkt. Biteko kwa sababu anafanya kazi za kizalendo. Kama ukiangalia kipindi kile alikuwa kwenye Wizara ya Madini alifanya kazi vizuri na leo anafanya kazi kwenye nafasi ya Unaibu Waziri Mkuu, na pia nafasi ya Waziri wa Nishati. Wakati anateuliwa, mimi nilisema huyu mtani wangu ataweza kweli kumudu nafasi zote mbili? Lakini leo tunampongeza kwa sababu amefanya vizuri na anaendelea kufanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Judith Kapinga, Naibu Waziri wa Nishati, dada yangu, anafanya kazi nzuri. Anatoa ushirikiano mkubwa sana kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati. Wakati anaingia pale Wilayani kwetu Mbinga tulikuwa na changamoto, baadhi ya vijiji vilikuwa bado havijafikiwa na umeme, na alipoingia alifanya kazi nzuri, alifanya kazi kwa bidii ya kusimamia kuhakikisha kwamba, vijiji vyote mpaka sasa hivi vimepata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie pia nafasi hii kumpongeza Eng. Mramba, Katibu Mkuu wa Wizara. Pia nawapongeza Dkt. Mataragio na Dkt. Kazungu Manaibu Katibu Wakuu. Pia, bila kuwasahau Wakurugenzi kutoka kwenye taasisi mbalimbali zinazosimamiwa na Wizara ya Nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii nimpongeze sana Meneja wa TANESCO wa Mkoa Ruvuma na Meneja wa TANESCO wa Wilaya Mbinga, kwa jinsi wanavyojitahidi kutatua changamoto mbalimbali zinazotokana na hitilafu za umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majukumu mengine ya TANESCO, lakini bado TANESCO ina jukumu kubwa la kuhakikisha Wizara ya Nishati inasimamia uzalishaji wa umeme, inasimamia usafirishaji wa umeme na inasimamia usambazaji wa umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipitia taarifa ya Waziri wa Nishati ambaye ni Naibu Waziri Mkuu, ukiangalia takwimu za uzalishaji kufikia mwezi wa Nne tulikuwa tunazalisha megawati 4,031, lakini ukiangalia kwenye matumizi, tulikuwa tumefikia megawati 1,921.44. Kwa hiyo, unakuta kabisa kwamba kuna tofauti, yaani kuna ziada ya megawati 2,110. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mtazamo huu unaona kwamba ziada hiyo siyo kwamba imetokana na kwamba tumetosheka kwenye matumizi ya umeme, hapana. Bado tuna changamoto, inatakiwa tufanye kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba tunaweka miundombinu ya kutosha kusafirisha umeme, lakini pia tunaweka miundombinu ya kutosha kusambaza umeme kwa wananchi katika maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu lingine ambalo lilikuwa ni mpango mzuri sana wa Serikali ni kuhakikisha kwamba inapeleka umeme vijijini na inapeleka umeme kwenye maeneo ya mjini. Naomba nichukue nafasi hii niipongeze sana Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba umeme umepelekwa vijijini takribani vijiji vyote katika Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali inaendelea kusambaza umeme kwenye maeneo ya mjini kwa sababu miji yetu inazidi kukua. Kwa hiyo, kwa hilo naomba niwapongeze sana na ninaomba mwendelee kuhakikisha kwamba umeme huu unasambazwa katika hayo maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu lingine ni kuhakikisha kwamba tunasimamia kufanya utafiti na kuhakikisha kwamba tunafanya extractions ya kwenye mafuta na gesi. Nalo naiomba Serikali iendelee kuweka msisitizo mkubwa sana kwenye maeneo hayo mawili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze pia Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka kipaumbele kusimamia kwenye kuhakikisha kwamba kuna matumizi ya nishati safi. Hilo ni suala la msingi, kwanza linarahisisha upatikanaji wa nishati kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukiangalia taarifa ya Wizara ya Nishati kwenye masuala ya uzalishaji umeme, tunakuta kwamba 67.4% umeme huo unazalishwa kwenye vyanzo vya maji. Kwa hiyo, tusiposimamia utunzaji wa maliasili kwenye misitu na vyanzo vya maji, ni wazi kwamba hivi vyanzo ambavyo vinazalisha umeme kuna siku tutakuja kukwama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba Wizara waendelee kusimamia kuhakikisha kwamba tunapata nishati safi ya gesi kama tulivyoanza kugawa, lakini na vitu vingine ambavyo ilitakiwa viendelee kuhakikisha kwamba tunalinda maliasili ya misitu ili kutunza uoto wa asili na kuhakikisha kwamba tunapata umeme wa maji kwa muda wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu lingine la Wizara ya Nishati ni kuhakikisha kwamba tunazalisha gesi kupitia LNG. Kwenye LNG tuna uhakika wa kupata umeme wa kutosha, na pia tunakuwa na uhakika wa kupata umeme kwa ajili ya kutumia majumbani. Vilevile tutaendelea kupata umeme gesi kwa ajili ya kutumia kwenye magari yetu, na hiyo itatusaidia sana kupunguza kutumia fedha nyingi za kigeni kuagiza mafuta kutoka nje. Kwa hiyo, naomba Serikali iendelee kuweka mkazo mkubwa kuhakikisha tunaimarisha umeme wetu kwa kupitia LNG. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna njia nyingine ya kupata umeme kupitia jotoardhi. Niliona wakati wa kongamano la umeme jotoardhi wakati inafanyika Dar es Salaam ilionekana Mbeya tayari wameanza kufanya utafiti na kuanza kuzalisha umeme huo. Kwa hiyo, naomba Serikali iendelee kuwekeza fedha nyingi sana kuhakikisha kwamba tunazalisha umeme kupitia jotoardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata bahati katika nchi yetu tunazalisha na tuna maeneo mengi sana yenye makaa ya mawe. Kwa mfano, nikichukulia eneo la Liganga, sisi kule Mbinga tunazalisha makaa ya mawe, lakini Liganga tumepata bahati kuna makaa ya mawe, na madini ya chuma yako pale. Kwa hiyo, ni wazi kwamba kama Serikali itawekeza fedha nyingi sana kwenye kuzalisha umeme kupitia makaa ya mawe, wakati wa kuvuna chuma, hatutatumia gharama kubwa sana ya kupata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile njia nyingine mojawapo ya kuongeza umeme ni kuzalisha umeme kupitia makaa ya mawe. Katika literature mbalimbali ambazo nilizisoma nilikuta kwamba kuna wenzetu wa India, kuna kampuni moja inaitwa Adam Power Generations Limited, inazalisha umeme megawati 17,500 kwa kupitia makaa ya mawe. Wanasafirisha makaa ya mawe kutoka Tanzania na sehemu nyingine, lakini sisi makaa ya mawe tunayo Tanzania na tuna eneo moja ambalo tunaweza tukazalisha makaa ya mawe tukavuna chuma na tukayeyusha kupitia makaa ya mawe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi zote nilizotoa pamoja na mchango mwingine wa nyongeza ambazo nimechangia upande wa Serikali ili iweze kufanya, lakini bado kuna changamoto kwenye eneo langu la Jimbo la Mbinga Mjini. Kama nilivyosema awali kwamba Serikali imejitahitadi, imesambaza umeme katika vijiji vyote vya Jimbo la Mbinga Mjini na vijiji 78, na pale mjini umeme unaendelea kusambazwa, lakini kuna changamoto kubwa sana ya kukatika umeme mara kwa mara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo naomba Serikali kwanza iendelee kuimarisha miundombinu ya kusambaza umeme, lakini pia tujengewe kituo kidogo cha kupooza umeme ili kuhakikisha kwamba umeme ule unaimarika katika maeneo yale. Pia kama tulivyosema, tumefanikisha kupeleka umeme kwenye vijiji vyote, lakini bado tuna changamoto ya kupeleka umeme kwenye vitongoji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wale wanahitaji sana kupata umeme na wengi wapo kwenye vitongoji ambavyo vijiji vyao vimepata umeme. Kwa hiyo, naomba Serikali iendelee kupeleka umeme na kuusambaza kwenye vitongoji mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto zote ambazo nimezisema, lakini pale wilayani kwangu kuna changamoto ya gari kwa wale watumishi. Wilaya ya Mbinga ina majimbo mawili na maeneo ya Mbinga maeneo mengi ni miinuko, gari iliyopo pale ni pickup ambayo ni ya muda mrefu. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati katika bajeti yao waangalie ni namna gani tutakavyopata gari ili iweze kuwasaidia wale watumishi kwenda kufuatilia na kuhakikisha kwamba wanapeleka umeme kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)