Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ngara
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kipenzi cha Watanzania, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan Mheshimiwa Rais ambaye amejipambanua nchi hii, kwa kuhakikisha fedha zinapelekwa vijijini kwenda kutatua matatizo ya wananchi ni Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye amehakikisha huduma ya majiko ya gesi inaanza kusambazwa vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amehakikisha katika kipindi kifupi vijiji vyote vya Tanzania vinapata miundombinu ya umeme, Mheshimiwa Rais huyu amehakikisha hata bwawa la kufua umeme la Rusumo lililopo wenye Jimbo la Ngara nalo linajengwa linakamilika, kila Mtanzania anasema Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan mitano tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mitano tena ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan haijaja hivi hivi ni kwa sababu Mheshimiwa Rais huyu amegusa maisha ya Watanzania, si tu amepeleka nuru ya mwanga wa umeme vijijini ni kwa sababu Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameondoa vibatari vijijini, kwa sababu wananchi ambao walikuwa hawana umeme wamekuwa wakiendelea kutumia vibatari hasa kwenye vijiji na sasa jambo hilo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameliondoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata wale wanaosema no reform no election, wale wengine wa mlengo wa kushoto na wenyewe kimya kimya wanakubaliana nami kwamba Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan mitano tena, hata kama wanaisema kimoyo moyo. Mimi na wananchi wa Jimbo la Ngara tunaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anaendelea kuchapa kazi, tunamuombea afya njema ili aweze kuendelea kuwatumikia Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, wewe pamoja na viongozi wenzako wa Wizara ya Nishati kwa kuweza kuelewa na kutafsiri vizuri maono ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Wizara hii ya Nishati, hakika katika kipindi chako Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko tumejifunza funzo moja la tofauti kati ya kukatika kwa umeme na kukatika katika katika kwa umeme. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma ulikuwa unashangaa huku unaangalia mpira umeme unakatika paa! Wananchi wapo kwenye shughuli zao umeme unakatika, lakini sasa hivi tumeshuhudia maboresho makubwa kwenye Wizara hii ya Nishati hasa upande wa TANESCO, ambapo umeme unapotaka kukatwa wamejitahidi wateja wanapewa taarifa mapema, mwenye kujiandaa anafanya maandalizi na taarifa za kisasa zimeboreshwa katika kiwango ambacho wanawaeleza Watanzania kwamba umeme utakatika muda kadhaa na matarajio ya huduma ya umeme kurudi ni muda kadhaa, hivyo watanzania wanaweza kujipanga. Wale wanaomiliki mitambo ya kuzalisha kwa kutumia umeme wanaweza kujipanga na kufanya shughuli zao, hakika Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko umeboresha huduma ya customer care baina ya TANESCO na wananchi hongera sana Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, wewe na wenzako kwa kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huko tunapoelekea tutajifunza funzo linguine, tutakuja kujifunza tofauti na kukatika na kutokatika kwa umeme. Tunafahamu maendeleo ni hatua na hatua moja huanzisha hatua nyingine, kazi yenu mmeifanya vizuri hongera sana Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaelekeza mchango wangu kwanza kwenye eneo la kuongeza matumizi ya umeme vijijini, wakati tunashukuru kwa kupongeza Serikali kufikisha miundombinu ya umeme kwenye kila makao makuu ya kijiji, bado mahitaji ya umeme ni makubwa kuliko kipindi chochote kile. Wananchi kwenye vitongoji wanasubiria kupata umeme na kiu yao ni kubwa, ninaomba maboresho ya kuongeza matumizi ya umeme kwenye vitongoji yaanze mara moja hasa kwenye mwaka huu wa fedha 2025/2026.
Mheshimiwa Mwenyekiti, malengo mapana iwe ni kuhakikisha tunawapelekea wananchi kwenye vitongoji umeme ili inapofika mwaka 2030, asilimia kubwa ya wananchi kwenye vitongoji vya Tanzania wawe wamepata nishati ya umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maboresho mengine kwenye kuongeza tija na matumizi ya umeme kwenye vijiji na kwenye vitongoji kuna hizi transformer ambazo imewekwa zenye KVA 50 msema ukweli ni mpenzi wa Mungu, hizi transformer uwezo wake ni mdogo, lazima nikiri na niseme kwamba uwezo ni mdogo kwa sababu tumekuwa tukiwalaumu REA na TANESCO ni kwa nini wananchi hawapewei huduma ya umeme, yamkini ni kwa sababu hofu yao ni kwamba wataongeza load ya umeme matokeo yake transformer zitashindwa kuhimili mahitaji ya umeme ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu na ushauri wangu kwa Wizara ya Nishati na TANESCO, tunaomba muanze sasa kutufungia transformer zenye ukubwa wa KVA 100 hadi KVA 200 hii inaenda kusaidia wananchi wengi kuweza kuunganishwa kwenye huduma ya umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuongeza matumizi ya umeme, ninaomba Wizara hii ya Nishati na TANESCO pamoja na REA muweze kuanza ku-push mitungi ya gesi inayoendana sambamba na majiko yanayokubali kupika kwa kutumia umeme na kwa kutumia gesi hii itawasaidia wananchi wakati mwananchi anasubiria kwenda kununua mtungi wa gesi aweze kuunganisha jiko lake la kupikia kwa umeme na umeme uliopelekwa majumbani. Umeme mpaka sasa hivi matumizi yake ukienda vijijini kwa sehemu kubwa wanatumia kwa ajili ya mwanga na sehemu kidogo wanatumia kwa ajili ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuwasaidie ku-push ajenda hii tusiishie tu kusambaza mitungi ya gesi ndugu zangu wa REA, tusambaze mitungi ya gesi inayoendana na majiko yanayokubali kupika kwa kutumia umeme na kwa kutumia gesi na hata ikiwezekana kwa kutumia makaa, kama jiko hilo hilo unaweza ukaweka mkaa likapika tutafurahia kupata teknolojia hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza matumizi ya umeme vijijini, ninashauri Wizara ya Nishati muanze ku-push ajenda ya kuondoa kodi kwenye vifaa vya kieletroniki vinavyotumika jikoni na sebuleni hapa ninazungumza matumizi ya TV, majiko ya umeme, blender za kusagia juisi na vitu vingine watanzania tunapowapelekea umeme vijijini, tuwasadie na kupata vifaa vinavyotumia huo umeme ili kuendeleza kurahisisha maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawaomba Wizara ya Nishati pushini ajenda ya kuondoa kodi kwenye vifaa hivi ili Watanzania waweze kuvipata kwa pesa kidogo ambayo wanaweza kuhimili. Nina uhakika jambo hili Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko analiweza, wale wanaomwongelesha wamwache tupo tunazungumza na yeye! Mwenyekiti awe unatusaidia katika eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko utusaidie ku-push hii ajenda Watanzania waweze kupata access ya vifaa vinavyotumia umeme ambavyo kodi yake imepunguzwa ili kuwe na mantiki ya kupeleka umeme kwenye vijiji na kwenye vitongoji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ninalotaka kuzungumzia ni namna gani TANESCO na REA wanajipanga kurejesha huduma ya umeme inapotokea umeme umekatika ama inapotokea miundombinu ya umeme imeungua. Hivi nimesimama hapa nina vijiji vitano ambavyo transformer zimeungua na wananchi wanasubiria huduma ya umeme kwa muda mrefu tumeendelea kuwatafuta TANESCO, TANESCO wanarudisha mpira kwa REA, REA inarudisha mpira kwa mkandarasi hivi ninavyozungumza Vijiji vya Mkalinzi, Kititiza, Mkubu, Mumilamila na Mganza, wananchi hawa transformer zimekatika muda mrefu, zimeungua wananchi hawana huduma ya umeme. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri anapokuja kuhitimisha hoja hii uje na majibu, aje na suluhu ili niweze kukubaliana, nisiweke pingamizi kwenye bajeti hii. Aje na suluhu ni lini wananchi wangu hawa watapata huduma ya umeme ambayo imekatika.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ndaisaba, nilikuwa nangoja umalize naona humalizi muda wako umeisha.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na ninaunga mkono hoja. (Makofi)