Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Bahati Keneth Ndingo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mbarali

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuwa mchangiaji wa mwisho jioni hii ya leo. Nami nianze kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake kubwa za kuhakikisha umeme unafika kwenye maeneo yote ya wananchi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati kabisa, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuteua timu imara ya Wizara ya Nishati ikiongozwa na kaka yetu, kiongozi wetu Naibu Waziri Mkuu, kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko. Kwa kazi kubwa kubwa wanayofanya akisaidiwa na mdogo wangu Mheshimiwa Judith Kapinga, kwa kweli wanafanya kazi njema. Nilikuwa najiuliza, timu ya hii Wizara na Wasaidizi wao kule; Katibu Mkuu na Wakurugenzi, ni watu humble sana na wanafanyakazi vizuri sana, lakini nikajua ni jitihada za Naibu Waziri Mkuu na zile hotuba zake za kila wakati kutufundisha. Kwa hiyo zinachangia pia kila wakati kujielimisha na hivyo kutuboresha zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, aendelee kutupatia zile hotuba za kufikirisha, za kimaisha ili tuendelee kutafakari na kujisahihisha na kujikosoa ili tuweze kuwa bora kila wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tushukuru sana wananchi wa Mbarali, tunashukuru sana Serikali kwa kazi kubwa ambayo mmetufanyia ya kuhakikisha tunapata umeme. Sisi kwenye kazi ya vijiji, vijiji 102 vilivyopo Wilaya ya Mbarali tayari mmetupatia umeme, tunashukuru sana kwa jitihada hizo, lakini kwenye upande wa vitongoji, kati ya vitongoji 712 tayari tumepata umeme kwenye vitongoji 510 ni kazi kubwa, wanastahili pongezi na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuna kazi ya vitongoji 202 na nimefarijika leo asubuhi nilimwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusiana na Mkandarasi kufika, amenihakikishia wiki hii mkandarasi atafika. Hivyo sasa, vitongoji vile 15 na nimeona vitongoji 53 tayari mmeshatangaza tender, kwa sasa tutabaki na vitongoji 134 kwa siku zijazo kupatiwa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawashukuru sana, tunawasubiri kwa hamu sana, tunahitaji umeme uwake maeneo yote, kwa sababu sasa hivi umeme siyo jambo la luxury tena, ni hitaji la msingi, ni Uchumi, ni ajira. Kwa hiyo, tunawatakia kila la heri na tutafurahi zaidi mkitusaidia tupate hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wilaya ya Mbarali tumeshapokea shilingi bilioni 9.2 kwa ajili ya shughuli ya kupeleka umeme. Hizi ni fedha nyingi na Wilaya yetu tunashukuru sana kwa kazi kubwa hii ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu amefanya. Sasa naomba kwa unyenyekevu sana Jimbo la Mbarali lina changamoto kutokana na jiografia yake, lakini tuna changamoto kubwa, na wale watu hawana usafiri. Jimbo hili lina changamoto ya usafiri, lazima upite mashambani ndiyo ukatafute kijiji kilipo. Kwa hiyo, hata nguzo ikianguka ni lazima mtu akae siku mbili au tatu, aazime gari kwenye Wilaya ya jirani ndiyo wakafanye shughuli hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imekuwa ni changamoto kubwa sana, na wananchi sasa imekuwa kilio wanapopata tatizo inachukua siku tatu, nne ili waweze kwenda kuhudumiwa. Naomba sana sana tusaidiwe tupate gari la nguzo ili Wilaya hii ambayo jiografia yake inasumbua sana waweze kupata usafiri huu na kuweza kuhudumiwa kwa wakati. Vilevile magari ya watumishi ni changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo ni changamoto, tunatambua Serikali wanayo jitihada kubwa ya kuhakikisha kumtua mama kuni kichwani, na hilo zoezi limefanyika kwa kweli wanajitahidi, lakini tunaomba, kuna mitungi ilikuja ya bei elekezi. Kwa mazingira haya, niishauri tu Serikali kwa siku zijazo, lazima tuangalie mazingira tuliyonayo. Sisi kule vijijini mtu yuko radhi kutoka tu hapo nje akikuta kuna kuni, anaichukua na kuiweka jikoni, maisha yakaendelea. Sasa mpaka umwelimishe kwamba zina athari na vitu kama hivyo, itachukua muda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hata kama ni ruzuku, hebu tuangalie kwa sababu mitungi mingi huko vijijini sasa hivi ikishaisha gesi, haiendi tena kwenye mzunguko kutokana na gharama kubwa. Kwa hiyo, hebu mfanye tathmini kubwa ya kuhakikisha kwamba tunawasaidia wale ambao wako karibu na wanaweza wakapata kuni hata kwa shilingi 2,000, kwa kuwandolea mzigo mkubwa, hebu tuangalie ili tuweze kuwasaidia ili azma ya Mheshimiwa Rais ya kwamba wanawake sasa watuliwe kuni kichwani iweze kutumia kulingana na nishati hii kupatikana kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, tunafahamu sasa hivi shida iliyopo ni kukatika umeme kwa ajili ya kurekebisha miundombinu, na changamoto hii pia imekuwa kero kwa wananchi. Basi angalau tuwe tunapata taarifa kuliko kutokee tu hitilafu ghafla. Angalau watengeneze utaratibu kwamba leo tuna matengenezo ya umeme maeneo fulani na maeneo fulani umeme utazimika saa fulani na saa fulani ili kuondoa hasara ambazo zinaweza zikapatikana kwa kuzimika haraka bila taarifa yoyote. Hiyo itatusaidia ili tuweze kupata umeme wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. Ahsante kwa kuchangia. (Makofi)