Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vunjo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa fursa hii. Ninaomba nianze kwa kukushukuru wewe pamoja na Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wengine wa Bunge kwa namna mnavyoendesha Bunge hili. Niwatakie kila la kheri kwenye uchaguzi unaokuja ili wapigakura wenu wawarudishe hapa kwa kishindo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba katika kuchangia Wizara hii, kwanza ni lazima tumpongeze Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo amewezesha Wizara hii ya Nishati inayoongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kuiwezesha kutekeleza mambo makubwa sana katika hii nchi ndani ya kipindi kifupi cha miaka minne. Ninataka niseme kwamba kuna mengi ambayo tumeyaona pamoja na kukamilisha ile miradi migumu sana kama ule wa Bwawa la Nyerere kwa wakati tulioutarajia na kuweza kufanya hii nchi ijitosheleze kwa uzalishaji wa nishati angalau kwa kipindi hiki ambacho tumefikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kwamba tuna ziada sasa ya umeme na ni kitu ambacho watu wengi hawakutarajia kwamba tutafikia hapo. Pia, ninashukuru kwamba hiyo ziada Wizara hii imeendelea sasa kuunganisha gridi yetu kwenye Power Pool ya Afrika Mahariki pamoja na SADC, which means kwamba pengine hata sisi tunauza umeme kwa nchi fulani ambayo hatujaweza kuambiwa, lakini ninaamini ni mafanikio makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba pengine tumshukuru sana na tumpongeze sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuzindua Benki ya Ushirika jana. Hilo ni jambo kubwa sana ambalo ninaamini watu wengi hawajaelewa kilichofanyika, lakini sisi tuliokuwa tunafuatilia ni Taasisi au ni Benki ambayo imechukua muda mwingi sana na kazi kubwa sana ya Mheshimiwa Rais mwenyewe pamoja na Waziri wa Kilimo na wale wengine wanaohusika kuweza kuanzisha hiyo Benki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema mambo ya Benki hapa kwa sababu ninaunga mkono hoja ya kwamba kwa gharama kubwa za uunganishaji wa umeme kwenye yale maeneo ya miji na miji midogo, ninaamini sasa TANESCO inaweza kwenda kutafuta fedha ya mikopo ili waweze kugharamia hizo gharama za kuunganisha wananchi kwenye umeme na halafu wakalipa ule mkopo kwa kutumia kuongeza ile gharama ya invoice ya umeme. Ninaamini ni vigumu sana kwa wananchi wengi kujiunga kwa shilingi 350,000 na zaidi kwa maeneo mengine kwenye umeme bila kupewa nafasi ya kulipa kidogo kidogo kwa hiyo gharama ya kujiunganisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue pia fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, nimpongeze pia Naibu wake pamoja na Watendaji wake kwenye hizi taasisi. Mheshimiwa Waziri ana taasisi nyingi na Watendaji wake wote wanaonekana ni Watendaji waadilifu, ni Watendaji ambao wana-deliver (wanafanya ili waone matokeo chanya). Ninasema kwamba hawa watu ninaamini kazi na utu vinaendelea na ninaamini kwamba wataendelea kusonga mbele kwa namna hiyo na kwa slogan hiyo ya “Kazi na Utu, Tunasonga Mbele.”
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
TAARIFA
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kunambi, taarifa.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampa taarifa Mheshimiwa Mzee wangu Kimei kwa kupongeza. Ninampa taarifa kwa sababu tulikuwa tuna changamoto ya umeme kwenye vijiji lakini kazi hiyo imekamilika. Ni matumaini yangu sasa Serikali inakwenda kukamilisha umeme kwenye vitongoji ikiwemo Kitongoji cha Mlima Mbwanda kule Mlimba, Ahsante.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Kimei unaipokea taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kunambi?
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kupunguza muda wangu kwa kulikubali hilo, lakini ninampongeza na yeye amepata umeme kwake na ataendelea kupata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hivi kwamba kazi imefanyika na kwenye Jimbo langu nilivyopata Ubunge mwaka 2020 tulikuwa tuna vitongoji 191 ambavyo havina umeme. Leo hii ninavyozungumza hapa vitongoji vimebaki 40 tu ndiyo havina umeme. Ninaamini hivyo vinaenda kukamilishwa siku za karibuni kwa sababu kuna ule mradi wa vitongoji 15 ambapo tayari tumeanza kuona kuna wakandarasi wanatekeleza kwenye vitongoji vya Umasaini na Kimala pale relini Kata ya Kahe Magharibi; Karango A na B - Mwika Kusini; Kiruiche, Kalimani na Kisimani kwenye Kata ya Makuyuni; Kwakipura - Mwika Kaskazini; Kiraracha kwenye Kata ya Kilwa Vunjo Kusini; Msufini - Kilwa Vunjo Mashariki; na Reli juu, Kahe Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo inatekelezwa na hivyo tunapunguza hata hiyo 40 ambayo tumesema. Ninashukuru sana kwamba Serikali imetekeleza ahadi yake kama ilivyofanya na kwamba hivi vingine 40 vilivyobaki navyo vitaenda kupata Wakandarasi na fedha ili tuweze kuona kwamba Wanavunjo wanajivunia nchi yao, wanajivunia maeneo yao na miradi yao ambayo wanatekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba katika mambo yangu ya jumla kabla sijaenda mengine ya Vunjo huko, niseme kwamba mimi ninaamini kwenye Gridi Imara. Gridi Imara sasa ndiyo jambo kubwa na ndiyo mradi ambao tunatakiwa tuutekeleze kwa nguvu zote. Nimeona bajeti yake ni ndogo, mimi ninaamini kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ataenda kupigania tupate fedha ya ziada ili Gridi Imara sasa iweze kutekelezeka kwa sababu tunaona umeme unakatika katika, lakini siyo kwa sababu umeme ni mdogo, ni kwa sababu ya uimara mdogo wa usambazaji wa umeme ule. Kwa hiyo, hilo ninaona ni jambo la maana sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ninafikiri ni la umuhimu ni ile Project ya LNG. Watu wengi wameizungumzia kidogo jana, lakini ile project imekaa kwenye drawing board kwa muda mrefu. Tumekuwa tukiambiwa inakamilika, lakini tunamwomba Mheshimiwa Waziri ajaribu kutoa msukumo zaidi kwenye utekelezaji wa huu mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi tena Vunjo sasa niseme hivi; vijiji na vitongoji kadhaa kama nilivyosema vimepata umeme lakini kuna wananchi wanakaa mbali sana na zinapopita zile line za umeme. Kwa hiyo, ule mradi wa umeme jazilizi ni mradi pia ambao unahitajika kwa sababu kusema ukweli watu wengi ambao wanaona umeme umepita lakini hawawezi kuuvuta kwa sababu uko mbali na ni gharama kubwa kuweka zile nguzo inakuwa ni jambo gumu sana. Kwa hiyo, ninaomba kwamba sasa Serikali ione uwezekano wa kusukuma umeme jazilizi ili kupunguza gharama za wananchi kujiunganisha kwenye huu umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Vunjo kuna wananchi 784 ambao wanadai fidia kwa vile walipisha maeneo yao kupitisha umeme wa Kilowati 132 yenye umeme mkubwa kutoka Chungu kwenda Wilaya ya Rombo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hawa wananchi wengi wapo kwenye kata yangu mojawapo. Kwa hiyo, tunamuomba sasa Mheshimiwa Waziri tusilaze damu hawa wananchi wakalipwe hiyo fidia yao. Fidia yao tayari imeshahakikiwa na Wizara yako wakishirikiana na Wizara ya Fedha. Ni fidia ambayo ni kama shilingi bilioni 7.6, siyo fedha nyingi, ninaamini kwamba wanakwenda kulipwa kwa sababu kusema ukweli wanasononeka licha ya kwamba Rombo wamefaidi na tunataka wafaidi huo umeme, lakini wao wanaona kwamba ni haki na kila Serikali ina hiyo sera ya kulipa fidia bila kuchelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niseme hivi, kwa vile ninazungumza mambo ya fidia na huyu ni Naibu Waziri Mkuu, ninaomba pia nimbebeshe ambalo siyo la kwa kwake kabisa. Kuna fidia ya wananchi wa pale Gona na Njiapanda wamepisha ujenzi wa Kituo cha Kukagulia Mizigo cha Pamoja (One Stop Centre ya Kukagulia Mizigo) pale kwenye maeneo ya Gona na Njiapanda. Pia, wengine kule Mabungo ambapo napo wamepisha ujenzi wa kituo kama hicho. Kwa hiyo, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu ninaomba unisaidie kusukuma hiyo, kwa sababu iko Wizara ya Fedha na TANROADS, lakini tokea mwaka 2013 wanapeleka haya madai yao na bado hawajapata kitu. Mheshimiwa ninaomba utusaidie kwenye hilo.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Kimei hii ni kengele ya pili. Kwa hiyo, tunaomba ...
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninaunga mkono hoja ya Wizara ya Nishati. (Makofi)