Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipatia nafasi na nguvu na afya kusimama kwenye Bunge lako Tukufu siku ya leo. Napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye Wizara hii kwa kuwapa fedha, kwa kuhakikisha kuwa umeme unawaka na watu wanapata umeme wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko ambaye ni Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Mheshimiwa Waziri wa Nishati kwa kazi kubwa aliyoifanya kwenye sekta hii ya umeme, kuwa wananchi wengi amepata umeme wa kutosha. Pia, namshukuru Naibu wake Mheshimiwa Judith Kapinga, Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu na Wizara yote kwa ujumla, pamoja na Kamati ambayo inashughulikia jambo hili la nishati. Nawapa pongezi kwa sababu, wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia kuhusu Bwawa la Mwalimu Nyerere, ambalo linatoa umeme wa maji. Kweli, tunashukuru sana Mheshimiwa Dotto Biteko na Naibu wako wamefanya kazi kwa sababu, sasa hivi mitambo yote tisa imekamilika, umeme unaingizwa kwenye grid na hivyo, umeongezeka mpaka megawati 4000, pamoja na vyanzo vingine vya umeme kama solar, jua na mambo mingine ambayo yanaongeza umeme. Kwa hiyo, sasa hivi tuna imani umeme umeongezeka na tunaweza kuuza hata nchi za nje. Kwa kweli, Tanzania tunajidai kwa uongozi wa Mama Samia, ambaye anatuongoza vizuri kwenye hii sekta ya Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ya kukatikakatika kwa umeme hata Mkoa wetu wa Morogoro umeme unakatika ingawa tuna vyanzo vingi vya umeme, kuna Kidatu na Bwawa la Mwalimu Nyerere. Kwa hiyo, ninashauri kuwa hili suala la kukatikakatika kwa umeme liangaliwe kwa sababu, umeme unapokatika vifaa vinaharibika, TV zinaharibika, fridge zinaharibika, mboga kwenye fridge zinaharibika. Kwa hiyo, ni vizuri uweze kuangaliwa usiwe unakatikakatika, la sivyo Mheshimiwa Dkt. Biteko anafanya kazi nzuri, ila hili jambo la kukatikakatika linatia doa. Inaonekana kuna hitilafu mbalimbali, siyo kusema umeme ni kidogo ila hitilafu nyingine, nyaya zinaweza zikashikana, zikafanya nini, kwa hiyo, watu wapate taarifa kama tulivyosema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kusambaza umeme, hasa kwenye vijiji na vitongoji. Mkoa wetu wa Morogoro, vijiji vyote kwa wastani vimepata umeme ila tatizo liko kwenye vitongoji. Kwa hiyo, ninashauri kuwa, Mheshimiwa Waziri liangalie suala hilo la kupata umeme kwenye vitongoji kwa sababu, kila mmoja anafurahia kupata umeme, anapenda kupata umeme; umeme ni muhimu kwa binadamu, umeme ni muhimu kwa nchi yetu, umeme unakuza uchumi, umeme unaendesha viwanda, umeme ni kila kitu. Kwa kweli, umeme ni jambo zuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana hata hawa wakandarasi ambao wanawaweka kwenye kusambaza umeme waweke harakati kubwa kama fedha zipo, kusudi waweze kuweka umeme kwenye vitongoji vyetu. Kwa sababu, Mkoa wangu wa Morogoro, ukweli wameanza kuweka kwenye vitongoji, lakini vitongoji vingi pamoja na Taifa kwa ujumla bado havijapata umeme ila naamini kwa jitihada yako tutapata umeme, kama ilivyopangwa ila jitihada ziweze kuongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa nishati safi na salama. Kwa kweli, majiko haya ya gesi, elimu imeenea, watu wanapenda sana kutumia nishati hii nzuri, inakufanya uwe na afya, ufurahie wewe mwenyewe wakati unapopika, lakini tatizo ni moja tu, bei bado iko juu. Waziri aangalie jinsi ya kuwapunguzia bei kusudi kila mmoja aweze kumudu kununua hii mitungi au mtungi unavyokwisha aweze kujaza kwa sababu, unakuta akinamama kweli wana mitungi, wanafurahia, lakini gesi inapoisha hana shilingi 23,000 ya kujaza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba iangaliwe, ili kusudi waweze kuitumia, iwe endelevu, isiwe wanapata tu ndiyo mwisho. Iwe endelevu kusudi hata akinababa, kuna akinababa wengine wanapika, ni babalishe na wenyewe wanafurahia kutumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninaliongelea ni kuhusu usambazaji, hasa wa umeme majumbani. Tunasema mijini ni shilingi laki tatu, vijijini ni shilingi 27,000, lakini kumbuka hata wewe unatoka huko mjini, kuna wengine wanatoka mjini hawamudu shilingi laki tatu kuingiza umeme, lakini wanaupenda. Kwa hiyo, ninaomba kadri tunavyozidi kupata umeme mwingi nchini kwetu halafu vyanzo vinakuwa vingi, kuna makaa ya mawe yanazalisha umeme, kuna maporomoko ya maji yanazalisha umeme, ninaomba waweze kuangalia kuingiza umeme kwenye nyumba zetu bei iweze kuangaliwa kadri tunavyopata umeme mwingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo wananchi wamenituma ni kuhusu bei ya nguzo za umeme. Wanatamani kuweka, lakini wakati mwingine unakuta bei inakuwa juu kuingiza nguzo kama tatu kufika nyumbani kwake au ngapi, wakati mwingine unakuta ni shida sana. Kwa hiyo, ninaomba sana na lenyewe waliangalie kusudi wananchi waweze kupata umeme wa kutosha, wafurahie maisha na waweze kufanya biashara ndogondogo. Kwa mfano, kusaga unga unatumia umeme, viwanda vidogovidogo hivyo unatumia umeme, mwanga unatumia umeme, yaani vitu vingi unatumia umeme; wanafunzi kusoma wanatumia umeme, sasa hivi ni science and technology tunatumia umeme. Kwa hiyo, ninaomba sana hiyo bei ya umeme iangaliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafurahi sana, kwa kweli, ukiwa na umeme unafurahi sana; watu wengi wanapenda umeme, watu wengi wanapenda nishati safi. Kwa hiyo, ninaomba sana hizo bei ziweze kuangaliwa, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Biteko ambaye ndiye Waziri wa Nishati na Wizara nzima nafikiri umenisikia, nimeongea kwa kifupi, nimechangia kwa kifupi. Yale ndiyo nimetumwa na wanawake wa Morogoro na wananchi wa Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)