Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kondoa Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
3
Ministries
nil
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia hoja katika bajeti hii ya Wizara ya Nishati. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu, pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoturahisishia siasa zetu na kazi zetu kule majimboni kwa kuleta fedha nyingi kwa ajili ya miradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu pamoja na Naibu Waziri wa Nishati, kwa kazi kubwa wanazozifanya za kuhakikisha kuwa wananchi wetu wanaondoka kwenye nishati chafu na kuingia kwenye nishati safi. Kwa kweli kazi wanayoifanya ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze na kumshukuru Engineer Hassan, DG wa REA, anafanya kazi kubwa sana. Pia Meneja wetu wa Mkoa Bwana Donald Shamba naye ni kijana mchapa kazi, amepiga mzigo mkubwa sana na bila kumsahau Meneja wangu wa Wilaya Engineer Bakari Kalulu. Kwa kweli ninawashukuru kwa sababu wamewatendea haki sana wananchi wa Jimbo la Kondoa Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilikuwa na karoho ka kutaka kushika shilingi ya bajeti hii ya Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu. Hata hivyo, baadaye katika kuwaza na kufikiria nikakuta nikaangalia mambo mema mengi aliyoyafanya nikakuta kale karoho kanaondoka kenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifika kwenye kiti cha Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu wakati tunazungumzia kwenye masuala ya mitaa kupelekewa umeme kwa zile laki tatu, laki sita na kuendelea. Nilikwenda kumweleza juu ya hali mbaya ya wananchi wangu; kutokana na mitaa yao kuwa sawa na vijiji tunaomba tupunguziwe bei. Akatoa maelekezo kwa Engineer Hassan. Kwa kweli nilikwenda kwa maelekezo yake na nikapatiwa maeneo ambayo hayakuwa na umeme. Mtaa mzima haukuwa na umeme. Kata nzima ya Suruke ilikuwa haina umeme, lakini leo kata yote na mitaa yote hiyo imefikishiwa umeme na wamewashiwa umeme. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Judith.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sikuchoka, nikamwambia kuhusiana na suala la mitaa mingi kuwa haina umeme, akanichomekea kunipa vile vitongoji 15. Leo hapa ninapozungumza mkandarasi yupo anavuta waya. Kwa hiyo, baada ya muda kwa kuwa nguzo zimesimama maana yake watu wale watawashiwa umeme. Ninamshukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sivyo hivyo tu, mwezi uliopita niliuliza swali hapa. Tulipeleka nguzo kwenye Mtaa wa Chemchem – Kingale na tukapeleka nguzo kwenye Mtaa wa Tampoli – Kingale wakati mitaa hii hata umeme mkubwa ulikuwa haujafika; wakasimamisha nguzo na tulikuwa tunasubiri kupata nguzo kwa ajili ya kufikisha umeme mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikauliza swali hapa, Mheshimiwa Kapinga akawa ameruhusu tupelekewe nguzo 88. Nilipokwenda kwa Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu akakubali nguzo zote 188 ziende. Pia hivi ninavyozungumza zimekwishafika nguzo 110 jimboni. Maana yake ni kwamba, hii kazi ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyaona hayo nikagundua kwamba yeye ni mchapa kazi, Naibu Waziri ni mchapakazi na watendaji wa Wizara yake ni wachapakazi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru, baada ya kwenda kwake akaniongezea tena vitongoji sita ambavyo ni Kwa Mtwara, Guruma, Churumai, Kunduchi, Guta na Gulai. Maeneo haya hayakuwa na umeme kabisa; leo tayari ameyaingiza kwenye tenda (mfumo). Ninajua kuwa baada ya muda mkandarasi ataingia na watu wale watawasha umeme. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na ninamshukuru pia msaidizi wake pamoja na watumishi wote wa Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ambalo ninadhani Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu akilifanya nitakuwa nimevunja rekodi yangu mimi mwenyewe. Akilifanya jambo hili atanisaidia kuwa nimevunja rekodi yangu mimi mwenyewe kwenye jimbo lile. Maana rekodi ya waliotangulia nilikwishaivunja muda mrefu sana. Sasa, tukishirikiana mimi, yeye pamoja na Mheshimiwa Rais, tutaivunja rekodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mtaa unaitwa Mongoroma kuna Kituo cha Afya kikubwa sana ambacho Dkt. Samia Suluhu Hassan alitupatia fedha tukakijenga, hakina umeme. Kwa hiyo, akinisaidia kupeleka pale nitakuwa nimevunja rekodi yangu mwenyewe…
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Mtaa wa Hachwi na…
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ally Makoa, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mpembenwe.
TAARIFA
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba, hiyo rekodi haitavunjwa kwake yeye tu; hata pale katika Jimbo la Kibiti, imevunjwa rekodi kwa Mheshimiwa Waziri kwa maelezo ya Mheshimiwa Rais kutupelekea umeme katika kata za visiwani ambazo tulikuwa hatutegemei kupata umeme. Sisi tunaendelea kushukuru kwa sababu watu wenyewe ni wale wale.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ally Makoa, unapokea taarifa hiyo?
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipokea taarifa hiyo kwa sababu ninaona namna ambavyo mimi mwenyewe nilivyovunja hiyo rekodi. Ninaamini na wao watakuwa wamevunja rekodi katika maeno yao. Kwa hiyo, Mheshimiwa Naibu Waziri, nilikuwa na maombi hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hii mitaa mitatu; Mongoroma ambako kuna kituo cha afya kikubwa, Chandimu na Hachwi, ambapo Hachwi ina maeneo mawili, Kutumo na Hachwi yenyewe. Ninaomba mitaa hii, kwa sababu tayari amekwishamaliza vijiji vyote nchi nzima, sasa siyo hekima tukasema tumemaliza vijiji halafu kuna mitaa imebaki. Kwa hiyo, nilikuwa ninamwomba atakapokuwa ana-windup hebu just awatajie hawa watu wa Mongoroma, Hachwi na Chandimu awaeleze ni namna gani nao utakwenda kuivunja hii rekodi ya kuhakikisha mji ule wote unang’aa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja na ninashukuru sana. (Makofi)