Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninashukuru pia kwa kupata anafasi ili niweze kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii ya Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri wake kwa kazi nzuri ambayo wanafanya. Kwanza katika kumsaidia Mheshimiwa Rais kuweza kutimiza azma yake ya kuhakikisha kwamba anasambaza umeme kwenye vijiji na vitongoji vyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wangu wa Songwe sisi tunavyo vijiji 307, katika vijiji vyote 307 vitongoji vyote tayari vimeshafikishiwa umeme. Vijiji vipo 307 na vitongoji 1489 katika hivyo vitongoji 1489 tayari umeme umeshafikishwa katika vitongoji 749 na sasa hivi vimebakia vitongoji 740.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hivyo vitongoji 740 tayari katika awamu hii nyingine tumepata vitongoji 540 ambavyo hivyo vitongoji 540 Wilaya ya Ileje imepata vitongoji 107, Wilaya ya Momba imepata vitongoji 161, Wilaya ya Songwe imepata vitongoji 74, pia Wilaya ya Mbozi imepata vitongoji 205. Ombi letu wananchi wa Mkoa wa Songwe tunatamani kwamba hivi vitongoji ambavyo tumevipata 540 kazi hiyo iweze kukamilika kwa wakati ili wananchi hawa waweze kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile vitongoji vile 200 ambavyo bado vitakuwa havijaweza kupatiwa umeme tunaamini kwamba vitongoji hivi vingine 540 vitakavyo kamilika basi wananchi hawa ambao wanakaa katika vitongoji hivi 200 nao waweze kufikishiwa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa nizungumzie hali ya upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Songwe. Kwa miaka mingi sana hali ya upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Songwe imekuwa siyo ya kuridhisha, tumekuwa na changamoto ya muda mrefu ya kukatikakatika kwa umeme, changamoto hiyo inatokana na kwamba Mkoa wa Songwe tumekuwa tukitegemea stesheni ya umeme kutoka Mwakibete – Mbeya, kwa hiyo kwa miaka mingi Waheshimiwa Wabunge tulikuwa tukiomba kwamba nasi tuweze kupatiwa stesheni yetu ndani ya Mkoa wa Songwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru sana jitihada mbalimbali za Serikali ambazo zimefanywa zimesaidia sana kuweza kupunguza tatizo la kukatika umeme katika Mkoa wa Songwe. Mimi kama Mheshimiwa Mbunge ninakiri kwamba sasa hivi angalau sasa tunaona kwamba hali kidogo imetengamaa tofauti na ilivyokuwa zamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri aliyoifanya ndani ya Mkoa wa Songwe, vilevile kwa kuunganisha Mkoa wetu wa Songwe katika gridi ya Taifa ambayo lane yake inatoka Iringa inakuja Mbeya inapita Songwe, ikitoka Songwe inaenda Sumbawanga inaenda mpaka Zambia. Tayari ndani ya Mkoa wetu wa Songwe Mheshimiwa Rais ameanza Mradi wa Kujenga Kituo cha Kupooza Umeme katika Kata ya Nkangamo. Kituo hicho kitagharimu zaidi ya bilioni 250, tayari mradi huo tangu uanze kutekelezwa mwaka jana mwezi Mei tunatarajia kwamba utakamilika mwezi Mei, 2026.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matarajio yetu wananchi wa Mkoa wa Songwe kwamba, mradi huo utakapokamilika kwa kiasi kikubwa sana utasaidia kumaliza tatizo la kukatikakatika kwa umeme ndani ya Mkoa wa Songwe, lakini tunafahamu kwamba mradi huo utakapokamilika utasaida sana kuweza kuchochea ukuaji wa kiuchumi na shughuli vile vile za kijamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu kwamba Mkoa wa Songwe ni Mkoa ambao upo kwenye lango la SADC, kwa hiyo ni Mkoa wa kimkakati. Tutakapokuwa na umeme wa uhakika ndani ya Mkoa wetu wa Songwe tafsiri yake ni kwamba, tutaweza pia kuvutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza na kufungua viwanda ndani ya Mkoa wa Songwe na hatimaye Mkoa wetu wa Songwe utapata maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri ameshakuja mara kadhaa ndani ya Mkoa wetu wa Songwe, vilevile amekuwa akijibu maswali kwamba lini kituo hicho kitaweza kukamilika. Nami kama Mheshimiwa Mbunge juzi nilipita pale nikakuta tayari tumefikia kwenye utekelezaji wa 18%, tunaweza tukajiuliza ndani ya mwaka mmoja tumefikia utekelezaji wa 18% tafsiri yake ni kwamba umebakia mwaka mmoja tu ili mradi huo uweze kukamilika. Je, ndani ya huo mwaka mmoja 82% ambazo zimebaki zitakuwa zimekamilika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, uweze kufika ndani ya Mkoa wetu wa Songwe, tumemwona ametembelea kwenye vituo vya kupooza umeme pale Urambo pamoja na Kidatu na sisi wananchi wa Mkoa wa Songwe tunatamani afike ndani ya Mkoa wa Songwe ili uweze kutembelea kituo chetu cha kupooza umeme pale Nkangamo ili tuweze kujua kwa nini kasi ya ukamilikaji wa kile kituo ni ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Songwe tunatamani hata ikiwezekana pamoja na kwamba mradi inabidi ukamilike inabidi ukamilike mwezi Mei, 2026 tunatamani kwamba mradi huo ikiwezekana ukamilike kabla ya muda huo, kwa sababu tumeshuhudia pia kwenye miradi mingine imekamilika kwa wakati. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Nishati wananchi wa Mkoa wa Songwe wanakusubiri sana Songwe ili kwa pamoja tuweze kujua ni nini ambacho kinasabisha mradi huo uende taratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia nizungumzie hali ya utendaji wa Shirika la TANESCO ndani ya Mkoa wa Songwe. Tunafahamu kwamba Mkoa wa Songwe ni mpya, jiografia ya mkoa wetu haijakaa vizuri. Jiografia sisi ni ya milima na asilimia kubwa ni maeneo ambayo ni ya vijijini. Watendaji wa Shirika la TANESCO ndani ya Mkoa wa Songwe wanapata shida sana kutokana na kwamba hawana vifaa vya kutosha hususani magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TANESCO ndani ya Mkoa wa Songwe wanayo magari mawili tu, ambayo magari hayo mawili ndiyo ambayo yanatumika kwenye Wilaya ya Mbozi, lakini ukienda kwenye Wilaya ya Momba ambayo ni lango la SADC hakuna gari hata moja, hivyo inapelekea pale ambapo itakea changamoto labda transformer imeharibika au nguzo zimeanguka wananchi wanachelewa sana kupata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye Wilaya ya Ileje huko nyuma tulikuwa tuna gari moja lakini tangu lile gari limepata ajali mpaka sasa hivi bado hatuna gari lolote ndani ya Wilaya ya Ileje. Zinapotokea hitilafu inawalazimu kwenda kuazima magari kitu ambacho ni gharama sana. Ukienda kwenye Wilaya ya Songwe ambayo ndiyo Wilaya ya uchimbaji, kule sisi tunachimba dhahabu, lakini bado TANESCO ndani ya Wilaya ya Songwe hawana gari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri sisi tunafahamu kwamba wewe ni mchapa kazi na wananchi wa Mkoa wa Songwe wana imani kubwa sana na utendaji kazi wako kwa sababu tumekuwa tukikuona mara kwa mara ukichukulia hatua na kufanyia kazi mambo mengi ambayo Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiyasema ndani ya Bunge hii. Ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri, katika bajeti hii ninajua kwamba mnayo bajeti ya kununua magari, miongoni mwa yale magari ambayo wameyapanga kwenda kuyagawa kwenye mikoa mingine mimi niombe Mkoa wetu wa Songwe upate kipaumbele kwa sababu kwanza ni mkoa ambao ni mpya, lakini jiografia yetu sisi ni mbaya ili basi changamoto zinazotokea wananchi wale waweze kupata huduma kwa haraka kama inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nikushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)