Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kiteto
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi. Nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia kwa miradi mingi sana ya umeme nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema vijiji vyote kuna umeme na hakuna kijiji hakina umeme, sasa tunamaanisha kazi aliyofanya Dkt. Samia kwa miaka minne ni ya mfano. Kwa hiyo, kwa kweli, tunampongeza kwa dhati sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza Mheshimiwa Dkt. Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kweli, kwa kazi kubwa anayofanya; mzee wa kusema na kutenda. Kwa kweli, tunampongeza kwa kazi za Wizara na kazi anayoifanya kumsaidia Mheshimiwa Dkt. Samia. Kwa wale wanaofuatilia kwa karibu, Mheshimiwa Dkt. Biteko ameongeza kasi kubwa sana kwenye masuala ya nishati nchini, lakini mzee, ziara zake tunazifuatilia sana, anaponya watu wengi sana na anazungumza vizuri sana; watu ni walewale, ambapo kwa kweli, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu tunampongeza sana. Yeye ni kati ya viongozi ambao ni very humble sana na silaha kubwa kwenye uongozi ni kuwa humble. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri, Wakili Judith Kapinga, naye kwa kweli, anafanya kazi nzuri sana ya kumsaidia Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu. Ni kijana, lakini anafanya kazi nzuri sana, anapeperusha bendera ya vijana vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tumpongeze Katibu Mkuu, Wakurugenzi na mameneja wa Mikoa. Ninazungumza habari ya Mkoa wa Manyara na Dodoma kwa sababu, Kiteto kwa TANESCO tunaitikia Mkoa wa Dodoma, lakini Mameneja wa Wilaya kwa kweli, wanafanya kazi nzuri sana. Kwa mfano, wa Kiteto wameanzisha WhatsApp group la kutupa information kila wakati za kukatika kwa umeme na pale panapotokea hitilafu. Huo ni ubunifu kwa hiyo, kwa kweli, lazima tuwapongeze kwa kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachowaomba tu, kwa sababu wateja wao wengi wana namba zao za simu, kwa wale ambao hawawezi kuingia kwenye WhatsApp group, hizi message zikiwa zinakwenda kwa wateja wao kupitia mitandao ya simu ninadhani itasaidia kuboresha huduma kwa wateja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiteto miaka mine, mitano iliyopita tulikuwa na vijiji 29 ambavyo havikuwa na umeme, ikiwemo tarafa nzima anakotoka Mheshimiwa Mbunge. Hata hivyo, tunavyozungumza sasa, vijiji vyote 29 vina umeme na vitongoji 161 vina umeme; tumebakiza kama 118 hivi. Kwa kasi inayoendelea mimi sina shaka kabisa kwamba tutamaliza hili jambo na Watanzania wengi wanapenda sana umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa nilete ombi moja hapa. Kuna Kitongoji kinaitwa Kilimawanga, Kijiji cha Mbigili na Mwenyekiti wa kitongoji hicho anaitwa Nelson Elisha Chibada. Kwa nini ninamtaja huyu? In fact, kama kuna wenyeviti ambao wanafanya kazi nzuri sana kwa kutoa taarifa za wananchi huyu Mwenyekiti wa Kitongoji anaongoza, Kiteto nzima. Ninaamini hata anaweza akawa anaongoza nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila wakati anapiga simu akisema habari ya umeme kwa wananchi wake. Umeme anaouhitaji ni wa kilometa 2.2 tu (umeme mdogo LV) na ni milioni 32 tu. Kwa hiyo, mzee wa kusema na Kutenda; mimi ninajua ameshaanza kuandika hapa na ninajua kuwa akwishaanza kutoa maelekezo. Milioni 32 ni kidogo sana na hawa wananchi wa Kijiji cha Mbigili ni wachapa kazi wazuri sana. Inawezekana hata leo wamejaa kwenye TV wanasikiliza, watapata majawabu yao leo na kwa kweli yeye mzee wa kusema na kutenda, ninajua atamaliza hili, la hiki kitongoji. Hivi vingine tunaweza tukasubiri mpango wa Serikali, lakini angalau kwa hiki Kitongoji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa katikati, pamoja na kazi kubwa iliyofanywa, Kiteto tumekuwa na shida ya umeme. Siyo kukatika, ni kukatikakatika, kwa muda mrefu sana inawaunguzia wananchi vifaa vyao na ilileta kero kubwa sana. Niliwahi pia kumpigia Mheshimiwa Naibu Waziri na Mkurugenzi wa REA kuelezea jambo hili. Ninajua kazi iliyokuwa inaendelea, ilikuwa ni kufanya mifumo hii ya zamani irekebishwe; tunaelewa kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli sasa shida nyingine kubwa ya Kiteto, sisi tunapata umeme line moja tu kutoka huku Dodoma. Ikikatika sehemu moja miji yote ya Kiteto hakuna umeme. Kwa hiyo, tukizungumza na wataalam, kama watajenga switching station hapa kwa majirani zetu na mtambo wa kupooza unaotoka Kilindi na tukawa na line nyingi za Kiteto, watatusaidia sana. Ninaambiwa ni fedha ndogo tu, takriban bilioni tatu sijui. Wakitusaidia hilo angalau watafanya wananchi wa Kiteto siyo button moja tu ikikatika basi wilaya nzima inakosa umeme kwa sababu ya line moja. Kwa hiyo ninamwomba Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu alichukue hili kwa uzito wake ili wananchi wa Kiteto nao wapate neema hii ambayo Dkt. Samia analeta kwa Watanzania wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi nyingi sana zimefanyika Kiteto. miradi ya REA IIII - Round II imekamilika, Miradi ya UVIKO imekamilika, miradi ya ujazilizi inaendelea kwenye vitongoji 37, miradi ya ujazilizi HE2A kwa vitongoji 15 inaendelea. Kweli kazi inaridhisha kabisa na timu yao iliyopo huko inafanya kazi nzuri sana. Tukipata hii switching station na kituo hiki cha kupoozea cha Kilindi ili isaidie Kiteto kupata line nyingi, ninadhani watakuwa wamemaliza suala la umeme Kiteto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dkt. Samia amefanya kazi nyingi sana na tumepata miradi mipya mingi sana. Tumejengewa sekondari tano, minara ya simu takriban 14, na yote hii inahitaji umeme. Hivyo ningetoa ushauri kwamba tuwe na fedha maalum ambayo kazi yake ni kulenga hii miradi mikubwa iliyoletwa na Mheshimiwa Dkt. Samia. Tulenge taasisi za dini na taasisi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiteto wanapata mnara wa Radio Tanzania kwa mara ya kwanza tangu uhuru. Sasa leo tusipopata huduma hiyo bora kwa sababu ya kukosa umeme; ninadhani ni ushauri wetu kwa unyeyekevu mkubwa sana. Hii miradi mipya ya shule shikizi takriban 20; kuna miradi mingi imekamilika ambayo inahitaji transformer kama sita au saba tu (Mbeli huko, NdiIali, Sunya, Olpopong’i, Mbigili, Zambia, Kisima cha Maji Engusero, Kibaya Mjini na Mafichoni). Pia minara ya simu katika maeneo ya Kinua, Partimbo, Loolera, Songambele, Loltepes, Olpopong’i, Makame, Orkiush; vyote hivi vikipata umeme na transformer hizi, hali ya umeme Kiteto itakuwa njema sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sisi ambao tunaitikia mikoa mingi. Tuko Manyara lakini ki-TANESCO tuko Dodoma. Wakati mwingine kwenye mikutano hii ya RCC hatupati taarifa nzuri sana ya ki-TANESCO kwa sababu tunaitikia mkoa mwingine. Ushauri wetu, mawasiliano yawe bora kati ya mameneja wetu hawa ili na sisi tunaoitika Dodoma Ki-TANESCO tuwe tunapata taarifa hizi kupitia Mkoa wetu wa Manyara. Kwa mfano, Mkoa wa Manyara tu Simanjiro wanaitika Kilimanjaro na Kiteto wanaitika Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya kwa sababu hii ni kengele ya pili, niwatakie kila la heri na tupitishe bajeti hii haraka sana ili watu wakafanye kazi. Ninashukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)