Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Tumaini Bryceson Magessa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa fursa hii aliyotupatia tena ya kuchangia katika Wizara ya Nishati Mwaka huu wa Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa wasilisho zuri la hotuba hii ambalo limesheheni mambo mengi, ambayo ni mafanikio na maombi, kwa ajili ya bajeti inayofuata. Nimpongeze sana Naibu Waziri wa Nishati kwa kazi kubwa anayofanya ya kumsaidia Waziri wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu kuhakikisha kwamba, kazi hizi zinatekelezeka; bila kuwasahau wataalam, Katibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu wawili wa mafuta na yule wa umeme pamoja na Nishati Jadidifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wako wakurugenzi mbalimbali wakiwemo wa REA, EWURA na PURA kwa sababu, Wizara hii imesheheni mambo mengi ambayo yanatumiwa na wananchi wetu. Kwa hiyo, niwapongeze wataalam wote kwenye Wizara kwa kazi kubwa ambayo inafanyika kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napitia hotuba hii nikagundua bajeti ya mwaka jana ilikuwa takribani shilingi trilioni 1.88 na ya mwaka huu imekwenda shilingi trilioni 2.25, maana yake ni kuna mambo makubwa mengi yanakwenda kufanyika. Kwa hiyo, kuwapongeza kwangu ni kwa sababu ya hayo waliyofanya na ambayo wanategemea kwenda kuyafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Ukurasa Namba 116 utaona mafanikio mengi yameandikwa hapo, ambayo yanatokana na utekelezaji wa bajeti iliyopita, kwanza kuongezeka kwa uwezo wa mitambo ya uzalishaji, installed capacity, ambayo imekwenda mpaka takribani megawati 4000 na 31.71 katika hii na vyanzo mbalimbali vinaonekana hapo. Ukiangalia utaona vyanzo, kwa mfano, mitambo inayozalisha kwa kutumia maji inatuletea karibu megawati 2000.7, ukiangalia mitambo ya mafuta ni megawati 101, Tungamotaka 10.55 megawati na umeme jua una megawati tano, unaweza ukajua nchi hii ina jua, lakini tumeweza kupata umeme jua megawati tano tu, maana yake ni hatujafanya vizuri sana kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, ukiangalia huko ndani tuna plan ya kuwa na megawati 150, lakini kasi yenyewe nafikiri ni ndogo, iongezewe, ili tuweze kupata hiyo energy mix. Kwamba, uzalishaji wetu uwe na vyanzo mbalimbali, ili hata maji yakipata changamoto, basi tuwe tunaweza kupata atleast umeme wa kuweza kufanya nchi isiende gizani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile inaonekana tuna harakati, tuna mchakato mzuri wa jotoardhi. Mpaka sasa bado jotoardhi halijaonekana kwenye ile energy mix ya kwetu hapa nchini, niombe sana, hapa kwenye jotoardhi tufanye kitu. Wenzetu wa Kenya wanatakribani karibu megawati 1000, sisi bado tuko katika mchakato. Tuna kitu cha kujifunza kutoka kwa majirani zetu, ili tuweze kuhakikisha kwamba, jotoardhi kitu ambacho hakitakuwa na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi kitusaidie kuhakikisha kwamba, kwenye energy mix inatuletea umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mafanikio haya, kwanza nampongeza Mheshimiwa Rais na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kwa sababu, ni mara ya kwanza installed capacity yetu imekwenda kwa takribani 151%, kwenye hotuba hii inaonesha yaani umezalisha mara 151% more, inaonesha kabisa kwamba, kuna kazi kubwa imefanyika na mimi niwapongeze, kama tutaendelea kwa kasi hii maana yake ni tutakuwa na uwezo wa kukutana na demand yetu maana inabadilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia waliyopata mwaka jana na mwaka huu, imeshabadilika. Maana yake ni watu wengi wameanza kutumia umeme. Kwa hiyo, maximum demand tukienda baada ya muda mfupi itabadilika sana na baadaye mahitaji yetu yatakuwa makubwa sana. Kwa kuwa, sasa tumezalisha megawati 4000 tujitahidi kuona vyanzo tunavyoweza kuvipata, ili at least twende kwenye megawati 8000 kwa sababu, unajua mahitaji ya umeme ndani ya nchi hii yanaweza kuwa mara mbili au mara mbili na nusu baada ya miaka mitano tu inayokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewapongeza sana kwa sababu, inaonekana kwenye ripoti yetu kuna line nyingi zimejengwa za kilovoti 400; kuna line ya Singida kwenda Arusha, kuna line ya Kutoka Julius Nyerere kuja Chalinze, lakini kuna line ya kutoka Nyakanazi kwenda Kigoma. Hizi zitakupa uwezo mkubwa wa kufanya watu wetu waweze kupata umeme, lakini kuna line moja ambayo inatakiwa ije hapa Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ombi langu kwamba, kutoka hapa Dodoma kwenda kuunga Singida, line hii ijengwe kwa wakati, ili kuhakikisha umeme huu sasa hiyo networking imeshapatikana na namna hiyo tutakuwa na uhakika kwamba, hata tukitaka kuuza umeme kutoka Julius Nyerere tutauuza kwa urahisi. Leo hii tukiulizana, tukitaka kuuza umeme wa Julius Nyerere itakuwa ni changamoto, ile network tunafikaje huko Singida?

Mheshimiwa Mwenyekiti, itakuwa ni changamoto. Kwa hiyo, niombe sana hili lifanyike mapema, ili tuweze kuhakikisha kwamba, tunaweza ku-access kwa wenzetu hiyo Eastern Africa Power Pool tuhakikishe kwamba, tunaweza kuitumia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mradi wetu wa TAZA ambao unaenda kutuunganisha kule Kusini, nao ufanyike kwa wakati, uongezewe kasi, ili uweze kukamilika, lakini pamoja na haya kumeongezeka wateja. Wateja wameongezeka kutoka 2,766,745 sasa wanaonekana wamefika 5,449,278. Inaonekana kabisa katika miaka hii mitatu, minne, wateja wameongezeka sana. Kilichofanyika ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichofanyika ni kwamba, tunawapongeza REA kwa sababu, wamepeleka umeme vijijini. Sasa kazi kubwa tuliyonayo ni tuna vitongoji vingi, ukiangalia kwenye taarifa jumla tuna vitongoji kama 64,000, vilivyopata umeme ni kama 33,000 hivi kwa hiyo, vitongoji 31,000 bado havijapata umeme. Kuna kazi kubwa ndugu zangu, yule wa Rural Energy Master Plan, kuhakikisha wanapanga vizuri ni kiasi gani na wanapata wapi mafungu kwenye hizi bajeti zetu kuhakikisha kwamba, vitongoji vyote tulivyonavyo vinapata umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipolifanya hili wananchi wetu kule kwa sababu, wanaishi jirani wataanza kuna kama kuna watu wamependelewa na wengine wameachwa nyuma. Kwa hiyo, tulifanye hili ndani ya miaka mitatu, minne tuhakikishe kwamba, kila kitongoji kina umeme, ili kila mmoja ashiriki kutumia umeme, lakini vilevile ashiriki kujenga uchumi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ninataka kulisema hapa ni habari ya gesi asilia CNG, tunahitaji sana CNG. Mikakati yetu inaonekana kabisa, tulikuwa na vituo viwili mwaka 2021, sasa tuna vituo tisa, lakini vituo tisa havitoshi. Mimi na jirani yangu hapa tulikwenda Dar es Salaam kukagua tukagundua vituo bado vinahitajika sana, magari mengi sasa yanatumia CNG kule Dar es Salaam. Maaneo ambapo CNG ipo na ukiangalia kwenye takwimu wameonesha mwaka 2021 tulikuwa na takribani 29,000 leo tuna 188,000 maana yake ni multiplication yake utaona ongezeko ni kama mara saba hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweza kuhakikisha kwamba, Mradi wa LNG (Liquified Natural Gas) umefanikiwa tutaweza kuhakikisha gesi hiyo inaweza kufika Dodoma, itaweza kupelekwa Mwanza, itaweza kupelekwa Arusha na itaweza kupelekwa Mbeya. Mazingira hayo yatafanya watu wengi waingie kwenye matumizi ya LNG na kwa matumizi hayo kwa sababu, gharama imeshaonekana ni ndogo watu wengi watapata uchumi bora kuliko ilivyo leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai tu kwamba, hapa kwenye CNG tufanye kweli, wanasema Waswahili, kuongeza vituo. Ipo plan kwamba, mpaka mwaka kesho, kwenye ripoti hii, vituo vitakuwa 20 sawa, lakini Dodoma kutakuwa na vituo vingapi, ili magari ya Serikali yaliyo Dodoma yatumie gesi hii? Changamoto yetu iko hapo, lazima tuje na LNG. Kwa hiyo, niwaombe sana, kwenye hili tuhakikishe kwamba, tunakwenda kasi na kuhakikisha tunaweza kupata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, ninaona taa imewaka, kuna clean energy, hapa tumeingiza kwenye national energy compact. Watu wetu wameanza kutumia gesi, watu wetu tumewapelekea mitungi, lakini hatujawapelekea elimu ya kutosha, ili watumie gesi huko vijijini na bado hatujawapelekea vituo viwe karibu ili wakitaka ku-refill wasipate gharama kubwa kwenda kujaza mitungi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, umewasha taa, ninaomba kuunga mkono hoja. Ninaomba niishie hapo.